Hotuba ya kuaga ya Baba wa Taifa ukumbi wa diamond 1985

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,915
30,259
SIKU MWALIMU NYERERE ALIPOTOA HOTUBA YAKE YA KUWAAGA WATANZANIA YA NOVEMBA 5 MWAKA,1985 WAKATI ANASTAAFU URAIS KWA WAZEE WA DAR ES SALAAM.

‘"Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam; na wazee wa Tanzania. Nimeanza nao mapema sana; mapema kweli. Nilirudi kutoka masomoni, Uingereza Oktoba 1952 – miaka 33 nyuma. Wakati huo nikiwa kijana mdogo wa miaka thelathini na kidogo hivi.

Niliporudi nikakubaliana na wamisionari hapo Pugu (sekondari), nifundishe shuleni kwao. Lakini nikiwa shuleni – Chuo Kikuu – nilijua. Niliishaamua kwamba maisha yangu yatakuwa ya siasa. Niliamua hivyo: Nitafundisha kwa muda wa miaka mitatu, nione hali inavyokwenda na kuzoeana na wenzangu kabla ya kuanza maisha ya siasa.

Niliporejea nchini hapo Oktoba, nikaenda Butiama. Januari nikarudi Dar es Salaam. Nikaanza kazi. Nikataka kujua habari za African Association. Mzee Mwangosi anakumbuka. Yeye ndiye aliniambia habari za African Association. Aliisha niambia habari hizo tangu nikiwa Makerere – Chuo Kikuu – nikiwa mwanafunzi.
Pale, mimi na wanafunzi wenzangu tulikuwa tumeanzisha chama kinachoitwa Tanganyika African Welfare Association (TAWA) cha wanafunzi wa Tanganyika; mimi nikiwa katibu wao. Hapa tukaona mambo yanakwenda vizuri kidogo.

Tukaona kwanini TAWA iwe ya wanafunzi peke yao na siyo Tanganyika nzima. Kwa hiyo nikawaandikia baadhi ya watu Tanganyika. Nikasema, jamani ee, tumeanzisha chama, kwanini msianzishe huko matawi ya chama hicho?

Ndugu Mwangosi akapata barua hiyo. Alikuwa miongoni mwa waliopata barua hiyo. Akaniandikia – nikiwa Makerere – akasema: wewe kwanini unataka kuanzisha chama kipya? Kipo chama. Kipo chama cha TAA (Tanganyika African Association).

Kwa hiyo la maana siyo kuanzisha matawi, maana chama kipo na matawi yameenea; la maana ni kwamba hicho chama chenu mfute, na muanzishe tawi la Tanganyika African Association.

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Kwa hiyo mimi nikawa katibu wa katawi ka TAA hapo Makerere. Niliporudi Tabora na kuanza kufundisha pale St. Marys (sasa inaitwa Sekondari ya Milambo), nikachaguliwa katibu wa TAA wa jimbo ambalo makao yake makuu yalikuwa Tabora. Ulipofanyika mkutano wa TAA mjini Dar es Salaam, nilihudhuria nikiwa mjumbe kutoka Tabora.

Kwa hiyo nilikuwa naijua Tanganyika African Association. Nilipokuwa ninaondoka kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa nimeishaonja shughuli za TAA. Sasa niliporudi, baada ya kukaa Pugu siku chache, nikaja mjini Dar es Salaam. Nikauliza nani wanaongoza TAA?Nikaambiwa kuna jamaa mmoja anaitwa Abdul Sykes. Sasa ni marehemu. Abdul ndiye alikuwa katibu wakati huo.

Nilipelekwa na Kasela Bantu - ambaye naye aliteleza-teleza na hatunaye hapa (kwenye mkutano). Kasela Bantu alikuwa mwalimu mwenzangu. Tulifundisha pamoja Milambo. Nilipokuja Dar es Salaam, nikakuta anafanya kazi Redio (Tanganyika Broadcasting Corporation). Ni Kasela Bantu aliyenipeleka kwa Sykes.
Wakati huo mambo yalikuwa yanasinzia kidogo. Kwa muda mfupi mwaka ule, tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari. Kufika Aprili, TAA ikafufuka. Tukafanya mkutano hapo Anautouglou. Kwenye mkutano huu wakanichagua kuwa Rais wao – wa TAA.

Ninasema yote haya kwa shukrani kwa wazee. Jamaa hawa walikuwa watu wazima wa Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo Mzanaki, na Kiswahili changu si kizuri sana – cha matatizo.

Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni. Muda mfupi tu jamaa hawa wakaniamini haraka sana – katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais wa TAA. Hapo ndipo nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa madhumuni hasa ya shabaha ya kuleta uhuru.

Baada ya miezi 13, hapo 1954, tukaanzisha TANU. Jina hili lilipendekezwa na akina Abdul Sykes. Walikuwa wamelifikiria tangu zamani, walipokuwa askari vitani huko Burma (Vita vya Pili).

Miezi minne baada ya kuanza kazi Pugu nikawa ninakuja Dar es Salaam, kwa mguu; kila Jumamosi. Baadaye wazee wakanipa baiskeli nikawa ninakuja mjini kukutana na wenzangu; kufanya mikutano.

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Wazee wakaniamini upesi sana. Tukawa na uhusiano mkubwa sana. Wadogo wenzangu wengine walikuwa Abdul Sykes, Abass Sykes (mdogo wake), Dosa Aziz – waliokuwa wengi ni wazee.

Katika kuhutubia mikutano yangu, nilikuwa nikisema: Wazee na Ndugu zangu! Wazee hasa ndio walikuwa na mikutano ya awali ya TAA na TANU. Walikuwa na msimamo wa hali ya juu kabisa! Hawakuyumba hata kidogo! Vijana walikuwa na mashaka. Wengine walikuwa na vikazi vyao, waliogopa kuvipoteza.

Nalo jambo lenyewe ni la hatari – la kuzungumzia uhuru! Unaweza ukakosa kazi; na wapo waliopoteza kazi; wengine wakaacha kazi. Akina Rashid (Kawawa) waliona watoke kwenye shughuli hizo tuje tuungane katika chama.

Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye wa nchi nzima, wakatuunga mkono, na kila nilipokwenda, watu wa kwanza walionielewa, walikuwa wazee.
Nilikwenda Songea mwaka 1955 mara baada ya kujiuzulu. Huko wazee walinipokea na kunielewa. Nilianza safari za kuitembelea Tanganyika nzima. Nilikwenda Mbeya. Mkutano wangu niliufanya na wazee; kikundi kidogo cha wazee, ndani ya nyumba ya mtu.

Kwa mkutano huu wa Mbeya, wazee wakauliza: Unatafuta nini? Nikawaambia natafuta uhuru. Wale wazee, kwa sababu ya vita vya Maji Maji, na wanakumbuka, kabisa, wakaona mimi ninatafuta jambo la hatari. Tulifanya mkutano wa makini kweli. Wakauliza: Wewe unawezaje kuleta uhuru? Wewe una njia gani kudai uhuru na usitiwe kitanzi na Waingereza?

Tulielezana. Nikawaambia ninyi wazee, Waingereza wanawadanganya, Waingereza wametumwa na ule Umoja wa Mataifa uliokufa (League of Nations), waje kuishika Tanganyika kwa muda tu; watusaidie, na wakati tutakapokuwa tayari, watuachie tukajitawale.

Waingereza wanafanya ujanja; hawasemi. Vita vimekwisha (vya Pili) na Umoja wa Mataifa mwingine – mpya (United Nations Organisation – UNO) umewakabidhi Tanganyika kwa shabaha ileile. Sisi siyo koloni lao. Wamepewa dhamana tu.

Kwa hiyo nikawaambia wazee, hakuna haja ya kumwaga damu. Tuwaseme tu! Tuwashitaki kwa waliowaleta hapa kwamba hawafanyi kazi yao; wamesahau kabisa!

Wazee wakauliza: Eh, inawezekana? Nikasema inawezekana. Kazi yetu ya kwanza ilikuwa kuwaambia watu kwamba uwezekano wa kujitawala upo. Hilo lilikuwa la kwanza. Wazee walijua maana ya kujitawala. Walitamani kujitawala, lakini hawakujua waanzie wapi.

Vijana hawakuwa na habari kwamba kujitawala kunawezekana. Kwa hiyo kwa wazee sikuwa na matatizo. Wao hawakuwa na kazi; hawakumwogopa Mwingereza. Hawakuogopa kufukuzwa kazi. Baadhi walikuwa wafanyabiashara.

Mzee John Rupia (marehemu) alikua mfanyabiashara na kaidi kidogo. Aliwahi kutishwa na kunyang’anywa leseni yake ya biashara. Akaambiwa akiendelea kushirikiana na kijana mwenda wazimu (Julius Nyerere), atanyang’anywa leseni moja kwa moja. Rupia aliwajibu: Potelea mbali!

Nasema yote haya ikiwa njia ya kutoa shukrani kwa wazee na imani yao kwa vijana wakati huo.

Imani hujenga imani. Na mambo haya makubwa ya nchi, kama hayana baraka za wazee hayaendi. Magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi! Mimi nilipata baraka za wazee tangu zamani. Tangu awali kabisa.

Siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (Dar es Salaam). Akasema: Leo wazee wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku. Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa; wameniita kijana wao kuniombea dua. Mimi Mkristo, wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.

Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka. Zilipomalizika zilikuwa za Korani; sasa zikaja dua za wazee – za jadi.

Walikuwa na beberu la mbuzi. Wamechimba shimo. Wakaniambia simama. Nikasimama. Beberu akachinjwa, huku anaambiwa, “Twining (Twainingi) umekwisha!” (Edward Twining alikuwa Gavana wakati huo). Ndipo nikaambiwa: Tambuka! Nikavuka lile shimo. Hapo nikaambiwa na wazee: Basi nenda zako; tangu leo Twainingi amekwisha!

Sasa mimi Mkristo; hao Waislamu. Na mimi mkorofi-korofi katika mambo haya (ya kutambika). Lakini tulikuwa tunaelewana na wazee wangu hao. Kwa hiyo nilitambuka pale na kuambiwa: Nenda nyumbani salama. Twaining hawezi tena!

Wazee wangu wengine wanakumbuka tulikuwa tunakwenda Bagamoyo. Kwenye makaburi kule! Tunapiga dua huko kwenye makaburi na wazee wangu.

Baadhi yetu mtakumbuka safari moja jamaa wa Kenya, hawa akina Tom Mboya (marehemu) walishitakiwa. Tukasema tuwasaidie. Tuwasaidie vipi? Tukasema tufunge. Tukaomba nchi nzima kufunga siku hiyo. Tufunge! Tukafunga. Hakuna kula. Na siku ya kufunga tulikuwa na mkutano Bagamoyo. Tukaenda huko. Tukafanya mkutano hadi saa 12 jioni.

Baada ya mkutano tukaenda nyumbani kwa Mzee Mohamed Ramia (marehemu). Hapa ndipo tulikuwa tumefikia. Mimi nikamuuliza mzee: Sheikh, una Aspro? Akajibu: Kwa nini unataka Aspro? Nikajibu kuwa kichwa kinaniuma kwelikweli. Akasema subiri.

Tulisubiri hadi saa ya kufuturu. Tukafuturu vizuri. Mzee Ramia akaniuliza: bado unataka Aspro? Nikajibu kichwa sasa hakiumi. Kumbe ilikuwa njaa.

Nawaelezeni haya kwa sababu huko tulikotoka, tulishikamana sana. Tulishirikiana sana na wazee.
 
Unamaanisha tusiwaite wazee kuwahubiria ila tuwashirikishe, tuwatake ushauri? Kwamba kwenye jambo la kitaifa, hakuna tofauti za kiimani? Kwamba hakuna umaana wa vyama vingi, alikubali kuvunja chake na kuendelea na kilichopo?

Nimekuelewa sana, sina hakika kama wataafiki ukweli huo.
 
Mwalimu alikuwa Kiongozi rahim. Aliikuta TAA inasuasua akaipa uhai !

Huyu John Rupia hajapata kuelezewa vyema. Mfanyabiashara tena kipindi cha ukoloni akaweza kuwa-challange wakoloni!!
 
Mwalimu alikuwa Kiongozi rahim. Aliikuta TAA inasuasua akaipa uhai !

Huyu John Rupia hajapata kuelezewa vyema. Mfanyabiashara tena kipindi cha ukoloni akaweza kuwa-challange wakoloni!!
Mwalimu alikuwa Kiongozi rahim. Aliikuta TAA inasuasua akaipa uhai !

Huyu John Rupia hajapata kuelezewa vyema. Mfanyabiashara tena kipindi cha ukoloni akaweza kuwa-challange wakoloni!!
Platozoom,
Nimeeleza hali ya TAA kuanzia 1950 kuwa chama kilikuwa imara na kimeweka malengo ya kujigeuza na kuwa chama cha siasa bila kificho.

Hii ndiyo sababu wakaunda TAA Political Subcommittee mara tu Dr. Kyaruzi na Abdul Sykes walipoingia madarakani mwaka huo.

Lakini ikiwa unapenda kuamini kuwa TAA ilikuwa haina uhai nataka nikufahamishe kitu kimoja.

TAA ilipoteza nguvu Nyerere alipochukua uongozi mwaka wa 1953 si kwa kuwa alikuwa kiongozi dhaifu la hasha sababu ni kile kivuli cha Abdul Sykes.

Ukisoma jinsi Nyerere alivyoingizwa katika uongozi wa TAA utaelewa kwa nini.

John Rupia hakuwa mfanyabiashara peke yake.

Abdul Sykes alikuwa na biashara ya kitoa cha kuuza petroli Ilala mkabala na Bomani.

Dossa Aziz alikuwa na malori saba ya mchanga na kokoto na majumba ya kupangisha.

Mzee Rupia hakuwa mtendaji kama utendaji ulivyozooleka bali yeye alikuwa mfadhili mkubwa wa TANU na kwa ajili hii hakuna mengi sana ya kueleza kuhusu yeye.
 
Mm ni mfuasi wa Nyerere
Kwa sasa na soma vizuri mno, nataka nimfahamu zaidi. Uzi huu unamanufaa sana kwangu.
 
Mm ni mfuasi wa Nyerere
Kwa sasa na soma vizuri mno, nataka nimfahamu zaidi. Uzi huu unamanufaa sana kwangu.
Ed...
Mimi nimesoma kila makala na kitabu kilichomtaja Nyerere na nimeandika sura nzima katika kitabu cha Abdul Sykes kuhusu yeye.

Nimetafiti maisha ya Mwalimu toka siku ya kwanza alipokutana na Abdul Sykes mwaka wa 1952 ulipoanza udugu na urafiki wao.

Nimeandika mengi kuhusu Nyerere na nimemzungumza kwingi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Ingia: mohamedsaidsalum.blogspot.com na mohamedsaidsalum.com.


 
Hii hotuba nimeitafuta sana. Asante sana. Hapa ndio imefika mwishho?
My Next,
Hapana hotuba inaendelea.

Baada ya kuwaadhimisha Waislam na mchango wao kwake na juhudi zao za kupigania uhuru wa Tanganyika Mwalimu Nyerere anaendelea anasema kuwa upogo ulikokuwapo baina ya Wakristo na Waislam kwa ajili ya ukoloni yeye amerekebisha katika madaraka na elimu wakati wa utawala wake.
 
My Next,
Hapana hotuba inaendelea.

Baada ya kuwaadhimisha Waislam na mchango wao kwake na juhudi zao za kupigania uhuru wa Tanganyika Mwalimu Nyerere anaendelea anasema kuwa upogo ulikokuwapo baina ya Wakristo na Waislam kwa ajili ya ukoloni yeye amerekebisha katika madaraka na elimu wakati wa utawala wake.
Naomba unisaidie niweze kuipata yote, hii ni hotuba muhimu sana kwa historia ya Tanzania.
 
Huyu ndo alikuwa mzalendo wa kweli wengine wote wezi tupa kule
 
Back
Top Bottom