Historia ya Wasafwa wenyeji wa Mbeya wao huita imbeya au bheya

justin mwanshinga

Senior Member
May 22, 2014
179
619
Wasafwa ni kabila toka jamii ya wabantu wanaozungumza lugha yenye uhusiano wa moja kwa moja na kibantu yaani lugha ya kisafwa.
Kwanza tuangalie nini au chanzo cha neno Safwa.
Neno safwa;
Kihistoria wasafwa ni watu wanaopenda sana kuishi maeneo yenye mvua nyingi na ubaridi, hi ni kutokana na wao kuwa ni wakulima wa mazao yanayohitaji mvua mfano viazi mviringo, vitunguu swaumu, mahindi na numbu. Historia inasema kwamba kulitokea vita baina ya wasafwa na jamii zilizowazunguka wakigombea maeneo ya kilimo. Katika vita hiyo kuliibuka mapigano makali mno ambapo ilionekana kuna watu wanapigwa lakini hawafi. Kwa kisafwa mtu asiekufa huitwa au hicho kitendo huitwa ASIFWA yaani hafi. Kwa maana nyingine ili umuombee mtu mabaya na afe unatamka "asafwa" . Na moja kwa moja jamii hiyo ikaitwa safwa yaani kabila la wasafwa.

Asili na chimbuko la wasafwa.
Zipo nadharia nyingi zinazoelezea asili na chimbuko la wasafwa toka mbeya ambao ndio wenyeji haswa wa mbeya. Ikumbukwe hawa ni wabantu, hivyo basi ni jamii za kibantu toka afrika magharibi. Lakini nadharia na masimulizi haya yamegawanyika kama ifuatavyo,
1. Wasafwa ni wa kutoka ugogo dodoma.
Nadharia hii inasaidiwa na ukweli hasa kwenye salamu, kuna wasafwa wakisalimiana utaskia "mwagona gogo " , ambapo humaanisha kuwa wao ni kutoka ugogo Dodoma. Tatizo ni kwamba hawana uthibitisho wa kutokua wabantu hivyo nadharia hii huwa butu katika ukweli ijapokua wao huwamini hivyo.

2. Wasafwa ni kutoka ukinga makete.
Hapa napo kuna ushahidi, ambao unaelezea kuwa wasafwa ni jamii toka ukinga, nadharia hii inashibishwa na salamu pamoja na wasafwa waishio kata ya ilungu, igoma na ulenje mbeya vijijini. Katika suala la salamu baadhi husalimiana "mwagona nkinga " , wakimaanisha kuwa hujambo mtu toka ukinga. Pia wao huamini kuwa ni matokeo ya msafwa, mkinga, mnyakyusa na muwanji. Lakini nadharia hii Pia inashadadiwa na ukweli kwamba katika kata hizo ni kweli wapo wakinga wengi mno ambao kwa sasa hujiita wasafwa na wanafuata mila na taratibu za kisafwa. Ni dhahiri kuwa wapo watu na koo kama kyando, swallo, longopa, chaula, Enea na nyingine nyiiingi ambazo ni matokeo ya wazee wao kuhamia usafwani hasa tarafa ya tembela mbeya vijijini.

3. Wasafwa ni kutoka unyakyusani.
Nadharia hii ipo katika salamu, ambapo wapo wasafwa wanaosalimiana "mwagona hondya " ,
Wakimaanisha hujambo toka unyakyusani, . Ikumbukwe wasafwa huwaita wanyakyusa "wahondya " , nadharia hii inashibishwa na watu waishio tarafa ya Tembela mbeya vijijini hasa ilungu na igoma. Ushahidi wa nadharia hii unashibishwa zaidi na masimulizi ya wazee yahusuyo watu wa ajabu waliokua wanakula watu wenzao, kwa kisafwa waliitwa "Ayinga " . Hawa ni viumbe waliokua wanapatikana maeneo ya pembezoni mwa safu za mlima livingstone, ambao walisababisha jamii za watu wa kule hasa mwakaleli kukimbilia mbeya vijijini hasa maeneo ya ilungu na igoma. Mmoja wa wahanga hao ni ukoo wa Mwanginde Mkoma ambao unawakuta mwakaleli na ilungu mbeya vijijini.

Katika makala yangu ijayo nitawaleteeni masimulizi kuhusu watu wa ajabu waliokua wanakula wenzao huko usafwani na kuzunguka safu za mlima livingstone ambao Pia ni matokeo ya baadhi ya wanyakyusa wa enzi hizo kukimbilia usafwani.

4. Wasafwa ni wasangu
Hapa Pia salamu ndio ushahidi na kigezo cha Kwanza. Hawa husalimiana "mwagona nsangu au nsango au sango " , wakimaanisha hujambo mtu wa usangu. Hawa ni wengi uyole, mswiswi, igurusi, inyala na itewe. Wao huamini kuwa ni matokeo ya msafwa na msangu kwa baba. Ikumbukwe kuwa msangu alishirikiana na mbena kumshambulia muhehe ambapo baada ya kushindwa akamvamia msafwa.

5. Wasafwa ni kutoka Botswana.
Nadharia hii inashadadiwa na maelezo ya ufanano wa wasafwa na watu wa Botswana hasa katika ngoma za asili kama nyimbo na mtindo wa maisha. Inasemekana kuwa wasafwa walitoka Botswana wakaingilia Moja kwa moja njia ya msumbiji hadi makete kisha mbeya. Wengine hudai kuwa waliingilia dodoma . Ugumu wa nadharia hii upo katika ubantu maana kama ni ubantu asilimia kubwa ya jamii za kusini mwa jangwa la Sahara ni wabantu.

6.wasafwa ni kutoka nchini kongo.
Hapa ndipo penye maelezo mapana maana hawa ni wabantu na kwa kuthibitisha hilo Zipo shahidi toka koo mbalimbali kama Mwatumbo na Mwanshinga. Ifahamike kuwa wapo wanaoamini mwanshinga ni msafwa mkinga na Mwatumbo ni msafwa wa uwanji . Lakini historia inaonesha kuwa hawa ni wasafwa toka kongo hasa misitu ya kongo, ukweli huo unashibishwa na maelezo kwamba ,
Asili ya mwanshinga Ni historia ndeeeefu ambayo kwa ufahamu na masimulizi hapa Ni kurudi nyuma yaani kutrace back the background of Safwa tribe. Ambapo tunaambiwa wasafwa Ni kabila toka kundi la makabila yafahamikayo kma wabantu wanaopatikana hasa kusini mwa jangwa la Sahara wazungumzao lugha ya kibantu yenye ladha ya ubantu Na muingiliano Na makabila mengine ya kibantu.

Hivyo basi historia inasema WASAFWA Na mwanshinga kwa ujumla asili hasa Ni Africa magharibi hadi Sudan kusini, Na baadae wanahama kwa sababu mbalimbali . Ndipo wanasafiri hadi CONGO ya Leo hasa misitu ya Congo na pembezoni kwayo.

Baada ya miaka mingi WASAFWA Na mwanshinga kwa ujumla wanahamia mbeya kwa misafara miwili , ambapo mmoja unaingilia sumbawanga -tunduma hadi mbeya mjini Na baadae mbeya vijijini ya Leo.

Msafara mwingine unaingilia zambia- malawi- msumbiji Na kuingilia makete yaani ukinga hadi mbeya vijijini Na mjini Na hasaaa ukoo wa mwanshinga. Hawa na wengine wengi ndio wale wanaosalimia "mwagona kinga" . Wasafwa hawa wengi wao ni koo za kichifu na kwa maana hiyo hata Leo chifu wa mbeya ni msafwa wa jamii hii.
Lakini zipo nadharia zingine husema walitokea Botswana ijapokua haina mashiko Sana.

Baadhi ya shahidi kuwa walitoka Congo na huko Sudan kusini ni uwepo wa majina kama vile majina yapatikanayo Congo WAMBI, NGATELEE, MWINGA, MBWIGA, SELINA , SILYELELO n.k.
PIA
Kitendo Na tabia ya kupenda kuishi maeneo yenye mvua nyingi kma vile mbeya , Arusha Na Kilimanjaro Ni sawa Na mvua zipatikanazo misitu ya kongo.
PIA kupenda kilimo haswa viazi mviringo.
Misafara hiyo inasemekana ilitengana baada ya kutokea sintofahamu wakiwa njiani toka kongo, walipofika njiani wengine wakasonga kuelekea Zambia, malawi, msumbiji pembezoni mwa ziwa nyasa hadi makete ya Leo. Huko wakakaa na kuishi wakichangamana na wenyeji yaani wakinga na wawanji na baadae watoto wanazaliwa na wengine kuhamia mbeya vijijini. Hawa walikua ni wale wanaopenda kuhamahama na kwa kuwa tayari mbeya kulikua na wa safwa walioingilia Tunduma hadi mbeya mjini ikawa rahisi kwao kuingia mbeya kwa kupitia njia ya makete isyonje yaani hasa kata ya ilungu ambayo ilikua kama lango.
pia historia inaendelea kudai kuwa kundi la Wasafwa waliopitia Sumbawanga walikutana na wafipa wa Sumbawanga na wakaendelea na msafara kuelekea mashariki na baadaye ndio wanakuja wanakutana kwenye mgongano na wasangu ambapo muda huo kulikua na mvutano kati ya wasangu na wahehe chini ya mkwawa na hivyo wakaanza kusambaa maeneo ya Mbeya.

Hitimisho.
Wasafwa ni wabantu toka kusini mwa jangwa la sahara. Wasafwa toka mbeya ni mchanganyiko wa makabila kadhaa kutokana na muingiliano wa shughuli za kibinadamu. Lakini msafwa hasa ni yule mwenye asili ya kongo, Kwa hiyo tafiti mbalimbali zimehitimisha kuwa katika hizo nadharia 6 kuhusu asili ya msafwa nadharia namba 6 isemayo ni wabantu toka africa magharibi _ sudan kusini _ kongo kisha Tanzania ndio yenye ukweli na uhalisia maana wabantu wengi walitoka huko. Kwa hiyo nadharia tano zinazobaki zina uhalisia kwa asilimia ndogo sana kutokana na ukweli kwamba zinamezwa na hiyo namba 6. Hi ni kwa sababu zenyewe ni matokeo ya muingiliano wa kijamii baina ya wasafwa na jamii zingine . Ukweli ni kwamba vita, njaa na ustaarabu vilipelekea wasafwa kuingiliana na jamii nyingine. Mfano baada ya vita kati ya merere na chifu lyoto wa usafwa mabinti wawili wa kisafwa walitolewa kama zawadi kwa chifu merere baada ya kushinda. Kwa hiyo msafwa asili asie na mchanganyiko enzi hizo ni yule wa mbeya mjini.

MGAWANYIKO WA MAKUNDI YAUNDAYO KABILA LA SAFWA
Wasafwa wamegawanyika katika makundi makubwa matano na kimaongezi au matamshi wamegawanyika katika makundi kumi. Katika makundi hayo matano kuna ,
1. Wamporoto
Hawa ni wasafwa wanaozungumza kisafwa chenye ladha tofauti na makundi mengine. Hawa hupatikana kwa wingi na kwa kiasi mwakaleli number one, kiwira, isyonje, ndaaga, ntokela wilaya ya rungwe na baadhi ya maeneo ya maendeleo, tembela na ijombe mbeya vijijini.
Wao ni matokeo ya msafwa kwa wingi na mchanganyiko wa baadhi ya makabila.

2. Wasongwe
Ni wasafwa wazungumzao kisafwa chenye ladha ya kipekee na makundi mengine. Hawa huzungumza na kuelewana zaidi wao kwa wao maana ni wasafwa wa songwe. Wanapatikana na kuishi kwa wingi mbalizi, utengule usongwe, mshewe, usongwe, swaya, igale, iwindi na maeneo ya wilaya ya mbozi. Pia wapo Tunduma na mbeya mjini kwa kuhamia.
Pia
Mmalila na Mnyiha kihistoria wote walitokana na koo za Wasafwa ambao walitawanyika kwa lengo kujihami/kuzuia kushambuliwa na Maadui wakati wa mapigano yaliyokuwepo enzi hizo. Wasafwa wa utengule na mshewe ndio hasa inaaminika ni matokeo ya mnyiha wa leo na mmalila. Kuna mzee alisema Wamalila wametokana na neno "Malila" yaani sehemu ambayo maadui walikuwa wanayoishia na lengo kuu ni kwenda kuzuia maadui sehemu wanazoishia na kwa upande wa "Wanyiha" anasema ni neno lililotokana na sehemu ambako maadui walielekea au kukimbilia wakati wa mapigano hivyo basi hata matamshi yalikuwa yanabadilika kwa kadiri walivyokuwa wanakutana na kuchangamana na jamii zingne huko walikoelekea.

3. Wagulukha
Hawa wanaishi na kupatikana kwa wingi chunya, ikukwa, ihango, lwanjiro na mbeya mjini. Wao ni tofauti kidogo kimatamshi na wale wa maeneo mengine. Hawa wengi wameoa na kuolewa na wabungu toka chunya na kiasili wao ni matokeo ya vita kati ya merere na chifu lyoto mbeya mjini ya Leo.

4.wambwila
Hawa wanaishi na kupatikana kwa wingi ilungu, igoma, ulenje, makete na mbeya mjini. Hawa huzungumza kisafwa cha kipekee mno, wao Pia ndio lango kuu la mkinga kuingia mbeya mjini. Wanazungumza zaidi kisafwa kiitwacho kimbwila. Wengi wao huishi nje ya mji yaani milimani kwenye mvua nyingi kwa ajili ya kilimo hasa mbeya vijijini. Moja ya kata zenye wasafwa waliochanganya damu ni ilungu, ulenje na igoma na tarafa ya tembela kwa ujumla. Mfano ndani ya kata tajwa hpo juu, unakuta kuwa hao ni wasafwa waliotokana na mchanganyiko wa wasafwa, wasangu, wawanji, wakinga, wanyakyusa na wabena kiasi . Na kundi la mwisho ni

5. Wamalila
Upo utata kuhusu kundi hili kama ni kabila au kundi ndani ya kabila. Ifahamike kuwa neno wamalila kwa kisafwa lina maana ya uchafu mwilini uliowekwa kishirikina yaani " amalila " .
Sasa ukiwauliza wamalila wao husema asili yao ni botswana na wengine husema ni mlima mbeya sababu ambayo ni sababu ya asili ya msafwa kufikia yaani mlima mbeya. Kuhusu botswana historian haifafanui vyema.
Ila
Hili ni kundi ambalo kwa wasafwa ni kundi lililojitenga na wenzao kwa kiasi. Wanaishi tarafa ya isangati yote na maeneo ya usongwe.

pia katika kundi la wamalila kuna wamalila wapo kule na ushahidi wa kuthibitisha waliendaje kule ni kwamba ,
katika kipind cha mgogoro na mtemi merere kuna moja kati ya watu wa kisafwa alipambana kumuua askari mmoja wa mtemi merere na kukimbilia maeneo ya mbozi eneo hilo likiitwa ntandala na baadaye alioa huko ila hakuendelea kukaa huko aliamua kurudi ijapo hakufika eneo lake la nyumban ila huyo shujaa aliweza kuishi maeneo ya umalila na maisha yake yaliendelea hapoo alikuwa ni mtu kutoka ukooo wa Nswila watu wanopatkana kwa wingi maeneo ya iwindi hadi leo na kidogo umalila

Historia na Ifahamike kuwa mbeya haswa kulikua na makabila au jamii nne tu nazo ni wasafwa, wanyakyusa, wasangu na wanyamwanga.
Wajiitao walambia na wandali ni matokeo ya mnyakyusa, wamalila na wanyiha ni kutoka usafwa, wabungu wa chunya ni matokeo ya makutano ya kuoana kwa msafwa, msukuma na mnyamwezi kisha kukawepo mbungu. Baadae wakahamia wakinga, wabena na wawanji toka iringa

Hitimisho
Makundi haya yamegawanyika Pia katika matamshi, mfano ndani ya kata moja unakuta kuna utofauti mdogo kimatamshi.

NGOMA ZA ASILI
ngoma kuu ya asili ya wasafwa ni ngoma ichezwayo wakati wa sherehe, matambiko na mavuno. Ngoma hii maarufu huitwa " mbeeta " . Huchezwa kwa kutumia filimbi, pembe za wanyama, mbegu zilizo ndani ya makopo na vingine vingi. Ngoma za asili huchezwa kwa sasa hasa itewe, ikukwa na ifumbo. Hakika kwa kule bado wanaenzi asili.

KILIMO
Wasafwa ni kabila la wakulima ambao hulima sana viazi, mahindi, ngano, numbu, karanga, maharage na mazao mengine kama miti. Wasafwa Pia ni wafanyabiashara hasa viazi na vitunguu swaumu. Wasafwa hulima sana maeneo yenye mvua nyingi kama rungwe na mbeya vijijini.
Pia hujishughulisha na biashara

Kutokana na kilimo wametawanyika Tanzania na kwenda maeneo yenye mvua, wapo kwa wingi Arusha hasa Arusha chini na meru, wapo mang'ola karatu, muheza Tanga, west kilimanjaro, usa Arusha, muffindi iringa, njombe, makete na morogoro.

WASAFWA NA MBEYA
Neno mbeya ni neno litokanalo na lugha ya kisafwa likiwa linatamkwa ibheya likimaanisha chumvi. Wafanyabiashara walifika mbeya na kubadilishana chumvi toka chunya na mlima mbeya kwa bidhaa nyingine. Ilikua ni ngumu wageni kutamka neo ibheya na hivyo wakajikuta wanatamka imbeya. Baadae miaka ya 1927 wakati wa usanifishaji wa kiswahili neno hilo likasanifishwa na kuwa mbeya.
Pia
Maneno asilimia 90 ya maeneo ndani ya jiji la mbeya yanatafsiriwa kwa kisafwa.
Mfano neno mbalizi _ mbalisi
Loleza _ lolezya (sindikiza)
Uyole _ iyoole
Igawilo _ kigavilo ( sehemu ya kugawania )
Isyesye _ inzyesye
Iwambi _ wambi
Ijombe _ aina ya mti
N. k
Kiongozi mkuu wa kimila huitwa Mwene na kwa sasa Mwene ni Rockety mwanshinga.

MAJINA YA WASAFWA
Majina ni sehemu ya utamaduni wa wasafwa, mtoto hupewa jina kutokana na tukio au kumbukumbu flani. Mfano mtu akiitwa Nzala, huyo alizaliwa kipindi cha njaa.
Mbwiga _ mtoto wa kiume aliekua kwa kuumwa umwa na kupewa madawa
Mbozyo _ mtoto wa kike aliekua kwa kuumwa umwa na kutibiwa kwa miti shamba

Pia kuna jina kwa Kisafwa "Nkundi'.
Jina hili anapewa mtoto ambaye watangulizi wake wote wamefariki. Zamani kulikuwa na shida kubwa ya kufa watoto kwa mfuatano katika familia, na kwahiyo basi mtoto aliyekua vyema alipewa jina la Nkundi, maana ya Inkundi kisafwa ni vumbi. Sasa wazazi walitoa jina hilo kwa kuonesha kukata tamaa kuwa hata huyo aliyezaliwa atakuwa mali ya vumbi.

"Esose' kwa Kisafwa maana yake ni kuzaa mtoto asiye na baba rasmi. Zamani hii ilikuwa ni tukio la nadra sana na ilionekana ajabu sana kusikia binti wa fulani "asosile umwana"
Vinginevyo siku za huku baadaye majina haya yamekuwa yakitumiwa tofauti na maana zake halisi kutokana na ukweli kwamba akina bibi wanarithisha majina yao ili yaendelee kuwepo hata baada ya wao kutoweka.

Wapo watoto sasa hivi wanaitwa 'Matundu' bila maana halisi ya neno hilo.
Matundu kwa kisafwa ni majani ya mmea wowote. Mtu alipoitwa Matundu ilimaanisha kuwa amepatikana kwa njia za madawa ya majani asilia.

Pia yapo majina ya koo na mengi huwa na MWA...... mwanzoni mfano mwalingo, mwanyanje, mwaihoyo, mwantinda, mwandele, mwanzanga, mwasote, mwanzanga, mwangoka, mwanandodo, mwaanzala , mwanyonga , mwanzonga , mwalyambi ,mwajafu, mwansanga , mwanguku , mwaamudu, mwalyego, mwandiya , mwasoni, n. k.
Pia wapo akina
manzozi, magwilla, sijanga, sijonjo, simwinga, yilyelelo, ndabhishe, masimbani , lyoto , lingo, Ngatele , Ndaduu, Ndilwene , Ndangano, Gwilla , zyoni ,malema , nzalu, sewa, selina, Nsolo, sambwe , nzambwe , mponzi , zella , Ndongole ,Nzongwa, shitambala, fwokile, selela, na mengine meeengi.

Koo kuu za wasafwa ni ,
Mahinya
Malema
Zambi
Zella
Ringo
Mponzi
Ndabhishe
Ngatele
Lyoto
N.k

Siku hizi watoto wengi wa mbeya yaani wakisafwa hupewa majina kutokana na ama baba ni mpenzi wa mchezaji fulani au mwanamziki. Wapo kwa sasa watoto huitwa Ronaldo, Beckham, Rooney, Nelly, Awilo, Yesu, lowasa, kikwete, mess, Zidane na mengine meengi

DINI NA MIUNGU
Wasafwa wengi wao ni wakristo na wapagani. Ni ngumu sana kumkuta msafwa mwislamu. Wale wapagani husali maeneo ya misitu maarufu "maganjo " kama lile lililopo pale jijini mbeya. Wengi bado wanaamini katika miungu. Ni ukweli kwamba 50% ya wasafwa ni wakristo na 50% wapagani.

Uchawi mkuu kwa wasafwa huitwa ITUNGA na wale wauaji wa kichawi huitwa MBUDA. Mambo haya ni ya kimila hivyo imekua ngumu sana kuwabadilisha baadhi ya watu .

Yapo mengi sana kuhusu wasafwa na mbeya yao, ila kwa kuhitimisha tu kwa hii historia fupi ni kwamba hawa wasafwa ndio wenyeji wa mbeya. Ni wabantu wazungumzao kisafwa kibantu.
Salamu yao kuu ni Mwagona.
_______________________________________________________

Shukrani za pekee kwa wazee wote niliopata simulizi zao wakiongozwa na babu zangu, bibi na watalamu kadhaa. Pia heshima kwa wote mlioongezea kwenye groups mbalimbali. Kama una nyongeza karibu sana kwa maoni.

Napatikana
Facebook Justin Mwanshinga
Mwanshingaj@gmail.com
Twitter Justinmwanshinga
Instagram Justin Mwanshinga
Jamii forum Justin Mwanshinga.
 
Wasafwa nimeishi nao mbeya ni watu poa Sana ila ukimchokoza msafwa vita yake huwa haiwez kuisha ni watu wa kulipa kisasi .

Mkoa wa mbeya kama unataka kuoa mwanamke bora kuoa msafwa ni wachapakaz na wavumilivu sana kwenye ndoa na wana misimamo sana .
 
Wasafwa nimeishi nao mbeya ni watu poa Sana ila ukimchokoza msafwa vita yake huwa haiwez kuisha ni watu wa kulipa kisasi .

Mkoa wa mbeya kama unataka kuoa mwanamke bora kuoa msafwa ni wachapakaz na wavumilivu sana kwenye ndoa na wana misimamo sana .

Nilikuwa na girl friend Msafwa. It was a pleasure having her as a girl friend.

Asante mleta mada kwa kushare hii kitu.
 
Historia nzuri sana. Kama mwenyej wa mbeya nimefurahi kujua historia ya hawa majirani zetu.
 
Wasafwa nimeishi nao mbeya ni watu poa Sana ila ukimchokoza msafwa vita yake huwa haiwez kuisha ni watu wa kulipa kisasi .

Mkoa wa mbeya kama unataka kuoa mwanamke bora kuoa msafwa ni wachapakaz na wavumilivu sana kwenye ndoa na wana misimamo sana .
Mie ninae mmoja na mungu akipenda next year naweka ndani kabisa. Bonge moja la mwanamke!
 
Nipo hapa Msafwa upande wa mama! Baba yake na babu yangu alitokea Botswana akaja ku settle Utengule Mbalizi!! Aliitwa NKWETSO! Wasalipa jomba
 
6 Reactions
Reply
Back
Top Bottom