Hotuba ya Munishi kwa taifa la Tanzania | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hotuba ya Munishi kwa taifa la Tanzania

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by tindikalikali, May 7, 2011.

 1. tindikalikali

  tindikalikali JF-Expert Member

  #1
  May 7, 2011
  Joined: Jan 14, 2011
  Messages: 4,883
  Likes Received: 96
  Trophy Points: 135
  "Maovu ya CCM sasa basi" Mwinjilisti Faustin Munishi

  Wananchi wapendwa yangu ni machache sana leo. Maisha yetu na watoto wetu ni muhimu kuliko chama chochote cha siasa. Hakuna sababu ya kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa, wakati chama husika ndicho sababu ya kuharibika kwa maisha yetu ya sasa na baadaye. Nazungumza kuhusu CCM. Inasikitisha kuona kwamba wananchi Tanzania wameyazoea maovu ya CCM kiasi cha kukata tamaa ya kujikomboa.

  Kwao maovu wanayofanyiwa ni kawaida iliyozoeleka, na hawaoni sababu ya kufanya chochote kujitoa kwenye makucha ya CCM. Niko hapa kuwapa sababu za kuanza harakati za kujikomboa. Tunataka ukombozi kwa sababu ni haki yetu. Lazima tujikomboe kwani tusipofanya hivyo hakuna atakayefanya kwa ajili yetu. Maisha yetu ndiyo yanayoharibiwa, kwa hiyo hakuna mhadhiriwa nambari moja kama mwananchi wa Tanzania. CCM inawatesa Watanzania, wengine inawaua kosa lao ni kusema CCM itoke madarakani kwani sera zake zimeiharibu Tanzania.

  Maumivu Mateso Dhuluma Uonevu, na uchungu wote tunausikia, na mwisho wa kuvumilia umefika. Kifo mara nyingi huwa ndio mwamuzi kati ya uchungu na maumivu makali, huupumzisha mwili usiteseke tena. Tusipochukua hatua kwa kuogopa kuuawa, mateso na maumivu ya CCM yatafanya kile tunachokiogopa. Tayari yameua wengi, na wengi wako mbioni kufuatia mkondo huo.

  Swali langu kwenu ni hili: Mnataka CCM iue wangapi ndipo mseme imetosha liwalo na liwe? Kwangu naona imetosha, SASA BASI. Liwalo na liwe, tutachukua hatua za haraka kujikomboa. Je tuchukue hatua gani? Kwamba tumefikia mahali pa kujiuliza swali hilo, hiyo ni hatua nzuri ya mwanzo. Nani anayeweza kusema kwamba mateso ya CCM hayajamhadhiri kwa lolote? Atakuwa anasema uongo. Kila Mtanzania mdogo kwa mkubwa, ameonja maovu ya CCM.

  Siyo nia yangu kuamsha hisia zenu kinyume na CCM bali nia yangu ni kuwafanya muipende kiasi cha kuitoa madarakani. Kuitoa CCM ndani ya mawazo yenu ni rahisi kama ilivyoingia. Swali la kujiuliza ni Je CCM iliingizwaje kwenye mawazo na fikra zetu? Jibu lake ndiyo njia ya kuitoa na kuisahau. Sitaki tufanye kosa la kuitoa CCM kwa mbinu wanayoitumia kubaki madarakani. Tutakosea kwani tutakuwa tukifanya kile wanachokijua zaidi yetu. Kwa hiyo mawazo kwamba tutaitoa CCM kwa mtutu wa bunduki msahau.Tena hatuwezi kutumia chama kingine cha siasa kuitoa CCM, kwani hakutakuwepo na tofauti.

  TUTAITOA CCM MADARAKANI BILA SIASA
  " Siasa ni uongo, kwa hiyo hatuwezi kuutumia uongo kuwatoa waongo."

  Siasa ni uongo, kwa hiyo hatuwezi kuutumia uongo kuwatoa waongo. Ndugu wananchi, asiwadanganye mtu. Hakuna siasa nzuri. Wanasiasa wote duniani mbinu zao zinafanana tofauti ni mahali mbinu hizo zinapotumika. Kwa hiyo rais wa Amerika hana tofauti yeyote na wanasiasa wetu hapa Tanzania sema kiwango cha uongo wanachotumia wanasiasa wa nchi zilizoendelea kinazidi kile kinachotumiwa na wanasiasa wa nchi zinazojaribu kuendelea.

  Kifupi hakuna nchi iliyoendelea duniani.Kilichoendelea ni mbinu za kuwaibia wananchi walio wengi mali yao ambayo ni haki yao, na kuiingiza kwenye mkondo wa kisiasa ambao unalindwa na uongo pamoja na silaha kali. Kwa hiyo mbinu ya kwanza kuwatoa CCM madarakani ni kutambua kwamba wanasiasa wote duniani ni waongo. Pili ni kutokusikiliza uongo wao ambao hupeperushwa na vyombo vya habari kila siku. Ni vizuri mjue kwamba hakuna vyombo huru vya habari katika dunia inayoongozwa na siasa. Kwa hiyo someni habari magazetini, pia sikilizeni redio. Lakini mjue asilimia tisini ya yale mnayoona na kusikia kwenye vyombo vya habari ni takataka kama siyo uongo na mbinu za kuwafanya mnunue bidhaa. Kwa sababu wanasiasa wengi siyo waandishi wa habari, kazi hiyo hufanywa na wanataaluma hiyo kwa malipo.

