HISIA ZA EDO KUMWEMBE: Simba SC itacheza na ''Wasoweto wagumu'' zaidi

Joseverest

JF-Expert Member
Sep 25, 2013
51,992
69,391
SIMBA wameileta timu nyingine kutoka Afrika Kusini ambayo ilikuwa haijawahi kugusa ardhi ya Tanzania. Mamelodi Sundowns wamewahi kugusa hapa. Manning Rangers wamewahi kugusa hapa. Santos wamewahi kugusa hapa.

Zilibaki Kaizer Chiefs na Orlando Pirates tu. Timu mbili kubwa Afrika Kusini. Moja ni ya tajiri Ivan Khoza, nyingine ni ya tajiri Kaizer Motoung. Kaizer walikuja msimu uliopita wakaondoka wakiwa wanakumbatiana kwa furaha licha ya kuchapwa mabao 3-0. Walishamaliza mechi Soweto wiki moja iliyopita. Na sasa Simba wanatuletea watani wao wa jadi, Orlando Pirates. Kule kwao unaweza kuwaita kwa kifupi tu kama Pirates. Watakuja hapa wiki ijayo wakiwa ni mtihani mgumu kwa Simba kuliko pambano la Kaizer Chiefs. Utakuwa mtihani mgumu hasa.

Kuna sababu nyingi kwamba huu ni mtihani mgumu kwa Simba. Mtihani wa machozi, jasho na damu. Wanaonekana kujiandaa kukabiliana na Wazulu lakini waongeze juhudi na maarifa. Juzi walikubali kuuachia ubingwa wa Ligi Kuu pale Moshi baada ya kuwaacha nje wachezaji mastaa kujiandaa na pambano hili. Lakini haitoshi. Waongeze maarifa hasa. Kwanza ni kwa sababu pambano la kwanza litachezwa nyumbani Temeke halafu pambano la pili ndilo litachezwa Soweto, Afrika Kusini. Simba watalazimika kumaliza kazi Dar es Salaam kabla ya kusafiri kwenda ugenini. Haitakuwa kazi rahisi kufunga mabao mengi dhidi ya Pirates. Kwa kifupi to Pirates ni bora kuliko Kaizer Chiefs. Wanaweza wasiwe mabingwa kwa sababu ubora wa Mamelodi umekwenda mbali zaidi na kuwageuza Chiefs na Pirates kuwa wanyonge wao, lakini katika hizi timu mbili kati ya Chiefs na Pirates ni wazi kwamba Pirates wapo vizuri zaidi.

Katika nchi ambayo inategemea wachezaji wengi wazawa katika kikosi cha timu ya taifa, Pirates ina wachezaji wengi mahiri ambao wanatamba na kikosi cha Bafana Bafana. Hawa ni kina Thembinkosi Lorch na wengineo. Haishangazi kuona katika miaka sita iliyopita Pirates wamecheza fainali mbili za Afrika.

Haishangazi kuona pia kwamba katika hatua ya makundi wao ndio wamefunga mabao mengi zaidi na kufungwa machache zaidi. Wamefunga mabao 15 na kufungwa matano tu. Labda walikuwa na wapinzani wenye afya duni, lakini inakupa picha kwamba wao ni watu wa namna gani. Ni watu hatari. Wakati Simba wakifikiria kuichapa Pirates mabao mengi nadhani pia wanapaswa kufikiria namna ya kuanza kuzuia ufungwaji wa mabao mengi ugenini. Ni tiba ambayo imeanza kukosa sawa kwao. Kila msimu katika michuano ya Afrika lazima wataruhusu mabao mengi ugenini.

Fikiria walivyofungwa mabao mengi ugenini. Dhidi ya Al Ahly, Vita, TP Mazembe, Kaizer Chiefs, na hata majuzi wameruhusu mabao mengi pale Benin dhidi ya Asec Mimosas. Iko wapi tiba hii? Wamepita makocha tofauti lakini wote wanapokea vipigo hivi.

Matumaini makubwa kwa Simba ni kuona kama watarudia kile walichokifanya dhidi ya Zamalek katika ardhi ya Misri miaka 20 iliyopita. Walishinda bao moja Dar es Salaam halafu wakafungwa bao moja Misri. Wakaenda katika matuta na kupata yote huku Hayati Christopher Alex Massawe akishindilia penalti ya mwisho.

Nini kilitokea? Simba sio tu kwamba walikuwa na wachezaji bora wanapokuwa na mpira, lakini walikuwa na wachezaji wavumilivu pindi wanapokuwa hawana mpira. Hawa wa leo sio wavumilivu hasa ugenini na kama wanataka kuitoa Pirates inabidi waanzie hapo.

Pengine mechi ambazo Simba walifungwa mabao mengi ugenini katika miaka ya karibuni hazikuwa ngumu kuliko ile. Tatizo ama makocha walikosa mbinu au wachezaji hawakuwa na uvumilivu katika kukabiliana na mashambulizi ya wapinzani. Lakini inawezekana pia wakati mwingine Simba hawa wanajiamini na kucheza kila mechi kama vile wapo nyumbani. Wanaacha mianya mingi ya kushambuliwa huku pia wakiendelea kuwa wabovu katika mipira iliyotengwa. Mara ngapi wameruhusu mabao ya kona na krosi?

Kitu kingine ni kujaribu kupima kama suala la VAR litakuwa na msaada mkubwa kwa wageni au wenyeji. Tuhesabu matukio kadhaa ambayo yalitupa nafuu tukiwa nyumbani au yaliwapa nafuu wenyeji wakiwa makwao. Matukio yaliyotupa nafuu ni mengi zaidi. Mojawapo ni bao la Berkane. Lingesimama kama kungekuwa na VAR. Kumkosa Clatous Chotta Chama katika michuano hii ni tatizo jingine. Katika nafasi yake hakuna mchezaji ambaye amejihakikishia nafasi. Ina maana kwamba hakuna ambaye amevaa viatu vya Chama ingawa juzi ilinishangaza kuona kocha anamuweka nje pambano dhidi ya Polisi Tanzania ingawa hachezi michuano ya Shirikisho. Kumkosa Bernard Morrison ugenini pia ni tatizo jingine. Kama hauna Chama, kama hauna Hassan Dilunga, basi Morrison ni mchezaji ambaye anasababisha mambo yatokee. Mara ya pili hii Simba inamkosa Morrison katika ardhi ya Afrika Kusini kwa sababu ambazo bado hazijaelezwa kiundani. Mwisho wa siku Simba itabakia kuwa Simba tu katika Uwanja wa Mkapa. Imeonyesha hivyo mara nyingi. Hata hivyo kwa wachezaji wa kizazi hiki, hii ni mechi ya maisha yao. Itakuwa mara ya pili Simba kwenda nusu fainali katika michuano mikubwa ya Afrika kama wakifanya hivyo.

Waliwahi kwenda nusu fainali mwaka 1974 dhidi ya Mehal Al Kubra. Mwaka 1993 walipokwenda fainali za CAF tunaweza kusahau kwa sababu ile ilikuwa michuano ya tatu kwa ukubwa. Ilianzishwa ghafla na tajiri mmoja kutoka Nigeria na haikuwa na tija iliyopitiliza kama michuano ya Ligi ya Mabingwa au Shirikisho.

Hii ni michuano hasa ambayo Simba wana fursa ya kujiwekea heshima. Bahati mbaya, kwa mtazamo wangu wao ndio wamepewa timu ngumu zaidi katika michuano kwa timu ambazo zimebaki. Afadhali wangepewa Waarabu wa Libya au TP Mazembe ambayo kwa sasa ipo katika ubavu wetu.

Na endapo Simba watavuka katika hatua hii nawapa nafasi ya kwenda fainali moja kwa moja. Sidhani kama kutakuwa na kizuizi kwao. Na kama wakifika fainali nani anajua ambacho kitatokea? Lolote linawezekana.

Chanzo: Mwananchi
 
Wachambuzi wa michongo , Kwani wao wanaionaje Simba.

Mpaka hapo alipofikia Simba kajituma sana , ni heshima kubwa kwa klabu na Taifa.

Kwani Simba Sisi hatuhitaji matokeo ,Pirates wajipange zikipungua sana wanakula 3.
 
Wachambuzi wa matembele katika ubora wenu uyo pirates wenu endeleeni kumpeti peti j,tatu mrudi tena na nyuzi zenu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom