Hongera kikwete kuizika CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hongera kikwete kuizika CCM

Discussion in 'JF Chit-Chat' started by Quinty, Apr 17, 2011.

 1. Quinty

  Quinty JF-Expert Member

  #1
  Apr 17, 2011
  Joined: Mar 25, 2010
  Messages: 463
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  BABA wa Taifa hayati Julius Nyerere aliwahi kusema: "Upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM''. Kauli hii sikuielewa na sikujua lengo la kusema vile wakati yeye ni miongoni mwa waasisi wa chama hicho tawala.

  Lakini kadiri muda ulivyokwenda sasa maneno yale tayari yanapiga hodi, kelele katika mawazo yangu na kuweka mwangwi mkuu katika fikra hata kwenye njozi zangu.

  Binafsi nakumbuka kipindi kile cha Mwalimu Nyerere kama pakitokea migawanyiko au migongano yoyote ile iwe ndani ya chama au nje ya chama chake TANU/CCM, alitumia busara na hekima kwa kuitisha vikao mapema na kulizungumzia tatizo husika.

  Leo hii baada ya yeye kufariki dunia, mambo yamekuwa vuluvulu, busara zimekuwa haba, siasa nazo zimegeuzwa vijiko vya kuliibia taifa, sasa kuna nyufa kwenye chama chake alichokiacha.

  Rejea kuibuka kwa matabaka ya walionacho na wasiokuwa nacho pia kuwepo makundi (mitandao) ndani ya chama na nje ya chama.

  Ninachopenda kusema kupitia makala hii ni kwamba hali ya chama hicho kikongwe barani Afrika leo kama ni kweli na kilichofanyika mjini Dodoma (kujivua gamba).

  Naomba nikiri kwamba nilivyoangalia mchakato mzima na kufuatilia mwenendo ulivyokuwa, ndipo nilipoyakumbuka yale maneno ya Nyerere alivyousia kuwa upinzani wa kweli utakaoifurumusha CCM utatoka ndani ya cha hicho tawala.

  Leo nikubali kwamba hayawi, hayawi, sasa yamekuwa ndani ya CCM baada ya kuyazika yaliyokuwa mienendo (dira) maadili ya uongozi, dalili zilizopo sasa na huko tuendako kama ndivyo tulivyoshuhudia, ilivyotangazwa na vyombo vya habari mjini Dodoma (kuvunjwa sekretarieti).

  Naweza kusema kuwa kazi ya kuisambaratisha CCM sasa imeshaanza, aliyeianzisha ni Rais Jakaya Kikwete ingawa najua ni jambo la bahati mbaya sana kwamba rais wetu halijui hilo na pengine niseme anaweza kudhani ni hadithi za kufikirika.

  Najua waliomsifia Kikwete kuwa yeye ni ‘Chaguo la Mungu' walifanya hivyo kwa kubembeleza masilahi na kujikomba, walishindwa kujua upande wa pili wa shilingi kuwa alichaguliwa kubomoa si kujenga. Nani leo atabisha? Rejea serikali yake kukumbwa na utitiri wa kashfa na asizishughulikie!

  Nasema anakuja kubomoa kwani kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ugumu wa maisha kwa mwananchi unavyoshamiri na bei za bidhaa zinapaa mithiri ya ndege ya rais iliyonunuliwa kwa gharama za wavuja jasho walioambiwa wale majani ili usafiri huo ununuliwe.

  Rais anayekiri kuwa mambo ni magumu na wananchi wake wawe wavumilivu lakini viongozi na watendaji wengine wakitafuna (ufisadi) wa rasilimali za taifa kwa faida yao bila kuchukuliwa hatua za kisheria ua kinidhamu, tumuweke kwenye kundi gani?

  Ufisadi hivi sasa ndiyo imekuwa sifa kubwa kwa kiongozi, kutumikia wananchi hivi sasa hakupo tena kila anayepata wadhifa hufikiria kujinufaisha badala ya kuwaangalia wale waliompigia kura.

  Uteuzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali umekuwa ukifanyika kwa lengo la kulindana, kulipana fadhila, kirafiki na vigezo vinginevyo ambavyo kimsingi havipaswi kuangaliwa wakati wa uteuzi.

  Rais Kikwete, haonekani kubadilika kwa kutowachagua watu kwa sifa na vigezo walivyonavyo, uswahiba, umtandao umekuwa ukiendelezwa kwa kificho au kwa uwazi.

  Nakumbuka aliyewahi kuwa Rais wa Kenya, Daniel arap Moi, kipindi kile ama kwa kujua au kutojua alijikuta akipigilia misumari ya mwisho kwenye jeneza la chama chake cha KANU kilichokuwa kikitawala pale alipolazimisha Uhuru Kenyatta agombee urais badala ya Mwai Kibaki aliyekuwa akionekana ndiye chaguo la watu wengi.

  Moi alionywa kuwa uamuzi wake huo unalenga kukiua chama chake lakini hakusikia, matokeo yake KANU ilianguka na Kibaki akafanikiwa kuwa rais kwa kupitia muungano wa vyama vya upinzani (NARC)
  Kilichotokea Kenya ndicho ninachokiona kwa CCM ambapo baadhi ya wanaosema ukweli na kukosoa ufisadi ndio wanaoshughulikiwa kwa madai ya kukiyumbisha chama na wengine walishughulikiwa kwenye michakato ya chaguzi mbalimbali za chama na zile za kitaifa.

  Ninachopenda kusema baada ya kulisoma somo lile la Kenya, nikaangalia mambo yalivyo CCM ninaona dalili za kifo cha chama hicho chini ya Rais Kikwete kimewadia na upinzani wa kweli utatoka humo.

  Leo hii CCM wanapowaadhibu wakemea ufisadi ambao wamejizolea umaarufu mkubwa inategemea nini? Makada hao wakiamua kujiengua chamani na kujiunga na upinzani nina uhakika huo ndio utakuwa mwanzo wa kubomoka kwa chama hicho tawala.

  Ni ulevi wa madaraka na kutosoma alama za nyakati ndiko kunakowafanya baadhi ya makada wa CCM kuimba wimbo kuwa chama hicho kitatawala milele pasi na kuungalia ukomavu wa vyama vya upinzani unaoonekana sasa.

  Nawaomba Watanzania wenzangu wale wote wapenda mabadiliko na maendeleo, Tumwombe Mungu huko tuendako walioenguliwa CCM wajiunge na upinzani ili tupate mabadiliko kwenye nyanja mbalimbali.

  CCM inaweza kuwa kwenye benchi la upinzani kama KANU au UDF ya Malawi, yote haya yanawezekana kama wale waonaofanyiwa fitna ndani ya chama tawala wataamua kuchukua maamuzi magumu na kujiunga na upinzani ili waendelee kupigania mgawanyo sawa wa rasilimali za taifa.

  Najua makada wa CCM wasingependa kusikia chama chao kitakuja kuwa cha upinzani na hivi sasa wanajifariji kuwa wamejivua gamba lililokuwa likiwapa sifa mbaya kwa wananchi, wanajidanganya.

  Nasema wanajidanganya bure kwani ile migawanyiko, matusi,kuvuana nguo tulikoshuhudia siku za hivi karibuni ndani ya chama hicho na jumuiya zake ni cheche za kukimaliza chama hicho.

  Ukweli ni kuwa saratani inayoitafuna CCM ipo ndani ya damu, hivyo kujivua gamba hakutaweza kukinusuru chama hicho, kwani rais ni yule yule, watu ni wale wale, sitarajii mambo mapya baada ya uamuzi huo unaoitwa ni mgumu.

  CCM na serikali yake watazidi kuumizwa na kushindwa kutekeleza ahadi ilizozitoa kwa wananchi katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005, 2010 hasa ile ya maisha bora kwa kila Mtanzania. Hii ni saratani.

  Rejea pia vigogo wengi wa CCM hadi leo wanakabiliwa na tuhuma za wazi zikiwemo zile za kughushi hata vyeti vya taaluma, kukwapua mabilioni ya fedha kupitia Kampuni za Meremeta, Kagoda, Deep Green.

  Chama hicho pia kinadaiwa kuhusika na wizi mkubwa wa Fedha za Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) zilizokuwa zimehifadhiwa Benki Kuu, fedha hizo inasemekana ndizo zilizompa Rais Kikwete ushindi mwaka 2005.

  Niseme kuwa hata kuhusishwa kwa kada wa CCM na aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Andrew Chenge, kuhusishwa na ufisadi mkubwa wa rada lakini bado ni mbunge!

  Pia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuhusishwa na ufisadi wa kutisha wa Kampuni ya kufua umeme ya Ricmond/Dowans, ambao unatikisa nchi hadi leo halafu eti ni mbunge wa chama kile kile! (‘Tushajivua gamba bwana')
  Rejea kauli ya Rais Kikwete hivi karibuni kwenye NEC, "katika kipindi hiki cha mazongo mazongo yetu, wananchi wamekata tamaa na ninyi ndio wenye mamlaka ya hali hiyo''.

  Nilishituka nikajiuliza hapa rais wetu anampiga chenga nani au anamdanganya nani wakati mambo yote ndani ya serikali na chama ni lazima yapitie mezani kwake, maana yeye ni mwenyekiti wa chama na kiongozi wa baraza la mawaziri?

  Rais Kikwete amesahau kuwa yeye ndiye aliyewapigia kura mwaka jana tena kwa kuwanadi kuwa hao ni hazina ya chama, mapanga ya zamani yenye makali mapya, sasa anapotoa muda wa kupima wenyewe ana lengo gani?

  Naomba kwa faida ya Watanzania na wale wote waliopewa miezi mitatu kama wapo au wanatarajia kuondoka, nitanukuu katiba yetu ya mwaka 1977 ambayo yeye (Rais) anailinda sehemu ya ibara ndogo ya (4)ya ibara ya 132 inasema hivi:

  "Katiba inapiga marufuku viongozi wasio waaminifu, wanaopendelea au wasio waadilifu, wachochezi wa rushwa katika shughuli za umma, wanaohatarisha masilahi ya taifa na ustawi wa jamii. Katiba inawataja hao viongozi ni kuanzia; Rais, Makamu wa Rais,Waziri Mkuu, mawaziri, spika, waziri kiongozi (Zanzibar),wakuu wa mikoa, mabalozi, makatibu wa wizara,wabunge na wengine wote. Bila kusahau kile kifungu cha sheria ya maadili ya umma namba 13 ya 1995 kinachoweka wazi hatua za viongozi wezi na mafisadi kuchukuliwa.

  Mmeisikia katiba hiyo mliyojivua gamba na ambao mnasubiri kuvuliwa? Msomaji wangu na Mtanzania mwenzangu leo ukiulizwa mantiki ya Rais Kikwete kushindwa hata kutaja mali zake au awabane wenzake wataje, wewe utajibu nini?

  Rejea kila mtu leo ni msemaji ndani ya awamu ya nne, yako wapi yale maisha bora tuliyoahidiwa miaka sita sasa tangu Kikwete aingie madarakani? Yako wapi ikiwa leo mama zetu wanapewa bajaji au kujifungulia nje ya hospitali huku watawala wakishindana kununua mashangingi kwa fedha za masikini?

  Ushahidi wa kushindwa kwake Kikwete leo upo, kuna jambo moja kubwa na la maana sana ameshaanza kulifanya, anakiua chama chake, tumsaidie kwa sababu ni ukombozi kwa Watanzania.

  Wakati tukimuunga mkono Rais Kikwete kwa kuiua CCM, tuwape changamoto wale wote walioondolewa kwenye sekretarieti kwa kuwaambia ‘wasiogope kujiondoa ndani ya chama hicho tawala.
   
 2. Mlengo wa Kati

  Mlengo wa Kati JF-Expert Member

  #2
  Apr 18, 2011
  Joined: Feb 16, 2011
  Messages: 2,733
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 0
  Pombe za mchana mbaya sana!
   
Loading...