Hotuba ya Mwenyekiti wa UVCCM Taifa katika kilele cha matembezi ya UVCCM-Zanzibar

babutz

Member
Dec 24, 2016
68
80
JUMATATU 09 JANUARI 2017.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar (MCC)

Ndugu Vuai Ali Vuai Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar

Mheshimwa Mboni Muhita, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM Taifa,

Mheshimiwa Mama Asha Balozi Mkwe wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Ndugu Shaka Hamdu Shaka Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Taifa

Wajumbe wa Kamati kuu ya CCM na Halmashauri kuu ya CCM Taifa mliopo.

Waheshimiwa Mawaziri, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wabunge

Ndugu Wenyeviti wa CCM wa Mikoa

Viongozi mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi na jumuiya zake

Wananchi, vijana wenzangu

Mabibi na mabwana

Kidumu Chama Cha Mapinduzi.

Ama kwa hakika leo ni siku adhimu na muhimu miongoni mwa siku muhimu katika maisha yetu vijana wa Chama Cha Mapinduzi na kila mwananchi wa Tanzania, pia kwa uzito wa pekee wa Mapinduzi yetu matukufu na mustakabali wa kizazi chetu kilichotokana na tokeo la kufanyika kwa Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964.

Siku hii ya leo kuelekea Januari 12, 2017 ni muhimu sana kwa sababu ile dhamana tuliopewa, tuliokabidhiwa, kurithishwa na wazazi wetu, tumeendelea kuilinda na sasa kutufikisha miaka 53 .

Mheshimiwa Mgeni rasmi

Umuhimu wa dhamana hii ni nyeti mno, hutegemea sana maarifa, hekima, busara na ujasiri utokanao na nguvu za waliopewa jukumu la kuilinda dhamana yenyewe na utayari wao, malengo na misimamo yao ambayo si legelege wala tepetepe .

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tunampongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein sambamba na kuwapongeza kwa dhati kabisa marais wetu wote wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar toka awamu ya kwanza hadi ya saba kwa kuendelea kuyalinda, kuyatetea na kuyaendeleza Mapinduzi yetu kwa vitendo. Aidha tunawpongeza pia Marais wote wa wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia awamu ya kwanza hadi awamu ya tano kwa kuyalinda Mapinduzi uetu.

Ni imani yetu kwamba bila ya wao kuonyesha umakini, upendo na kufahamu mantiki na maana ya Mapinduzi, pengine yangedhoofika, kuchuja maadui wa uhuru wetu wengefaulu kuyazima.

Mheshimiwa Mgeni rasmi

Mimi sio mzungumzaji leo kazi yangu nikukaribisha wewe baada ya kuyapokea matembezi yetu uzungumze nasi vijana wako tulioko hapa na wananchi wanaotusikiliza kupitia redio na television kwa vile tukio hili linarushwa moja kwa moja (Mubashara)na vyombo kadhaa naomba kwa ufupi sana nigusie maeneo mawili matatu.

Januari 12 mwaka 1964 kama alivyotangulia kueleza Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM siku hiyo ndiyo siku halisi ya ukombozi kwa wananchi wanyonge wa Zanzibar ambao kwa miaka mingi walikandamizwa, kunyimwa haki huku wakidhibitiwa na makucha ya utawala wa kibwenyenye chini ya sultan wa Zanzibar na msururu wa vibaraka wake.

Kabla ya mwaka 1964 Waafrika wenyeji wa Zanzibar waliishi katika maisha duni na dhalili, walitengwa katika nchi yao wenyewe, hawakupewa haki wala fursa kama ilivyotokea baada ya Januari 12 mwaka 1964 pale bendera ya kikoloni iliposhushwa na kupandishwa bendera ya Zanzibar ambayo hadi sasa inaendelea kupepea.

Tumepeperusha bendera yenye rangi ya kijani, weusi na buluu na kuikataa kata kata bendera bandia iliokuwa ikiwakilisha ufalme wa Oman kwa hadaa ya kuwekwa alama ya karafu kama kiini macho. Bendera inayopepea hivi sasa haitashuka chini hadi kiama kinapotokea.

Kuendelea kupepea kwa bendera yetu na kuwepo kwa Serikali, na Rais kunajieleza kwa vitendo kuwa waafrika tuko makini katika kulinda uhuru wetu tunaamini hilo linawaumiza sana mawakala wa wapinga mapinduzi, kunawasokota matumbo na kuwakosesha raha kwa kuona Mapinduzi ya Zanzibar yakiendelea kuishi na kushamiri kwa kusonga mbele.

Lazima tufike mahali tuwe wakweli, tupende kujenga dhana ya uwazi, utayari na kutoa tahadhari pale tunapoviona viashiria hatarishi usoni mwetu au mambo yanapokuwa hayaendi kama inavyokusudiwa hususan wanapojitokeza watu miongoni mwetu ambao nyakati za alfajiri hujiita na kujigamba nao ni wana Mapinduzi, lakini unapofika usiku wa manane hugeuka na kuwa wapinga Mapinduzi.

Tunawataka wajirekebishe, wafuate taratibu, waheshimu sheria zilizotungwa na waache undumilakuwili kwa sababu wapo wanaoturamba visogo kwa kushirikiana na wapinzani wa mapinduzi huku wakiamini iko siku tutashindwa uchaguzi. Tunawakanya na kuwaasa, wakiendelea tutawasemu hadharani kwa ushahidi wa matendo yao.

Mheshimiwa mgeni rasmi.

Naomba nikumbushie jambo moja muhimu sana ambalo tuliliomba mbele ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein.

Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa mara nyingine tunakukumbusha kuhusu sanamu ya Jemedari Mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar kuwekwa juu ya jengo la mnara mpya wa kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar ulipo Muembe Kosonge.

Sisi Vijana wenu tunakiri Mheshimiwa Dk Shein ameandika historia ya aina yake kwa uamuzi wa Serikali yake kujenga mnara ule wa kumbukumbu ya Mapinduzi yetu, tungependa kuyaona majina ya wana mapinduzi 14 wa mstari wa mbele yakiandikwa mbele na kusomeka katika mnara ule.

Kwa kuwa viongozi wetu mnakabiliwa na majukumu mazito ya kiserikali tumeona ni vyema kuwakumbusha ama sisi Vijana wenu mturuhusu tukalihamishe sanamu la Mzee Karume kutoka pale Bwawani Hoteli na kuliweka juu ya mnara wetu pale Mwembekisonge.

Wenzetu upande wa Tanzania Bara wakati wakipata uhuru Disemba 9,1961, walipandisha mwenge wa uhuru juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro. Vijana wazalendo bado tunaamini kuwa kilichokufa mwaka 1972 ni kiwiliwili cha Mzee Karume, fikra, mawazo, busara na malengo yaliowekwa na Mzee wetu kwa kushirikiana na wenzake, hayajafa, hayatakufa ila yanatakiwa kuendelezwa kama ufanyavyo Dk Shein katika Serikali anayoiongoza.

Mheshimiwa Mgeni rasmi

Leo ni Januari 2017 mwaka huu Chama cha Mapinduzi na jumuiya zake kimekabiliwa na uchaguzi wa kuwapata viongozi watakaokivusha chama katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2019 Tanzania bara na uchaguzi mkuu 2020 panapo uhai.

Kwa upande wa UVCCM mimi ndio nakamilisha kipindi changu cha uongozi cha miaka mitano ndani ya jumuiya yetu pamoja na mafanikio na changamoto za hapa na pale ni jambo la kushukuru kuwa mimi nimedumu katika kipindi cha uongozi wangu.

Napenda kutumia hadhara hii kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu kabisa Mheshimiwa Dk Ali Mohamed Shein Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk, John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nawashukuru pia Ndugu Abdulrahman Omari Kinana Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Mheshimwa Majaliwa Kassim Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wewe mwenyewe Mheshimwa Balozi Seif Ali Iddi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mstaafu

Hakika leo ninaposimama kwa mara ya mwisho katika matembezi haya kuadhimisha Mapinduzi napata hisia kali za wema na mapenzi makubwa mliyonionesha na mliyoendelea kunionyesha katika uongozi wangu hasa katika tukio hili kubwa la kila mwaka, la kihistoria.

Namuomba mwenyezi Mungu azidi kuwapa nguvu na kuwafanyia wepesi katika kila jambo na awape umri mrefu

Ni imani yangu Mwenyekiti wa UVCCM ajae atasimamia vyema haya na nyinyi mkimunga mkono kama ilivyokuwa kwangu kwa minajili ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Makamu.

Pia napenda kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na Mama Asha Balozi Mke wa Makamu wa Pili wa Rais nakumbuka kila leo mara ya kwanza kufanya matembezi haya 2015 tuliyazindua Mkoa wa Kaskazini Pemba na vijana sisi tukatembea Pemba nzima na Unguja hakika mama zetu hawa walithubutu kuziacha familia zao na baba zetu kwa zaidi ya wiki mbili wakafuatana nasi Pemba tokea hatua za maandalizi hadi kukamilika matembezi tena wakitowa hadi akiba zao za mikobani ili vijana wao tufanikishe kazi ya Chama na waliendelea hivyo katika matembezi ya kila mwaka.

Namshukuru Mama Salma Kikwete na Mama Janet Magufuli nao kwa michango na misaada yao ya hali na mali kwetu vijana wenu katika kufanikisha mambo ya msingi ya kuimarisha chama chetu.

Nawashukuru Wajumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa, Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Maafisa wandamizi wote wa Chama na Serikali kwa kuwa nasi karibu katika miaka mitano mfululizo tukiandaa matembezi haya hatuna cha kuwalipa hakika mumeonesha na kudhihirisha uzalendo wenu kwa vitendo.

Nawashukuru sana vijana wenzangu jambo hili limekuwa ni kiunganishi na kianzio kizuri cha mahusiano, udugu, urafiki na huruma miongoni mwa vijana wa Unguja, Pemba na Mikoa mbali mbali ya Tanzania bara tokea mwaka 2013- 2017.

leo utashangaa wako vijana ambao hawajakosa hata mara moja kushiriki matembezi haya na wako wengine ukitaka kuwakosesha nafasi kwao ni ugomvi ni faraja ilioje kuona vijana wenzetu wamepata muamko katika mambo muhimu na nyeti ya kuimarisha na kuibua vuguvugu la uhai chama chao bila kujali malipo ya aina yoyote sambamba na kuhimili na kuvumilia changamoto mbali mbali wakiwa katika matembezi hadi tunakamilisha.

Vijana wenzagu tunawashukuru sana mumetupa moyo na mumekuwa mkitutia nguvu, ari na shime ya kuyaendeleza matembezi haya.

Mheshimiwa Makamu kama nilivosema leo ndio matembezi yangu ya mwisho kuadhimisha sherehe hizi za Mapinduzi inshallah miaka 54 ya Mapinduzi na sherehe za Mapinduzi zijazo tutakuwa na Mwenyekiti mwingine kwa mujibu wa kanuni yetu naomba univumilie nishukuru kwani asieshukuru kwa kidogo hata kikubwa hawezi shukuru.

Namshukuru Makamu Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Mboni Muhita na ninawashukuru sana wajumbe wangu wa kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa kwa kutanguliza maslahi mapana ya chama na Taifa mbele, siku moja wangalijaribu kupinga au kukataa jambo hili leo na siku zilizopita tusingalikuwa hapa ila nawashukuru kwa kusimama kidete kushauri, kushiriki na kuhakikisha kila mwaka matembezi haya yanafanikiwa.

Nawashukuru sana sana watendaji Katibu Mkuu UVCCM Taifa, Manaibu makatibu wakuu Bara na Zanzibar na kwenye jambo hili Naibu Katibu Mkuu Zanzibar shukrani za pekee kwa aliyetangulia na aliyepo tunafahamu kazi kubwa mnayokabiliana nayo katika kuandaa jambo hili. Wakuu wa Idara, Maafisa Makao Makuu na Afisi kuu Makatibu wa Mikoa na Wilaya nyote nawashukuru kwa heshima hii tulioipatia Jumuiya yetu .

Tumefanya kazi kubwa sana katika kuijenga jumuiya kwa mipango mbinu na mikakati mbali ya kuimarisha chama chetu nadhani kama kuna mtu atataka kujua yote tuliyoyafanya atasikia taarifa yetu ya utekelezaji wa mpango kazi wa UVCCM 2012- 2017 wakati wa mkutano mkuu wetu hapo baadae.

Umoja wa Vijana wa CCM tunatoa shukrani za pekee pia kwa wasanii wote pamoja na waandishi wa habari kwa kuwa pamoja nasi katika muda wote wa mihula mitano tukitekeleza jambo hili, mchango wenu una thamani kubwa kwa CCM na UVCCM.

Mheshimiwa Mgeni rasmihafla hii ni yako, vijana mbele yako na wananchi wanotusikiliza na kutuangalia wanakusubiri wewe uwahutubie, hivyo unisamehe kwa kutumia muda katika kuelezea kiini cha kutokea kwa Mapinduzi yetu matukufu ya mwaka 1964 kwa sababu binafsi naamini bila Mapinduzi leo nisingekuwa nimesimama mahali hapa niliposimama na kuhutubia.

Baada ya kusema maneno hayo naomba sasa kukukaribisha ili uzungumze na wananchi wa Tanzania nzima kupitia hafla hii kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar

Kidumu Chama Cha Mapinduzi
 
Back
Top Bottom