Huyu ndiye mtanzania halisi

Huyu ndiye mtanzania halisi

Mbombo Nunu

Member
Joined
Feb 10, 2018
Posts
92
Reaction score
124
Wandugu,
Baada ya makala yangu ya jana kuhusu uraia kwa watu wa mipakani kama Kyela, naona napata maswali mengi kutoka kwa vijana kuomba ufafanuzi. Niliwahi kuandika makala kama hii mwaka 2012 lakini siioni. Nitajaribu kuandika tena. Mimi sio mwanasheria kwahiyo nitatumia a layman's language.

Ili isiwachoshe wasomaje, nitaikata makala hii katika vipande vipande.

URAIA WA TANZANIA
Masuala ya uraia nchini Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Uraia ya Tanzania ya mwaka 1995 Sura 357 kama ilivyorejewa mwaka 2002, pamoja na kanuni zake za mwaka 1997. Sheria hii imeanisha aina tatu za uraia wa Tanzania ambazo ni;
1. Uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa
2. Uraia wa Tanzania kwa kurithi
3. Uraia wa Tanzania kwa kujiandikisha.

URAIA WA TANZANIA WA KUZALIWA.
Mtu aliyezaliwa Tanganyika kabla ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja wa wazazi wake alizaliwa Tanganyika.

Mtu aliyezaliwa Tanganyika baada ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja wa wazazi wake alikuwa raia wa Tanganyika.

Mtu aliyezaliwa Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi alitambulika kuwa ni raia wa Zanzibar wa kuzaliwa.

Mtu aliyezaliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku na baada ya Muungano, atatambulika kuwa ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa ikiwa mmoja wa wazazi wake ni raia wa Tanzania.

Mtu hawezi kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa kama wakati wa kuzaliwa kwake hapa nchini, wazazi wake wote hawakuwa raia wa Tanzania. Aidha, mtu yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kabla Muungano, hatatambulika kuwa ni raia wa Tanzania mara baada ya muungano.

Uraia wa wengi wetu uko katika kundi hili. Ni raia wa kuzaliwa.

PART II URAIA WA KURITHI

Mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika kabla ya uhuru alitambuliwa kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi endapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika.

Mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika baada ya Uhuru na kabla ya Muungano alitambuliwa kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi, ikiwa baba yake alikuwa raia wa Tanganyika.
Sheria ya Uraia ya Tanganyika ya mwaka 1961 haikutoa fursa kwa mama kumrithisha uraia mtoto wake aliyezaliwa nje ya nchi. Hivyo mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika katika vipindi tajwa hapo juu hakutambulika kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi kupitia mama yake.

Mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika hakutambuliwa kuwa raia wa Tanganyika kwakurithi iwapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika kwa kurithi. Raia wa kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Tanganyika. Hii sheria inawakumbuka hawa watoto tunaowazaa tukiwa nje ya Tanzania. Japo wao ni raia wa Tanzania lakini watoto wao kama pia watazaliwa nje ya TZ hawatakuwa raia wa TZ.

Mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar kabla ya Muungano atakuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi endapo baba yake ni raia wa Zanzibar.
Vile vile, Sheria ya Uraia ya Zanzibar haikuruhusu mama raia wa Zanzibar kurithisha uraia kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Zanzibar. Kwa maana nyingine, mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar katika kipindi hicho hakutambuliwa kuwa ni raia wa Zanzibar kwa kurithi kupitia kwa mama yake.

Mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar hakutambuliwa kuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi ikiwa Baba yake alikuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi. Raia wa Zanzibar kwa kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Zanzibar.

Mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania siku na baada ya Muungano atakuwa raia wa Tanzania kwa kurithi endapo mzazi wake mmoja ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa au kuandikishwa.
Mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania hawezi kuwa raia wa Tanzania kwa kurithi iwapo baba/mama yake ni raia wa Tanzania kwa kurithi. Hapa mama sasa anaweza kurithisha uraia wake kwa mtoto.

Mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kurithi, kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ile ile mara baada Muungano.
Katiba pendekezwa iliwatambua hawa watu kama raia wa kuzaliwa. Bahati mbaya imetupwa kwahiyo wanabaki kuwa na uraia wa kurithi.

PART III
URAIA WA KUJIANDIKISHA.
Mtu yoyote ambae siyo raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzaliwa au kurithi anaweza kuomba uraia wa Tanzania wa kujiandikisha kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura 357 ya mwaka 1995.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kumpa au kutompa uraia wa Tanzania mgeni anaetaka kuomba uraia wa Tanzania anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:

(i) Mwombaji awe na umri kuanzia miaka 18 na uwezo wa kufanya maamuzi yanayokubalika kwa mujibu wa sheria za nchi,

(ii) Awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miezi 12 mfululizo kabda ya kutuma maombi ya Uraia,

(iii) Katika muda wa miaka kumi kabla ya miezi kumi na mbili hiyo awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kihalali kwa muda usiopungua miaka saba.

(iv) Awe anafahamu vizuri lugha ya Kiswahili au Kiingereza,

(v) Awe na tabia njema,

(vi) Awe na manufaa kwa taifa, yaani awe alichangia na anaendelea kuchangia katika ukuzaji wa uchumi,
sayansi na teknolojia na utamaduni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na

(vii) Awe anakusudia kuishi moja kwa moja ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ombi lake la uraia litakubaliwa.

