Kalamu Yangu
JF-Expert Member
- Dec 21, 2016
- 1,099
- 1,042
Ndoto za mafanikio, na hadithi tamutamu,
Zimegeuka kilio, na ilishaniisha hamu,
Sijaona kimbilio,hali imekuwa ngumu,
Nimeamua kurudi, sina kitu mkononi.
Yaniumiza safari, iliyojaa mashaka,
Nyumbani wana habari, leo anarudi kaka,
Wote wasubiri gari,kaka atoka kusaka,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Gari linaenda mbio,laniwaisha mateso,
Nawaza kile kilio,kwenye wake mama uso,
Ila sina kimbilio,nishaiandaa leso,
Nimeamua kurudi, sina kitu mkononi.
Yale maneno mazuri, niliyompa mamangu,
Ausubiri uzuri,Mungu auleta kwangu,
Sasa leo ni shughuli,narudi nina machungu,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Na maagizo lukuki, wajomba na dada zangu,
Sasa ni kama mkuki, yachoma mtima wangu,
Mengine siyakumbuki,yote namwachia Mungu,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Mwanangu rudi nyumbani,wala hutolala njaa,
Twakuhitaji jamani,hautamani dagaa?
Achana na ya mjini,utarudi kushangaa,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Haujamuua mtu, ama kuiba chochote,
Huko kweli kuna utu,humfahamu yeyote,
Ulevi usithubutu,utaja poteza vyote,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Wala usije kuiba,kuturidhisha nduguzo,
Vya kuiba hutoshiba,vya kuiba siyo pozo,
Urudi nyumbani baba,tutolee viulizo,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Usizihofie tambo, nilizotamba zamani,
Zile tambo za kitambo,kisa kufika chuoni,
Kejeli ni kama nyimbo,zavuma 'kiwa ngomani,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Nasikia una mwana, na ameishia kwa mama,
Wala usijegombana,mwanangu hauna boma,
Huna chochote cha mana,mwana akipata homa,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Ulijaribu kulima,soko likakugeuka,
Ingawa umeshasoma,ila wamekugeuka,
Na rafiki yako Juma,kukubeba atachoka,
Nimeamua kurudi, sina kitu mkononi.
Kipaji ulitumia,kutimiza zako ndoto,
Kaishia kuumia,kuumwa kama mtoto,
Pole mwanangu tulia,moyo usiwe mzito,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Umepata marafiki,waliokuvumilia,
Sijekuwa mnafiki,hawapendi ukilia,
Wamekuepusha dhiki,vingi wamekupatia,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Wafikishie salamu,wale walotenda mema,
Hata wasio na hamu,walikwacha wakisema,
Yatoe kwenye fahamu,yale yaliyokuuma,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Tuione sura yako,kibebe na cheti chako,
Huo ni ushindi kwako,na sisi wazazi wako,
Anajisifu babako,anajisifu dadako,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Maneno hayo ya mama,yaingia mtimani,
Tangu wakati nasoma,pesa niliitamani,
Ila sasa imegoma,najikuta safarini,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Niliutamani unga,nivute ama niuze,
Maisha haya kuunga,ndugu usiniulize,
Ingawa sikujidunga,kidogo nijiingize,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Kazi niliziomba,nikajaacha mwenyewe,
Kwa watu nikajikomba,nusura mi niolewe,
Nilishafanya na shamba,mavuno nisiyaelewe,
Nimeamua kurudi,sina kitu mkononi.
Nilishapiga debe, nipate na ya sabuni,
Ama mizigo nibebe,nipate ujira duni,
Kwote sikupata shibe,tangu juni hadi juni,
Nimeamua kurudi, sina kitu mkononi.
Narudi sasa nyumbani,nilikosa na nauli,
Nayona nyumba bondeni,pia na watu kwa mbali,
Simanzi kuu moyoni,basi ngoja nisali,
Nimeamua kurudi,sina kitu mfukoni.
"Kauli za Makabwela 2017"