ACT Wazalendo
JF-Expert Member
- May 5, 2014
- 643
- 1,603
TAARIFA KWA UMMA
Serikali Iwasikilize Wamiliki wa Mabasi.
Kwa wiki sasa, sekta ya usafirishaji imeingia mushkeli baada ya Chama cha wamiliki wa mabasi Tanzania (TABOA) kutishia na hata kusitisha huduma zao kwa baadhi ya mikoa hapa nchini.
Chanzo cha mgomo huo, kinatajwa kuwa ni kutokana na mabadiliko ya mfumo wa ukatishaji tiketi kwa njia ya kielektroniki ambao Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) inataka wamiliki wa mabasi kutumia mfumo mpya ujulikanao kama POS.
Baadhi ya wadau wa biashara ya usafirishaji abiria nchini wanadai mfumo huo mpya unawalazimisha kuwa na kiasi cha fedha katika laini ya simu au wakala wa huduma za fedha kwa makadirio yanayolingana na nauli tarajiwa kwa idadi ya viti vya basi ili kuweza kufanyakazi.
Mfumo huo unatajwa kusababisha matatizo kadhaa yakiwamo baadhi ya wamiliki wa mabasi kupigwa faini za mara kwa mara na hata wengine kufungiwa magari yao kutokana na kutokujua vema matumizi ya mfumo huo.
Kutokana na mkanganyiko huo, sisi ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kupitia Latra kuitisha kukao na wamiliki wa mabasi ili kujadiliana kwa pamoja mfumo gani rafiki utumike kukata tiketi za abiria ili kuondoa malalamiko na misigano isiyokuwa ya lazima.
Pili ACT Wazalendo tunaitaka Latra kufanyakazi kwa kuzingatia weledi wa kitaaluma na kukumbuka kwamba mifumo inayotumia teknolojia ya kisasa inayoingia nchini ni mipya kwetu, hivyo inahitaji muda wa kutosha kwa wadau kuielewa na kuitumia kwa ufasaha.
ACT Wazalendo tunaona badala ya Serikali kulumbana na wamiliki wa mabasi na hata kutishia kuwafungia au kuwapiga faini zisizo na tija, ni wakati sasa wa kufanyia kazi malalamiko yao kwa kina sambamba na kutoa elimu kwa wadau faida ya mfumo huo mpya.
Aidha sisi ACT Wazalendo tunaona kwamba wakati Latra inaendelea kutatua changamoto za mfumo huo mpya, iwaruhusu wamiliki wa mabasi kuendelea kutumia mashine zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) maarufu EFD's licha ya kuwa nazo zinakabiliwa na changamoto za mtandao kulingana na jiografia ya nchi yetu.
Sisi ACT Wazalendo, tunaamini njia pekee ya kutatua changamoto ni kukubali kusikilizana kwa njia ya mashauriano na kusikilizana.
Imetolewa na:
Janeth Joel Rithe
N/Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma.
Leo Machi 12, 2021