Hukustahili kufa Katarina…..!

Hukustahili kufa Katarina…..!

Mtambuzi

Platinum Member
Joined
Oct 29, 2008
Posts
8,809
Reaction score
15,438
african-girl.jpg

Picha haihusiani na habari hii.....

Alikuwa ni mtumishi wa nyumbani wa shemeji yangu ambaye aliolewa na kaka yangu binamu, kwa bahati mbaya huyo kaka yangu alishafariki na hata mkewe yaani huyo shemeji yangu na yeye alikuja kufariki pia miaka mitano baadae tangu kaka afariki. Hawa ndio walionilea na kunisomesha nilipokuwa Arusha.
Huyu binti alikuwa na umri wa miaka 15 wakati huo.

Nakumbuka ilikuwa ni mwanzoni mwa mwaka 1991, ndio aliletwa kufanya kazi kwa shemeji yangu hapa jijini Dar, kwani baada ya kaka kufariki familia yake ilihamia Dar. Nakumbuka nilikuwa naenda kwa shemeji yangu kila wiki kumjulia hali yeye na wanae.
Huyu Binti ambae alikuwa akijulikana kwa jina la Katarina mwenyeji wa kule Iringa alitokea kunipenda kweli na hakuficha hisia zake, kalikuwa ni kabiti kazuri na kadogo sana na kalikuwa na heshima ile ya kijijini hasa. Siku moja shemeji yangu aliniambia kwa utani lakini, kuwa Katarina ananipenda na kama nikitaka kuoa basi nisitafute mwanamke mwingine bali Katarina angenifaa zaidi.

Sikutilia maanani kauli ya shemeji yangu, na niliichukulia kama utani tu. Nilikuwa kila nikienda kwa huyo shemeji yangu Katarina atahakikisha ananipikia na kuniandalia maji ya moto ya kuoga tena kwa heshima na nikishaoga kama nitalala pale kwa shemeji yangu alipenda sana kupiga soga na mimi na alikuwa akivutiwa sana na simulizi zangu za uongo na kweli.Ilitokea nilipata kazi moja ya muda mfupi ambapo nililazimika kwenda mkoani Morogoro ambapo nilikaa kwa miezi sita niliporudi nilikaa kama mwezi mmoja kabla sijaenda kwa shemeji yangu ambaye alikuwa kiishi Mbezi ya Kimara kumjulia hali.

Siku moja nilijikuta nikipata hamu sana ya kwenda kumuona shemeji yangu na nakumbuka ilikuwa ni Disemba mwaka 1992. Nilipotoka kibaruani jioni nilikwenda kwa shemeji yangu, lakini nilipofika nilikuta kuna mtumishi mwingine pale nyumbani, nilikaribishwa na kwa bahati mbaya shemeji yangu hakuwepo nyumbani alitoka kidogo kwenda kwa shoga yake aishiye mtaa wa pili.
Kumbuka kwamba kipindi hicho kulikuwa hakuna simu za mkononi, ilibidi nikae pale sebuleni peke yangu kwani hata watoto wa shemeji walikwenda kwa marafiki zao kusoma tuisheni. Nilikaa pale sebuleni peke yangu kama saa moja na nusu na ndipo shemeji akarudi na aliponiona alifurahi sana.

Tulizungumza mambo mengi sana lakini sikusikia akimzungumzia Katarina, mwishowe ikabidi nimuulize. "Shemeji, tangu nimefika hapa sijamuona Katarina, mchumba angu, je yuko wapi?" Niliuliza kwa masihara.
Niliona uso wa shemeji yangu ukisawajika kwa huzuni na alinyamaza kimya kwa sekunde kadhaa, kabla hajasema kitu alimuomba yule binti aliyenipokea ambaye niliambiwa ni mtumishi wa pale nyumbani amletee maji ya kunywa.

Muda wote tukisubiri maji yaletwe tulikaa kimya na alionekana kuwaza sana, hali ile ilinitisha sana. Mara maji ya kunywa yakaletwa, alikunywa funda kadhaa za maji kisha akaweka ile glasi chini na kushusha pumzi ndefu.
"Shemeji ni jambo la kusikitisha kukujulisha kuwa Katarina alifariki wiki iliyopita na taarifa hizo tumezipata juzi" Alisema shemeji yangu kwa upole, niliposikia taarifa ile kuna kitu kilinichoma moyoni kama msumari wa moto na nilijihisi kama natetemeka na kijasho chembamba kilinitoka.

"Amefia wapi, aliugua nini, na amezikwa wapi?" yalinitoka maswali mengi mfululizo.

