Ingelikuwaje Nyerere angelikuwa Mzanzibari?

Gavana

JF-Expert Member
Jul 19, 2008
33,232
8,781
by zanzibar daima, posted in kalamu ya ghassani


TANZANIA tuliyonayo sasa ni kati ya ishara ioneshayo kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliishi juu ya ardhi hii ya Mungu Muumba. Hatuwezi kuizungumzia Tanzania – chimbuko, asili, mafanikio na matatizo yake – bila ya kumtaja na kumuhusisha yeye.

Hatuna haja ya kujenga sanamu lake kumkumbuka na kumuenzi, madhali tu Tanzania ingalipo na inaendelea kubakia hai. Tanzania ni sanamu la Nyerere linalotosha kuyaakisi maisha, mawazo, khulka na uongozi wake. Kupasi kwa Tanzania ni kupasi kwake na kufeli kwa Tanzania ni kufeli kwake.

Hivi sasa tunaingia katika kipindi cha maombolezo ya kifo chake. Namna tunavyoomboleza katika kipindi hiki, kunatokana na vile tulivyomchukulia katika maisha yetu. Kuna waliomchukulia kuwa ni kiumbe kitukufu chenye thamani kubwa mno kiasi ya kwamba wangelitamani aishi hadi baragumu la Kiama lipulizwe. Kwao, huyu alikuwa rafiki, mpenzi, mkombozi na mwalimu. Alikuwa malaika!

Lakini pia kuna waliomchukulia kuwa ni kiumbe kikorofi na hivyo kufa kwake ndicho kitu chema pekee alichowafanyia. Kwao, Nyerere alikuwa mchoyo, adui, mkaidi. Alikaribiana na Subiani!

Na bado kwa wengine, kuwepo na kutokuwepo kwa Nyerere hakukumaanisha chochote katika maisha yao. Hawakujuwa khabari zake, wala naye hakujuwa zao. Hawakuhisi kuwepo kwake wala sasa hawahisi kuondoka kwake. Alikuwa kile wanachokiita Waingereza “non entity!”

Ndiyo, hatuwezi kuwa sote na wazo au hisia moja juu ya kitu au mtu fulani. Wala tusiwalazimishe watu wote walione jambo kama tunavyoliona sisi, maana hivyo sivyo akili za wanaadamu zinavyofanya kazi. Nyerere hakuchukiwa na watu wote, lakini pia hakupendwa na kila mtu. Nyerere alikuwa maarufu lakini si kwamba alijuilikana na kila mtu!

Kwa Wazanzibari, hata hivyo, Nyerere hakuwa non entity, bali mtu aliyeishi na aliyemaanisha kitu katika maisha yao. Alichokimaanisha chaweza kuwa chema au kibaya kulingana na ufahamu wa mtu na mtu. Na ni kwa sababu hiyo, kwamba Nyerere alikuwa na nafasi katika maisha ya Zanzibar, Wazanzibari na Uzanzibari, ndiyo maana ninaandika makala hii kuomboleza kifo chake kilichotokea miaka minne iliyopita.

Najaribu kugeuka nyuma kuziangalia siku zilivyopita katika uhai wa Mwalimu Nyerere. Umri na uwezo wangu ni mdogo mno kuweza kuziona zote, lakini hizi chache nizionano zatosha kunipa picha.

Kwamba zake hazikuwa siku za kawaida kama za Mohammed Ghassani, bali za mtu aliyekuwa mtawala mwenye ushawishi mkubwa katika mwenendo wa siasa za nchi hii, Afrika na dunia nzima kwa jumla. Nyerere alikuwa na jina na satwa kubwa!

Mimi ni Mzanzibari. Nyerere hakuwa Mzanzibari (na sijuwi hata kama alitamani kuwa angalau kwa siku moja tu kati ya siku hizo zote alizoishi), lakini kwa udadisi wa kitoto najiuliza: hivi ingelikuwaje kama naye angelikuwa Mzanzibari? Ingelikuwaje kama angelikuwa ndiye Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar? Je, angelifikia pahala pa kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kwanza hata huu Muungano wenyewe ungelikuwepo? Na kama ungelikuwepo, nafasi ya Zanzibar ingelikuwa ni ipi kwawo?

Nasema pengine huu ni udadisi wa kitoto tu (na mutanisamehe kwa utoto wangu), lakini katika wakati huu wa kuomboleza kifo cha mtu aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuifikisha Zanzibar hapa ilipofika, neno hili ‘ingelikuwa’ ndiyo ruwaza pekee ya kujipumbaza. Na kujipumbaza ndiko kulikobakia!

Jibu la mwazo ninalolipata kwa maswali hayo ni kwamba, kama Mwalimu Nyerere angelikuwa Mzanzibari, basi Muungano huu usingelikuwepo. Kama ungelikuwepo, basi yeye ndiye ambaye angelikuwa Rais wake. Na baada ya hapo, hata siku moja nchi yangu ya Zanzibar isingelifikia pahala hapa ilipo sasa, pa manung’uniko ya mkubwa kummeza mdogo.

Nitafafanua. Kwanza, sina hakika ikiwa Mwalimu Nyerere (hapana shaka angelikuwa akiitwa Maalim Nyerere) angelimkubalia mwenzake wa Tanganyika (angelikuwa Mzee Abeid Amani Karume) kuziunganisha nchi zao. Anavyoonekana, kupitia fikra na maandishi yake, ni kwamba aliuthamini sana uhuru wa nchi yake na alikuwa anaishuku kila hatua ambayo aliidhani kuwa inatishia mamlaka na madaraka yake. Kwa mfano, pamoja na sababu milioni zinazoweza kutolewa za kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, ya kuchelea nafasi na nguvu ya Tanzania katika eneo hili ni moja wao.

Kwa hivyo, hata kama Kijizanzibari chake kingelikuwa ni kidogo hivi, lakini Maalim alikuwa ni mtu aliyeujali na kuuhisi uhuru. Haielekei kwamba angeliipeleka Zanzibar sentimita moja mbele kuelekea kusiko uhuru. Ni kweli kwamba alikuwa akizungumzia umoja wa Bara la Afrika na pia akizungumza dhidi ya ‘vidola vidogo vidogo’, lakini palipohusika uhuru aujuwao yeye, alikuwa na pua kali ya kunusa harufu ya kutawaliwa. Ikijitokeza dalili tu, huigundua na mapema na akajiepusha nayo.

Si tunakumbuka alivyounga mkono jitihada za jimbo la Biafra kujitenga na Nigeria mwaka 1967? Wakati huo ilikuwa ni miaka mitatu tu tokea Zanzibar iwe sehemu ya Tanzania, ilhali Biafra ilishakuwa sehemu ya Nigeria kwa miaka na kaka. Lakini kilichomfanya aunge mkono kujimegua kwake yalikuwa madai ya uhuru zaidi. Uhuru!

Kwa hivyo, ni wazi kuwa kama angelikuwa ni yeye ndiye kiongozi wa kidola hiki kidogo cha Zanzibar, asingelikubaliana kamwe kuungana na jidola lile kubwa la Tanganyika. Angelikhofia uhuru wake – angelikhofia kutawaliwa tena kwa mlango wa nyuma.

Kuna wakati aliwahi kuzungumzia The Second Scramble, kinyang’anyiro cha pili. Ilikuwa ni katika hadhara na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam ambapo alieleza khofu yake kwa mwenendo wa siasa za kilimwengu. Kwamba namna unavyokwenda, basi Afrika ilikuwa imo katika hatari ya kunyang’anyiwa tena kwa mara ya pili na mataifa makubwa.

Kinyang’anyiro cha kwanza kilichomalizika kwa Mkutano wa Berlin wa 1884-5, kiliyawezesha mataifa hayo kugawana Afrika kwa mafungu kama nyanya sokoni. Kukawa na fungu la Afrika ya Kiingereza, ya Kifaransa na ya Kijerumani. Basi kama Maalim Nyerere angelikuwa ndiye Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wa wakati ule, kisha mwenzake wa Tanganyika akamjia na wazo la kuziunganisha nchi zao, angelitoa hotuba kali kwa wasomi wa Zanzibar na kisha akatunga kitabu chini ya jina la The Second Colonization, kuonesha wasiwasi na khofu zake juu ya kile ambacho kingelikikumba kijinchi chake kidogo mbele ya jinchi lile kubwa.

Lakini hebu tuache hiyo. Natuseme kuwa kwa wakati ule Maalim Nyerere wa Zanzibar angelikuwa hana hiari illa kuingia katika Muungano na Tanganyika. Kwamba, kwa upande mmoja, siasa za ndani zilimlazimisha apate kipenu cha kujibanza ili kuyanusuru madaraka na ushawishi wake na, kwa upande mwengine, matakwa ya mataifa makubwa yalimtaka afanye hivyo.

Bila ya shaka, pande zote mbili zingelimtanza Maalim Nyerere. Anajuilikana kwamba licha ya ujasiri wake, huyu alikuwa ni kiongozi aliyekhofu sana kupoteza madaraka na ushawishi wake. Alikuwa pia akiuhusudu sana uungwaji mkono kutoka mataifa makubwa. Kwa tabia zake hizo, kuna baadhi ya wakati alijikuta akifanya maamuzi yaliyomgharimu hata hishima na kauli yake, alimradi tu yambakishie vitu hivyo mikononi mwake.

Mfano mmoja ni pale alipoiomba Uingereza iingilie kati kile kilichodhaniwa kuwa ni mapinduzi ya kijeshi dhidi yake, siku chache tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964. Kwa tafsiri alizokuwa amezijenga ni kwamba Uingereza lilikuwa ni taifa la kikoloni na la kibeberu, kwa hivyo ilikuwa aibu kwa nchi huru kuomba msaada wa mkoloni na beberu hata miaka mitano bado tokea beberu huyo aondoshwe kwa fedheha ya kutokutakiwa nchiningwa! Lakini wakati huo alikuwa anatetea madaraka yake. Ubeberu na ukoloni wa Muingererza ni kitu kimoja na madaraka ya Maalim Nyerere ni kitu chengine. Panapohusika maslahi, haikuwa vibaya kwa beberu kumnusuru ‘mzalendo’ huyu!

Basi hapa napo, pamoja na sababu nyengine, angelijikuta akikabiliana na hoja na haja ya kuendeleza madaraka na ushawishi wake ndani ya nchi na wakati huo huo nia ya kuvuna sifa za mataifa makubwa. Hivyo, kwa hakika, ndivyo vitu vilivyouumba Muungano huu. Marekani na Uingereza zilizitumia khofu za akina Karume na Nyerere juu ya kukuwa kwa ushawishi wa akina Abdirahman Babu ili wapate muradi wao wa kupambana na Ukomunisti.

Kwa hivyo, licha ya ujanja na akili zake, Maalim Nyerere wa Zanzibar angelijikuta ameshasukumwa ukutani na hana uamuzi illa kutenda kwa mujibu wa mwenendo wa matukio. Angelijikuta yu mtumwa wa mazingira. Kuwa mtumwa wa mazingira na kuburuzwa na mtiririko wa matukio, bila ya shaka, lilingelikuwa tusi kubwa kwa mwanafunzi huyu wa Falsafa wa Edinburgh, shabiki mkubwa wa mawazo ya Socrates na Plato.

Lakini angelijikaza kiume kumkata jongoo kwa meno na baada yake wala asingelionekana kujuta. Kwamba hiyo ndiyo iliyokuwa khulka yake – kutokujutia makosa yake. Siku zote, hata kama nafsini mwake alijuwa kabisa kuwa ameshateleza, hakutaka waliomzunguka waujuwe udhaifu huo. Badala yake, alijitahidi kuonesha kuwa yeye alikuwa sahihi na sisi wengine tuliomzunguka ndio tuliokosea kulitafsiri tendo au neno lake. Mfano mmoja wapo ni njozi yake iliyopotea katika Azimio la Arusha!

Basi, katika hali kama hiyo, hata kama angelikuwa Mzanzibari, Maalim Nyerere angelijiingiza katika Muungano huu. Lakini mara tu baada ya kuingia, angelichukuwa hatua za haraka na za makusudi kujihakikishia kuwa hapotezi zaidi ya alivyokwishapoteza. Kitu cha mwanzo ambacho angelikipinga kwa nguvu zake zote ni kuyatoa sadaka madaraka yake yote mikononi mwa mwenzake wa Tanganyika. Na hapa hata hainipitikii kama angelikubaliana na wazo la muungano wenye muundo wa serikali mbili. Thubutu!

Si unajuwa usomi wake? Angelisimama akaichambuwa mifumo yote ya miungano ulimwenguni na kisha akaonesha, kwa data kabisa, kwamba hakuna muungano wa aina hiyo. Angelisema aidha muungano huwa wa serikali moja (unitary) au wa shirikisho (federal). Au ikibidi kuwapo na uhusiano mwengine ni kama ule wa Uingereza na Ireland ya Kaskazini, ambao, kwa hakika, ni uhusiano baina ya mkoloni (Uingereza) na koloni lake (Ireland). Hapo angelimtaka Karume achaguwe moja.

Na hata baada ya kukubaliana kuwa uwe huo wa serikali mbili, naamini kuwa sasa angelipendekeza na kushinikiza kuwa yeye ndiye awe Rais wa Muungano huo. Si tunamjuwa alivyokuwa mwepesi wa kutafuta huruma, kujenga hoja na kulazimisha jawabu? Angelihutubia kwa masaa matatu, bila kumeza mate, akionesha kwa vipi ni muhimu na ni lazima kwa hiki kijidola chake kidogo kupewa madaraka ya kutosha katika muungano. Angelisema kuwa kufanya hivyo kungelikuwa ni kuonesha nia njema, kwamba hakuna dhamira yoyote ya kuimeza na kuifuta kabisa Zanzibar katika ramani ya ulimwengu.

Angeliteta na kulitetea wazo la mkubwa kuonesha mapenzi na huruma kwa mdogo ili kumfanya mdogo aamini kuwa maisha yake hayako hatarini. Angelifanya hivi kwa nguvu na sauti zake zote hadi waliopo wote wakaingia maji, wakalainika.

Wakampa akitakacho. Si tunakumbuka alivyokuwa na uwezo wa kulazimisha jawabu katika mikutano yake huku akizungumza kwa kila aina ya sauti – mara gonda, mara kisauti chembamba, mara ya kawaida, mara ya kunong’oneza – kulingana na hadhira imsikilizayo na, au, uzito wa ujumbe alioupeleka kwao?

Baada ya kufanikiwa kupata akitakacho kutoka kwa mwenzake Karume, sasa Maalim Nyerere angelikwenda mbele zaidi kuitawalisha Zanzibar juu ya Tanganyika. Kwa mfano, ili kuonesha kuwapokuwapo na utukufutukufu wa Zanzibar ndani ya muungano huo, angeliita nchi hii Zantania: Zanzibar kwanza, Tanganyika baadaye.

Kisha wizara zote ambazo zingelikubaliwa kuwa za Muungano na muhimu, kama Fedha, Ulinzi na Usalama, Mambo ya Ndani na ya Nje, zingelikuwa na makao yake makuu Zanzibar na angelihakikisha kuwa zinaongozwa na Wazanzibari tu (au kwa mbali wale ambao angeliwaita Zanzibari-oriented, yaani waliotayarishwa kuitumikia Zanzibar). Hata mabalozi wanaoiwakilisha Zantania, wangelikuwa ni wastani wa 20:1, yaani kila Wazanzibari 20 kwa Mtanganyika 1.

Vipi kuhusu bendera kama utambulisho wa Taifa moja huru na lililoungana? Nadhani bendera ambayo ingelitumika aidha ingelikuwa ile ya baada ya uhuru iliyokuwa na karafuu katikati. Sasa ingeliongezwa na nazi, vipande vya dhahabu na madini ya Tanzanite (yangeliitwa Zantanite). Au, labda, ingelikuwa ile ya ASP. Kwani kungelikuwa na ubaya gani, na hii ni bendera tu.

Wimbo wa taifa, je? Kuna kasida maarufu inayoitwa ‘Talaal Badru ‘alayna ambayo kihistoria inaaminika kuwa ilisomwa kwa mara ya mwanzo na wanawake na watoto wa Madina wakati walipokuwa wakimkaribisha Mtume Muhammad (SAW) katika mji wao baada ya kuwa amehama kwao Makka. Kutokana na historia yake hiyo kufungamana na ukweli kwamba zaidi ya asilimia tisiini na nane ya Wazanzibari ni Waislam, basi Maalim Nyerere angelipendekeza kuwa huo ndio uwe wimbo wa taifa. Ambaye angelimuita mdini, shauri yake!

Basi hapo akina Abeid Karume na Thabit Kombo, ambao wangelikuwa wametoka Mrima, wasingelikuwa na jinsi illa kukiwachia Kijizanzibari kiduchu kuwa na madaraka makubwa na Jitanganyika lao kubwa likawa limetiwa shemere. Wao wangelibakia kulalamikia ofisi ndogo tu, Lumumba: “Kambarage anajifanya mjanja!”.

Kuanzia hapo maagizo yote ya kuiendesha Tanganyika kiuchumi, kisiasa na kijamii yangelifanyika pale Kisiwandui. Wao wangelikwenda Chimwaga kuyapigia kofi na kuyapitisha tu. Kila siku wangelibakia kuazimia tu: “mara hii tukikutana, tutamueleza kuwa anavyofanya sivyo”. Lakini siku hiyo kamwe isingelifikapo!

Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kiakili, nia yake ya kutokupoteza na ujasiri wake wa kuwavuna watu, Maalim Nyerere angelifahamishwa na watu wake hali ilivyo kwa wenzetu wa Mrima. Kwamba kuna watu ndani na nje ya serikali ambao hawapendezewi na jinsi alivyojikusanyia madaraka yote mikononi mwake. Watu hao walikuwa wamefikia pahala pa kuapa kuwa hawatostahmili tena kuiona nchi, iliyopigania uhuru wake kwa kucha na meno na hata ikafika kufanya mapinduzi, kwamba imetiwa shemere na nchi nyengine.

Kwa kuwa angelilijuwa hilo, basi Maalim Nyerere angelifanya jitihada za kiakili na za kinguvu kuhakikisha kuwa ufalme za Zanzibar unaendelea kuwapo na kulindwa kwa gharama yoyote ile. Kwa mfano, ghafla moja angelilivunja Baraza la Mawaziri na wakati wa kuliunda tena, angeliwachukuwa wale wote ambao angeliwaona kuwa ni hatari kwa ufalme wa Zanzibar na kuwapa nafasi zitakazohakikisha kuwa hawakai tena Tanganyika milele.

Wakati huo huo, kwa kuwa ulinzi na usalama ni miongoni mwa vipengele vya Muungano, basi angelitumia mwanya huo kupeleka vikosi vyetu ya jeshi katika ardhi yote ya Tanganyika. Angelihakikisha kuwa kila mkoa mmoja wa Tanganyika una kambi mbili za jeshi, ambazo zinaongozwa na kusimamiwa moja kwa moja kutoka Zanzibar. Lengo lingelikuwa ni kuwatisha wale Watanganyika waliobakia kuwa wasithubutu kuleta fyokonyoko zao dhidi ya Muungano.

Hili kijuujuu lingeliitwa kuwa ni jeshi la watu wa Zantania, lakini hasa lingelikuwa ni jeshi la watu wa Zanzibar, ambalo jukumu lake kubwa ni kuhakikisha kuwa ufalme wa Zanzibar unaendelea kutukuka na kutanuka. Lisingelikuwa na kamanda wala meja wa Kimrima. Tungelikuwamo akina yakhe watupu. Hapana shaka, kutokana na uchache wetu, basi ingelibidi sote tuwe majeshi, au hata kwa kupokezana baina ya wafanyakazi wa serikali na majeshi. Kwamba leo unakuwa kambini na kesho unarudi ofisini.

Unajuwa kuna watu wengine wababe. Hata baada ya kukubaliana kuwa Zanzibar ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kwa maswala yote ya nchi yakiwemo yale ya Mrima, kungeliweza kutokezea viongozi wengine wa Tanganyika ambao hawalikubali hilo. Kwa mfano, angelitokezea kiongozi wa Mrima kuiunga nchi yake na Jumuiya ya Misaada ya Vatican (VAT-AID?). Basi huyo angelikiona kilichomnyoa kanga manyoya.

Maalim Nyerere wa Zanzibar angelimuambia akome kuiendesha nchi kama milki yake, kwamba asiuchezee Muungano. Kwamba Muungano ni mkubwa kuliko yeye. Na haraka angelitakiwa ajitowe katika jumuiya hiyo. Kamwe Maalim Nyerere asingelizingatia kuwa kujiunga huko kungelisaida kuikwamua nchi kutokana na matatizo ya kiuchumi, ambayo yeye (Maalim) ni sehemu ya matatizo hayo. Angelizingatia tu kuwa tendo hilo linahatarihsa Muungano na, hivyo, ufalme wake na utukufu wa Zanzibar. Itakuwaje bwana watu wakiuke katiba!

Na wababe wengine kutoka Zanzibar kwenyewe wanaojidai kutaka serikali tatu, wangelimjuwa kuwa yeye ni nani. Hata kama angelikuwa amekwishang’atuka, basi angelifunga safari kutoka nyumbani kwake, Michamvi Kaye, na kuja moja kwa moja hadi Kikwajuni, pale Baraza la Wawakilishi. Angeliwashikisha adabu viongozi hao na kuwaambia kama hawakubaliani na Muungano huu, basi bora wahame chama na waunde chama chao. Maana sera ya chama kilichopo madarakani, na ambacho wao ni wanachama wake ni serikali mbili.

Angeliwashambulia kwamba wao ni mahasidi wa Muungano, kwamba wanapandikiza chembe chembe za ubaguzi na kwamba kilichowasukuma ni uchoyo wao kwa wenzao wa Mrima. Kwa hakika, Maalim Nyerere angelikaribia kutokwa na machozi, kama si kulia kabisa. Mwisho angelimalizia kwa kuwalaani kwamba kama wangelivunja Muungano huu au kama wangeliunda serikali yao ya Zanzibar, basi yeye akifa asije akazikwa katika ardhi ya Zantania. Akitoka hapo, angelikwenda kuandika kitabu chake Uongozi wetu na Khatima ya Zantania, ambapo angelianza kwa beti za kuililia Zantania ambayo aliipenda na kuichukulia kama mwanawe mzazi. Angeliomboleza kuwa sasa mwanawe huyu, watu walikuwa wanataka kumtoa roho!

Na, je, vipi kuhusu mafuta ya Zanzibar? Ama haya nina hakika kabisa kuwa yasingepata kamwe kuwa jambo la Muungano. Tungelikuwa tunachuma karafuu zetu wenyewe na tunachimba mafuta yetu wenyewe. Na kama kuna mtu kutoka Mrima ambaye angelibisha hilo na kujidai ati “mbona almasi na dhahabu ni za Muungano, kwa nini mafuta yasiwe?”, basi Maalim Nyerere wa Zanzibar angelimtosha kwa jawabu.

Angeliitisha mkutano wa waandishi wa habari kule kwenye nyumba yake ya mapumziko, Mazizini, na kuwaambia maneno mazito:

“Nawatumeni mukawaambie hao wanaohoji kuchimba mafuta yetu. Kwamba Mungu aliyoiumba ni Zanzibar akawapa Wazanzibari. Akaumba na Tangayika akawapa Watanganyika. Ni sisi, mimi na mwenzangu Abeid, ndio ambao kwa matashi, haja na mahitaji yetu na watu hawa nchi hizi, tukaiumba hii Zantania na kuwapa. Kuanza hapo ndio watu hawa wakawa ni Wazantania. Kabla ya hapo hapakuwa na Zantania. Mafuta yetu yalikuwepo na kugunduliwa kabla ya Zantania kuwepo, lazima walijuwe hilo. Yalikuwa yetu na yataendelea kuwa yetu leo na hata milele. Ikiwa wameshachoka na yale makubaliano yaliyoiumba Zantania, wanaweza kusema, maana hili si zao la fikra za Kiungu, kwamba hazitenguki. Ni zao la fikra za kibinaadamu tu, zangu mimi na Abeid. Sasa waamue moja, ama warudi kwa kile alichowapa Mungu au waendelee na hiki tulichowaumbia sisi. Lakini sio kuingia katika eneo letu la udhibiti, umiliki na urithi”.

Salamu zingelifika na hao waliodai wangeliubana kimya. Si hasha kesho yake, ndio hao hao ambao wangeliandamana kulisifu jibu hilo hilo la Al-Hakir Maalim Julius Kambarage Nyerere!
 
Umeandika vizuri,ingawa ukweli unaouma ni kuwa kwa namna yeyote ile Nyerere asingekuwa mzanzibari vinasaba vyake vinaonyesha hivyo.
 
Back
Top Bottom