figganigga
Platinum Member
- Oct 17, 2010
- 27,624
- 62,458
Wakati vyama vya siasa vikiendelea kupiga jaramba kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na halipo kwa ajili kukikumbatia chama chochote cha siasa.
Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE juzi, alisema tafsiri iliyoanza kujengwa na baadhi ya wanasiasa kwamba jeshi lipo kwa ajili ya kukikumbatia chama tawala siyo sahihi.
"Polisi akifanya vizuri atahojiwa tu asipofanya vizuri atalalamikiwa tu, kimsingi sisi tupo kwa ajili ya kuhakikisha amani inakuwepo, Jeshi la polisi halipo kwa ajili ya kudhibiti vyama vya upinzani," alisema.
IGP Mangu alisema Jeshi la polisi halipo kwa ajili kudhibiti wapinzani kwa kuwa mikoani vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya mikutano mingi kuliko Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini havidhibitiwi vinapofuata taratibu na sheria zilizopo.
"Huko kwingine ambako wapinzani wanafanya shughuli za kisiasa hakuna polisi kiasi kwamba hawawadhibiti tuje tuwadhibiti hapa Dar es Salaam, siyo hoja ya msingi yaani tukio moja la kuzuia maandamano ya CUF ndilo linachukuliwa tunadhibiti wapinzani," alihoji na kuongeza kuwa: "Nenda katika kila mkoa uliza mikutano ya kisiasa iliyofanyika kwa mfano mwaka uliopita baina ya vyama vya upinzani na chama tawala utakuta wapinzani wanafanya mikutano mingi sana kuliko CCM.
IGP Mangu alisema kama kungekuwa na huo udhibiti wapinzani wasingeweza kufanya mikutano mingi na kwamba mikutano ya chama tawala imekuwa ikizuwiliwa lakini hilo halisemwi.
Kuhusu madai kwamba Jeshi la Polisi linatumia nguvu kubwa kudhibiti wapinzani, alisema tafsiri ya nguvu kubwa ni pana na inategemea anayezungumza ana maana gani.
"Tunaangalia uhalali wa jambo, kama tunaona jambo linaweza kuleta athari za kiusalama tunazuia kwani yakitokea ya kutokea tutakuja kuulizwa tulikuwa wapi hadi yakatokea," alisema.
Kwa muda mrefu sasa vyama vya upinzani vimekuwa vikilitupia lawama Jeshi la Polisi kwamba linatumika na chama tawala kudhoofisha nguvu ya vyama hivyo.
Chanzo:Nipashe