Shemeji yangu alinisimulia kuwa, aliamua kumtafutia shamba boy wake wa zamani kibarua katika kiwanda fulani cha wahindi kwa kuwa alitarajia kuoa na kabla ya kuanza kazi alimtuma kwao Singida akamletee shamba boy mwingine ili amfundishe kazi awe ni mrithi wake kabla hajaanza kazi.
Alikwenda Singida na akaja na huyo kijana na baada ya kumfundisha kazi na kumudu, alikwenda kuanza kazi yake katika kampuni hiyo ya wahindi na kumuacha yule kijana mpya pale nyumbani. Kumbe kuna siku yule kijana shamba boy mpya alimbaka Katarina, lakini alimtisha kuwa akiseme atamuua na kukimbilia kwao Singida asionekane tena.Katarina aliogopa kusema na akabaki kimya akiugulia maumivu baada ya kitendo kile. Haikupita muda, yule binti alianza kuumwa umwa na kutapika kusikoisha, ikawa kila anachokula anatapika. Utendaji wa kazi ukapungua na akawa anatumia muda mwingi sana kulala. Shemeji yangu akajenga wasiwasi ikabidi amdadisi kama ana mimba.

Awali Katarina alikataa katakata, kuwa ni mjamzito lakini shemeji alimtishia kuwa atampleke Hospitali kesho yake akapime ili kujiridhisha Katarina alikiri kuwa ni mjamzito. Sasa Shughuli ikawa kwenye kumtaja mhusika, Katarina alikata kabisa kumtaja mhusika shemeji ilibidi atumie mbinu ya kumtisha kuwa atampeleka Polisi na ndio akamtaja yule kijana lakini alisema kuwa alitishwa sana kuwa akimtaja atamuua ilibidi shemeji amfuate yule kijana chumbani kwake ili kumdadisi lakini kumbe yule kijana alikuwa akifuatilia ule mzozo kupitia dirishani na aliposikia jina lake likitajwa kuhusika na ile mimba alitoweka haraka sana asijulikane alipokwenda.


Ilibidi shemeji abaki na ule mzigo, kwanza alikuwa ni mjane pili hakuwa na mfanya kazi wa Ng'ombe maana yule kijana katoweka na pia mtumishi wake wa ndani yaani Katarina ndio huyo ni mjamzito, na yeye ni mtumishi serikalini, ilikuwa ni kaazi kweli kweli.
Ilibidi afanye mawasiliano na marafiki zake na kwa kushirikiana na yule boy shamba wake wa zamani alifanikiwa kupata mfanyakazi wa ng'ombe mwingine, na baada ya wiki akapata House girl mwingine.

Baadae alimshauri Katarina arudi kwao Iringa na alimuahidi kumpa pesa ya kutosha ili imsaidie kujifungua na akijifungua alimtaka arudi kwake ili aendelee na kazi. Ni kweli Katarina alikubali japo shingo upande na alikuwa na wasiwasi jinsi atakavyopokelewa nyumbani kwao na wazazi wake.
Baada ya wiki moja Katarina alipakiwa ndani ya basi na kurudishwa Iringa na yule Shamba Boy wa zamani ambaye alitafutiwa kazi na shemeji katika kampuni ya wahindi. Shemeji aliandika barua ndefu kueleza mkasa uliompata Katarina ili wazazi wake wasije kumuadhibu.

Aliporudi kutoka Iringa yule shamba boy aliyempeleka alisimulia kuwa walipokelewa lakini kwa wasiwasi kutokana na hali aliyokuwa nayo. Na kama si ile barua aliyoandika shemeji, basi yule shamba boy angelipishwa mahari na kuozeshwa yule binti, lakini ile barua iliposomwa ndio wakaamini japokuwa wapo walioitilia mashaka kuwa huenda imetengenezwa makusudi ili kumnasua yule kijana. Hata hivyo yule binti alikanusha kuwa yule kijana aliyefuatana naye hahusiki.


Baada ya kupita mwezi mmoja shemeji yangu alipokea taarifa kuwa Katarina alifariki wiki moja iliyopita baada ya jaribio la kutoa mimba kushindikana. Taarifa zaidi zilisema kuwa alipata manyanyaso pale nyumbani kwao kwa wazazi wake kutokana na kwamba walikuwa wanamtegemea na baada ya kurudi pale nyumbani wakawa wana hali ngumu na hivyo kumtupia Katarina lawama kuwa amekuwa mzembe kaharibu kazi kwa umalaya.


Katarina alikusudia kuitoa ile mimba ambayo ilishatimiza miezi sita kwa kutumia miti shamba na ndipo ikashindikana na akapoteza maisha.
Nilishikwa na butwaa wakati wote shemeji yangu alipokuwa akinisimulia mkasa huo wa Katarina.

Leo hii ni miaka 20 imepita tangu binti huyu afariki Dunia.

RIP Katarina.
 
R.IP KATARINA
pole sana Mtambuzi kuwa mjane wakati kijana mdogo sana
 
Last edited by a moderator:
R.IP KATARINA
pole sana Mtambuzi kuwa mjane wakati kijana mdogo sana
amu nawe, mbona unapotosha bana.....
Miaka hiyo nilikuwa bado mdogo na wala nilikuwa sifikirii kuwowa....LOL

Ahsante kwa pole hata hivyo.
 
Last edited by a moderator:
Kaka habari za vifo vya kutoa mimba enzi hizi imekua kama kawaida, nilipokuwa nafundisha shule moja pale Sinza-Dar es salaam tukawa tunajadili kitabu cha Tamthiliya cha KILIO CHETU (ni tamthiliya nzuri sana na ile ya ORODHA) basi wanafunzi wale wa kike wakanijibu waksema kuwa, Mwalimu kupata mimba ni kuamua mwenyewe na kuzaa ndio kabisaaaa, tunajua kila kitu. kwa mara ya kwanza nilishangazwa sana maisha ya vijana wetu wa siku hizi, ngoja niiishie hapa kwa leo
 
Kaka habari za vifo vya kutoa mimba enzi hizi imekua kama kawaida, nilipokuwa nafundisha shule moja pale Sinza-Dar es salaam tukawa tunajadili kitabu cha Tamthiliya cha KILIO CHETU (ni tamthiliya nzuri sana na ile ya ORODHA) basi wanafunzi wale wa kike wakanijibu waksema kuwa, Mwalimu kupata mimba ni kuamua mwenyewe na kuzaa ndio kabisaaaa, tunajua kila kitu. kwa mara ya kwanza nilishangazwa sana maisha ya vijana wetu wa siku hizi, ngoja niiishie hapa kwa leo

Na hapo umezungumzia hapa Dar, huko vijijini hali ni mbaya, kwani idadi ya mabinti wanaokufa kutokana na mimba za utotoni ni kubwa kuliko unavyofikiria, kupata takwimu sahihi sio rahisi kwa sababu vifo vingi haviripotiwi katika mamlaka zinazohusika na badala yake watu huzika kimya kimya.............
 
stori imeugusa sana moyo wangu, imenisikitisha sana. Mabinti wengi wa kazi wananyanyasika majumbani na hawana msaada wa kuwakwamua. R.I.P Katarina
 
Na hapo umezungumzia hapa Dar, huko vijijini hali ni mbaya, kwani idadi ya mabinti wanaokufa kutokana na mimba za utotoni ni kubwa kuliko unavyofikiria, kupata takwimu sahihi sio rahisi kwa sababu vifo vingi haviripotiwi katika mamlaka zinazohusika na badala yake watu huzika kimya kimya.............
Wakati nasoma Form One shule moja iko Tanga tulimzika Binti aliyejulikana kwa jina la Doris akiwa form two, tuishie hapo hapo ila pia nikiwa nafundisha shule moja iko Rufiji it was the same same story acha wale ambao wanazaa wengi wao huishia kaburini, nakubaliana na wewe kaka, ukiuliza mamlaka za juu tutanye nini wanachosema ni kuwa ni kiherehere chao....
 
stori imeugusa sana moyo wangu, imenisikitisha sana. Mabinti wengi wa kazi wananyanyasika majumbani na hawana msaada wa kuwakwamua. R.I.P Katarina

Ni kweli mkuu, ni msiba ambao ulinigusa sana na ninaamini binti yule hakustahili kufa, nilikuwa nafikiria labda wazazi wake wasingemnyanyasa kwa kitendo chake cha kubeba mimba, labda angemudu kujifungua salama...

Yote ni kazi ya Mungu.

RIP Katarina
 
Wanawake(wasichana) wa kazi ni kati ya kundi la watu wanaonyanyasika katika ajira zisizotambulika kiserikali.
Wapo ambao hupewa si mimba tu, bali hata maambukizi ya ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa.
 
Ooh my God! Ingawa ni tukio la zamani,,ila limeniuma sana, R.I.P KATARINA
 
Pole sana Mtambuzi! But all in all wewe kweli ni kisima cha habari zenye kusisimua!
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom