Halisi
JF-Expert Member
- Jan 16, 2007
- 2,802
- 617
Maoni ya Mhariri wa RAIA MWEMA
Igeni ya Lukuvi kumaliza ufisadi
Juni 23, 2010
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi hivi karibuni alifanya kitu ambacho viongozi wengi wa nchi hii hupata kigugumizi kukitenda.
Baada ya kujiridhisha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa tendo la jinai kutendeka, Lukuvi alichukua hatua za kufaa katika juhudi zake za kusafisha kile ambacho jamii kwa muda mrefu imekuwa ikikipigia kelele kwamba kuna mchezo mchafu unaochezwa katika ofisi za ardhi nchini.
Matokeo ya hatua yake ni kufikishwa mahakamani kwa Ofisa wa Ardhi wa Wilaya ya Kinondoni mkoani mwake ili sheria ichukue mkondo wake.
Lukuvi ameivunja ile dhana potofu kwamba hatuwezi kuchukua hatua bila kufuata taratibu za uajiri na tukiwabana sana wanatuambia tukimchukulia mtu hatua halafu akifungua kesi mahakamani tukishindwa serikali itapata hasara.
Hakika ni dhana hiyo inayowafanya watendaji wengi serikalini kuwa na viburi vya ajabu wakiendelea kufanya madudu ambayo si tu yanawaumiza wananchi, bali pia yanaleta hasara kubwa kwa fedha za walipa kodi.
Mifano ipo mingi mno. Bila shaka wasomaji wa gazeti hili watatuunga mkono kwamba ni dhana hiyo potofu ndiyo inayowapa jeuri watumishi wa serikali wanaoshirikiana na watu wengine kufanya madudu Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Imefikia mahali mtendaji wa serikali anakua na jeuri hata ya kumsingizia mkuu wa nchi na kuwadharau hata Waziri, Katibu Mkuu wake na Bodi ya Wakurugenzi lakini hakuna anayethubutu hata kumkemea hadharani, achilia mbali kuchukua hatua kutokana na kuisababishia serikali hasara.
Ufisadi katika nchi hii ulianza taratibu na kadri siku zinayokwenda ndivyo unavyozidi na unaingia hadi kuathibiri mifumo ya kisiasa. Pamoja na mamlaka husika kuonekana kutochukua hatua zozote tunadhani kwamba kelele tunazopiga kurekebisha hali isiyoridhisha hatimaye itazaa matunda.
Sisi Raia Mwema tunasema kwamba tutaendelea na juhudi zetu licha ya baadhi ya watu kutaka kutukatisha tamaa kwa maneno kwamba tutalainika au tayari tumeshalainika. Kwetu ni aluta kontinua kuifanya Tanzania iwe sehemu salama kwa kila Mtanzania.
Kwa vile tunaamini ya kuwa nchi hii inafuata utawala wa sheria, ipo siku moja kelele hizi tunazozipiga zitamnyima usingizi mwenye nyumba na hatua za kufaa zitachukuliwa kama ambavyo Lukuvi amefanya katika juhudi zake za kurekebisha kasoro zinazipigiwa kelele katika sekta ya ardhi.
Igeni ya Lukuvi kumaliza ufisadi