Huruma ya Dowans inatoka wapi? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Huruma ya Dowans inatoka wapi?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Quinty, Feb 27, 2011.

 1. Quinty

  Quinty JF-Expert Member

  #1
  Feb 27, 2011
  Joined: Mar 25, 2010
  Messages: 463
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Kutoka Tanzania Daima
  KWA takriban miaka mitatu sasa sinema ya mitambo ya kampuni ya kuzalisha umeme wa dharuFra ya Dowans imezidi kushika kasi kwenye macho,vichwa na masikio ya kila mwenye kiu na habari pamoja na nishati ya umeme.

  Sinema hii kwangu imeshnichosha licha ya baadhi ya watu wenye kuheshimika hapa nchini kuitumia kwa lengo la kujinufaisha kwa namna wanayoijua wao hasa katika kipindi hiki cha mgawo wa umeme.

  Baada ya Dowans na TANESCO kufikishana kwenye mahakama ya kimataifa inayoshughulikia migogoro ya kibiashara na TANESCO kuamriwa kulipa fidia y ash bilioni 94, sasa sinema hiyo imebadili upepo.

  Dowans sasa wanaionea huruma Tanzania kwa kukaa gizani wakati mitambo ya kuzalisha umeme ipo, kampuni hiyo inataka kuzungumza na TANESCO ili kuangalia uwezekano wa kupunguza fidia wanayoitaka.

  Ili kuwaonyesha kuwa wana huruma zaidi, mmiliki wao Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi, anayeishi Oman aliamua kuja hapa nchini, ili kuzungumza na TANESCO namna watakavyoweza kulimaliza skata hilo kwa njia iliyo bora.

  Eti mmliki huyo ameguswa na Tanzania kuwa gizani kiasi cha kutuhurumia, anasema aliwaandikia barua TANESCO ili wafanye mazungumzo lakini Shirika hilo mpaka sasa limekaa kimya.

  Mkurugenzi wa Fedha wa Dowans, Stanley Munai, anasema wanataka walipwe kiasi cha sh bilioni 36 (dola milioni 24) ambazo ndiyo thamani ya umeme iliyowauzia TANESCO kabla ya mkataba wao kuvunjwa mwaka 2008.

  Ni vema kabla ya kuanza kushabikia au kufurahia huruma hii ya Dowans tukajiuliza ni kwa nini imekuja hivi sasa? Kwanini baadhi ya viongozi hasa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba wapo mbele kuuaminisha umma kuwa hatuwezi kuwa na umeme wa uhakika bila Dowans.

  Makamba, anashauri TANESCO waingie mkataba wa muda mfupi na Dowans ili umeme upatikane, hazungumzii matokeo ya kesi baina ya pande hizo mbili na wala hazungumzii uzembe wa serikali ambayo kwa takriban miaka minne imeshindwa kununua mitambo kama ya Dowans au kuzidi hiyo.

  Mwenyekiti huyo anataka jamii ione TANESCO ndiyo wanaokwamisha mazungumzo na Dowans ili kupata umeme wa uhakika, lakini hazungumzii watu waliotufikisha hapa tulipo, je mtu huyu ana nia njema na taifa?

  Hivi ni kweli hatuwezi kuwa na umeme wa uhakika pasipo na Dowans au ndiyo viongozi wetu wanaitumia kampuni hiyo kujinufaisha?

  Kimsingi ujio wa mmiliki wa Dowans na kasi ya viongozi wetu vinatia shaka, vinaonyesha wazi kuna ajenda ya siri au ulaji ndani ya sakata hilo, TANESCO wanataka waburuzwe kwa matakwa ya wachache.

  Hebu tujiulize Dowans wanatuonea huruma na kusamehe sehemu ya deni wanalotudai bila kutegemea chochote? Jibu ni hapana wanafanya hivyo wakijua fika wataanza kuuza umeme wao kwa shirika hilo muda si mrefu.

  Huruma hii ya Dowans ni ya kuogopwa sana, Tunahitaji muda wa kufikiri zaidi juu ya huruma hiyo ambayo inaweza kuwa mzigo mkubwa kwetu kuliko hata ule wa awali tuliouvunja.

  Haiingii akilini kuwa Dowans ambayo ni kampuni ya kibiashara ikasamehe zaidi ya mili 55 bila kuwepo mazingira ya kupata fedha hizo kwa mlango wa nyuma kama inavyofanyika katika mikataba mbalimbali ambayo Tanzania huingia na wale tunaowaita kuwa ni wawekezaji.

  Tunahitaji umakini mkubwa wa kupokea huruma hii na ikiwezekana kila kitu kiwekwe wazi katika sakata hilo ili TANESCO isije ikatumbukizwa kwenye mtego wa watu wachache ambao kila kukicha hupanga mbinu za kutafuna rasilimali za taifa.

  Tunachotakiwa kukifanya hivi sasa ni kuibana serikali itekeleze miradi ya kuzalisha umeme kama walivyoahidi miaka mingi iliyopita na wala si kushabikia umeme wa kampuni za dharura.

  Inatia aibu na kusikitisha kuona Tanzania yenye dhahabu, tanzanite, mito, bahari, maziwa, makaa ya mawe, chuma ikiendelea kuwa katika giza ilhali nchi zisizo na vitu hivyo zikiwa na umeme wa uhakika na mwingine zinauuza nje ya nchi zao.

  Afrika Kusini ina idadi ya watu milioni 40 kama tulivyo sisi na ina uwezo wa kuzalisha megawati 42,000 lakini sisi hatuna uwezo hata wa kuzalisha megawati 1000, hii ni aibu na kamwe hatuwezi kuendelea kama umeme utaendelea kugawiwa kwa mafungu.

  Leo hii uchumi unalega lega kwa sababu ya viwanda vingi vinashindwa kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa na pia vimeshawafukuza kazi baadhi ya watu ili kubana matumizi lakini wananchi wanaendelea kuwa wapole kwa madai kuwa kutopatikana kwa mvua za kuyajaza mabwawa ya kuzalisha maji ni mapenzi ya Mungu.

  Hakuna mapenzi ya Mungu hapa, bali ni mipango mibovu na ulaji wa watawala wetu ambao wanajua fika kama nchi itakuwa na umeme wa uhakika hawatoweza kupata tenda za kuuza mafuta au kuingiza majenereta hapa nchini.

  Wananchi hivi sasa wamekata tamaa ya maisha, hawajui kesho itafikaje, ahadi ya maisha bora yatapatikana katika Tanzania yenye neema hivi sasa haisikiki tena, porojo za siasa, maneno matamu matamu na matumaini yasiyokamilika ndiyo yanayozungumzwa kila kukicha na wanasiasa wetu.

  Mazingira tuliyonayo hivi sasa yanaonyesha wazi kuwa viongozi wetu wameshindwa kubuni mbinu na mikakati imara ya kutuoa kwenye umasikini tulionao, suluhisho la pekee ni kuwawajibisha na tutafute wengine wenye uwezo wa kutukwamua kutoka hapa tulipo.

  Kama tutaendelea kuvumilia ngonjera za Dowans, Bajaj kwa wajawazito, meli kubwa na nyinginezo kamwe hatutaweza kuachana na giza linalotukabili pamoja na hali duni ya maisha
   
Loading...