KAPTENI AKISEMA INA MAANA GANI HASA?
Baada ya Capt. John Charles Tesha kutoa sauti ya video yenye maneno mazito mitandaoni, hali ya taharuki imetanda jijini Dar es Salaam huku watu wakiuliza kulikoni. Wakati watu wengine wakihangaika kutaka kujua, Capt. Tesha ni nani hasa, sisi tunaona ni vizuri tukakielezea cheo cha Captain. Yeye mwenyewe alijitambulisha kama Capt. Tesha, lakini baadaye, mitandaoni watu wanamtaja kwa jina la Capt. John Charles Tesha.
Captain kama cheo cha kijeshi, kinamaanisha afisa wa jeshi aliye chini ya Meja (Major) lakini juu ya Luteni (Lieutenant). Kwa ujumla, Captain ndiye anayeelezwa kuwa ni "great soldier, strategist and experienced commandor' yaani askari mwenye mikakati na mwenye uzoefu wa kupigana.
Katika mfumo wa majeshi ya nchi za magharibi kama Marekani na Uingereza, Captain ni afisa mwenye uwezo wa kuongoza kikosi cha askari wapiganaji kuanzia 60 hadi 200 kulingana na mazingira. Kwa hiyo, Capt. Tesha anaweza pia kuwa na kikosi cha watu wasiozidi 200 chini yake na ambao wanaweza kupokea amri yake moja kwa moja bila kuhoji na kutilia shaka na kisha kuitekeleza.
Katika nchi zilizotawaliwa na Ufaransa, hasa za Afrika Magharibi, mapinduzi mengi ya kijeshi yaliyongozwa au yanaongozwa na askari walio na cheo cha Captain. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kiuhalisia, Captain ndiye askari ambaye anaweza kuongoza watu wengi zaidi. Maafisa wengine, huongoza vikosi ambavyo ndani yake kuna watu wenye vyeo wa Captain na hivyo, ili afisa wa juu amri yake itekelezwe ni lazima pia ipite kwa afisa mwengine hadi imfikie Captain ambaye huamrisha askari wapiganaji ambao wako chini yake.
Hata askari waliokuwa wamemuasi Nyerere mwaka 1964 hawakuwa askari wa vyeo vya juu, bali walikuwa hawa hawa wapiganaji. Kikosi kikiasi, hakuna cha Jenerali, Luteni Jenerali, Meja Jenerali, Brigadia Jenerali wala Kanali; wote hao watajificha wakisubiri ujasiri wa hao 'makapiteni' wanaowatii kama watapokea amri zao kupambana na kikosi kilichoasi.
Kwa ujumla, hakuna mtu yeyote mwenye akili timamu na mwenye uelewe wa mambo ya jeshi ambaye atafurahia maasi ya jeshi. Ukilisikiliza kwa umakini kauli ya Capt. Tesha, utabaini ya kuwa Captain akichukua nchi wakubwa wote watapata kibano.
Katika historia ya Tanzania, haijawahi kutokea Captain wa Jeshi akatoka hadharani kusema au kutoa tahadhari kwa Jenerali au Mkuu wa Majeshi. Tuichukulie kauli ya Capt. Tesha kama ishara muhimu kwetu sote kama taifa na hivyo tukae chini kutafakari kwa kina maneno yake. Badala ya kumjadili Capt. Tesha, tujikite katika kujadili ukweli na uhalisia wa maneno yake!
Kukanusha juu ya uwepo wa mtu mwenye jina la Capt. Tesha Jeshini au la hakutasadia sana hasa kama maneno aliyosema yana ukweli! Kama maneno hayo ni ya uwongo basi pia hata kukanusha hakuna maana kwani uwongo pia hauna utamaduni wa kujitetea, ukasimama!
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Itunge, Dar es Salaam; 4 Oktoba 2025; Saa 2:20 usiku.