Hivi ni vazi ama sare ya taifa? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hivi ni vazi ama sare ya taifa?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by sulphadoxine, Feb 3, 2012.

 1. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #1
  Feb 3, 2012
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  KWA TAKRIBANI mwezi mmoja sasa Wizara ya Habari, Utamadani na Michezo imekuwa ikitoa tangazo kwenye vyombo mbalimbali vya habari linalowataka watanzania wenye sifa mbalimbali kujitokeza ili kusaidia kubuni vazi la taifa kwa namna anayoweza mbunifu lakini kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa ikiwa ni pamoja na uwepo wa rangi za bendera ya taifa.

  Wizara hiyo iko katika jitihada za kuhakikisha kuwa Tanzania pia inakuwa na vazi ambalo kwa jinsi ya kawaida kabisa laweza kumtambulisha mtanzania katika jamii nyingine na hata kama si mtanzania basi aweze tu kunasibishwa na utanzania kutokana na vazi lake kama ilivyo kwa ndugu zetu wa Nigeria, Afrika Kusini, Uganda na hata Rwanda na Burundi.

  Kwangu binafsi hii si mara ya kwanza kusikia au kusoma tangazo kama hili kwenye vyombo vya habari nikiwa na kumbukumbu kuwa jambo hili limewahi kujitokeza katika miaka ya nyuma ingawa mpaka sasa hatujaambiwa mchakato huo uliishia wapi au ni kwa kiwango gani wabunifu wetu wa mavazi waliweza kuifanya kazi hiyo kwa kadri ya maelekezo yaliyokuwepo wakati huo.

  Hata hivyo, nachelea kuwa mwepesi wa kukubaliana na hoja ya ubunifu wa vazi la taifa hasa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na maana halisi ya chimbuko la vazi la taifa au jamii fulani na mpaka kufikia hatua ya kukubalika na watu wa jamii nzima bila kutofautisha mila na desturi zao hasa pale panapokuwa na makabila tofauti na yenye mila tofauti pia.

  Kila nilipofuatilia chimbuko la mavazi ya taifa au jamii fulani nakuta kila vazi lina mizizi ya mbali kabisa ya jamii husika na pengine hata likitokana na mazoea ya jamii hizo kutumia vazi hilo au kuhamasishwa kutokana na vazi kutumika na watu wenye daraja fulani katika jamii hiyo kwa muda mrefu na hivyo kuwafanya watu wengine kupenda kuvaa hivyo.

  Tofauti na ilivyo hapa kwetu ambapo sasa wabunifu wa mavazi wanaambiwa wajitokeze ili kubuni vazi ambalo litakuwa vazi la taifa kwa kuzingatia uwepo wa rangi za bendera ya taifa. Mimi nayaona mavazi ya taifa ya nchi nyingine kuwa tu na muundo au mtindo fulani ambao huweza kutambulisha kuwa vazi hilo ni la taifa fulani bila kuwa na rangi zozote za bendera ya nchi hiyo.

  Hivi kweli katika dunia pana ya sasa yenye utandawzi wa daraja la juu, tunategemea kuibuka na vazi gani hilo ambalo litakuwa na muundo wa tofauti kabisa na mavazi yaliyopo tayari katika jamii za dunia ya sasa kiasi cha kumtambulisha mtu katika utanzania wake eti kwa sababu tu yatakuwa na rangi za bendera ya taifa?


  Hapa Tanzania, tunao ndugu zetu wamasai ambao kwa kuwatazama tu mtu hutambua kuwa hawa wanatoka katika jamii ya kimasai hasa kwa mavazi yao yaliyozoeleka kwa kujitanda nguo kubwa kama shuka na kuacha bega moja nje ambayo huku hufahamika kama “lubega”, na kujitanda shanga shingoni na mikononi, lakini pia hata kama mtu si mmasai pale atakapovaa vazi la muundo huo watu wote hutambua kuwa amevaa vazi la kimasai.

  Kadhalika wako wengine katika ukanda wa kati wa nchi hii hasa katika mikoa ya Dodoma na Singida ambao pia wameweza kwa muda mrefu kujitanabahisha kwa jamii nyingine kwa uvaaji wao wa nguo aina ya kaniki, nguo hizi ambazo aghalabu huwa na rangi nyeusi huweza kuwatambulisha jamii ya Wagogo, Wanyaturu na wengineo wa kada hiyo hasa wakina mama ambao hupenda kujifunga kuanzia eneo la kifua na kuacha mabega wazi. Inasemekana kwamba kutokana na ukame unaotawala katika maeneo hayo ya kati kati ya nchi, vazi la kaniki linakuwa na umuhimu wa pekee kwa sababu ‘linamhifadhi’ mvaaji kwa mtazamaji hata kama hatofua nguo husika kwa wakati!


  Utofauti huu wa mavazi hujitokeza hata kwa jamii za watu wa nchi nyinginezo duniani ambapo kwa kuwatazama tu unawatambua kwa urahisi kwamba wanatoka jamii gani. Mfano, ni rahisi kumgundua mama anayetoka katika jamii ya Kihindu kwa vazi lake aina ya Sari au mwanaume wa jamii hiyo aliyevaa Pajama na Kanzu fupi. Hata Mwarabu ni rahisi kumjua kutokana na mavazi yao, majoho na vilemba.

  Hili pia ni rahisi kuliona kwa jamii za watu wa Nigeria ambao huvaa kanzu kubwa kama joho lenye kufanana na suruali yake, likiwa katika muundo wa pajama pamoja na kikofia kidogo chenye mfanano na nguo zilizovaliwa, na ndivyo ilivyo hata kwa jamii nyingine zenye mavazi yanayofahamika kwa wengi.

  Lakini, hata kama utayachunguza mavazi hayo kwa jamii zote nilizozitaja na hata zile ambazo sijazitaja hapo ila wazifahamu kwa uelewa wako, kamwe hutaona uwepo wa rangi za bendera za taifa husika ambako mtu huyo anatoka. Kadhalika katika mavazi hayo huwezi kukuta hata nembo ndogo tu ya bendera ya nchi hiyo wala alama yoyote ya kumwonesha mtu utaifa wa mvaaji bali tu kwa uvaaji wake utamtambua.

  Sasa, kinachonipa wasiwasi ni juu ya hilo vazi ambalo leo wabunifu wa mavazi ya Tanzania wanaambiwa wabuni lakini kwa kuzingatia uwepo wa rangi za bendera ya taifa au nembo ndogo ya bendera ya taifa au ngao ya bibi na bwana, je, tutakuwa tunatengeneza vazi la taifa au sare ya (timu ya) taifa?

  Hapo juu nimegusia kidogo juu ya chimbuko la mavazi katika jamii ambalo sasa kwa jinsi ilivyo na mfumo wa maisha ya kisasa tutakuwa hatutengenezi vazi la taifa ila sare ya taifa ambayo mara nyingi hutumika katika matukio fulani ya kitaifa. Ndio maana utaona kuna sare ya CCM, Chadema, timu za mpira na kadhalika.


  Katika kufatilia na kuelewa kwangu vazi la jamii au taifa hujitanabahisha kwa nasibu kama ilivyo kwa chimbuko la lugha fulani ambapo jamii hailazimiki kukutana na kujadiliana kwa pamoja kuwa hili sasa liamuliwe kuwa vazi la jamii yao, tena mengi ya mavazi ya mataifa na jamii za sasa yalijitokeza katika kipindi ambacho nyingi za nchi hizo hazikuwa na bendera zao za kisiasa na hivyo kulazimika kuweka rangi za bendera katika mavazi hayo.

  Kwa kuwa mavazi ya jamii nyingi yalijitokeza kwa kuzingatia uasili wa jamii zenyewe yaliweza kukubaliwa na kutumika kwa urahisi na jamii zote bila ya kuwepo kwa mivutano yoyote kwa watu wake, sasa vipi kwa Tanzania ambako sasa kuna makabila na watu wenye imani tofauti, vazi hilo litapokelewa na kukubalika na jamii hizo bila kuonekana kuwakwaza baadhi ya watumiaji wake?

  Na kama ni hivyo, hebu tujiulize vazi hilo litakalopitishwa kuwa vazi la taifa litakuwa ni lile litakalotumiwa na watanzania wa pande zote mbili, yaani Tanzania bara na visiwani, na je, ni kweli kwamba wenzetu wa Zanzibar wao hawana vazi lao la kuwatambulisha kama watanzania wanaotokea visiwa vya Unguja na Pemba?

  Napata utata kidogo juu ya vazi hilo ambalo yaonekana kuwa ni kitu muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu kiasi cha kupewa msisitizo mkubwa kiasi hicho ingawa zoezi kama hilo halikutoa matunda yaliyokusudiwa miaka ya nyuma ambapo watanzania walitakiwa kujitokeza kwa zoezi na masharti kama hayo.

  Mara nyingine najiuliza kuwa ni nani aliyewaambia akina mama wa Tanzania wanapokuwa katika shughuli za msiba kwamba wanapaswa kuvaa vipande vya khanga au vitenge kwa kujifunga moja kiunoni na nyingine kujitanda kichwani, huku wale wasiokuwa na mavazi kama hayo wakijitahidi japo kuazima ili waweze kuhudhuria shughuli kama hizo. Je, hii haingeweza kuwa chimbuko mojawapo la vazi la jamii ambalo halina utata na linapokelewa na jamii yote?

  Ndiyo maana nasema kitu hiki hakibuniwi na jamii kama tunavyodhani bali mara zote huwa ni cha asili ya wenyeji na kina mazoea ya karne na karne kwa sababu mara nyingi historia inatuonesha kuwa vitu vingi vya kubuni au kuiga hupita na kusahaulika upesi bali lakini vile vya asili hudumu milele.

  Kama tuna kumbukumbu nzuri kuna wakati fulani aliyekuwa waziri mkuu wa China hayati Chuo en Lai aliibuka na mtindo fulani wa mavazi yasiyo na ukoa wa juu (kola) yakawavutia watu wengi siyo tu wa nchini pake bali hata wa mataifa mengine waliiga kuyashona na kuyavaa huku wakiyaita kwa jina la kiongozi huyo miongoni mwao akiwemo hayati Baba wa Taifa, Mwl. J.K. Nyerere.

  Hata kiongozi na mwasisi wa taifa la Zambia, Keneth Kaunda alibuni vazi lake lililobeba jina lake na likaenea na kupendwa sehemu kubwa ya Afrika hasa ya mashariki lakini yote hayo yamepita kwa sababu tu halikuwa vazi la asili kama yalivyo mavazi ya Wamasai, Wagogo, Wanyaturu na Wamakonde na kwa kuwa yalikuwa ya kubuni tu, kwa maana kwamba hayatokani na asili ya wananchi husika, yalipita na kusahaulika haraka. Siyo hao tu wengine ni Mobutu na mzee Nelson Mandela ambaye baada ya kutoka gerezani alitoka na mtindo wake wa mashati yaliyowavutia watu wengi pia.

  Ninachotaka kuonesha hapa ni kwamba vazi rasmi halibuniwi kwa kutafuta maoni kama yale ya katiba mpya la hasha, ni mtindo na mazoea tu yanayoibuka kama nasibu na hatimaye kuvutiwa na kupendwa na watu au jamii kubwa.

  Hivyo basi kumbe mitindo hii ya mavazi ya kitaifa kama nilivyokwishaandika hapo mwanzoni mwa makala hii siyo tu kwamba ilibuniwa rasmi na mataifa hayo kupitia mchakato kama huu tunaoendelea nao hapa nchini petu, bali mitindo hiyo huibuka tu ama kwa nasibu, mila, desturi au tamaduni za taifa husika tena ikirithiwa kwa mazoea toka kizazi hadi kizazi kwa karne nyingi na siyo kitu cha kubuni kupitia kamati, vikao na kukusanya maoni.

  Ninamaliza makala hii kwa kusema, huu ni mchakato wa kuunda “sare” ya taifa kama ile ya timu ya taifa na siyo vazi la taifa. Nasema hivyo nikiwa pia na mashaka juu ya mwitikio wa Watanzania kulivaa vazi hilo lisilo la asili kama kaniki na khanga au yale mavazi ya kimasai na makabila mengine niliyokwishayataja. Wasiwasi wangu ni kwamba litatoweka haraka sana kama Chuo en Lai na Kaunda suti kwa kuwa siyo la asili kutoka mojawapo ya makabila yetu.
   
 2. KakaJambazi

  KakaJambazi JF-Expert Member

  #2
  Feb 3, 2012
  Joined: Jun 5, 2009
  Messages: 15,030
  Likes Received: 3,231
  Trophy Points: 280
  Huo ni ulaji wa wachache. Mwisho wa siku itashindikana ila waandaaji washakula perdiem.
   
Loading...