Januari 27: Mkapa hasameheki na si peke yake

aleesha

JF-Expert Member
Oct 17, 2016
776
1,121
Mwaka jana ulimalizika kwa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Benjamin William Mkapa, kuchapisha wasifu wa maisha yake ya kibinafsi, kikazi na kisiasa kwa jina “My Life, My Purpose”, ambapo kwenye uzinduzi wa kitabu hicho, miongoni mwa yaliyopewa nafasi ya kutajwa, ni tukio la mauaji dhidi ya raia wasio hatia yaliyotokea kuanzia tarehe 26 Januari 2001 na kuendelea kwa msururu wa matukio kadhaa kwa siku kadhaa baadaye.

Wako waliouawa, waliojeruhiwa, waliobakwa, waliolazimika kuwa wakimbizi na waliopoteza mali. Ingawa hakuomba radhi moja kwa moja kwenye kitabu hicho, Mkapa anatajwa kuwa alikiri kuwa mauaji hayo yaliutia doa utawala wake na alikubali kuwa, madhali yeye ndiye aliyekuwa amiri jeshi mkuu wa Jamhuri, basi ndiye mwenye dhamana ya yaliyotokea. Sehemu kubwa ya matukio hayo iliripotiwa visiwani Zanzibar, hasa hasa Pemba, lakini ukweli ni kuwa sehemu nyengine kadhaa za Tanzania nazo zilikumbwa na mkono wa chuma wa utawala wa Mkapa.

Leo ni tarehe 27 Januari, siku ambayo sehemu kubwa ya dhuluma hiyo ilitendwa. Ni siku ya giza kwa Jamhuri nzima ya Tanzania, ni siku ya msiba kwa ndugu na jamaa wa madhulumu. Ni bahati mbaya kwamba, kama taifa, Tanzania haiitambuwi siku hii kuwa hivyo, ingawa walioguswa na maafa yale moja kwa moja hawajawahi kuisahau. Mimi ni miongoni mwao.

Wakati yanatokea, Nakumbuka kila kitu kuhusu dhuluma hii. Naikumbuka sauti ya Bi Msimu, jirani yetu muuza chapati, ambaye kwa kujuwa kuwa akipaza sauti yake kutoka jikoni siye tulioko barazani tungelisikia, alipoanza kusikia bunduki zinaalika, akabwata: “Wauweee wamalizee hao Wapembaaa!” Kwa muda wote uliobakia baada ya siku hiyo, Mimi na mwenzangu Hamida tuligoma kununuwa chapati zake wala kualakiana naye kwa lolote lile.

Naziona hadi sasa ninapoandika sura za askari wa jeshi la polisi, nasikia sauti za risasi za moto, naihisi harufu ya jasho, vumbi na machoni inanijia picha ya mmoja wa marafiki zangu aliyeuawa. Huyu alikuwa mfadhili wetu. Sisi tunakwenda chuoni kusoma, hatuna pesa ya kula, tunapitia kidukani kwake, anatuagizia sahani ya chipsi mayai.

Siku (kama si miaka) kadhaa baada ya hapo, niliandika na kuandika na kuandika ili kuyaweka matukio haya kumbukumbuni. Nilitumia zaidi ushairi na mara chache niliandika makala. Kuna tungo zangu kadhaa ambazo zinahusiana moja kwa moja na siku hii na zile ambazo zinahusu hisia nzito za baada ya siku yenyewe. Ningekuwa mchoraji ningefanya hivyo hivyo pia. Jumla ya yote ni kitu kilichomo ndani kabisa ya nafsi yangu - nacho ni kwamba sikusamehe wala sikusahau!

Kwa hivyo, kwamba Mkapa kwenye kitabu chake amekiri kutokea kwa uovu huu dhidi ya watu wangu, hakukubadilisha chochote kwenye hisia zangu. Nilishaandika shairi mwaka 2001 baada ya hotuba yake ya Muafaka wa Pili, ambapo niliikataa pale pale kauli yake ya kunyoosha mkono, maana niliuona mkono wake umerowa damu.

Na niliendelea kuamini hivyo maana ni yeye aliyekuwa amiri jeshi mkuu tena kuelekea uchaguzi uliofuatia na akamwaga vikosi vingi mno vya kijeshi ndani ya ardhi ya Zanzibar kiasi cha kwamba alipoulizwa na mwandishi Jonathan Powers wa jarida la Christian Monitor kuhusu hilo, naye alimrejeshea swali: “Kwani jeshi la Marekani linafanya nini Iraq?”

Lakini Mkapa hakuwa peke yake na bado si peke yake asiyestahiki msamaha kwenye hili. Anao wenzake. Aliyekuwa waziri mkuu wake, Fredrick Sumaye, aliyekuwa makamu wake, Marehemu Dk. Ali Omar Juma, aliyekuwa waziri wake wa mambo ya ndani, Mohammed Seif Khatib, na aliyekuwa mkuu wake wa jeshi la polisi, Omar Iddi Mahita. Orodha hii inawagusa pia wale waliokuwa chini yao na ambao mkufu wa amri na utekelezaji wa amri hizo uliwagusa. Maana wako ambao waliamua kuukaidi, miongoni mwao Askari Shaibu ambaye alifutwa kazi kwa kukataa kuwafyatulia risasi waandamanaji.

Vile vile, kama ripoti ya Shirika la Haki za Binaadamu la Human Rights Watch ilivyobainisha, mauaji yaliratibiwa vyema na vikosi vya Jamhuri ya Muungano na vya Zanzibar, yakiwemo makundi yaliyoundwa na CCM - siku zile tukiwaita Melody. Viongozi wa serikali na chama hicho upande wa Zanzibar wanabeba dhamana ya moja kwa moja kwa kila roho iliyotoka, kwa kila damu iliyomwagwa na kwa kila heshima iliyovunjwa.

Ukweli ni kuwa hata baada ya mauaji hayo, hakuna kilichobadilika ndani ya fikra zao, maana makundi hayo yaliendelezwa na yanaendelezwa hadi leo.

Kubwa zaidi ni kuwa kile kilichosababisha maandamano ya amani na ambayo yalikuja kuwa kisingizio cha kufanya mauaji hayo, bado kimeendelea hadi sasa. Nacho ni dhuluma za kijamii na kisiasa dhidi ya kundi moja la watu ambalo linachukuliwa na dola kuwa ni adui wa kudumu.

Nimalizie kwa utungo huu UMMA BARABARANI ambao nao unatimiza miaka 19 leo hii tarehe 27 Januari 2020:

Vuu! Vuu!
Nasikia umati wavuma
Natupa macho kuutazama
Waja mchakamchaka, wapuma
Macho yalengalenga machozi, yauma
Anga limejaa sauti zao, wasema:
“Lete haki, ondosha dhuluma
Twataka kheri, hatutaki nakama!”

Navutwa nayo tukufu kalima
Nami barabara naiandama
Naungana na umma
Naandamana
Nadai haki yangu!

Kisha mara mbele yetu, wanasimama
Waitwao walinzi wa usalama
“Chawanyikeni! Dola inasema!”
Dola ni nani, ikiwa si sisi umma?
Twasonga mbele mikono tumeshikana
Kwa mapenzi, kwa umoja, mbele twajisukuma!

Mara tu! Tu! Tu!
Risasi kwetu zamiminwa
Yatirika damu ya waadhama
Yaachana mikono il’oshikana
Zaagana roho zil’opendana
Vizuka
Mayatima
Vilema
Bado umma barabarani!
 
Aombe msamaha kwa lipi? Alichokifanya Mkapa madhara yeke ni madogo kuliko angeacha hilo vuguvugu kuendelea kumbuka sacrifies ni lazima kwenye utawala wowote. Pia yeye aliapa kuulinda Muungano na ndio kazi Namba 1 ukiwa Raisi wa Tanzania. Hata ungekuwa wewe lazima ungefanya kama alivyofanya Mkapa.
 
Aisee umenikumbusha kisa kimoja pale chukwani, mama mmoja alinisimulia mengi sana juu ya madhila na masaibu waliyokutana nayo huko visiwani Pemba,

Kama mwenyewe alikiri basi hamna budi kumsamehe maana duniani hakuna mkamilifu

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Aombe msamaha kwa lipi?? Alichokifanya mkapa madhara yeke ni madogo kuliko angeacha hilo vuguvugu kuendelea kumbuka sacrifies ni lazima kwenye utawala wowote,Pia yeye aliapa kuulinda Muungano na ndio kazi Namba 1 ukiwa Raisi wa Tanzania.Hata ungekuwa wewe lazima ungfanya kama alivyofanya Mkapa.
Kwani maandamano yalikua ya kupinga Muungano?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Aisee umenikumbusha kisa kimoja pale chukwani, mama mmoja alinisimulia mengi sana juu ya madhila na masaibu waliyokutana nayo huko visiwani Pemba,
Kama mwenyewe alikiri basi hamna budi kumsamehe maana duniani hakuna mkamilifu

Sent using Jamii Forums mobile app
True hata clip zipo YouTube kwa ajili ya vizazi vinavyo juu ya unyama waliotendewa ikiwemo kinamama kuachwa uchi selo wakikaguliwa na polisi wa kiume wa kuwazaa
 
Aombe msamaha kwa lipi?? Alichokifanya mkapa madhara yeke ni madogo kuliko angeacha hilo vuguvugu kuendelea kumbuka sacrifies ni lazima kwenye utawala wowote,Pia yeye aliapa kuulinda Muungano na ndio kazi Namba 1 ukiwa Raisi wa Tanzania.Hata ungekuwa wewe lazima ungfanya kama alivyofanya Mkapa.
Si kweli kwani waliopita na wajao hawawezulinda muungano? Tawala za kishenzi ndo utayakuta hayo na si kila tawala
 
Aombe msamaha kwa lipi?? Alichokifanya mkapa madhara yeke ni madogo kuliko angeacha hilo vuguvugu kuendelea kumbuka sacrifies ni lazima kwenye utawala wowote,Pia yeye aliapa kuulinda Muungano na ndio kazi Namba 1 ukiwa Raisi wa Tanzania.Hata ungekuwa wewe lazima ungfanya kama alivyofanya Mkapa.
Hoja yako haina maana kabisa. Kwani walikuwa wanaandamana kutaka kuvunja muungano?

Mbona kuna nchi nyingi ambazo watu wamewahi kuandamana na hakuna madhara yoyote?

Ni kwenye tawala za kidikteta ndiko ambako maandamano huishia kuwaondoa watawala, na muda mwingine kusababisha nchi kuparanganyika. Na sababu kubwa ni hasira za umma pale ambapo watawala huwa waneua waandamanaji.
 
Ulipona mshukuru Allah

Maana kumbe sio Mkapa tu, ni wengi tu....watu wa chini, askari wote, wake zao, ndugu zao

Mwisho umejikuta mpaka wewe mwandishi haupaswi kusamehe wala kujisamehe

Ondoka kwenye hicho kifungu; Mkapa hajui hata jina lako
 
Njoo upande wa pili; waandamanaji walichinja askari kama kuku; mbona hilo husemi.
"Since they ( the government) are incapable or unwilling to protect us, we must do whatever is necessary to protect ourselves" Malcom X
 
Hoja yako haina maana kabisa. Kwani walikuwa wanaandamana kutaka kuvunja muumgano?

Mbona kuna nchi nyingi ambazo watu wamewahi kuandamana na hakuna madhara yoyote?

Ni kwenye tawala za kidikteta ndiko ambako maandamano huishia kuwaondoa watawala, na muda mwingine kusababisha nchi kuparanganyika. Na sababu kubwa ni hasira za umma pale ambapo watawala huwa waneua waandamanaji.
Wengine tulikuwa kijijini huko hatujui hebu wekeni mizani sawia.
Eti waandamanaji nao walichinja askari kama kuku?
Halafu askari walipiga watu hadi nyumba za ibada?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom