Mwanahabari Huru
JF-Expert Member
- Mar 9, 2015
- 14,242
- 34,917
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI OFISI YA RAIS – UTUMISHI NA UTAWALA BORA, MHESHIMIWA RUTH HIYOB MOLLEL (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI (KRUB) KUHUSU UTEKELEZAJI WA MPANGO WA BAJETI MWAKA 2015/2016 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017
(Yanatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwa heshima kubwa napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwakunipa afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge hili Ili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais- Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuwa humu Bungeni, kukishukuru chama changu cha DEMOKRASIA NA MAENDELEO kwa kuniamini na kunipa fursa hii adhimu niliyopatiwa, pia nimshukuru Kiongozi wa Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa imani yake kwangu ya kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Nje ya Bunge kwa masuala yote yanayohusu Utumishi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Spika, Kwa upekee niwashukuru wabunge wenzangu wote kwa ushirikiano walionipa kila nilipohitaji na hatimae kufanikisha maandalizi ya Maoni haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Pia niishukuru familia yangu kwa uvumilivu na msaada wanaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu.
Mheshimiwa Spika, Na mwisho lakini si kwa umuhimu ni kwa wadau wote ambao wameshiriki kwa njia moja au nyingine katika kutoa ushauri au maoni yao binafsi au kupitia maandiko yao kwenye machapisho au mawasilishao mbalimbali.
2.0 UTAWALA BORA KATIKA UTUMISHI WA UMMA
2.1 Malalamiko kuhusu utendaji usiozingatia Utawala Bora katika Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Spika, sekta ya utumishi wa umma ni sekta inayotoa huduma katika jamii na ndio sekta ambayo kwa maana rahisi inayouza bidhaa inayotengenezwa na kuuzwa na Serikali.
Hivyo basi wale wanaotoa huduma hiyo wanaposhindwa kutoa huduma hiyo kwa viwango stahiki maana yake ni kwamba Serikali imeshindwa kukidhi matakwa na matarajio ya wananchi ambao ndio wateja wake.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kitabu cha mwongozo kilichotolewa na mwamvuli wa asasi za kiraia, zinazojihusisha na Utawala Bora pamoja na uwajibikaji, kimetoa tafsri ya neno Utawala kuwa ni matumizi ya mamlaka ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika kusimamia masuala ya nchi kwenye ngazi zote.
Aidha Utawala Bora ni matumizi ya mamlaka ambayo yanakuwa na uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu, usawa na unaofuata utawala wa sheria. Ili kutekeleza dhana ya utawala bora mambo yafuatayo lazima yazingatiwe:
Matumizi sahihi ya Dola na vyombo vyake
Matumizi mazuri ya rasilmali kwa faida ya wananchi
Matumizi mazuri ya madaraka na muda
Kujua na kutambua madaraka na mipaka yake kwa mujibu wa katiba na sheria
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka serikali hii ya awamu ya tano kujitazama na kujihoji kama inafuata misingi ya utawala bora katika utendaji kazi wake wa kila siku tangu ilipoingia madarakani ama la !
2.2 MATUMIZI MAZURI YA RASILIMALI.
2.2.1. Rasilimali watu
Mheshimiwa Spika Tangu awamu ya tano iingie madarakani, tumeshuhudia “Majipu Mengi yakitumbuliwa” ikiwa ni jitihada za kupiga vita rushwa na ufisadi, ajenda ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KRUB) na wananchi kwa ujumla kwa muda mrefu. Sambamba na hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametengua teuzi za makatibu Wakuu na Manaibu 24 kuaanzia tarehe 6 Aprili 2016, imechukua takriban miezi mitano (5) kabla ya viongozi hao kuelezwa kuhusu hatma yao. Baadhi wamestaafishwa kwa lazima na baadhi kwa kufutwa kwa nafasi za kazi, ijapokuwa nafasi hizo zimejazwa na wateule wengine.
Mheshimiwa Spika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzani, Rais anayo mamlaka ya kufukuza, kusimamisha na kutengua uteuzi wa wateule wake, pamoja na mamlaka hayo ana wajibu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo kuwapa haki zao baada ya kuwastaafisha kwa lazima.
Kwa kuwa wengi wao hawajatimiza miaka sitini (60) na baadhi hawajafika hata miaka hamsini (50), kwa kuwa hawakutenda kosa lolote na kwa kuwa wamepongezwa katika barua zao kwa kuitumikia Serikali vizuri, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri ifuatavyo;
Serikali iwalipe kifuta jasho au” golden handshake” kwa mujibu wa taratibu na uzoefu wa miaka iliyopita uliotumika kuwalipa watumishi waliostaafishwa kwa lazima na Serkali.
Serikali ijenge utumishi wa umma imara, endelevu na wenye kujiamini kwa kuwa ndio ingini ya maendeleo katika kutekeleza sera za Serkali iliyoko madarakani
Mheshimiwa Spika baada ya Mhe Rais, kuanza kutumbua majipu, mawaziri, naibu Mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nao wameanza kusimamisha watumishi tena wa ngazi za chini, bila kutafakari mamlaka waliyo nayo.
Haiwezekani, katika dhana ya utawala Bora ukamsimamisha kazi mkurugenzi, ukamuacha Mtendaji Mkuu wa shirika au Wizara husika. Kiongozi anayewajibishwa kwanza ni Mtendaji Mkuu kwa sababu ameshindwa kusimamia watumishi walio chini yake. Huu si utawala bora na inasikitisha, hatua hiyo inaleta hisia za uonevu na matumizi mabaya ya mamlaka.
Mheshimiwa Spika, tofauti na wanyama ambao wao hujeruhi kwa kujilinda, Binadamu ana hulka ya chuki, visasi na upendeleo na ndio maana zimewekwa sheria, kanuni na taratibu za kudhibiti hisia hizo ili haki itendeke. Rasilimali watu ndio nyenzo kubwa ya kuleta maendeleo katika nchi yoyote duniani. Wanahitaji kuwezeshwa kwa kupatiwa mazingira mazuri ya kazi, vitendea kazi, bajeti, mafunzo na kuthaminiwa ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, Aidha KRUB inaitaka Serikali kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopitishwa na Bunge lako tukufu ili haki itendeke kwa wote na kuepuka kesi za madai zinazoweza kuisababishia serikali hasara kubwa. Vile vile, wale wote watakaokutwa na hatia za ufisadi na rushwa wachukuliwe hatua za kinidhamu pamoja na kufilisiwa mali zao kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Mheshimiwa Spika, viongozi wa kisiasa nao,wanaoteuliwa wapate mafunzo ya utawala bora, uongozi na maadili, na wapitishwe katika mchakato wa uchunguzi ili kupata Viongozi wa Kisiasa wenye maadili na weledi katika nafasi zao kwa sababu viongozi wakisiasa ni kioo cha jamii, hivyo uadilifu wao ni muhimu ili kujenga imani ya wananchi kwa Serkali.
Mheshimiwa Spika, maslahi bora kwa watumishi, ni nyenzo muhimu inayomotisha watumishi kufanya kazi kwa bidii, bila bajeti ya kutosha kwa mwaka husika, malengo hayatafikiwa. KRUB inaishauri serikali kuchagua vipaumbele vichache na bajeti kubwa ikaelekezwa kwenye maeneo hayo, kuliko utamaduni uliozoeleka wa kutenga bajeti kidogo kidogo kwa kila eneo mwishowe miradi na utekelezaji wa shughuli zingine hutekelezwa nusu nusu bila kukamilika.
2.2.2 MKATABA WA MISINGI NA KANUNI ZA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BARANI AFRIKA WA MWAKA 2011 (THE AFRICAN CHARTER ON VALUES AND PRINCIPLES OF PUBLIC SERVICE AND ADMINISTRATION, 2011)
Mheshimiwa Spika ,itakumbukwa kuwa Bunge hili liliridhia mkataba wa misingi na kanuni za utumishi wa umma na utawala barani afrika wa mwaka 2011 tarehe 25 Machi, 2015
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 3(1) ya Mkataba huu inatambua “usawa wa watumiaji wote wa Utumishi wa Umma na Utawala.” Ibara ya 3(2) inakataza “… aina zote za ubaguzi kwa msingi wowote, ikiwa ni pamoja na asili ya kutoka, rangi, jinsia, ulemavu, dini, ukabila, msimamo wa kisiasa, uanachama wa chama cha wafanyakazi au vyama vingine halali.” Ibara ya 3(7) inahusu uhamasishaji na hifadhi ya haki za binadamu za ‘watumiaji’ na ‘Mawakala wa Utumishi wa Umma.’
Neno ‘watumiaji’ limetafsiriwa kwenye ibara ya 1 ya Mkataba kumaanisha “mtu yeyote wa asili au wa kisheria anayehitaji huduma ya utumishi wa umma.” Kwa upande wake, maneno ‘Mawakala wa Utumishi wa Umma’ yametafsiriwa kwenye ibara hiyo hiyo kuwa ni “mfanyakazi au mwajiriwa yeyote wa dola au wa taasisi zake, ikiwa ni pamoja na wale walioteuliwa au kuchaguliwa kuendesha shughuli kwa jina la, au kwa niaba ya, Dola, katika ngazi zake zote.”
Mheshimiwa Spika, Misingi iliyotajwa katika ibara ya 3 ya Mkataba huu imefafanuliwa kwa ufasaha mkubwa katika Sura ya IV ya Mkataba inayohusu ‘Haki za Mawakala wa Utumishi wa Umma.’ Hivyo, kwa mfano, ibara ya 14(1) inazitaka mamlaka za Utumishi wa Umma na Utawala kuendeleza usawa miongoni mwa mawakala wake. Ili kufikia lengo hilo, ibara ya 14(2) inaelekeza kwamba “Utumishi wa Umma na Utawala hautahamasisha au kuendeleza ubaguzi kwa misingi ya asili, rangi, jinsia, ulemavu, dini, ukabila, msimamo wa kisiasa au sababu nyingine yoyote.”
Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 15(1), “Mawakala wa Utumishi wa Umma watakuwa na uhuru wa maoni kwa kuzingatia hadhi yao kama watumishi wa umma.” Vile vile, kufuatana na masharti ya ibara ya 15(2), “Mawakala wa Utumishi wa Umma watakuwa na haki ya kuunda au kujiunga na mashirika, vyama vya wafanyakazi au makundi mengine ili kuendeleza na kulinda haki zao kwa mujibu wa sheria za nchi.” Muhimu zaidi, ibara ya 15(3) inatamka wazi: “Bila kujali sheria za nchi, uanachama au ukosefu wa uanachama katika chama cha siasa hautaathiri, kwa namna yoyote ile, utumishi (‘career’) wa mtumishi wa umma.”
Mheshimiwa Spika, Ni wazi, kwa mujibu wa masharti haya ya Mkataba huu tunaotakiwa kuupatia nguvu za kisheria katika nchi yetu kwa kuridhia Azimio hili, kwamba watumishi wote wa umma wa ngazi zote wana haki ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi pamoja na, inter alia, vyama vya siasa vyenye usajili halali kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Kwa mujibu wa ibara ya 34 ya Mkataba huu, Tanzania ilikuwa na haki ya kuweka masharti, yaani reservations - kwa lugha ya sheria za kimataifa – wakati wa kusaini Mkataba huu, badala yake haikufanya hivyo na iliusaini na kuridhiwa na Bunge .
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni , inaitaka serikali kulieleza Bunge hili ni kwanini imewafukuza kazi baadhi ya watumishi wa umma ambao waligombea nafasi mbalimbali za kisiasa kama vile ubunge wa Majimbo na Viti maalum ile hali ikijua wazi kuwa wanavunja mkataba wa kimataifa ambao waliusaini na kuridhiwa na Bunge hili?
3.0 WATUMISHI HEWA SERIKALINI
Mheshimiwa Spika, kuanzia tarehe 15 Machi, 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli, aliwaagiza Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania Bara kusimamia zoezi la kuhakiki watumishi wa umma katika Mikoa yao kwa lengo la kubaini wanaoitwa ‘watumishi hewa.
Mheshimiwa Spika, Hii sio mara ya kwanza kwa Serikali ya Tanzania kufanya uhakiki wa watumishi wa umma ili kuondoa watumishi hewa. Itakumbukwa kwamba, mwaka 1993 Serikali ilisimamisha kwa muda utaratibu wa kulipa mishahara ya watumishi wa umma kwa kuipitishia kwenye akaunti zao benki. Badala yake, Serikali ilihakiki watumishi wa umma kwa kuwalipa mishahara yao kupitia dirishani, yaani malipo ya moja kwa moja kwa watumishi husika.
Watumishi ambao hawakujitokeza kuchukua mishahara yao dirishani walihesabika kuwa ni ‘watumishi hewa’ na majina yao yaliondolewa katika ‘payroll.’ Hata hivyo uhakiki huo ulishindwa kuondoa tatizo la ‘watumishi hewa’ambalo liliendelea kuwa sugu katika utumishi wa umma.
Mheshimiwa Spika, Uhakiki mwingine wa watumishi wa umma ulifanyika mwaka 2006 na mwaka 2011.Jitihada za Serkali ya awamu ya nne nazo hazikufua dafu. Serikali iliendelea kupoteza mabilioni ya fedha kutokana na malipo ya mishahara na marupurupu ya watumishi hewa.
Aidha, kama sehemu ya jitihada za kuondoa tatizo hili, tangu miaka ya katikati ya tisini, Serikali ilianzisha mfumo wa taarifa za utumishi na malipo ya watumishi wa umma uitwao Lawson.
Chini ya mfumo huu, taarifa za watumishi wa umma ambao utumishi wao umekoma kwa sababu yoyote ile zinapoingizwa katika kumbukumbu za mahala pao pa kazi, hupelekwa moja kwa moja Hazina kwa ajili ya hatua zaidi kama vile kuwaondoa katika ‘payroll’ na kuandaa malipo yao ya pensheni, kiinua mgongo, n.k. Kwa sasa mfumo wa Lawson umepelekwa katika mikoa na halmashauri zote za wilaya katika Tanzania Bara, mfumo huu pia umeshindwa kuondoa tatizo la watumishi hewa.
Mheshimiwa Spika, Sababu kubwa ya kushindikana kutatuliwa kwa tatizo la watumishi hewa ni kukosekana kwa uadilifu katika mfumo mzima wa utumishi wa umma. Watumishi hewa ni tatizo la kutengenezwa kwa makusudi. Mabilioni yanayopotea kila mwaka kutokana na malipo ya watumishi hewa yanakwenda kwenye mifuko binafsi ya viongozi na watendaji hao.
Mheshimiwa Spika, Hawa ndio ambao wamehakikisha kuwa jitihada zote za nyuma za kupambana na tatizo hili hazifanikiwi. Na hawa ndio watakaohakikisha kuwa jitihada za sasa za Mhe Rais Magufuli zinakwama. Viongozi na watendaji hawa wa Serikali hawapo katika ngazi za chini za utumishi wa umma wilayani na mikoani peke yake. Wako katika ngazi zote katika mfumo mzima wa utumishi wa umma.
Mheshimiwa Spika, Ndio maana licha ya kelele na jitihada zote, licha ya taarifa rasmi za kila mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuonyesha ukubwa na upana wa tatizo hili, hakuna kiongozi wala mtendaji wa idara ya Serikali au taasisi zake yeyote ambaye amewajibishwa kutokana na idara au taasisi yake kukutwa imelipa mishahara ya watumishi hewa.
Mheshimiwa Spika, Kwa kadri tunavyofahamu, hakuna kiongozi au mtendaji wa Serikali au taasisi wa ngazi yoyote ambaye amewajibishwa kwa sababu ya kuwa na watumishi hewa. Aidha, zoezi la uhakiki limefanywa na wahusika wa tatizo lenyewe. Kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa, Wakuu wa Mikoa ndio wakuu wa utumishi wote wa umma katika mikoa yao.
Aidha, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Serikali za Mitaa ndio waajiri wa watumishi katika halmashauri zao. Kwa sababu hiyo, Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri wanahusika moja kwa moja na uwepo wa watumishi hewa katika mikoa na katika halmashauri za Serikali za mitaa. Na hawa ndio ambao wamepewa jukumu na Mhe. Rais Magufuli la kuwabaini watumishi hewa katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, Kwa kutoa taarifa zinazoonyesha uwepo wamaelfu ya watumishi hewa katika mikoa na halmashauri zao, viongozi na watendaji hawa sasa wamejitia hatiani kwa kuonyesha kuhusika kwao na tatizo hili. Tunasubiri kuona hatua zitakazochukuliwa na Mhe Rais Magufuli dhidi ya Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa halmashauri ambao, kwa makusudi au kwa uzembe wao, wamesababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika mikoa na halmashauri zao.
Mheshimiwa Spika, Lipo tatizo la pili ambalo limechangia kuwepo au kukua kwa tatizo la watumishi hewa katika utumishi wa umma. Tatizo hilo ni udhaifu mkubwa wa Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ndio Tume Rekebu yenye jukumu la kuhakiki raslimali watu katika utumishi wote wa umma. Kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizotolewa na Tume hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa hivi karibuni, Tume hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa yanayokwamisha utendaji kazi wake.
Kwa mfano, Tume hiyo haina watumishi wa kada mbali mbali, vitendea kazi vya aina mbali mbali kama vile magari, kompyuta na vifaa vingine vya ofisi. Na katika mwaka huu wa fedha, Tume ya Utumishi wa Umma imepatiwa 9.3% ya fedha iliyotengwa kwenye bajeti kwa ajili yake. Katika mazingira haya, Tume hiyo imeshindwa kabisa kutekeleza majukumu ya kuhakiki watumishi wa umma katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu. Kama kweli tunamaanisha kupambana na tatizo la watumishi hewa serikalini tunataka kuona fedha za kutosha zinatengwa kwa ajili ya tume hii.
Mheshimiwa Spika, Tatizo la tatu ambalo limechangia kuwepo au kuongezeka kwa watumishi hewa ni kutokuwepo kwa mfumo mmoja wa rasilimali watu unaojumuisha na kuunganisha mifumo mingine yote. Kwa mfano, kwa utaratibu wa sasa, mfumo wa kusajili uzazi na vifo uliopo chini ya RITA haujaunganishwa na mfumo wa utumishi wa umma wala na mifumo ya hifadhi ya jamii kama vile NSSF, LAPF, PSPF, n.k.
Kwa sababu ya mifumo hiyo kuwa inajitegemea, yaani ‘stand-alone systems’, taarifa zinazoingizwa katika mfumo mmoja hazipelekwi katika mifumo mingine. Kwa mfano, taarifa za vifo zinazotolewa na RITA haziingizwi katika mifumo ya utumishi wa umma wala ya hifadhi ya jamii ili majina ya wahusika yaweze kuondolewa katika ‘payroll’ na orodha za malipo ya pensheni au kiinua mgongo. Matokeo yake ni kuwepo kwa watumishi hewa, yaani watumishi ambao wameshafariki dunia lakini taarifa zao hazijapelekwa kunakohusika na wanaendelea kulipwa mishahara na Serikali.
Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inaitaka serikali kama kweli iko ‘serious’ katika kupambana na tatizo hili la watumishi hewa ichukue hatua zifuatazo ili kulimaliza tatizo hili kama ifuatavyo;
Wakurugenzi Watendaji na Makatibu Tawala wa mikoa waliosababisha watumishi hewa wakati mfumo wa kuwaondoa upo, wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Tume ya Utumishi wa Umma wapewa watumishi wa kutosha, magari na vitendea kazi ili watekeleze jukumu lao la kuhakiki watumishi wa Umma na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Serikali iunganishe mifumo ya rasilmali watu inayojitegemea “Stand alone systems”. Namba ya kitambulisho cha taifa iunganishwe na mfumo wa vizazi na vifo, mfumo wa malipo serkalini, mfumo wa malipo ya pensheni, mfumo wa mlipa kodi nk. Hivyo mtumishi anapofariki, kustaafu au kuacha kazi mfumo wa Lawson nilioutaja hapo juu unamwondoa mara moja katika orodha ya watumishi wa Serkali.
4.0 KUIMARISHA TAASISI ZA UTAWALA BORA
4.1 Taasisi ya Kudhibiti na kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Mheshimiwa Spika ,Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa ili mapambano dhidi ya Rushwa na Ufisadi nchini yaweze kuendelea kwa kasi ni lazima TAKUKURU iimarishwe kwa kupatiwa rasilimali watu na bajeti ya kutosha ili kutekeleza majukumu yake. Aidha , ni rai yetu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hii muhimu na nyeti apewe uhuru na mamlaka kamili ili awe na Mamlaka ya kutekeleza majukumu yake kwa Uhuru bila ya kuingiliwa na mamlaka yoyote ile .
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaona kuwa ni wakati muafaka sasa ukaletwa mswada wa sheria hapa Bungeni ili kumpa Mamlaka Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kufungua kesi mahakamani mara baada ya uchunguzi wake kukamilika badala ya hali ya sasa ambapo ni mpaka aombe kibali kutoka kwa DPP na tumeshuhudia kuwa DPP amekuwa mzito kutoa vibali hivyo na badala yake TAKUKURU inaonekana imeshindwa kupambana na Rushwa na Ufisadi Nchini.
Mheshimiwa Spika, ni jambo la ajabu sana kusikia kuwa eti Serikali imewazuia watumishi wa TAKUKURU kwenda masomoni nje ya nchi kwa kigezo kuwa inabana matumizi. Serikali inapaswa kuelewa kuwa wala rushwa na watoa rushwa kila mwaka wanabadili mbinu zao na hivyo ili uweze kukabiliana nao huna budi kuwa na watumishi wenye weledi wa kutosha katika Nyanja hiyo na njia pekee ya kuwa na watumishi wa aina hiyo ni kuwaongezea ujuzi watumishi kwa kuwapeleka masomoni ndani na nje ya nchi .
4.2 Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma
Mheshimiwa Spika, tume hii ipo kwa mujibu wa Katiba na sheria zetu na ni wajibu kwa Viongozi wote kutangaza mali zao kwa wakati, kwa mujibu wa sherai, hata hivyo baadhi ya viongozi huchelewa kutangaza mali zao na wakati mwingine baada ya kukumbushwa mara mara, vile vile wanapotoka madarakani ni wachache sana wanaotangaza mali zao .
Mheshimiwa Spika, Tume hii ina watendaji wachache sana na imepewa jukumu la kufuatilia taarifa za mali na madeni ya watumishi wa umma na viongozi wa kisiasa kuanzia ngazi ya juu hadi kwa Madiwani , majukumu haya ni makubwa sana kwa Tume ambayo haina ofisi nchi nzima na hivyo kupelekea kushindwa kuyamudu majukumu yake vyema kutokana na ukubwa wa kazi husika.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inashauri kuwa ili tume hii iweze kuyamudu vyema majukumu yake ni bora sasa ikawezeshwa kufungua ofisi kila mkoa na kuajiri watumishi ambao watakuwa na wajibu wa kushughulikia fomu za Madiwani na watumishi wengine wa Halimashauri ili Tume ikabakia na majukumu ya kushughulikia watumishi wa umma ngazi ya Kitaifa pamoja na Wabunge.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaishauri kuwa Mali na Madeni ya Viongozi itangazwe kwa uwazi wakati viongozi wanapoingia madarakani na wakati Viongozi wanapotoka madarakani watangaze kwa uwazi tena mali na madeni yao ili kuwapa wananchi fursa ya kupima kama kiongozi husika ametumia madaraka yake kujilimbikizia mali.
5.0 MGAWANYO WA MAENEO YA KIUTAWALA
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 2(2) imeweka bayana mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kuigawa nchi katika maeneo ya kiutawala, inasomeka ‘Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar .Rais aweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika Mikoa, Wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge’
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwa na utaratibu ambao umeshamiri kwa kasi wa kugawa maeneo mbalimbali ya kiutawala nchini ikiwa ni pamoja na Vijiji, Kata, Wilaya na Mikoa. Aidha ugawaji huo unajenga utamaduni kwa wananchi kutaka maeneo yao yaendelee kugawanywa mara kwa mara na serikali.
Mheshimiwa Spika, wakati nchi yetu inajipatia uhuru kulikuwa na Majimbo 10 ambayo yalirithiwa toka kwa Mkoloni. Kutokana na mamlaka aliyokuwa nayo Rais Nyerere mwaka 1966 alianzisha Mikoa 15, ambapo kwa sasa idadi ya Mikoa ni zaidi ya nusu ya Mikoa aliyoanzisha Rais wa kwanza wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, hoja hapa sio tu kuanzisha Mikoa na maeneo mengine ya utawala bali ni namna serikali inavyongeza matumizi ya masuala ya kiutawala badala ya mapato hayo kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo. Hii inathibitishwa na Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji vipya vingi vilivyoanzishwa bado havijapata huduma muhimu kwa ajili ya kuanza kazi ikiwemo ukosefu wa ofisi.
Mheshimiwa Spika, utaratibu huu kwa baadhi ya maeneo umeanza kuleta viashiria vya ukabila pamoja na migogoro ya mipaka na mgawanyo wa rasilimali, hili si jambo la kupuuzwa hata kidogo. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kusitisha zoezi la kugawa maeneo ya utawala na badala yake pawepo na utaratibu mwingine ambao utahakikisha maeneo hayo yakigawanywa kiutawala kuwe na mpango wa namna ya kupata mapato ya kujiendesha kuliko hali ilivyo sasa ya kutegemea serikali kuu na fedha nyingi kutumika kulipa mishahara ya watumishi na kujenga miundombinu mipya badala ya kutumika katika miradi ya Maendeleo.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni , inaishauri serikali ya awamu ya tano katika kutekeleza kwa vitendo mpango wa kuthibiti matumizi makubwa ya uendeshaji wa serikali iamue kusitisha utaratibu huu wa kuigawa nchi katika vipande vidogovidogo vya utawala kwani hii ni kuongeza zaidi gharama za uendeshaji wa serikali na mapato kidogo yanayokusanywa yaelekezwe katika kuendeleza miradi ya Maendeleo.
6.0 MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII (TASAF)
Mheshimiwa Spika , kwa mujibu wa randama ya wizara uk 19 kifungu cha 2.4.3 (ii) kinasomeka kama ifuatavyo, nanukuu “kiasi cha shilingi bilioni 275.9 zimehawilishwa kwa kaya maskini milioni 1.1 kama ruzuku kufikia mwezi Machi 2016 .Ruzuku hii ilihawilishwa kwa kaya zote masikini zilizoandikishwa Tanzania Bara pamoja na Zanzibar”
Mheshimiwa Spika, fedha hizi ni nyingi sana kama zingetumika vizuri na kwa ufanisi. Kwa kitendo cha kuzigawa kwenye kaya masikini tena kwa mfumo wa fedha taslimu kamwe haziwezi kuondoa kiwango cha umaskini kwenye kaya hizo kwani mfumo huo sio endelevu hata kidogo.Ukitazama mgawanyo wa ruzuku hiyo utaona wazi ya kuwa kila kaya ilipata kiasi cha shilingi 250,818 au kila mwanakaya alipata kiasi cha shilingi 55,180.Hivi kweli kiasi cha shilingi 55,818 kwa mwaka kinaweza kumuondolewa mwananchi umasikini?
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya ukaguzi maalum wa ufanisi katika mfuko huu na kuangalia kama kuendelea kugawa fedha badala ya kuanzisha miradi kunaweza kuwaondolea wananchi umaskini wa kutupwa. Maana zipo tuhuma kuwa wapo baadhi ya watumishi wa Halimashauri ambao huwaweka ndugu na jamaa zao kama watu masikini ile hali sio na masikini halisi wakiachwa.
7.0 MAPITIO YA BAJETI NA MATUMIZI YA 2015/16 NA BAJETI YA 2016/17
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais Menejimenti Utumishi na Utawala bora, iliidhinishiwa na Bunge lako Tukufu 37,717,620,000 mwaka 2015/16 kwa matumizi ya kawaida na kwa mwaka wa fedha 2016/17 wameomba kuidhinishiwa 30,503,648,814 ikiwa ni punguzo la 7,213,971,186.
Kwa upande wa bajeti ya maendeleo 2015/16 waliidhinishiwa 6,259,944,000 na mwaka huu 2016/17 wameomba jumla ya 7,500,0000,000. Kutokana na unyeti wa Ofisi hii ambayo ndio inasimamia uendeshaji wa Serikali, bajeti iliyotengwa ni finyu sana, hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalishauri Bunge kuongeza Bajeti hii ili zipatikane fedha za kutosha na ziweze kuelekezwa Zaidi kwenye kuimarisha mifumo ya utendaji serikalini ili taifa liweze kupiga hatua ya kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha unaoisha, Ofisi ya Rais fungu 30, ziliidhinishwa jumla ya shilingi 310,329,016,000/- kati ya hizo shilingi 3,833,959,000 zilikuwa ni mishahara na shilingi 306,495,057,000/- zilikuwa ni matumizi mengineyo kwa ajili ya idara ya utawala (usalama wa taifa, baraza la usalama la taifa, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, mkurabita, taasisi ya uongozi n.k)
Kwa mwaka huu wa bajeti 2016/17 fedha zinazoombwa ni jumla ya shilingi 354,637,917,000/-. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa vitengo na idara na watumishi bado ni wale wale, hivyo mfano wa kubana matumizi ulitakiwa uonekane kutoka kwa Kiongozi. Lakini Bajeti ya matumizi ya kawaida badala ya kupungua imeongezeka kwa kulinganisha na ile ya mwaka jana. Ni bora viongozi tutembee katika yale tunayoyaongea.
7.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha, kama nilivyoainisha hapo juu, kusimamisha/kufukuza watumishi sio mwarobaini wa kujenga utumishi wa umma uliotukuka. Mifumo na miundo ya utawala bora iimarishwe na kusimamiwa, hatua zilizoanza kuchukuliwa kudhibiti matumizi holela ya kodi za wananchi uendelee na wanokiuka wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, ikibidi mali zao zitaifishwe kwa mujibu wa sheria. Mipaka ya madaraka izingatiwe ili haki itendeke. Viongozi wa kisiasa wawe mstari wa mbele katika uadilifu,uwajibikaji, uwazi na uzalendo, na watumishi wengine wataiga.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaendelea kuweka msisitizo wa Hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni wa kuitaka Serikali iheshimu Katiba ya nchi na Sheria za nchi katika kutekeleza majukumu yake. Katika hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni imebainika kwamba Serikali hii inaongozwa kiholela bila kufuata instrument inayoweka mwongozo wa muundo wa wizara na kazi zake jambo linalopelekea kila waziri kutekeleza majukumu yake kwa kutumia utashi na uwezo binafsi wa kufikiri; imebainika kuwa Serikali imevunja ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwanyima wananchi haki ya kupata habari kwa kukataza vyombo vya habari vya umma na vile vya binafsi kurusha moja kwa moja mjadala wa Bajeti Bungeni; imeabinika vilevile kwamba Serikali imevunja kifungu cha 41(1) cha sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 na kifungu cha 18(3) na (4) cha Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 ambavyo kwa pamoja vinaitaka Serikali kuleta Bungeni nyongeza ya bajeti ili kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha zilizoidhinishwa awali hazikutosha kutekeleza majukumu yaliyokusudiwa, lakini Serikali mara kadhaa imefanya matumizi ya fedha za umma nje ya fedha zilizoidhinishwa na bunge bila kuomba bunge liidhinishe bajeti ya nyongeza.
Hivyo basi, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa hii ni dharau kubwa kwa bunge na uvunjaji wa ibara ya 63(2) na 63 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayolipa Bunge mamlaka ya kuisimamia na kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni naomba kuwasilisha.
RUTH HIYOB MOLLEL (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI-OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA