Mti wa maajabu ulivyonifanya kuishi jijini Dar bila kazi

mwitasa

Senior Member
Dec 28, 2013
199
476
Mwaka 1995 Baada ya msoto wa kutosha nikaona nitazeekea kijijini kabla ya umri wangu kwa kilimo kisichokuwa na tija. Niliamua kutafuta plan B. Nikamwandikia rafiki yangu wa utotoni barua aliyekuwa akiishi Dar kuwa maisha ya kijijini yamenishinda hivyo nimeamua niende Dar kutafuta kazi na kuwa nitafikia kwake..

Baada ya kupokea barua yangu alinikubalia na kunirudishia majibu na kunipa ramani alikokuwa akiishi huku akinisisitiza kuwa nikifika mitaa hiyo aliyokuwa anajitafutia riziki nimuulizie kwa jina la tuliza koo na siyo jina lake la nyumbani kwa kuwa alikuwa halitumii kule. Nilifurahi sana baada ya kupokea majibu yale kwa kuona ndoto yangu ya kupata maisha mazuri kama imetimia. Sasa nikabakia na mtihani mmoja kichwani "natoa wapi nauli ya kunifikisha huko"?

Nilijaribu kuomba kwa ndugu wanikopeshe nauli bila mafanikio. Nyumbani sikuwa na kitu changu cha kuuza kupata nauli. Baada ya kuwaza takribani kwa wiki moja hatimaye nikapata wazo la namna ya kupata nauli. Wazo pekee ambalo lilibaki kama mkombozi wangu lilikuwa ni kumwibia mzee wangu mfugo wa ng'ombe aliyekuwa akifugia kwa rafiki yake kijiji cha pili nikauze.

Lakini mtihani wa pili ulikuwa nitafanikiwaje kumtoa huyo ng'ombe kwa rafiki yake bila wao wawili kujua na nitamfikishaje mnadani na je kama sitafanikiwa kumpata mteja siku hiyo itakuwaje na nikifeli hili zoezi nikirudi nyumbani mzee si ataniua kwa kipigo? Nikaamua liwalo na liwe.

Siku tatu kabla ya siku ya mnada uliokuwa unafanyikia kwenye kijiji cha tatu nikaenda kwa mwenyekiti wangu kuomba aniandikie kibali cha kuuza ng'ombe wangu mnadani nikampa elfu mbili akaniandikia. Siku hiyo hiyo nikaaga kwa mzee kuwa naenda kumsalimia rafiki yake huyo alikokuwa anafugia ng'ombe nikamwambia nitakaa huko walau siku 4 kumsalimia.

Nilipofika kwa rafiki yake nikampa salamu za mzee na kumweleza nitakuwa hapo kwa siku 4 kumsaidia mambo ya shamba na kuchunga mifugo akafurahi sana. Siku iliyofuata baada ya kutoka shambani nikapeleka mifugo malishoni jioni nikairudisha. Ikafuatia siku ya mnada asubuhi wanaenda shambani nikasingizia kuumwa mikono nikawaambia nitapeleka ng'ombe malishoni mapema wakanikubalia. Saa 2 asubuhi nikatoa ng'ombe wote ili kuwapeleka malishoni nikiwa na kamba kwenye kibegi nikifika huko nifunge yule ng'ombe wa mzee niwatelekeze hao wengine watarudi wenyewe. Ile nataka kuwaondoa kutoka kwenye zizi anafika kijana wake wa miaka kama 13 anasema baba kasema leo twende wote kuchunga, nikahisi kuishiwa nguvu. Ikawa mtihani wa tatu, moyoni nikasema liwalo na liwe twende itajulikana huko huko.

