Ifahamu dhana ya Utoaji Huduma kwa Jamii

Ifahamu dhana ya Utoaji Huduma kwa Jamii

beth

JF-Expert Member
Joined
Aug 19, 2012
Posts
3,881
Reaction score
6,377
Utoaji wa huduma kwa jamii ni mgawanyo wa huduma muhimu kwa jamii kulingana na mahitaji ya jamii husika. Huduma za jamii ni bidhaa au mahitaji ambayo ni muhimu kwa maisha na ustawi wa jamii

Huduma hizi za kijamii mara nyingi hugharamiwa na Serikali ingawaje kuna huduma nyingine zinachangiwa na wananchi. Mfano wa huduma za kijamii ni Elimu, Afya, Maji na Barabara

Pia, huduma hizo hujumuisha nishati, pembejeo za kilimo, masoko na masuala mtambuka ikiwemo haki za binadamu. Huduma hizi ama hutolewa moja kwa moja na Serikali au kwa ushirikiano baina ya Serikali na wafadhili/wahisani, taasisi za kidini au asasi za kiraia

Ripoti hii imejikita katika huduma zifuatazo; maji, kilimo, afya, elimu, masoko, mifuko ya kuinua jamii kiuchumi na masuala mtambuka ya haki za binadamu na jinsia. Ili kukidhi mahitaji ya jamii (wapokea huduma), watoa huduma wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia dhana ya uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wapokea huduma

Kwa upande wa Serikali (Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Idara na Mawakala wa Serikali), wanawajibika kutoa huduma kwa jamii kwa kuzingatia misingi ya uwazi, usawa na haki za binadamu. Hii ni pamoja na kutoa ufafanuzi na uthibitisho pale unapohitajika na wananchi

Wananchi wanahaki ya kushirikishwa na jukumu la kushiriki kwenye shughuli za jamii, pamoja na kudai uwajibikaji kwa watoa huduma

Huduma za jamii zinapaswa kutolewa kwa kuzingatia misingi mitatu muhimu ya uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji kama inavyoelezwa hapa chini;

Uwazi: Ni hali ya Serikali kutekeleza majukumu yake bila usiri, na kuwahabarisha wananchi kuhusu huduma husika ili waweze kufuatilia utendaji wa Serikali kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Serikali kufanya kazi kwa uwazi kunapunguza hatari ya vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na jinsia. Vilevile, utendaji kazi wa Serikali kwa uwazi kunaimarisha imani ya wananchi kwa serikali yao. Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 132(5)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Kifungu cha 5(2)(c) cha Sheria Na.6 ya Fedha za Umma ya mwaka 2001

Uwajibikaji: Ni Hali ya Serikali kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na kubeba dhamana ya kutoa ufafanuzi na uthibitisho pale wananchi watapohoji utoaji wa huduma kwa jamii. Kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 “Serikali (viongozi na watendaji) itawajibika kwa wananchi”., hivyo Serikali inawajibika kwa wananchi na wananchi wana wajibu wa kuiwajibisha Serikali yao

Ushiriki/ushirikishwaji wa wananchi: Ni hali ya uhusishwaji wa makundi yote ya jamii katika kupanga, kufanya maamuzi kwa mambo yanayowahusu na kufuatilia ufanisi wa huduma za jamii zinazotolewa na Serikali. Kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (d), ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, “Wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba”. Na Ibara ya 146 (1) ya Katiba hiyo inampa nafasi mwananchi kushiriki na kushikirishwa na Serikali za Mitaa katika kupanga mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao za kuishi

WAJIBU Institute
 
Umeme wenyewe nguzo zimeishia Kwa wenye nazo,, maji tumepewa mabomba Kama sinema tu maji hayatoki miezi miwili imepita Sasa hizo zingine nitajuaje Kama zinalidhisha ama laa yaani nchi yetu Kwa Sasa mwenye nacho mpishe
 
Back
Top Bottom