  Kwa hiyo hamtakosea kama mtasema kwamba waandishi wa habari wameshirikiana na wanasiasa kuifikisha hali yetu kimaisha ilipo. Uzuri wa waandishi wa habari, ni kwamba wanaweza kirahisi kurudiwa na fahamu zao, na kuwageuka wanasiasa na kuungana na sauti ya wanainchi. Tatizo ni kwamba walikuwa hawajui kama mnajua. Wakijua kwamba nimewaambia na mbaya zaidi wajue kwamba sasa mnajua yale waliyowaficha muda mrefu, watajikomba kuwaumbua wanasiasa. Hapo tuwe tayari kusikia mengi. Watakapogeukana hiyo ni furaha tele upande wetu.Tutakuwa tumempata msaidizi katika vita yetu ya kuwatoa CCM madarakani.

  WANASIASA HUTUMIA VYOMBO VYA DOLA KUWANYANYASA WANANCHI "Kila inapobidi majeshi yote hutumika kulinda maslahi ya wanasiasa. "

  Siyo rahisi wanasiasa warudiwe na fahamu zao, hasa ukitilia maanani kwamba wamezoea ukubwa na kutaka kuabudiwa kama 'miungu' wadogo. Kwa hiyo watatumia kila mbinu kubaki madarakani. Mbinu wanayoijua zaidi ni ile ya kutumia vyombo vya dola kama polisi na majeshi yote ya angani nchi kavu na majini, bila kusahau vikosi vya siri ambavyo hutumiwa kuwanyamazisha wapinzani.

  KAZI IKO HAPA.

  Wananchi wapendwa sipendi kuwaficha niwaambie kibarua kilicho mbele yetu ni rahisi. Nitakosea sana nikifanya hivyo. Jukumu langu ni kuweka wazi mbele yenu kila pingamizi tutakalokutana nalo, na kuwaeleza mbinu na njia sahihi ya kupambana na adui yetu. Majeshi yote yameundwa na wananchi wa TANZANIA. Polisi kwa lengo la kulinda mali zetu wananchi, na majeshi yale mengine wanasema lengo lao ni kulinda mipaka ya nchi yetu.

  Hiyo ndiyo lugha wanayotumia wanasiasa kutuonyesha kwamba majeshi yako kwa ajili yetu wananchi kumbe ni kinyume chake. Kila inapobidi majeshi yote hutumika kulinda maslahi ya wanasiasa. Mnakumbuka yaliyowapata wananchi wa Zanzibar walipojaribu kuipinga CCM. Wananchi zaidi ya sabini walipoteza maisha yao, huku wengine wakikatwa viungo vya miili yao ili kuwafundisha adabu.

  Yaani watanzania wako tayari kuua wenzao kwa ajili ya wanasiasa. Hiyo ndio kazi iliyo mbele yetu. Mjue kuna watu walio tayari kuua kwa ajili ya CCM na viongozi wake. Na tayari walifanya hivyo mchana jua linawaka bila kuogopa kamera za TV. Inataka moyo, lakini msisahau nguvu iliyo katika KWELI. Ukweli utatuweka huru mbali na wanasiasa waongo. Kweli ni NENO la Mungu ambalo ndiyo silaha yetu yenye nguvu zote.

  TIINI MAMLAKA HATA CCM?
  "Tuna haki na uhuru wa kuikataa CCM, na Mungu aliyetupa hawezi kutunyanganya haki na uhuru huo. Ni mali yetu, aliyetupatia ni Mungu na tumeamua kutumia haki na uhuru huo kuikataa CCM ya wauaji. "

  Wacheni waje wakitumia silaha, sisi tutawakabili kwa NENO la Mungu. Kwa imani yote yawezekana kwa waaaminio. Imani yetu kwa Mungu tusikubali iyumbishwe na chochote. Siyo matisho ya CCM wala kejeli zao.Mara zote wananchi ndio wengi kuliko risasi zote CCM walizojilimbikizia. Sauti ya wengi ndiyo sauti ya Mungu.

  Tukisema kwa sauti kubwa kwamba 'CCM CHAMA CHA MAJAMBAZI HATUKITAKI,' hiyo ndiyo itakayokuwa sauti ya Mungu. Na hakuna awezaye kushindana na MUNGU. Tuna haki na uhuru wa kuikataa CCM, na Mungu hawezi kutunyanganya haki na uhuru huo. Ni mali yetu, aliyetupatia ni Mungu na tumeamua kutumia haki na uhuru huo kuikataa CCM ya wauaji. Watakaopingana na uamuzi wetu kuikataa CCM, hao ndio watakaokuwa wakipingana na agizo la Mungu. Ndiyo watakuwa wameasi mamlaka ya Mungu. Kwa hiyo lazima waitii mamlaka yetu wananchi, kwani hiyo ameiweka Mungu mwenyewe. CCM iliwekwa na mtu mmoja, ni sawa ikitolewa na watu.

  Walitudanganya kwamba wanafanya uchaguzi ili iwe kana kwamba iliwekwa na watu, lakini tumegundua janja yao.Maoni ya wengi hayajawahi kuheshimiwa katika uchaguzi wowote ule tuliowahi kuwa nao. Kwanza tulikuwa tukichagua nini kinyume cha nini? Uchaguzi lazima uwe kati ya Shetani na Mungu, na siyo kati ya shetani na mashetani. Chaguzi tulizowahi kuzifanya kabla ya vyama vingi vya siasa, zilikuwa kati ya Shetani na kivuli. Chaguzi tulizofanya wakati wa vyama vingi vya kisiasa, zimekuwa kati ya Shetani {CCM}na vijishetani {vyama vya upinzani} ambavyo navyo vitakua kumfikia Shetani mwenyewe. Sasa tunataka uchaguzi wa kweli. Tuchagua kati ya Shetani na Mungu. Duniani hakuna uchaguzi zaidi ya kuchagua MUNGU na Shetani. Hakuna kitu cha tatu wananchi msidanganyike.

  GIZA NA NURU
  " Msije mkanilaumu kwamba nilisema siasa ni dini ya shetani."

  Dunia imekuwa na historia ya kupenda giza kuliko NURU, ndio maana wengi wanapenda siasa ambayo ni giza nene. Nuru ya injili sasa inaangaza duniani kote. Inatufundisha kuikataa siasa ambayo hutumiwa na shetani kuyatekeleza malengo yake ya kuharibu, kuchinja na kuua. Msije mkanilaumu kwamba nilisema siasa ni dini ya shetani. Lakini hata kama ulimi wangu ungeteleza niseme hivyo, ningekuwa nimekosea nini? Je sasa nimesema hivyo? Hapana. Nilichosema ni kwamba siasa ni chombo anachotumia sana Shetani. Hatuwezi kumkataa Shetani na kuikubali SIASA chombo anachokitumia. Tumkatae jongoo na mti wake. Wananchi! Siasa ni mbaya na hilo mnalijua fika. Wengi mtaniuliza nini mbadala wa siasa? Jibu langu ni KWELI. Neno la Mungu ndiyo KWELI.

  UJAMAA NA UBEPARI
  "Ujamaa ulisikika mzuri masikioni, lakini kwa sababu aliouleta alikuwa Nyerere mwanasiasa muongo, kila kilichovutia hakikutekelezeka."

  Watu tofauti kwa nyakati tofauti wamekuwa na mawazo tofauti kuhusu mfumo gani unaofaa kumwongoza mwanadamu. Wengine waliufuata mfumo wa ukomunisti kama akina Nyerere, wakashindwa kabisa. Mbaya zaidi walitumia miaka zaidi ya 30 kuyajaribu mawazo yao ya ujamaa Tanzania. Matokeo yake yalikuwa kuiacha Tanzania ikiwa imeharibiwa na sera zao mbovu, na hata sasa hatuna sera kamili tunayoifuata.

  Tanzania siyo mabepari wala siyo wajamaa kama alivyotaka Nyerere. Sisemi ubepari ni bora kuliko ujamaa, kwani sera zote hizo ni za kisiasa. Kwangu zote ni mbovu kwani zinakosa KWELI ndani yake. Ujamaa ulisikika mzuri masikioni, lakini kwa sababu aliouleta alikuwa Nyerere mwanasiasa muongo, kila kilichovutia hakikutekelezeka. Badala ya aliyeanzisha kukiri kwamba alikuwa amesema uongo, alitumia uongo mkumbwa kuutetea uongo mdogo aliouanzisha. Miaka ikapita na tulichoambulia watanzania ni umaskini wa kutisha.

  Nyerere alitutaka tuamini kwamba dunia yote inapita kwenye matatizo kama yetu watanzania, na wakati huo huo polisi waliwakamata wananchi waliopatikana na sabuni, dawa za meno na mafuta ya kupikia kutoka Kenya. Ilikuwa ni sawa na kukamatwa na madawa ya kulevya. Wengi wakati huo tuilijiuliza: Ikiwa dunia yote ina mateso kama yetu, mbona hapa Kenya wao wanaogea sabuni? Tofauti na sisi tunaotumia maziwa ya mpapai kuogea? Tena mbona wenzetu wanatumia dawa za meno wakati Nyerere anaziita anasa? Kweli kuogea sabuni ya REXONA au kutumia dawa ya meno ya COLGET ni anasa? Nyerere mwanasiasa muongo alitutaka tuamini hivyo.

  Wengi walimuamini na mpaka leo hawataki makuu. Waliukubali umaskini, na hawataki kuchukua hatua zozote kupambana nao. Japo Nyerere alisema adui zetu ni umaskini ujinga na maradhi, alitufundisha kuwapenda na kuwakubali maadui hao. Nasikitika kusema kwamba kuna watu waliomwamini Nyerere kinyume cha Amin wa Uganda. Waliomwamini Nyerere walikosea sawa na waliomwamini Amin. Watu hao wawili walileta madhara kwa nchi zao, lakini ya Nyerere Tanzania yalizidi.

  Ninachotaka kusema ni kwamba mifumo yote ya siasa ilishindwa. Sasa tuufuate mfumo wa Injili ambao hauwezi kushindwa. Injili ni uwezo wa Mungu, sioni haya kusema Injili ndio mkombozi wa dunia. Itaikomboa dunia kutoka katika minyororo ya uongo ya wanasiasa. Lazima tuiamini Injili kama kweli tunataka ukombozi. Dunia ni ya Mungu na haiwezi kuongozwa kwa siasa za watu ambazo ni uongo. Dunia itaongozwa na KWELI ya neno la MUNGU.

  WANASIASA NA MFUMO WA BIASHARA NCHINI
  "Inasikitisha kuona wananchi ndani ya nchi yao wakiteseka, huku wanasiasa na wageni wachache wakimiliki njia zote kuu za uchumi."

  Duniani kuna vita nyingi na tetesi za vita. Yote hayo ni matunda ya wanasiasa. Shetani anawatumia kuua na kuharibu maisha ya watu. KWELI imekuja ili tuwe na uzima, kinyume na shetani aliyekuja kuua. Utajiri wa dunia uko mikononi mwa wanasiasa. Mnajua ni kwa nini? Ili utajiri huo utumike kununua kila wanachokihitaji. Nanyi wananchi ni moja ya bidhaa ambayo wanasiasa hupanga kuinunua. Mnanunuliwa wakati wa kura ili kutia saini chaguzi ambazo washindi hujulikana kabla ya siku ya kura.

  Hawataki mjiendeleze ili muwe rahisi kununuliwa. Ndio maana wengi wenu hamjiwezi kimaisha na hiyo haiwasumbui wanasiasa kwani wanapenda mbaki kama mlivyo ili wawatumie. Hata wale wanaojaribu kujipatia riziki zao za kila siku kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo, bado wanasiasa hawaachi wafanye hivyo. Kila siku tume ya jiji hupewa kazi ya kuusafisha mji, na wafanyabiashara ndogo ndogo ndio uchafu unaotakiwa kusafishwa mijini. Siyo ajabu kwani huo ni mpango kamili unaolenga kuwanufaisha wafanyibiashara waliounganishwa kisiasa. Hawa ndio wale ambao hupewa tenda za serikali ili wagawane mapato na wanasiasa.

  Kuna wengine wa asili ya kiasia ambao nao hupewa kumiliki maeneo yote muhimu ya kibiashara. Makubaliano ni kwamba mapato wayagawane na wanasiasa. Inasikitisha kuona wananchi ndani ya nchi yao wakiteseka, huku wanasiasa na wageni wachache wakimiliki njia zote kuu za uchumi. Hali hii haipaswi kuwa hivyo. Wananchi wanatakiwa wapewe uhuru wa kufanya biashara popote katika nchi yao. Udogo wa biashara usiwe ndio sababu ya kumsumbua mwananchi, kwani hata hizo biashara kubwa ziliaza zikiwa ndogo. Wananchi wanaoiamini KWELI wanatakiwa waruhusiwe kufanya chochote chema katika nchi yao.

  Hali hiyo ndio itakayochochea ubunifu utakaopelekea kugunduliwa kwa vitu vingi kwa ajili ya maisha ya kila siku ya mwanadamu. Ugunduzi huo ndio unaoweza kuinua uchumi wa nchi husika kinyume na nchi nyingine, kwani "akili ni nywele na kila mtu ana zake." Na wale wanaogundua vitu, wanapaswa kulipwa sawa sawa na ugunduzi wao. Hapo taifa litakuwa limejitengenezea wanasayansi wake, wanaoweza kuvumbua vitu ambayo wengine hawana, na wakiviitaji taifa linapata pesa za kigeni kuinua uchumi wa nchi.

  Sekta ya elimu nayo itakuwa imeboreshwa kwani elimu kwa watoto wetu itazingatia zaidi vitu tulivyogundua wenyewe, kinyume na elimu ya sasa ambayo misingi yake ni mengi yaliyofanywa na wengine, huku tukipima uwezo wetu katika kuyaiga. Ndiyo maana maisha ya waalimu katika nchi nyingi ni duni. Wanasiasa hufundishwa na waalimu, lakini kimaisha wametofautiana sana. Waalimu mishahara yao ni midogo sana kulinganisha na wanasiasa ambao kila kukicha hujiongezea mishahara na marupurupu mengi.

  Katika nchi ambayo inaongozwa na KWELI bila siasa, waalimu ndio wanaotakiwa kupata mshahara wa kuwatosha kumudu maisha yao kama siyo uliowazidi wanasiasa. Hata kama watawazidi wanasiasa kimshahara kuna ubaya gani? Hilo ni swali tu. Msije mkasema niliwaambia mishahara ya waalimu izidi ya kila mtu. Lakini waalimu ndio humfundisha kila mtu. Sasa inakuwaje kila mtu anampita mwalimu kimshahara? Hapo nimetoka maana naona maswali hayaishi kichwani mwangu. Mengine mtajijazia wenyewe.

  RAIS BILA WALINZI?
  Watalinda nini wakati KWELI inajilinda yenyewe?

  KWELI na uongo ni kama mafuta na maji. Huwezi kuvichanganya hata kama utajaribu kufanya hivyo. Kweli inajilinda yenyewe na haihitaji kulindwa na silaha kali. Uongo lazima ulindwe kwa kutumia silaha kali, kwani hawajui wale waliodanganywa wakierevuka watafanya nini. Ndio maana dunia nzima inafikiria kuhusu silaha kali kuliko chakula cha wanadamu wanaoikaa. Waangalie wanasiasa wanavyolindwa. Watu zaidi ya mia moja hawafanyi kitu kingine duniani ila kumlinda mwanasiasa.

  Naheshimu kila taaluma ya mtu, lakini siwezi kumshauri yeyote awe mlinzi wa mwanasiasa. Kwa nini ufe kwa ajili ya uongo ambao hukuusema? Tena kwa mshahara gani basi? Yaani wenzio wako ndani wanakula vinono nawe unaungua jua nje? Sawa ni kazi yako. Unaipenda. Sina la kuongeza. Lakini ikiwa mimi ndiye nitakayekuwa kiongozi katika nchi itakayokuwa ikiongozwa na KWELI bila siasa, basi sitaki walinzi. Watalinda nini wakati KWELI inajilinda yenyewe?

  Unamkumbuka mmoja wa wanafunzi wa Yesu aliyejaribu kufanya kazi ya kumlinda? Alikata sikio la mmoja wa askari waliokuwa wanamkamata Yesu. Aliambiwa aurudishe upanga wake kiunoni kwani YESU ni KWELI iliyotoka kwa Mungu na hakuhitaji kulindwa na mapanga au bunduki. Pesa wanazotumia wanasiasa kununulia silaha za kujilinda, zinatosha kumaliza baa la njaa duniani kote.

  Yaani nina maana kila mtu duniani anaweza kula milo mitatu kwa siku. Tena chakula kizuri. Lakini pesa zote wanatumia wanasiasa kununulia silaha kali za kujilinda na wale waliowadanganya. Mwisho wao umefika. KWELI itawatoa madarakani bila kutumia silaha. Ole wao. Silaha walizojiwekea watazifanyia nini? Mbinu za vita zimebadilika. Hatutatumia mbinu walizozizoea.

  Nguvu ya kweli ya INJILI itawakata makali yao. Injili ni NENO la Mungu ambaye ndiye KWELI yenyewe. Je wanasiasa watashindana, au kupigana na Mungu? Kila la kheri katika vita yao hiyo. Watatoweka mmoja baada ya mwengine. Hawatajua ilikuwaje, wala hawaruhusiwi kujua. Pesa na utajiri havitawasaidia wakati huo. KWELI haipimi uzito wa mtu kulingana na vitu alivyo navyo. Mtu ni mtu hata kama hana vitu. Mtu huunda vitu, lakini vitu haviwezi kuunda mtu. Vitu ni kwa ajili ya mtu, lakini siyo mtu kwa ajili ya vitu.

  WANASIASA HUTUMIA DINI KUTAWALA
  Makanisa mengi yameanzishwa na kufadhiliwa na wanasiasa kwa kwa lengo la kuyatumia kisiasa, wakati lugha yao ni kwamba chama na serikali havina dini.


  Dini ni imani kwa Mungu wakati siasa ni imani kwa watu. Zote mbili ni itikadi zinazohitaji watu kufanikisha malengo yao. Ndio maana nawataka watu wa dini zote tuungane pamoja kuitoa siasa madarakani. Suala kwamba dini gani itatawala hilo lisitusumbue kwa sasa. Muhimu ni wote tutambue kwamba wanasiasa wanatutumia vibaya. Baada ya kutambua hayo tuachane kabisa na siasa. Kitakachofuata ni kila dini inayowania uongozi kujitokeza hadharani na kutangaza nia yao ya kutaka kuongoza. Wananchi wa dini husika, pamoja na wale wasio na dini, bila kuwasahau wale wa dini nyingine watakaoamua kujiunga na dini yenye sera nzuri kutoka kwa Mungu, Watachagua dini gani iongoze kwa kipindi kilichozoeleka cha miaka mitano.

  Baada ya miaka mitano tutachaguana tena. Pamoja na kwamba kila dini itakuwa na katiba yake, lakini lazima tuwe na katiba moja ya pamoja. Nayo ni ile itakayozingatia Imani kwa Mungu ambayo ndilo lengo la kila dini. Pamoja na kwamba dini fulani itachukua uongozi kwa kipindi cha miaka mitano, bado kila dini itawakilishwa katika baraza la makuhani ambalo ndilo litakalohusika na kuhakikisha kwamba amri kumi za Mungu zinafuatwa kikamilifu. Kwa hiyo hofu kwamba kutatokea michafuko ya kidini msahau kabisa. Badala yake dini zote zitaingia katika ushirikiano ambao haujawahi kuonekana tangu kuumbwa ulimwengu. Bado kila dini itakuwa huru kuendelea kufanya mambo yake yenyewe, bila kuomba kibali kwa wanasiasa kama ilivyo sasa.

  Hakutakuwepo na makanisa ua misikiti inayodhaminiwa na serikali. Makanisa mengi yameanzishwa na kufadhiliwa na wanasiasa kwa kwa lengo la kuyatumia kisiasa wakati lugha yao ni kwamba chama na serikali havina dini. Mambo yako hivyo karibu kila dini. Inasikitisha kuona kwamba wengine wanafikia mahali pa kudanganya kwamba watu wamepona kwenye mikutano yao ya kidini, kumbe ni waongo. Tayari tumewangundua kuwa ni wapambe wa CCM. Wanalindwa kama wanasiasa na huku wanajiita maaskofu. Wanatembelea magari ya kifahari na huku waumini wao ni masikini wanaodanganywa kwamba wakitoa watabarikiwa. Tayari viongozi wa dini wanawasaidia wanasiasa katika kuendeleza ukandamizaji na uonevu kwa waumini wao, ili mradi tu waitwe ikulu na wapewe magari na pesa. Hawana tofauti na wanasiasa tunaotaka kuwatoa madarakani. Kweli ya Mungu ni taa. Ikiwamulika, matendo yao yataonekana na kila mtu. Hawa ndio watakaokwenda pamoja na wanasiasa wakati dini ya kweli itakapochukua madaraka.


  MAUAJI YA KISIASA SIRI YAFICHULIWA

  Wanasiasa kwa makusudi wameziharibu taasisi zote. Duniani taasisi zote hufanya kazi kwa ajili ya wanasiasa. Nchi zilizoendelea wameendelea katika kujaribu kuficho hilo lakini nchi zetu jambo hilo liko wazi. Kwamba wana mbinu kali za kulificha, haiwatofautishi na wenzao katika nchi zinazoendelea. Inabaki kwamba kila taasisi duniani inalinda maslahi ya wanasiasa kwanza. Mahakama mara nyingi zinaonekana kupindisha ukweli, hasa pale ambapo mwanasiasa anahusika. Hebu fikiri kuhusu gari lililotekwa nyara katikati ya mji.

  Watekaji wanamlazimisha mwenye gari kuliendesha kuelekea wanakotaka. Baada ya safari ya kama kilomita mbili hivi, wanaacha gari la kwanza baada ya kulizinga jingine kwa mbele. Mwanye gari la pili anapigwa risasi na kuuawa hapo hapo baada ya kisichojulikana kuendelea kati ya watekaji na yeye. Wanayaacha magari yote mawili hapo baada ya kumwamuru mwenye gari la tatu kutoka ndani ya gari lake na kuwapa funguo. Wanaondoka na gari huku wakiwaacha wenye magari wote mahali pamoja, lakini mmoja ni marehemu na mwingine amebaki bila gari.

  Baada ya dakika kama tano hivi, Polisi wanawasili mahali hapo. Wakiwa katika kuwahoji wenye magari wawili, waandishi wa habari wa magazeti TV na Redio wanawasili mahali pa tukio. Usijali wataulizana nini hapo, lakini sikiliza redio na utizame TV jioni, halafu usome magazeti asubuhi yake. Utakayemsikia akitajwa kwamba aliuawa na majambazi waliojaribu kumpora gari, ndiye aliyekuwa amelengwa na taaluma zote hizo. Yaani habari yenyewe itasomeka hivi. MAJAMBAZI WAMUUA BWANA XXXX Aliyekuwa mhubiri wa INJILI bwana XXXX amefariki dunia baada ya majambazi kumfyatulia risasi.

  Wakiongea katika sehemu ya tukio, bwana JJJJ na bwana SSSS walisema kwamba walishuhudia majambazi wakimfyatulia risasi bwana XXXX baada ya mvutano ulioonekana kama Bwana XXXX alikataa kuwapatia majamabzi fungua za gari lake. Wakisimulia saidi kisa hicho, walisema kwamba walisikia mlio wa risasi mara mbili, na baadaye majambazi walitoka kwenye gari la huyo aliyekuja kujulikana baadaye kama Bwana XXXX. Walimwamuru Bwana SSSS atoke kwenye gari lake na awape funguo. Alitii, na majambazi waliondoka na gari lake ambalo mpaka sasa halijapatikana. Kwa sababu vyombo vyote vya habari vimelipa uzito suala hilo kwenye kurasa zao za kwanza, wananchi wanaiamini hadithi hiyo. Ndiyo lengo lilikuwa ifanyike hivyo ili wananchi waaminishwe uongo. UKWELI wa mambo ni kwamba bwana XXXX alikuwa mlengwa kwenye sakata yote hiyo.

  Kuna mtu aliyejua kwamba atapitia barabara hiyo saa hizo baada ya kutafiti nyendo zake kwa zaidi ya miezi mitatu. Taasisi zilizotumika kuwadanganya wananchi nazo zilihusishwa wengine wakijua na wengine bila kujua. Walioporwa magari yao ndio ambao hawakujua nini kilichokuwa kikiendelea. Ilikuwa hivi: Bwana XXXX aliwaudhi wanasiasa kwa kujaribu kuwaambia kwamba wanasiasa hawawatendei mema wananchi walio wengi. Walipochukizwa naye wakaamua kwamba atauawa. Pesa nyingi zikatolewa kwa ajili ya kazi hiyo. Walitakiwa watu kutoka katika taasisi mbili nyeti. Polisi na vyombo vya habari vilitosha kukamilisha zoezi zima.

  Kachero mmoja wa polisi alitumika kuzijua nyendo zote za Bwana XXXX, halafu mkuu moja wa kituo cha polisi alitakiwa kuwatoa vijana ambao watafanya kama wafanyavyo majambazi. Na huyo huyo ndiye aliyetakiwa kuvipigia simu vyombo vya habari kuviarifu kuhusu tukio, na jitihada zao za kuwafukuza majambazi.

  Lengo likiwa kutekeleza mauaji ya kisiasa, na kuyafanya yaonekane kama ujambazi wa kawaida. Walikosea. Kwanza hakuna ujambazi wa kawaida. Kwamba kuna ujambazi hiyo inaonyesha kushindwa kwa wanasiasa kuwalinda wananchi pamoja na mali zao. Pili: Kwamba wanamuua mtu kwa sababu tu amewakosoa chama tawala CCM huo ni wendawazimu nambari ONE. Wananchi mfano huu unaonyesha jinsi wanasiasa wanavyoweza kuzitumia taasisi kuyaficha maovu yao. Hii ni siri iliyofichuliwa katika mijadala ya Internet huko BCSTIMES .COM baada ya siri hii kufichuliwa na mtu aliyejiita AISHA AIESHI. Unaweza kujisomea mwenyewe kisa hicho kwa KUBONYEZA HAPA. Kuna matukio mengi ya zamani na hivi karibuni yanayofanana kabisa na mfano huu. Mauaji ya watu zaidi ya sabini kule Zanzibar, Kifo cha SOKOINE aliyekuwa waziri mkuu wakati wa Nyerere. Kifo cha KOMBE aliyekuwa mkuu wa kikosi cha usalama wa taifa wakati wa Nyerere, na wengine wengi.

  SASA BASI INATOSHA

  Ndugu wananchi yangu yalikuwa hayo machache. Msimame imara, wala msikubali kuyumbishwa na hawa wanasiasa. Mkatae kabisa mbinu zao za kutaka kuendeleza maovu yao kwa kuachiana viti. Nyerere alituachia MKAPA ili alinde madhambi yake.Naye Mkapa anataka kutuachia sijui nani ili alinde madhambi yake. Watalindana mpaka lini? Mwisho wao umefika.Sasa tunataka dunia isiyo na kitu kinachoitwa SIASA.

  Wametudanganya vya kutosha, wakatuibia vya kutosha sasa tunataka KWELI ya neno la Mungu iongoze Tanzania. Mungu ni pendo na anaipenda Tanzania ndio maana amenituma mtumishi wake kuwaletea ujumbe huu. Msijali kufurukuta kwao kwani wangefanyaje nao wanakata roho? Watawapeleka kwenye madanguro yao kuwatesa lakini msikate tamaa. Watatumia kila mbinu ikiwepo ya kuwafungulia kesi za uongo, msijali kwani hayo yote hayana budi kuja. Nguvu ya dola ni ndogo sana ukilinganisha na nguvu ya wananchi wamoja.Umoja wetu na imani yetu kwa Mungu ndiyo silaha kubwa ambayo kila mmoja wetu lazima awe nayo.

  Watahangaika kujua nani anayetupa nguvu tulizo nazo, lakini jibu watakalolipata litawarudisha hatua mia tatu nyuma. Wataanzisha magazeti kwa lengo la kuueneza uongo wao lakini watagonga mawe kwani wananchi tumeyashitukia magazeti ya hivyo. Watatumia pesa walizoiba kwetu kutununua kwazo, nasi tutatumia pesa bila kuwaunga mkono.Pesa ni zetu. Zikirudishwa hatuachi. Tutazitumia. Tuanze mara moja zoezi la kuchoma moto kadi za vyama vya kisiasa. Sisi ni waumini wa dini na hiyo inatutosha. Hatuwezi kuamini katika dini mbili, yaani siasa na INJILI. Moja ni ya shetani na nyingine ni ya Mungu.Sisi tumeamua kuwa upande wa Mungu. Mungu hawezi kutuacha watoto wake tuteswe na siasa za yule mwovu.
   
 2. tindikalikali

  tindikalikali JF-Expert Member

  #2
  May 7, 2011
  Joined: Jan 14, 2011
  Messages: 4,883
  Likes Received: 96
  Trophy Points: 135
  Rais bila walinzi inawezekana?
   
 3. Gsana

  Gsana JF-Expert Member

  #3
  May 7, 2011
  Joined: Aug 28, 2010
  Messages: 4,387
  Likes Received: 348
  Trophy Points: 180
  Mada ingenoga sana ukiondoa maneno dini na injili. Maana hapa kuna watu wapenda mabadiliko lakini hawaiamini injili. Nakushukuru.
   
 4. Pukudu

  Pukudu JF-Expert Member

  #4
  May 7, 2011
  Joined: Jan 7, 2011
  Messages: 2,970
  Likes Received: 735
  Trophy Points: 280
  kwa sehemu nakubaliana na munishi kuhusu ubovu wa siasa na jinsi gani siasa inachangia ktk unyonyaji wa walio wengi. Siasa ni mfumo wa minority kuwakandamiza majority. L
  Na suluhisho la haya yote ni TRUTH. Lakini napingana naye vikali kwa kusema kuwa dini ni suluhisho ya haya yote, tukumbuke kuwa dini ni mfumo ambao ulipewa nguvu na watawala ili waweze kuwamobilize watu na kuwaletea ustaarabu ambao watu wanakuwa less resistant, na tena dini zenyewe ktk mfumo wake hazina tofauti na siasa coz zote ni kuamini on mere words na kuwa na imani kwa hao watu ambao waumini huamini kuwa ni sacred. Na hili hata wanaphilosophy waliona thats why Karl Marx alisema ''Religion is like opium to the poor'' mimi nasema dini na siasa zote ni ganja kwa maskini kwani anapokuwa katika nyumba za ibada na ktk mikusanyiko ya kisiasa wanasikia habari nzuri zinzaowapa abstract hope ni matumaini ambayo hayapo bayana, matumaini yasiyo tangible.
  Cha muhimu ni sisi wananchi kutaka mambo yafuatayo:-
  Mamlaka yatoke kwetu kwenda kwa viongozi i.e. Tudai katiba ambayo inatupa mamlaka ya kuamua mambo yetu wenyewe kwa utaratibu fulani na viongozi wawe wanatekeleza na kusimamia yale tunayotaka sio wanayoamua wao.
  Tuwe na sheria kali zitakazotoa adhabu kali ikiwemo kifo kwa viongozi ambao watakiuka matakwa na maslahi ya wananchi.
  Wananchi wenyewe tuwe wachapa kazi, tufanye kazi kwa bidii, tusiwe wabinafsi tupendane na tuwe na ushirikiano. Ubaguzi ni sumu kubwa na ambayo wanasiasa hutumia ili kuendelea kutukandamiza.
  Thats all and i stand to be corrected and educated where am astray
   
 5. only83

  only83 JF-Expert Member

  #5
  May 7, 2011
  Joined: Oct 15, 2010
  Messages: 5,252
  Likes Received: 445
  Trophy Points: 180
  ...............Huyu jamaa achague moja,injili au siasa....mawazo yake ni mazuri lakini tatizo ni mchanganyiko wake..ni hatari sana kuchanganya siasa na dini...inaweza kuleta maafa ya kutisha na kuhuzunisha...
   
 6. nsimba

  nsimba JF-Expert Member

  #6
  May 7, 2011
  Joined: Oct 7, 2010
  Messages: 785
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  du! Ujumbe mzito wenye falsafa mpya ya maisha na utawala wa nchi! Dini kama chama cha siasa; sera ni amri kumi za mungu; waongozaji ni makuhani wa dini zote! Du! hiiii nayo kali... haya ipo kwa great thinkers!!
   
 7. Pharaoh

  Pharaoh JF-Expert Member

  #7
  May 7, 2011
  Joined: Mar 18, 2011
  Messages: 843
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Kwa hiyo Sokoine aliuliwa na Nyerere? haiwezekani kwani ilibaki miezi michache apokee urais, halafu Nyerere amelia sana baada ya kupata taarifa ya ajali
   
 8. Pukudu

  Pukudu JF-Expert Member

  #8
  May 7, 2011
  Joined: Jan 7, 2011
  Messages: 2,970
  Likes Received: 735
  Trophy Points: 280
  Umesahau ule msemo unaosema kuwa mchawi ambaye ameua huwa analia zaidi kuliko mfiwa na hukaa mbele kwa kulia sana si kigezo mi nafkiri hii issue ya sokoine ili kuondoa utata
   
 9. BONGOLALA

  BONGOLALA JF-Expert Member

  #9
  May 7, 2011
  Joined: Sep 14, 2009
  Messages: 13,784
  Likes Received: 2,393
  Trophy Points: 280
  Aje Tanzania tupambane na huu utawala wa ccm,si yeye kukaa nairobi na familia yake sisi huku tunapambana!!!au anasubiri tukifanikiwa ndiyo aje kutaka madaraka?yeye mwenyewe alikimbia nchi yetu kutokana na ujambazi aliokua anaufanya!
   
 10. Horseshoe Arch

  Horseshoe Arch JF-Expert Member

  #10
  May 7, 2011
  Joined: Aug 10, 2009
  Messages: 11,230
  Likes Received: 4,951
  Trophy Points: 280
  Haijalishi mleta ujumbe so far unasomeka...nimepitia mkuu
   
 11. T

  Tikerra JF-Expert Member

  #11
  May 7, 2011
  Joined: Sep 3, 2008
  Messages: 1,704
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 0
  Walipowadanganya mkatenganisha dini na siasa ndipo walipo wamaliza.Ila sikio la kufa halisikii dawa.
   
 12. Mamushka

  Mamushka JF-Expert Member

  #12
  May 8, 2011
  Joined: Feb 17, 2010
  Messages: 1,609
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Hivi huyu jamaa bado yupo sio. Sijaskia nyimbo zake longi kishenzi nadhani anatengeneza mazingira ya kuja kugombea ubunge.
   
 13. Horseshoe Arch

  Horseshoe Arch JF-Expert Member

  #13
  May 8, 2011
  Joined: Aug 10, 2009
  Messages: 11,230
  Likes Received: 4,951
  Trophy Points: 280
  Yupo tu Nairobi anaongoza kundi la "Bwana"...
   
Loading...