barafu
JF-Expert Member
- Apr 28, 2013
- 6,739
- 32,870
Muonekano wa nje wa ndege ya Boss wa Barrick Gold Corporation
Sehemu ya ndani ya Gulfsytream IV
Herry Oppenheimer akishuka katika uwanja wa ndege Mwadui 1952 kama vile alivyoshuka Thornton Lawson wa Barrick 2017
Siku kadhaa za "Makinikia" (japo TUKI wamesema tuite maboso na si makinikia) zimekuwa ni za kubandika na kubandua.
Toka katika kuta za masoko makubwa ya hisa ya London Stock Exchange,New York Stock Exchange nk,hadi viunga vya Tandale na Sitimbi,kila mwenye utashi wa kisiasa anaongelea juu ya Barrick,Magufuli na Makinikia,na usipomtaja Tundu Lissu,basi mjadala unakosa nakshi.
Lolote linalohusu Barrick,JPM au Tundu Lissu na maboso,limekuwa ni habari inayoweza kuuza ukurasa wa kwanza wa magazeti makubwa na madogo.
Hata ndege aliyokuja nayo "boss" wa Barrick toka Canada mpaka Dsm imekuwa ni "habari",ndiyo maana msemaji wa Ikulu ndugu G.Msigwa ameweka ujio wa ndege binafsi ya boss wa makinikia kama sehemu ya "Content" ya taarifa ya Ikulu kwa umma wa Watanzania.Ndege hiyo nayo imekuwa ni "habari",katika taarifa ya Ikulu,Mr Msigwa anaweka msisitizo wa "ujio Mr Thornton akiwa na ndege binafsi"
Thornton J.Lawson ametua Tanzania na ndege binafsi aina ya Gulfstream IV (GIV),yenye usajili wa Canada unaosomeka kama C-FHPM.Hii ni moja kati ya ndege za anasa zinazotumiwa na matajiri na viongozi wenye ukwasi duniani.Ni bahati mbaya au nzuri,kuna baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika,licha ya ufukara na umaskini wa wananchi wao,ndege jamii hii ni moja ya ndege zinazomilikiwa kwa usafiri binafsi wa marais hao.
Gulfstream ni ndege inayoweza kukaa hewani masaa zaidi ya 14 bila kugusa ardhi,uwezo wa kubeba tani 40 za mafuta na speed ya 980km kwa saa.Imetengenezwa kubeba abiria kati ya 09 hadi 11.
Hiyo ya boss wa Barrick imekuwa "configured" kubeba watu sita tu,chumba cha kulala,ukumbi wa mikutano,sehemu ya kupumzikia,choo na bafu.Kwa umuhimu wa ujio wa kibiashara katika ardhi ya makinikia,boss wa Barrick amesafiri toka Canada mpaka Dsm akiwa peke yake ndani ya chombo hicho kama abiria.
Kwenye "Flight Tracking History" ya ndege hiyo,inaonekana ilitoka Canada kuvuka bahari ya Atlantic,ikatua Nice Côte d' Azur International Airport katika jiji la Nice Ufaransa kwa ajili ya kujaza mafuta,na baadae kunyanyuka moja kwa moja kwa masaa saba na nusu hewani hadi katika ardhi ya Dar es Salaam.Majira ya 1945(UTC) ambayo ni sawa na saa 2245 za huko Afrika Mashariki Gulfstream IV iligusa ardhi ya Tanzania.
Hii inatokea baada ya Barrick kupoteza mvuto katika masoko makubwa ya hisa ya Ulaya na Amerika.Ujio wa Thornton,mazungumzo na baadae maafikiano juu ya "mgogoro" huu wa kiuchumi,unarudisha taswira chanya katika ulimwengu wa biashara ya madini iliyobebwa na familia za kiyahudi.
Masaa matatu baada ya mkutano wenye tabasamu mbele ya waandishi wa habari kati ya Rais wa nchi na Chief Executive wa Barrick Gold Corporation,hisa za Barrick zinapanda kwa kasi katika masoko makubwa ya hisa,na safari ya Thornton J Lawson,bingwa wa "fitna" za biashara ya madini inaonekana kuwa yenye mafanikio makubwa kwa wadau na wanahisa wa Barrick Gold Corporation.The deal is Done!!!
Hii inarudisha nyuma miaka zaidi ya 60,baada ya Dr John Williamson mmiliki wa mgodi wa Mwadui kuwawekea ngumu kampuni ya De Beers kuwa mshirika na mwanahisa wa almasi ya Mwadui.Hali hii ilifanya thamani na soko la almasi ya Afrika Kusini kuporomoka katika soko kuu huko London na De Beers kutikisika kiuchumi.
Machi 1952,kampuni ya De Beers ilimpandisha ndege mwanafamilia,mtoto wa kwanza wa mmiliki wa kampuni,Mr Herry Oppenheimer kwenda Mwadui na kuweka mambo sawa,ili kuimarisha soko la almasi ya Afrika Kusini kule London,na kujihakikishia umiliki wa asilimia kadhaa katika mgodi wa Mwadui.
Wakati Herry akipanda ndege kurudi Afrika Kusini,taarifa zilishafika London kuwa sasa almasi ya Mwadui na ile ya Afrika Kusini zitachanganywa katika soko kuu la London.Heshima ya Be Beers katika ulimwengu wa madini ikapanda maradufu na kwa faida kubwa.Historia ile ya mabeberu wa madini inajirudia,na wajukuu wetu wataikuta na kuisoma katika vitabu vya kumbukumbu.
Wakati mwaka 1992,Nicolas Oppenheimer mtoto pekee wa Herry Oppenheimer aliyegonga mwamba kwa Nyerere alipanda ndege kuja kuchukua 75% za mgodi wa Mwadui na kuiacha 25% isiyoeleweka mikononi mwa serikali,leo Thornton Lawson anapanda ndege toka Canada kuja Tanzania,kuweka mambo sawa ili kile wanachokibeba kwa "utapeli wa kisheria" kiangaliwe upya na kujadiliwa.
Tunaweza kuwa na tofauti za vyama na mtazamo wa kiitikadi,lakini hatuwezi kuwa vipofu wa kutotambua "kiburi cha rasilimali" ambacho Rais amejaribu kuwaonyesha mabepari wa madini,wakawasha ndege saa moja baada ya hotuba ya Rais na kuanza kuitafuta anga ya Tanzania kuja kuweka mambo sawa.
Zamani walitutumia tiketi za ndege tukawafuata katika hotel zao na kujadiliana juu ya mali zetu,sasa wanawasha ndege zao za kifahari na kutia mafuta kutufuata katika ardhi yetu.Hata kama watatushinda,lakini kiburi cha rasimali zetu tumewaonyesha.
barafu wa JF