Jangwani Dar wakihama na Serikali ihamie Dodoma?

Jan 16, 2007
721
176
Jangwani Dar wakihama na Serikali ihamie Dodoma?


Privatus Karugendo


WASOMAJI wangu nianze makala hii kwa kuwatakia heri ya mwaka mpya. Tumshukuru Mungu kwa wema wake kutuvusha kuingia mwaka wa 2012. Ni kwa neema na huruma yake na si kwa ubora wetu tumeendelea kuishi.
Ninawashukuru wote walionitumia utashi mwema wa mwaka mpya kwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi. Sikushindwa kujibu ujumbe kwa kila aliyenitumia bali naendeleza mgomo niliouanza miaka miwili iliyopita, kutotuma ujumbe mfupi wakati wa Krismasi na mwaka mpya.
Sababu ya msingi ni kupinga utamaduni huu wa kutajirisha kampuni za simu za mkononi wakati wa sikukuu. Ni wazi kampuni hizi zinatunyonya kila siku, hivyo ni bora kupunguza mirija yao wakati wa sikukuu.
Kama kutojibu ujumbe wenu kuliwakwaza, mnisamehe. Naomba makala hii basi iwe jibu la ujumbe wenu wa kunitakia mema mwaka huu mpya.
Kama nilivyotaja hapo juu tumeruhusiwa kuendelea kuishi hapa duniani kwa neema na huruma ya Mungu na si kwa ubora wetu. Kuna watu bora zaidi yetu wameshindwa kuuona mwaka 2012.
Ni imani yangu kwamba hatukuruhusiwa kuishi ili tuendelee kula na kunywa tu bila kutoa mchango wowote ule. Hatukurusiwa kuendelea kuishi ili tuyatafute madaraka kwa gharama zozote ili tuwakandamize na kuwanyanyasa wanyonge badala ya kuwaongoza.
Dunia ya leo ina changamoto nyingi, bila kujaliwa hekima na busara, tutaivuruga na kulivuruga taifa letu. Badala ya kutumia nguvu zetu kutafuta mali, fedha na madaraka, ni muhimu kuelekeza nguvu hizo kutafuta hekima na busara.
Tanzania, tunauanza mwaka 2012 tukiwa na changamoto nyingi; kuna suala la Katiba, Bunge kuyumba, uporaji ardhi, vurugu ndani vyama vya siasa, unyanyasaji wa kijinsia, vurugu vyuo vikuu, na vurugu kwenye dini.
Tusisahahu harakati za urais 2015, nafasi moja lakini mamia wanaiwania, uhaba wa chakula, mfumuko wa bei na hata kigugumizi cha kufanya uamuzi mgumu.
Tumeshuhudia Serikali ikitaka kutumia nguvu kubwa kuwahamisha wanaoishi Jangwani, Dar es Salaam, wakati Serikali hiyo hiyo, inashindwa kutumia nguvu hizo kuhamia Dodoma.
Mpango wa kuhamia Dodoma ni wa miaka mingi, lakini hadi leo Serikali imeshindwa kuhama kwa visingizio vinavyoelekea kufanana na vile vya watu wa Jangwani waliokumbwa na mafuriko mwishoni mwa mwaka jana (2011).
Swali ni je, watu wa Jangwani wakihama na Serikali ihamie Dodoma? Zile nguvu zitakazotumika kuhamisha watu wa Jangwani zitumike pia kuihamisha Serikali kwenda Dodoma?
Tumeshuhudia Serikali ikitumia nguvu zake kuwakamata "wachochezi" waandishi wa habari na wahariri na kushindwa kutumia nguvu hizo hizo kuwakamata wafanyabiashara wa mafuta wanaoficha nishati hiyo na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi hadi Musoma lita moja ya petroli kununuliwa kwa Sh. 10,000.
Kuna uchochezi zaidi ya kuficha nishati hii na kuwachonganisha wananchi dhidi ya Serikali yao? Usafiri unakuwa taabu na shughuli za uzalishaji zinakwama.
Kwa maneno mengine watu hawa ni wahujumu uchumi. Serikali iko kimya na nguvu zake hazionekani kuwakamata.
Tumeshuhudia Serikali ikitumia nguvu kuzuia maandamano ya wanaotaka kufikisha ujumbe kwa njia ya amani na wakati huo, Serikali hiyo hiyo ikishindwa kuwakamata wafanyabiashara wanaopandisha bei ya sukari.
Serikali ilitamka bei ya sukari isizidi Sh. 1,700, nenda madukani uone bei ya sasa. Wakati Serikali inataka kutumia nguvu kuwahamisha wanyonge wa Jangwani, kila Mtanzania anashangaa Serikali hiyo hiyo kushindwa kuwakamata wezi walioingia Benki Kuu na kuiba mabilioni.
Ilipobainika kuna wezi, wakajitokeza na kukiri waliiba na kwa dharau kubwa ‘wakarudisha' fedha hizo za wizi, haijulikani pamoja na riba au walirudisha kiasi kile kile? Hawakukamatwa!
Serikali yenye nguvu za dola inashindwa kuwakamata wezi wanaojitangaza, tena wezi wa mabilioni ya shilingi, badala yake inawakamata waandishi wa habari na wanafunzi wanaoandamana kudai mikopo ya elimu ya juu?
Hoja hapa ni kwamba tumeuanza mwaka na changamoto kubwa. Kwa vile ni nyingi, nijikite katika suala hili la Jangwani.
Nimemsikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq akisema; "Watu wa Jangwani wasipokubali kuhama kwenda Mabwepande, watatambua nguvu za Serikali".
Maana yake ni polisi watatumika kuwahamisha. Lakini inashangaza polisi hawatumiki kuihamisha Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Polisi hawatumiki kuwakamata wahujumu uchumi. Siandiki kuwatetea wakazi wa Jangwani, najua wako pale kinyume cha sheria pamoja na ukweli kwamba viwanja vyao vimepimwa na wana hatimiliki.
Naandika kushangaa jinsi hekima na busara isivyotumika. Serikali ina makosa, ilipima viwanja hivyo ikijua huo ni mkondo wa maji. Wananchi nao wana makosa kukubali viwanja hivyo wakijua ni mkondo wa maji. Maafa yametokea, nini kifanyike?
Mungu, anaturuhusu kuendelea kuishi kutumia bunduki na virungu kuleta amani na maendeleo, au kutumia hekima, busara na majadiliano?
Serikali imesikiliza hoja za watu wa Jangwani? Inajua sababu zao za kutaka kuendelea kuishi pale licha adha ya mafuriko?
Tamko la Mkuu wa Mkoa kuwahamisha watu wa Jangwani kwa nguvu linaonyesha wazi tunaishi dunia mbili tofauti. Kuna dunia ya wanyonge na dunia ya wakubwa. Mtu mwenye mshahara, posho, nyumba ya kifahari ambayo hata mafuriko yakiingia, maji yananyonywa haraka kwa mashine, ana gari la kifahari, ununuzi wa mahitaji yake ni kwenye maduka makubwa au nje ya nchi, akiugua hata mafua anakimbizwa India na Uingereza hawezi kuguswa na maisha ya watu wa Jangwani.
Watu wa Jangwani ni wa hali ya chini, wanaishi Jangwani si kwa kutaka bali hali ya maisha. Wanaishi karibu na soko, karibu na wateja. Wengi wao ni mamantilie, machinga, waosha magari, mafundi magari na pikipiki, kazi ambazo hazipatikani Mabwepande wanakohamishiwa.
Hawa tishio la maisha yao si mafuriko bali uwezo wa duni wa kujikimu kimaisha. Kufikiri kwamba wanakataa kuhama kwa jeuri, ni kudhihirisha kutokufahamu mazingira yao halisi.
Mtu wa Jangwani anauza mchicha Kariakoo, na kujipatia fedha za kusogeza maisha yake, anapika chakula na kuwauzia madereva wa daladala. Anapata kibarua kwenye majengo yanayojengwa usiku na mchana Dar es Salaam, anapata kazi ya ulinzi.
Kuna makondakta, wengine watumishi wa kazi nyumbani kwa matajiri, wapo wafagiaji barabara. Kwa ujumla, mazingira haya ya kumwezesha kujikimu hatayapata Mabwepande.
Nguvu za Serikali zikitumika kuwahamisha matokeo yake ni kuzitenganisha familia. Wanawake na watoto watakaa Mabwepande wakipata shida, wanaume na vijana watarudi katika uwanja wa ‘kusaka tonge'. Hili likitokea serikali haiwezi kukwepa lawama za kuwanyanyasa wanawake na watoto.
Hoja kwamba watu wa Jangwani wamejenga kwenye mkondo wa maji haina msingi kwa dunia ya leo. Holland, watu wanaishi baharini, si mkondo tu bali wanayafukuza maji na kutengeneza makazi ya watu.
Serikali inayowajali watu wake itaubadilisha mkondo wa maji kuwa makazi bora kwa kutengeneza miundombinu. Hata Jangwani kama kungekuwa na miundombinu mafuriko yasingeonekana.
Hata hivyo, kwa nini wahame wa Jangwani na si wa Msasani, Sinza, Tandale na Tabata Kisiwani? Huku kote yalikuwa mafuriko yaliyosomba watu na mali zao. Kwa nini wanyonge wa Jangwani pekee?
Je, wakihama maeneo hayo yatabaki wazi au tutashuhudia maghorofa yakijengwa? Je, haiwezekani hizi ni mbinu za wajanja wachache kuwahamisha watu wa Jangwani ili kugawa eneo hilo kwa wawekezaji wenye utaalamu wa kubadilisha mkondo wa maji kuwa makazi bora?
Na hili likitokea Serikali haiwezi kukwepa lawama za kuwatelekeza watu wake na kuwakumbatia wawekezaji wa nje. Busara si kuwahamisha watu, bali ni kutengeneza miundombinu na kuyajali maisha yao.
Wakati Serikali inataka kutumia nguvu kuwahamisha watu wa Jangwani kwa lengo la kuwaponyesha mafuriko, ikumbuke kule Mabwepande watakufa kwa magonjwa, njaa na watauawa wakiiba, maana bila kazi ya kujipatia kipato, vijana watajiingiza kwenye ujambazi na mwishowe kuuawa.
Serikali inataka watu hawa wahamie Mabwepande ndani ya Juma moja kuanzia sasa. Je, huko kuna hospitali, maji na shule? Watoto wa Jangwani, walikuwa wakisoma shule za mjini, watawezaje kutoka Mabwepande katika msongamano na nauli kubwa ili kusoma mjini?
Ni wazi kuna shinikizo la shule kufunguliwa, maana wahanga wa mafuriko wako kwenye shule. Hata hivyo, Serikali ina maeneo mengi ya kuwatunza watu hawa kwa muda hadi mipango mizuri itakapokamilishwa.
Kuna jengo la Machinga lililojengwa kwa mamilioni lakini machinga kwa sababu zao za msingi (machinga anamfuata mteja na si mteja kumfuata machinga) wamekataa kuhamia.
Jengo hili linaweza kutumika kuwapatia makazi ya muda wahanga wa mafuriko, ili waendelee na shughuli zao na watoto wao wasome badala ya kutumia nguvu kubwa kuwahamishia Mabwepande.
Tunapouanza mwaka wa 2012, tupige magoti mbele ya Mwenyezi Mungu na kuomba atujalie hekima na busara, atujalie kipaji na uwezo wa kuishi kwa kufuata sheria za nchi, kuwaheshimu wenzetu na kutambua haki zao za msingi.
Sote ni binadamu tunahitaji makazi bora, huduma bora, furaha na amani moyoni. Mungu atujalie uwezo wa kuongoza, uzalendo na kuipenda. Heri ya mwaka mpya wa 2012.


Source:Raimwema


 
Back
Top Bottom