Mgeni yeyote mwenye nia ya kuomba uraia wa kujiandikisha mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anatakiwa kufuata taratibu zifuatazo;

(i) Mwombaji anatakiwa kujaza fomu za maombi ya uraia ambazo zinapatikana katika ofisi zote za Uhamiaji za Wilaya,
Mikoa, Afisi kuu ya Uhamiaji Zanzibar na Makao Makuu ya Uhamiaji Dar es Salaam.

(ii) Mwombaji anatakiwa kutoa matangazo ya nia yake ya kuomba Uraia wa Tanzania mara
mbili mfululizo kwenye magazeti yaliyosajiliwa Tanzania.

Mchakato wa Kushughulikia Maombi ya Uraia Ili kuhakikisha kuwa wageni wanaopewa uraia ni wale wenye manufaa kwa Taifa, maombi yote yanapaswa kupitia na kujadiliwa katika vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama za: Ngazi ya Kata au Shehia (kwa upande wa Zanzibar)

Katika ngazi ya Kata au Shehia anayoishi mwombaji, ambapo atahojiwa na maombi yake kujadiliwa na kikao hicho na hatimaye ombi lake kupelekwa ofisi ya Uhamiaji Wilaya kwa hatua zaidi.

Katika ngazi hii, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itajadili maombi ya uraia yaliyowasilishwa kutoka ngazi ya Kata au Shehia, hatimaye maoni na mapendekezo yake hupelekwa katika ngazi ya mkoa.

Ngazi ya Mkoa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nayo itajadili maombi yaliyowasilishwa na kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusiana na ombi husika na hatimaye hutumwa kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, ambaye atatoa ushauri na mapendekezo yake kwa Mhe. Waziri mwenye dhamana ya masuala ya uraia wa Tanzania kwa maamuzi.

Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa Mwanamke aliyeolewa.

Mwanamke mgeni ambaye ameolewa na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wowote wa uhai wa ndoa yake, anaweza kuwasilisha maombi ya uraia wa Tanzania kwa kujiandikisha.

Ombi la uraia kwa mwanamke aliyeolewa linatakiwa kuwasilishwa pamoja na viambatanisho vifuatavyo;

(i)Cheti cha ndoa kilichosajiliwa na Mamlaka husika nchini
(ii) Pasipoti ya taifa lake ambayo haijaisha muda wake
(iii) Kibali cha kuishi nchini ambacho hakijaisha muda wake (Hati ya Mfuasi)
(iv) Vielelezo vinavyothibitisha kuwa mume wake ni raia wa Tanzania.Ombi la Uraia wa Tajnisi kwa Mtoto

Sheria ya Uraia ya mwaka 1995, inatoa fursa kwa mzazi au mlezi halali wa mtoto (asiye raia) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kumuombea mtoto huyo Uraia wa Tanzania. Baada ya maombi rasmi kuwasilishwa, Waziri mwenye dhamana ya uraia anaweza kuruhusu mtoto huyo aweze kupata uraia wa tajnisi.

Waziri mwenye dhamana na masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani) ndiye mwenye Mamlaka ya mwisho ya kutoa au kutotoa uraia wa Tanzania kwa mwombaji yoyote kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya mwaka 1995.

Hili kundi lilikuwa dogo ila sasa linazidi kuwa kubwa. Tumeanza kuchangamkia kuoana na Wakenya, Wacongo, Wamalawi, Wanigeria nk.

Kama kule kwetu, unaenda kuoa Malawi na kutulia. Huyo mke au mume sio raia. Hakikisha unafuta masharti yote ili usipate matatizo huko mbeleni. Pia hii sheria inapendelea wanaume. Ukioa, mkeo anaweza kujiandikisha muda wowote kuwa raia wa Tanzania. Lakini mwanamke ukiolewa na mgeni, mume wako kuna safari ndefu katika kuwa raia wa Tanzania.
 
Ningependa kujua kipengele cha kuulizwa vyeti vya bsbu na bibi na familia zote imo kwenye sheria.
 
ubarikiwe mkuu, Kazi hii ilipaswa kufanywa na ID ya Uhamiaji kama imo humu, kama tunavyelimishwa na TANESCO humu jf.
 
mhutu ni raia kweli kw hizo sifa
 
Nimeshangaa uhamiaji wameshindwa kuijua sheria yao wenyewe wanaanza kuhoji uraia wa babu baadala ya kuhoji uraia wa wazazi, kwa sheria ya uraia tuliyonayo mzazi mmoja tu anatosha kukurithisha uraia wake mfano endapo mama ni raia wa Tanzania basi mtoto wake aliyezaliwa hapa Tanzania ni raia wa Tanzania na nchi nyingi duniani mambo yako hivyo.
Maanake ni kwamba babu anaweza kuwa mkenya mjukuu akawa mtanzania, mfano kuna watoto wamezaliwa hapa Tanzania mama zao ni watanzania ila wazazi wao ni wachina, watoto hao ni raia wa Tanzania mfano rais wa TFF, hivyo sioni mantiki ya kuhoji vyeti vya mababu wa pande zote mbili.
Uhamiaji wajifunze kusimamia sheria zao vizuri wasitumike na wanasiasa.
 
Unaweza kunyang'anywa uraia ikibainika wewe ni tishio kwenye usalama wa nchi.
 
PASPORT YA TANGANYOKA IMEKUWA ISSUE KWELI KWELI UTAFIKILI TANZANITE
 
Back
Top Bottom