Hoja ya Prudence karugendo: NEC ni ya nani? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hoja ya Prudence karugendo: NEC ni ya nani?

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Rutashubanyuma, Jan 2, 2011.

 1. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #1
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 158,014
  Likes Received: 416,698
  Trophy Points: 280
  NEC ni tume ya uchaguzi au ya ushindi wa CCM?

  Prudence Karugendo
  MOJA ya vyombo nyeti katika uhai wa usalama wa nchi yetu ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
  Tume hii ndiyo imekabidhiwa jukumu la kutoa kauli ya mwisho ya ni nani anapaswa kuwa mhimili mkuu wa nchi yetu kulingana na matakwa ya wananchi.

  Hii maana yake ni kwamba chombo hiki kinapaswa kutoa kauli inayotafsiri matakwa halali na sahihi ya wananchi na siyo kutoa kauli kulingana na namna kinavyotaka chenyewe.

  Haipaswi pia kutoa kauli kulingana na namna kinavyoona inafaa kwa kutegemea tu uadhimu wa mamlaka kiliyopewa.

  Ila kwa vile mamlaka wakati mwingine hulevya upo uwezekano wa chombo hiki kutoa kauli inayokinzana na matakwa ya wananchi.

  Hivyo kauli yake kuonekana siyo tafsiri sahihi ya matakwa yao kitu kinachoweza kuifanya kauli hiyo ya mwisho ya chombo hicho kuonekana haramu na kusababisha tafrani. Hapo ndipo ulipo unyeti wa NEC.

  Chombo hicho kinapotetereka, iwe kwa kushindwa kuhimili nguvu ya kilevi kilichomo ndani ya mamlaka kinayokabidhiwa ama kwa kutumiwa vibaya na mamlaka iliyo juu yake, serikali, kinyume na kusudio lililokianzisha, ni rahisi chombo hicho kuigeuza nchi kuwa jahanamu.

  Mifano hai tunayo, tujikumbushe ya Zimbabwe, Kenya na yale ambayo yamekuwa yakijirudiarudia kule Zanzibar, kwa kutaja sehemu chache tu.

  Kwa kulizingatia suala hilo la unyeti wa NEC, moja kwa moja ndipo unapojitokeza umuhimu wa chombo hicho kuwa huru tofauti na ilivyo hapa nchini kwetu. Uhuru ninaousema unapaswa ujionyeshe tangu pale chombo hicho kinapoundwa.

  Inabidi uwepo utaratibu huru wa kuwapata wasimamizi wa chombo hicho ambao utakuwa hauwabani na kuwafanya waegemee upande fulani, wanapaswa wawe huru ili wasiweze kuegemea upande wowote.

  Huo ni utaratibu ambao unapaswa uwe tofauti kabisa na huu wa sasa ambao wasimamizi wote, au niseme watumishi wa tume hiyo, ni wateule wa serikali iliyo madarakani. Kitu hicho kinaifanya Tume ya Uchaguzi kuonekana kama idara ya serikali.

  Kwa wale ambao hawamo serikalini ni vigumu kuelewa vigezo vinavyotumika kuwapata watumishi wa Tume ya Uchaguzi kuanzia kwa mwenyekiti wa tume hiyo, wakurugenzi wake na watumishi wa chini yao.

  Kwa uzoefu uliopo ni kwamba uteuzi wowote ni lazima ulenge kwa mtu aliye tayari kuwa mtiifu kwa yule anayemteua au mamlaka husika.

  Ni uzoefu huo unaoweka kila kitu wazi na kuonyesha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyoteuliwa na serikali iliyo madarakani haiwezi kuwa huru.

  Haiwezi kuwa huru kiasi cha kubariki maamuzi yanayositisha uwepo wa serikali husika ambayo tume inakuwa imeahidi kuwa tiifu kwake na kuilinda kwa namna yoyote iwayo.

  Hapo ndipo tunapofika na kugundua kwamba hatuna tume huru ya uchaguzi.

  Na tunapokosa tume huru ya uchaguzi kinachofuatia ni nini? Ukosekano wa tume huru ya uchaguzi unamaanisha kuiweka demokrasia nyuma ya pazia na kubaki ikiimbwa tu bila yenyewe kuonekana jukwaani.

  Uchaguzi utaandaliwa kama alama ya demokrasia, kura zitapigwa lakini kitakachoamuliwa na wapiga kura hakitawekwa wazi kulingana na matakwa yao ila badala yake NEC itageuza.

  Itafanya hivyo kuonyesha kile kinachowafurahisha walioiunda tume hiyo. Wananchi watakuwa wamehangaika bure, pesa ya kodi zao itakuwa imeharibika bure katika mchakato mzima wa uchaguzi wakati mambo yakilazimishwa kubaki vilevile na Tume ya Uchaguzi isiyo na uhuru wowote wa kutangaza kilicho sahihi.

  Kwa mwonekano huo Tume ya Uchaguzi inabaki kuwa kiinimacho kinachotumika kuhalalisha udikteta wa watawala wasiowaamini wapiga kura, hususan katika sehemu kubwa ya Afrika.

  Bara la Afrika inaonekana demokrasia inafuatwa kwa wananchi kufanya chaguzi ambazo lakini, kwa vyovyote vile, matokeo ni lazima yaonyeshe yanawapendelea watawala walio madarakani ilihali katika hali halisi wapiga kura wanakuwa wameishawachoka na hawawataki.

  Hivyo tutaona kuwa tume za uchaguzi katika sehemu kubwa ya Afrika zinatumika kuifunika demokrasia wakati huohuo zikiwa zimeubeba udikteta wa watawala wasiopenda mabadiliko.

  Kumbe tume hizi za uchaguzi kwa maana nyingine ni kikwazo kwa demokrasia iliyo komavu na pia ni kikwazo katika juhudi zinazofanywa na jamii duni kujikwamua katika ufukara.

  Ni vigumu kuuondoa ufukara ambao jamii husika inakuwa imesababishiwa na utawala mbovu usiopenda kuondoka madarakani kwa njia za kidemokrasia.

  Ili kuondokana na ufakara wa aina hiyo ni lazima kuhakikisha kwanza mfumo mbovu wa utawala unaondoka madarakani.

  Kwahiyo juhudi zozote za kukwamisha mabadiliko hayo zinakuwa zimelenga kuidumaza jamii husika kwa kuzidi kuididimiza kwenye lindi la ufukara.

  Tanzania tunayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi, tangu tume hiyo iundwe ni zaidi ya miaka 15 sasa.

  Naweza kusema kwamba tume hii ni ile ile iliyoundwa tangu wakati huo ikiwa chini ya mwenyekiti wake, Jaji msitaafu Lewis Makame.

  Sina hakika kama wale walio chini yake wapo waliositaafu au kubadilishwa, ila mwenyekiti ni yuleyule ambaye amekuwa kwenye nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 15.

  Sidhani kama katika tume hiyo kuna kitu kustaafu kwa vile watumishi wake wengi ni wale ambao tayari ni wasitaafu. Zaidi ya hapo cha kuwastaafisha pengine ni kifo.

  Cha kufikiria ni kwamba kwa kipindi chote hiki cha zaidi ya miaka 15 bila tume hii kubadilishwa, ambapo imeweza kufanya kazi katika awamu tatu za marais tofauti.

  Bila shaka tume hiyo itakuwa ni ya manufaa kwa serikali zote tatu ilizofanya kazi chini yake. Naweza kusema kwamba tume hiyo imeonyesha uaminifu na utiifu mkubwa kwa serikali na hizo.

  Uaminifu na utiifu huo pengine ndiyo sababu ya serikali kutoona umuhimu wa kuifanyia mabadiliko tume hiyo.
  Lakini wakati tume hiyo ikionekana hivyo upande wa serikali, kwa upande wangu, kama mwananchi mpiga kura, naweza kusema kwamba sijawahi kuona chombo kilichovurunda majukumu yake kama hii kama hiki.

  Ikumbukwe jinsi tume hiyo ilivyovuruga Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 ambao ndio uliokuwa wa kwanza tume hiyo kuusimamia ukiwa unahusisha vyama vingi vya siasa.

  Katika hali ya kushangaza uchaguzi huo ilibidi ufutwe katika majimbo yote ya mkoa wa Dar es salaam kwa madai ya upungufu wa vifaa vya kupigia kura!

  Ilidaiwa kwamba vifaa hivyo havikuweza kufikishwa kwa ukamilifu katika vituo vya kupigia kura kwenye majimbo yote ya mkoa wa Dar es salaam.

  Lakini pamoja na hali kuwa hivyo mkoani Dar es salaam, ambako ndiko yaliko makao makuu ya Tume ya Uchaguzi, hali ilikuwa tofauti kwingineko mikoani.

  Kule wananchi walipiga kura bila matatizo yoyote na hakukuwepo na upungufu wa vifaa!

  Fikiria kituo cha kupigia kura kilichopo mita 50 kutoka makao makuu ya Tume ya Uchaguzi, ambako ndiko kulikohifadhiwa vifaa vyote vya kupigia kura, inapungukiwa na vifaa hivyo na kuwafanya wananchi washindwe kupiga kura.

  Lakini kituo kilichoko kilomita 2000 kutoka hapo eti kinakuwa na vifaa vyote na hivyo kuwawezesha wananchi wa kule kupiga kura bila matatizo yoyote!

  Hayo yalikuwa ni maajabu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania.
  Lakini wakati wananchi wa mkoa wa Dar es salaam wakilishwa madai hayo ya kizembe ya tume hiyo, wao walichokiona ni tofauti.
  Ni kwamba majimbo yote ya mkoa huo yalikuwa yaende kwenye kambi ya upinzani, kwahiyo tume tiifu kwa serikali ikaamua kuokoa jahazi.
  Bila shaka isingeweza kuliweka wazi hilo ndiyo maana yakatolewa madai hayo ya maajabu ya kushindwa kufikisha vifaa vya kupigia kura katika umbali wa mita 50 wakati imefikisha vifaa hivyo katika umbali wa kilomita 2000!
  Uchaguzi uliofuata wa mwaka 2000 nao ulijaa mapungufu ya aina ileile ya makusudi na ya kizembe.
  Lakini hatukuona hatua yoyote ya kuwajibika ili kuwarudishia wananchi imani kuwa yaliyokuwa yanatokea yalikuwa hayaifurahishi hata tume yenyewe.
  Ukaja uchaguzi wa mwaka 2005 kwa mtindo uleule.
  Sasa funga kazi ni huu uchaguzi wa mwaka 2010 maarufu kama uchakachuaji.
  Tumeweza kuona jinsi Tume ya Uchaguzi ilivyoendesha zoezi zima la uchaguzi bila kujitofautisha hata kidogo na serikali ambayo ilikuwa ni mshindani katika uchaguzi huo ambapo tume ya uchaguzi ndiyo ilikuwa mshika kipenga.
  Zoezi zima la uchaguzi limeendeshwa katika hali ya kutatanisha kabisa na kuwafanya wananchi wasiweze kuamini kama kuna kitu kinajitegemea kama Tume ya Uchaguzi.
  Imefikia wakati ikaonekana kama vile Tume ya Uchaguzi inapewa maelekezo mmoja wa washindani na kuyafuata badala ya yenyewe kutoa maelekezo.
  Tuliona jinsi madai mengi yaliyokuwa yanatolewa na vyama vilivyokuwa vinashiriki uchaguzi juu ya CCM kukiuka taratibu na kanuni za uchaguzi.
  Majibu yalivyokuwa yakijibiwa na Tume ya uchaguzi badala ya mshitakiwa, CCM, yalistaajabisha kwa sababu tume ilijigeuza mshitakiwa badala kuwa hakimu wakati CCM ikibaki kuwa msikilizaji!
  Hayo na mengine ndiyo yanayoifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania ionekane kama taasisi isiyokuwa huru na hivyo kuibua madai kutoka kwa wadau wa uchaguzi, wapiga kura na vyama vya siasa, ya kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.
  Hata kama madai hayo hayana maana, tume yenyewe, kama siyo kweli kwamba imepewa jukumu maalumu la kusimamia kitu fulani mbali na uchaguzi huru na wa haki.
  Ingebidi NEC, ijionee aibu kwa kushindwa kazi ikiwa inafanya chini ya kiwango kinachokubalika na hivyo kuamua yenyewe kuachia ngazi.
  Vilevile serikali nayo kama kweli haiitumii tume hiyo kama kichaka cha kuficha mambo fulani isingekubali tume hiyo iendelee na kazi kwa kiwango hiki cha udhaifu.
  Hiyo ni kwa sababu chombo chochote chenye utendaji wa kiwango kilicho chini ya asilimia 50 ni wazi kwamba kimeshindwa kazi.
  Tume ya Taifa ya Uchaguzi, bila aibu, ilitutangazia kwamba watu waliopiga kura katika uchaguzi uliopita ni asilimia 42 ya watu wote waliojiandikisha kupiga kura.
  Huo ndio uwezo wa utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Huyo rais aliyetangazwa na tume hiyo kuwa kapata asilimia 61 ya kura zilizopigwa atakuwa kachaguliwa na asilimia gani ya Watanzania wanaopaswa kupiga kura?
  Rais huyo anawezaje kujivuna kuwa yeye ni chaguo la kidemokrasia la Watanzania?
  Kwa mwenendo huu si itafikia rais achaguliwe na watu 100 katika watu milioni 40? Swali ni je, NEC ipo ili kuhakikisha watu wanafanya uchaguzi au ipo ili kuhakikisha rais aliye madarakani anashinda hata kwa kura sifuri baada wananchi wote kushindwa kujitokeza kupiga kura?
  Tuachane na hiki kiinimacho, ni lazima tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi ili demokrasia ya kweli isimame mahala pake.
   
 2. H

  HM Hafif JF-Expert Member

  #2
  Jan 27, 2011
  Joined: Aug 16, 2009
  Messages: 1,359
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Maneno sawia kabisa ndugu yangu Prudence karugendo nduguye Primus and Padre Prevatus karugendo.
   
 3. GATS

  GATS JF-Expert Member

  #3
  Jan 27, 2011
  Joined: Jan 6, 2011
  Messages: 240
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Hii tume ni mbovu kabisa inatakiwa ivunjwe na tume huru iundwe wasisubiri yaliyotokea Tunisia. Watanzania wamechoka sana kwa sasa. Kila mahali wanasema tumechoka. Ikifika wakaamua kuchukua hatua tutakuwa tumechelewa. Mwenye masikio na asikie.
   
 4. RayB

  RayB JF-Expert Member

  #4
  Jan 28, 2011
  Joined: Nov 27, 2009
  Messages: 2,754
  Likes Received: 88
  Trophy Points: 145
  NEC ni ya wenyewe
   
 5. Kaa la Moto

  Kaa la Moto JF-Expert Member

  #5
  Jan 28, 2011
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 7,666
  Likes Received: 164
  Trophy Points: 160
  Sema kusudio lako! Wacha kujiuma uma hapa nani kakuuliza mambo ya familia ya Karugendo?
   
Loading...