Tukafika malishoni kichwani nina mawazo sana jinsi ya kufanikisha swala langu kwa kumkwepa yule mtoto. Wazo nikaniijia tupeleke ng'ombe kwenye malisho ya mbali na tukifika huko nimwagize biskuti na soda kijijini sehemu ambayo kwenda na kurudi kwa miguu si chini ya masaa 3 na. Dogo kakubali nikampa elfu moja nikamuonya asiende nyumbani nikijua hadi analeta biskuti asiponikuta akirudi kutoa taarifa nyumbani ni masaa 5 hayo hadi wanaanza kunitafuta nishafikisha ng'ombe mnadani kumuuza na kutambaa. Nikamfunga ng'ombe mguu nikaanza kumswaga japo kwa mbinde sana maana alikuwa anang'ang'ana kurudi kwa wenzake.

Nikafika mnadani baada ya kama dakika 10 mteja wa kwanza anafika kumuulizia kaanza na laki moja nikamwambia atoe laki na elfu 50 kagoma akaongeza elfu 20 nikaona isiwe kesi sina hasara hapa nikamuuzia kwa 120,000 na kumpa nyaraka zangu tukaandikishana.

Nikakodi baiskeli kunipeleka barabarani nikapanda gari nikafika mjini. Nikakata tiketi ya treni kuondoka kesho yake na baada ya mwendo wa siku 2 nikaingia jijini Dar. Nikaanza kuulizia ramani na usafiri wa kunifikisha mtaani kwa rafiki yangu huku kichwani nawaza kwa nini rafiki yangu ameniambia Dar hatumii jina lake la nyumbani ila nimuulizie kwa jina la tuliza koo?

Nikafanikiwa kufika hapo mtaani rafiki yangu aliponielekeza kumbe palikuwa mjini kwenye stendi ya daladala watu walikuwa wako bize sana na walikuwa wengi. Kichwani natafakari kuwa huyu rafiki yangu atakuwa mtu maarufu sana hapa au huenda atakuwa tajiri sana kiasi cha kuulizia kwenye umati huu wakamfahamu.

Nikasogelea mama mmoja aliyekuwa anauza vitumbua nikaanza kumuuliza "mama nionyeshe nyumbani kwa tuliza koo". Kama mbogo mama yule sijui alikuwa kavurugwa na nini kaanza kunifokea kwa sauti acheni ushamba wenu wa vijijini huko husalimii watu unakuja kuulizia nyumbani kwa watu stendi umeona kuna nyumba za kuishi watu hapa kituoni au kakwambia mimi mkeo hadi nijue kwake". Nikajisikia aibu na kuondoka eneo lile kwa unyonge sana nikasogea mbele kidogo kuna gogo nikakaa nikaanza kutafakari.

Baada ya dakika 5 hivi nikaona dada mmoja ananisogelea akafika kwangu kaniuliza kaka samahani unatokea wapi na ulikuwa unamuulizia nani maana nilisikia mnazozona na yule mama anayeuza vitumbua pale haraka haraka kabla sijajibu swali lake nikajikuta nimemwamkia shikamoo.

Katabasamu kanijibu mimi ni mdogo kwako ilitakiwa ndiyo nianze kukuamkia kaka. Basi baada ya kumweleza, alichoniuliza ni kuwa ukimwona huyo Tuliza koo kwa sura unamfahamu? Nikaitikia ndiyo. Kaniambia nifuate. Kufika mbele kidogo kaniambia simama hapa hapa haitapita dakika 10 hujamuona. Akaondoka zake.

Ndani ya dakika 5 nikiwa makini kutazama kila anayekatiza mbele yangu mara nasikia upande wa pili wa daladala sauti nzito ikijirudia rudia "ndugu abiria kwa sh.50 tuliza koo na maji bariiidi". Mimi nikaendelea kusubiri pale pale kuona kama rafiki yangu atapita. Sikuweza kuunganisha doti kuwa lile jina la rafiki yangu la "Tuliza koo" laweza kuwa na mahusiano na huyo muuza maji. Mara nasikia hiyo sauti inazunguka kutokea upande wa pili wa daladala nilipo.

Lahaula! Kumcheki huyu hapa rafiki yangu John Masalu! A.k.a Tuliza koo alikuwa kachoka, nguo vumbi, kapauka, ndala zimeisha kuliko nilivyokuwa nategemea kumwona akija kijijini akitokea Dar akiwa nadhifu kanyoa Oo suti na tai. Kabla hajaniona nikaanza kujiuliza.

Hivi naota, ni yeye au nimemfananisha kama ni yeye labda kazi aliyokuwa anafanya mwanzo amefukuzwa. Nikaamua kumsogelelea nikamshika bega kabla hajageuka kunitazama vizuri akaanza kuniuliza nikupe ya sh. 50 au 100 kugeka kunitazama anakuta ni mimi rafiki yake kama hakuamini vile tukakumbatiana na kunipeleka kwenye kibanda cha soda kanichukulia soda. Kisha akaniambia kaa hapa nimsubirie hadi saa 12 jioni tugeuze kwake.

Kipindi namsubiria Kichwani nikabakia na maswali hivi elimu ya kidato cha nne rafiki yangu ameshindwa kutafuta kazi nzuri aje kuuza maji ya kupima ya kwenye mifuko? Huko alikopanga analipaje kodi na pakoje? Nikiwa kwenye lindi la mawazo mara nasikia sauti ya John kutoka nyuma yangu akiniita.

Oya oya mwanangu najua umechoka na safari na una njaa twende maskani tukapike huku akiwa kashikilia fungu la mchicha na vinyanya 3. Nikaamka tukapanda daladala kurudi kumbe alikuwa anaishi nje ya mji njiani ananiongelesha kwa bashasha huku akinitajia majina ya maeneo tulipokuwa tunapita nilikuwa namwitikia tu lakini kichwani najiuliza huyu rafiki yangu atakuwa na maisha magumu sana mgeni siku ya kwanza akanipikie mchicha badala ya kununua kuku au nyama au samaki?

Mara nasikia akimwambia konda shusha kituo kinachofuatia. Mara tukashuka . Tukaanza kukatiza kukatiza vichochoro kuingia nyumba zilizokuwa mbalimbali kuna maporimapori kiasi hatimaye tukaingia getoni duu kinyume na matarajio nilichokikuta!

Kanikaribisha ndani. Geto lilikuwa la udongo japo limeezekwa bati, halina umeme, chini hakukuwa na sakafu kulikuwa ni vumbi mlango wa mabati na wa kuegesha, madumu ya maji kibao na deli za barafu mkeka na kigodoro unene wa kigaja cha mkono. Kufika ndani kaniwekea maji ya kuoga narudi ndani nakuta moshi kama wa kukausha tumbaku na magogo ya miti mibichi kumbe anapika ugali na mchicha.

Tukala na kupiga stori kidogo huku ananipa moyo wa kupambana kiume bila kuchagua kazi na tutatoka kimaisha. Tukaingia kulala. Usiku huo pamoja na uchovu wangu wa safari sikusinzia mziki kunguni na viroboto wanapiga sindano za maana.

Ilipofika saa tisa alfajiri kaamka kwenda mabondeni kuchota maji karudi saa 12. Kesho yake kaanza kunionesha mazingira ili nipambane kivyangu. siku iliyofuatia nikaanza mizunguko mwenyewe ila yaliyonikuta acha.

Nikaanza kuzunguka mjini na bahasha ya vyeti vya mgambo kutafuta kazi jijini. Nikaamua kwenda Kariakoo . Sehemu ya kupandia na kushukia ilikuwa shule ya uhuru. Baada ya kuzunguka nikaibukia hadi kule shimoni kisha ikafika muda wa kurudi kutafuta kituo cha daladala si nikapotea nikashindwa kuelewa mashariki wala kusini ni wapi masaa 3 nimezunguka bila mafanikio huku niliondoka rafiki yangu kanitisha na matapeli wa mjini wakijua mimi ni mgeni. Kila nikielekezwa nasogea mbele napotea. Mwisho nikamwona polisi nikamkimbilia nikamweleza ukweli kanisindikiza hadi kituo cha daladala nikageuza geto.

Maisha yakawa magumu kushinda njaa ni kawaida nikaanza kutafuta vibarua vya kulima navyo vikaenda vikaishia nikaanza kusomba maji kuuza mtaani napo kukawa changamoto maana yalipatikana mbali na sikuwa na baiskeli. Wazo likaniijia nianze mradi wa kuuza kuni. Unakata porini unakuja kuwauzia wakaanga mihogo vitumbua na maandazi.

Siku ya kwanza Nikiwa na panga na shoka langu nikaona mti mkubwa mbichi si mbali na geto juu kuna kuni nzuri zimekauka si nikajisemea moyoni nimepata zali kuni nzuri hivi watu hawazioni? Au wanashindwa kupanda juu kuzikata? ewe bwana weee tembea uone mengi ukiona fisi mjini ujue kaletwa. Nilichokutana nacho kwenye huo mti sikuwahi kuwaza!

Kumbe sehemu hiyo aliyokuwa anaishi rafiki yangu ilikuwa wakazi wake wengi ni wazaramo na huo mti nilikuja baadae sana kujua ulikuwa makao makuu yao kufanyia matambiko. Baada ya kufika chini ya huo mti nilikuta chini kuna vyungu vingi vimetupwa huku kukiwa na hela za sarafu nyingi za shilingi 20, 50 na 100 zimetapakaa chini la shina lake kwa harakaharaka zinafika zaidi ya elfu 10 . Kwenye matawi kuna vitambaa vyeusi na vyekundu vimefungwa vinaning'inia. Huku nilikotokea sikuwahi kukutana vitu vya namna hiyo. Lakini roho ikawa inasita nikabaki kujiuliza maswali mengi kabla sijafikia maamuzi.

Je, kwa nini mti huu watu hawakati kuni licha ya kuwa jirani na makazi? Je fedha hizi za sarafu nyingi hivi na vyungu nani anakuja kutupa huku na kwa ajili ya nini? Je baadae waliotupa watazifuata? Je ina maana hakuna mtu aliyewahi kuziona na kuzichukua? Je hivyo vitambaa wamefunga watoto wakicheza au?.

Mwisho wa tafakuri wangu nikaja na jibu kuwa vile vitu na ule mti havikufika pale kwa bahati mbaya. Nikaweka shoka begani na panga mkononi na kuanza kurudi geto. Ombea vyote ila Usiombe njaa. Nikaanza kujiuliza Usiku uliopita nililalia mihogo miwili, asubuhi sijala kitu na sasa ni saa tisa, njaa inauma kweli kweli mfukoni sina hela na sijui nitakulala nini usiku . Nikaanza kujiuliza siku zote namwomba Mungu Kunipa riziki, je hii si miujiza kuniletea hela? Kichwani kikajiambia narudi kuzichukua liwalo na liwe..

Baada ya kufika kwenye ule mti nikatamka " kwa jina la Yesu kama hela hizi ni za mashetani yashindwe lakini kama kaniletea Mwenyezi Mungu mapenzi yake yatimizwe. Pamoja na kutamka hayo maneno ila wakati nataka kuinama kuanza kuzichukua nikawa na kawasiwasi. Nadhani nilikuwa na imani haba. Nikajiuliza siwezi kuinama kuchukua hela hizi nikapigwa makofi na mizimu yake au nikaganda nisiondoke? Nikapata wazo nisiwe na papara zile hela nichukue kidogo, kama elfu moja za kwenda kula siku moja na nikifanikiwa kesho yake nirudie zilizofuata.

Swali likaja nazichukuaje? Nitumie mkono au? wazo likaniijia nizikusanye kwa panga na kisha nizichote kwa panga kwa umakini kisha nitembee nazo hivyohivyo nikiona watu mbele yangu ndiyo nizihamishie mfukoni. Kweli nikafanya hivyo nilipokaribia watu nikajua lolote litakalonikuta watakuwa wameniona na kunisaidia. Hivyo nikaziingiza mfukoni. Nikatembea hadi kwa mkaanga chips nikaagiza na kula na kurudi geto.

Aliporudi rafiki yangu akaniuliza kama nilipata riziki ya kupata hela siku hiyo ya kula, nikasema ndio ila sikumwambia kuhusu hilo chimbo baada ya kuingia tamaa kuwa huenda nikimsimulia anaweza kusema twende tuchukue tukagawane. Heee usiku si tumbo lianze kuuma nikaanza kuharisha nikaingia wasiwasi huku rafiki yangu akiniuliza umekula nini leo?

Nilimweleza kuwa nimekula chips akaniondoa wasiwasi kuwa itakuwa ni mafuta ya chips watakuwa wameyatumia kwa muda mrefu hivyo yametengeneza sumu hivyo nikiharisha yakaisha tumboni nitakuwa sawa. Kweli baada ya kuharisha kama safari 4 tumbo likakaa sawa. Baada ya tumbo kutulia usiku uliyobaki nilikuwa nawaza tu kama kutakucha salama na zile hela zilizobaki nitazikuta? Ilipofika saa mbili nikabeba shoka langu, panga na mfuko wa rambo nikaelekea kwenye ule mti.

Nilikusanya zile hela zote nikatia kwenye mfuko wa rambo. Nilikagua kila mahali chini ya ule mti maana nyingine kumbe zilifunikwa na majani, nyingine zilikuwa zimeshika kutu. Nilipata mzigo wa maana. Nikafika geto nikaziosha zile zenye tetenasi. Kisha nikaenda kwa muuza chips mara hii nikaagiza chips mayai maarufu kipindi hicho (chips zege) na Fanta yangu baridi nikarudi geto kusinzia. Nyingine zikaendelea kunisaidia kwa matumizi ya takribani mwezi mzima.

Ule mti uliendelea kunifaa sana takribani kwa miaka mitano na sikutamani kuhama pale geto hata pale rafiki yangu alitoa pendekezo la kubadili maeneo ya kuishi nilimwambia tuishi pale pale. Ilinifikia kipindi nikienda kwenye mihangaiko yangu nikikosa riziki narudi kwenye ule mti, kuangaza angaza nakuta wazaramo wamedondosha mia mia zao nakusanya naenda kula mihogo ya kukaanga kipindi hicho Dar wakiziita chips dume namshkru Mungu nalala. Nilihama eneo lile baada ya kupata kazi mjini.

Watu wanapitia changamoto na shida nyingi sana kwenye utafutaji hadi kufanikia mafanikio nikiangalia nilipofikia kimaisha na nilipotoka huwa namshukuru Mungu sana. Tusikate tamaa katika utafutaji . Nimejaribu kufupisha simulizi hii ya kweli ya maisha yangu japo nilipofika Dar nilipitia changamoto nyingi sana kipindi cha utafutaji.
 
dahh pole sana dogo.Mungu mwema sana kuna wakati Mungu anakupitisha ili ujifunze kitu.Kilicho nisikitisha kwenye hadidhi yako ni kuiba ngombe ya mzee wako.
 
dahh pole sana dogo.Mungu mwema sana kuna wakati Mungu anakupitisha ili ujifunze kitu.Kilicho nisikitisha kwenye hadidhi yako ni kuiba ngombe ya mzee wako.
Sikuwa na namna za kutimiza ndoto zangu mkuu. Baada ya kufanikiwa nilimnunulia mzee ng'ombe 4 kumlipa ile ng'ombe yake na nikamjengea na kibanda cha kuweka mbavu akanipa baraka zake
 
Hapo unampa dogo 1000 ya biscuits ni chai
1996 Kuna mtu alinunua shamba sh 600

Au Stori yako iwe 2010 nakuendelea
 
Sikuwa na namna za kutimiza ndoto zangu mkuu. Baada ya kufanikiwa nilimnunulia mzee ng'ombe 4 kumlipa ile ng'ombe yake na nikamjengea na kibanda cha kuweka mbavu akanipa baraka zake
Ulimwambia kama umemuibia ng'ombe? Na yule rafiki ya mzee wako ulipotelekeza ng'ombe waliushia kusemaje?
 
Back
Top Bottom