Hofu ya Machafuko

Rev. Kishoka

JF-Expert Member
Mar 7, 2006
4,536
2,000
Natatizwa sana kuona Serikali ya KIkwete ikijiimarisha "kiulinzi" kupitia Jeshi, Polisi na hata Usalama wa Taifa eti kudhibiti na kuzuia machafuko wakati wa uchaguzi mkuu.

Serikali imeweka majesho yote kwenye Red alert, polisi wamekabidhiwa magari mmapya zaidi ya 700 leo na yanasambazwa nchi nzima.

Najiuliza, hatua hizi za kuonyesha ukakamavu na uimara wa ulinzi leo hii ambapo tunakaribia kutimiza haki yetu ya kidemokrasia na kikatiba inatokana na nini?

Iweje ghafla kuwe na umuhimu wa kuhakikisha ulinzi na usalama uko imara zaidi kwa tendo la kuaminiana na linalohitaji amani, busara na hekima kuhakikisha katiba yetu na demkorasia tunayo ihubiri na kujisifia kuwa na amani, utulivu na mshikamano ni kitu cha kweli na si ulaghai na kiini macho?

Ni kitu gani hasa ambacho si sahihi na kina walakini kufikia hatua wananchi wanaweza kukosa imani na utiifu kuanzisha fujo na Serikali kuonelea ulazima wa kutunisha misuli "kudhibiti" amani?

Najiuliza ni wapi tumekosea kwamba Serikali na hasa Chama Tawala kukosa kuaminika kwa wale ambao si wafuasi wa Chama Tawala?

Je ni nchi ya namna gani tunaijenga inapofikia Serikali iliyoko madarakani inaonekana imejenga mazingira yasiyo ya haki, demokrasia na utu kwa manufaa ya Taifa na kuwa na upendeleo au kulazimisha Chama kilichoko madarakani kitumie dola kujihakikishia muendelezo wa utawala wake?

Hisia za hujuma zilizoonyeshwa katika chaguzi zilizopita zimepuuziwa. Mazingira ya rushwa yameendela. Vitisho vya kidola na nguvu za dola na hata kauli kuashiria mwananchi akitumia haki yake kikatiba na kuchagua anachokipenda kwa utashi wake, kuna hatari ya nchi kuingia machafuko na hata kumwaga damu.

Hii imetokea hata wagombea wa urasi, Ubunge na Udiwani kutoa kauli za vitisho kwa wananchi kuwa wakiacha kupigia chama fulani (hasa chama Tawala), nchi itaingiwa matatizo au hata wananchi kutishiwa kunyimwa kusikilizwa au huduma za maendeleo.

Mwaka huu pekee, Mgombea wa Chama Tawala John Magufuli na mgombea mwenza Salma Suluhu wametoa kauli za kuonyesha kuwa wananchi wakiamua kupigia vyama vingine ambavyo si CCM, basi nchi itageuka na kuwa na taswira ya nchi zilioingia vita (libya, Misri) na kuwa chama tawala-CCM kikishinda, basi waliopigia kura upinzani wawakilishi wao hawatasikilizwa wala kukaribishwa ikulu.

Hali hii ilifanyika pia wakati wa Urais wa Mkapa wakati aliyekuwa Waziri Mkuu Sumaye, alipotoa kauli mkoani Kilimanjaro kuwa wakichagua upinzani, watapoteza huduma za maendeleo na mgawanyo wa fungu la fedha kutoka Serikali kuu.

Hata Waziri Mkuu anayeondoka Mizengo Pinda alipotoa kauli yake kuwa "Wapinzani Wapigwe tuu" au Spika wa Bunge (Makinda na Ndungai) kutumia wingi wa kura za Kibunge kuzima hoja, tulikuwa tunajengewa demokrasia ya namna gani?

Je ni kwa nini ulazima huu wa kutumia vitisho kuhakikisha Chama Tawala na Ssrikali zake zinaendela kuwa madarakani?

Ukitafakari hata sheria ya Mtandao (Cyber Crime) au ya Takwimu (Statistics), zimelenga kuleta udhibiti wa nini Serikali inakitaka na kuonelea ni sawa na si uhakiki wa mambo yanayosemwa au usimamizi wa sheria na kanuni.

Leo hii, Serikali imeipa jeshi la Polisi magari zaidi ya 700 kufanya doria na ulinzi wakati wa uchaguzi, kwa nini hatushituki na kuhoji kulikoni?

Serikali hii ambayo imeendelea kusema haina fedha, imetaka kukopa benk za biashara, imeangusha shilingi kwa kukosa thamani, haina fedha za kuzalisha umeme na kupoteza mapato ya uzalishaji kutokana na umeme haba, ilipata wapi fedha kujitutumua kuhakikisha Jeshi liko tayari na Polisi?

Je kulikuwa na ulazima wa kujiimarisha kijeshi kuhakikisha demokrasia na haki ya kikatiba ya kupiga kura inafanyika kwa usalama?

Je "usalama" huu ni kulinda maslahi wa Taifa au kulinda maslahi na ustawi wa mamlaka ya Chama Tawala?

Mwaka 2000-2001 tuliona vurugu za hali ya juu Zanzibar mpaka watu walitolewa kafara walipokuwa anapigania haki yao na kuhoji kudhulumiwa haki hii.

Tumeona kwa miaka 20 sasa, CCM ikituhumiwa kutima dola na kutoa mifano ya nchi zilioingia mifarakano na umwagaji damu kuhakikisha kinaendelea kuhodhi madaraka na dhamana ya kutawala nchi (si kuongoza, bali ni kutawala na hivyo kujiita Chama Tawala)!

Tumeshuhudia malalamiko ya ukiukwaji wa haki na kukosekana na mfumo usio na upendeleo kuendesha siasa na chaguzi zetu: Tume ya uchaguzi, msajili wa vyama, mahakama, polisi, sheria za uchaguzi, serikali za mitaa, usalama wa taifa na hata katiba, vikiegemea kuipa CCM upendeleo na kuihakikishia ushindi.

Je kuna maana gani basi kuwa na uchaguzi mkuu na kuhubiri demokrasia ikiwa mfumo mzima wa uendeshaji siasa, vyama na uchaguzi unategemea ridhaa ya CCM kama chama tawala?

Leo hii Wafadhili na waangalizi wa Uchaguzi wanakuja kufanya nini cha unafiki? kuhakikisha haki inatendeka au kuhakikisha usalama wa maslahi yao unatunzwa?

Leo watendaji wa CCM wanapotoa kauli na kufanya vitendo vya kusema hata kwa goli la mkono ikiwa ni kuashiria hata kwa dhuluma na si uhalali lazima CCM ishinde kunatupa Watanzania hisia gani?

Najiuliza, je kama katiba yetu ingekuwa thabiti na isiyo ya upendeleo, kama tume yta uchaguzi ingekuwa huru, kama Polisi, Mahakama, Usalama wa Taifa na Jeshi vingekuwa vyombo huru na si vijakazi wa Chama Tawala (urithi wa mfumo wa chama kimoja), leo tungekuwa na kutokuaminiana na hata kuwa na haja ya kutenga fungu la fedha kudumisha dola ya CCM na si kuzitumia fedha hizi kwa shughuli za maendeleo na kutatua kero za wananchi kama maji safi, zahanati na elimu?

Je magari haya 700 ya polisi yangeweza kujenga visima vingapi katika vijiji vyetu vyote?

Je magari haya 700 na ushee ya polisi kutishia watu yangeweza kutupatia magari mangapi ya kubebea wagonjwa au zimamoto?

Je magari haya 700 gharama yake ingeweza kutujengea vituo vingapi vya afya vidogo vidogo pamoja na zana kutoa huduma za msingi na kwanza za kiafya kuhakikisha kinga na si tiba?

Najiuliza zawadi hii kwa polisi kama ni takrima ya shukrani na kuwakumbusha Polisi kuwa CCM ni baba na mama yao na wajibu wao wa utiifu ni kwa CCM na si katiba ya nchi?

Jeshi letu lilipozawadiwa vifaa vipya vya kijeshi na hata leo kuzinduliwa ujenzi wa kuboresha kituo cha kijeshi Ngerengere ni kurubuni utii wa Jeshi kwa chama Tawala?

Je Katiba yetu, ingekuwa ni yenye demokrasia ya kweli kama wananchi walivyopendekeza (Rasimu ya Katiba ya Warioba), tume ya uchaguzi ingekuwa huru na mchakato mzima wa uchaguzi ungefanyika kwa umakini na haki, kungekuwa na ulazima wa wananchi kuambiwa wahakikishe wanalinda kura na kukaa mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura kulinda haki zao?

Je tume ya uchaguzi ingejiendesha bila utata wa Daftari la kupiga kura, uandikishaji wa upiga kura, uhgakiki, usalama na usimamizi wa kupiga kura, haki na usawa wa kutangaza matokeo ya kupiga kura je tungekuwa tunaitilia mashaka ya kuweka kambi ya mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura?

je leo hii tunapoona wagombea wa Chama Tawala wakitoa kauli chafu bila kukemewa lakini vyama vya upinzani wakikemewa na tume ya uchaguzi kwa kauli, aina ya kampeni au vipeperushi tunajiuliza upendeleo huu ni wa nini?

Tulipoona Red brigade ya Chadema au Vikosi vya ulinzi CUF, wakijijenga ilikuwa ni kwa ajili ya nini? ikiwa wao wanashurtishwa kufuta "vikosi" lakini Green Guard wa CCM wana nguvu kuliko hata polisi na wakuu wa Wilaya, hatuoni kuwa tuna tatizo la msingi?

Leo kauli za uchochezi mpaka kufikia Jeshi kuwa mguu sawa na batalioni kusambazwa kila kona ya nchi, je tunajilidna dhidi ya adui gani? Adui demokrasia?

Leo halaiki za ukakamavu na ubora wa vyombo vya ulinzi na usalama ni kuhitimisha na kukamilisha mbegu chafu iliyopandwa kwenye vichwa vya Watanzania kuwa wakichagua Upinzani badala ya Chama Tawala CCM nchi itachafuka?

Leo wagombea wa CCM waliokuwa na madaraka ya Kiserikali wanapotumia madaraka hayo kuabudiwa majimboni mpaka kuitwa Nkurunzinza (Mwakyembe Kyela, na wenginewe), kunatupa picha gani?

Ni taswira gani tunaipanda kwenye vichwa na mawazo ya watoto na vijana wetu watakaopiga kura siku za baadae? Tunajenga taifa la namna gani lenye kujaa vitisho na kuhalalisha utawala wa mabavu?

Je ni kwa miaka na chaguzi ngapi vyama vya upinzani viendelee kuishi kwa woga au kujilinda kishari na kueneza imani ya kutoiamini Serikali na Chama Tawala CCM?

Je ni gharama gani tumetumia mpaka sasa kulihujumu Taifa na Watanzania haki yao ya kidemokrasia kudumisha mfumo dume na dola wa Chama tawala CCM?

Je ni gharama gani za kibajeti na kifedha Serikali imeingina na itaingia na kuminya kodi zetu kujihakikishia ushindi na utawala wa kudumu badala ya kuunda mazingira safi na mfumo bora wa kusimamia haki ya kidemokrasia kwa mujibu wa katiba?

Ni damu nyingi kiasi gani na roho ngapi zipotee kutetea haki hii ya kuzaliwa?
 

Azimio Jipya

JF-Expert Member
Nov 27, 2007
3,364
1,195
Demokrasia ya kweli ni mjumuisho wa mambo mengi na muda wa safari yenyewe ... hautabiriki. Kwa kawaida huwa ni muda mrefu uliosheni changamoto kadhaa.
 

firstcollina

JF-Expert Member
Aug 8, 2009
349
195
Haya ni matokeo ya ubinafsi, na hali ya kujiona kuwa bora na wenye kustahili mema ya nchi kuliko wengine. Hakika hili si jambo jema kabisa, nijambo linalofaa kupingwa na kukemewa na kila mwenye kulitakia mema taifa letu tukufu la Tanzania

Ni dhahiri kuwa, tukiendele na mfumo huu wa kutotumia sera za kimaboresho baadala yake tukaendelea kutumia propaganda za vitisho ju ya usalama wa raia ni dhahiri tutalipeleka taifa letu mahali pabaya sana tenakwa gharamaya kodi za wavuja jasho (kodi za wananchi)

Ikumbukwe upo usemi usemao "....tunapanga kufanya na tunafanya tunayoyapanga...." usemi huu una maana sana, hasa katika taifa letu tukufu lenye rasilimali nyingi ambazo pamoja na kuanza kutumika kwa muda mrefu uliopita bado hazijaleta tija kwa taifa. Kwanini natoa msemo huu hapo juu? Nasema hivyo kwasababu kuu tatu-


  1. kama taifa hatupangi mambo ya msingi yanayowezaleta tija kwa jamii, kama tuapanga basi tunakuwa na ajenda ya siri nyuma ya pazia ajenda yenye kufanikisha maslai ya watu wachache kuliko wengi wanyonge wasio na nguvu za kiutawala (wananchi)
  2. Nia ya dhati yakuleta maadiliko ya kifikra, kiuchumi na kielimu katika jamii ya wazalendo haipo na ndio maana kama taifa tunashindwa kufanya mipango dhabiti na ya kudumu katika kufanikisha maendeleo tija miogoni mwa wanajamii. Maamuzi yetu yanaishia kuwa maamuzi ya kidhalimu mfano kushusha daraja la ufaulu, kuweka sheria kandamizi juu ya mawasiliano, haya yote naiuiza ni kwa manufaa ya nani?
  3. Mambo machache tunayoyafanya katika taifa si kweli kwamba yameenga kuoesha maisha ya watanzania la hasha bali yamelenga kuleta faida kwa wale wanayotekelezahiyo miradi kuliko walengwa wa hiyo miradi

Ndio maana unaona kiu kuu baina wa Tanzania katika kuleta mabadiliko. Ni dhahiri kwamba mambo haya yanayanywa na chama tawala siyo mambo ya kuungwa mkono katu asilani. Vyombo kama jeshi, polisi, mahakama ni vyombo huru vya uma hivyo si busara kuvitumia kuuadhibu uma kwa kuupokonya haki na wajibu wao wakikatiba kwa kisingizio cha machafuko
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom