Edo Kumwembe: Kwaheri kwasasa Fiston Mayele

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
998
ALIKUJA, aliona, alitawala, ameondoka. Fiston Kalala Mayele. Mara yangu ya kwanza kumuona ilikuwa ni katika jiji la maraha la Marrakeich pale Morocco katika maandalizi ya msimu mpya Julai 2022. Hakuwa jina maarufu miongoni mwetu. Baada ya virusi vya corona kuvamia katika kambi ya Yanga na kisha tukatawanyika, Yanga wenyewe huku Tanzania walikuwa wanasubiri kwa hamu kumuona Mzee wa kuwajaza, Herietier Makambo. Mayele akayapeleka maisha katika mkondo tofauti.

Usajili wa Makambo ulivuma kuliko wake lakini ilimchukua Mayele kipindi cha kwanza tu cha pambano la Ngao ya Jamii dhidi ya watani wa jadi kuandika jina lake katika historia ya Yanga. Jaribu kukumbuka namna alivyomfunga Aishi Manula baada ya kuunganisha kwa haraka pasi ya Farid Mussa.

Pale ndipo watu walishtuka kwamba huenda Yanga ilikuwa ina mfalme mpya badala ya Makambo ambaye walikuwa wamemsubiri kwa hamu baada ya kurejea kutoka Horoya ya Guinea. Baada ya hapo Mayele akaitambulisha staili yake ya ushangiliaji ya kutetema. Kilichoendelea baada ya jioni ile kimebakia kuwa historia.

Mayele ameacha alama katika soka letu. Anaondoka akiwa ameuzwa bei ghali. Bei ambayo hakuna mchezaji wa soka la Tanzania amewahi kuuzwa. Inasemekana ni dola milioni 1. Ni zaidi ya Sh2.4 bilioni za Tanzania. Pesa yetu ya madafu haina thamani.

Achana na alama ya pesa ambayo ameacha, kitu cha msingi zaidi ni alama ya mabao aliyofunga. Mayele hajafunga mabao mengi zaidi ya Meddie Kagere au Amiss Tambwe katika soka letu. Labda wao wamecheza muda mrefu zaidi kuliko yeye.

Kitu kikubwa ambacho ni aina yake ya mabao. Aliyafunga mabao kama mshambuliaji halisi zaidi kuliko hao wageni wengine. Alifunga mabao ambayo yalitustaajabisha kwa sababu alifunga katika mazingira magumu zaidi. ilikuwa nadra kwa Mayele kufunga mabao rahisi.

Aliwakumbusha vijana wengi wa Kitanzania namna ambavyo wana safari ndefu kufikisia hadhi ya kuitwa washambuliaji hatari. Mayele alikuwa mwepesi katika kugeuka, mwenye kasi na mwenye mashuti ya ghafla.
Msimu huu ulioisha alituonyesha hilo kiasi kwamba lilikuwa suala la muda tu kabla ya kuuzwa kwenda katika timu kubwa. Alikuwepo katika orodha ya washambuliaji hatari wa ndani katika Bara la Afrika kiasi kwamba aliitwa katika kikosi cha Congo na huko pia akafanikiwa kutetema.

Zaidi ya hayo ukweli ni kwamba ubora wa Mayele kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na uimara wake kimwili ambao sina shaka umetokana na nidhamu yake kubwa aliyokuwa nayo nje ya uwanja. Nawafahamu wachezaji wa Kitanzania na wageni ambao wangekuwa hawashikiki mitaani kama wao wangekuwa wanasifiwa kama Mayele.

Umaarufu wa Mayele uliwafikia kina dada zetu ambao kwa kiasi kikubwa walifurahia staili yake ya kushangilia. Ni wazi kwamba ulikuwa ni uamuzi binafsi wa Mayele mwenyewe kuendelea kuheshimu maisha yake nje ya uwanja. Jambo hili ni muhimu zaidi.

Lakini kuna nidhamu nyingine ambayo imemfanya Mayele aondoke kwa heshima Yanga. Inadaiwa kwamba Wacongo wenzake, Djuma Shaaban na Yannick Bangala hawakuondoka vema Yanga baada ya kutofautiana na uongozi katika masuala mbalimbali.

Katika mkumbo huo wa Wacongo Mayele, kama ilivyo kwa Jesus Moloko na Tuisila Kisinda hawakujiingiza katika mkumbo huo. Tofauti na kina Bangala ambao wameondolewa kinguvu, Mayele angeweza kuendelea kutetema Jangwani hata kama Yanga wasingepokea ofa kutoka kwa Mafarao.

Mayele pia anatuachia staili ya ushangiliaji ya aina yake ambayo inakuwa staili maarufu zaidi ya ushangiliaji katika historia ya soka letu. Labda hili lilipamba zaidi mabao yake ingawa ni wazi kwamba idadi ya mabao aliyofunga nchini siyo kubwa sana kulinganisha na mabao ya kina Kagere.

Kumbe kuna umuhimu kubwa kwa wachezaji kuwa na staili za kushangilia ambazo zinaongeza umaarufu wa kutambulika kwao (branding). Staili ya Mayele ilimtofautisha na wachezaji wengine ambao alikuwa anagombea nao kiatu cha mfungaji bora katika misimu miwili ambayo alikuwepo nchini.

Nini kinafuata kwa Mayele? Anakwenda katika ligi ngumu zaidi. Anakwenda katika majukumu magumu zaidi. kule Misri klabu moja inaruhusiwa kumiliki wachezaji watatu wa kigeni. Ni nafasi ambazo wenzetu huwa hawazichezei ovyo.

Mayele inabidi apambane kubakisha heshima yake klabuni hapo. Labda tuseme kwamba katika klabu hiyo atakutana na wachezaji hodari kuliko kina Tuisila Kisinda ambao walikuwa wanashindwa kumpikia vema. Hata hivyo, akifunga mabao kumi tu katika Ligi Kuu ya Misri itatosha kusema amekuwa na mafanikio nchini humo achilia mbali katika mechi za kimataifa ambazo Pyramids inashiriki.

Pamoja na kununuliwa kwa pesa nyingi na Mafarao hao lakini Wamisri na Waarabu wengine wa Kaskazini huwa hawaoni hasara kupata hasara kwa kuachana na mchezaji katika msimu wake wa kwanza tu kama hawajaridhika naye.

Tumeona hilo kwa kina Clatous Chota Chama, Tuisila Kisinda, Jose Luis Miquissone na wengineo. Si ajabu ghafla tu wakaamua kuachana na Mayele kama akishindwa kucheka na nyavu kama alivyofanya katika michuano ya Shirikisho.

Na kama hilo likitokea nadhani macho na masikio ya Mayele yatakuwa nchini Tanzania ambapo amekuwa akihusudiwa kama Mfalme. Na ndio maana nimemuaga kwa sasa Mayele. Wachezaji hawa wa kigeni wanavutiwa na ufalme wanaoupata katika maisha yetu.

Halitakuwa jambo la kushangaza kumuona Mayele akirudi nchini kama akishindwa kung’ara Misri. Siombei itokee hivyo. Katika nafasi yake wakati mwingine inakuwa rahisi zaidi kusonga mbele kuliko kurudi nchini.
Wakati kina Chama wakiwa wamerudi nchini, kuna washambuliaji wawili waliotoka katika Ligi ya Tanzania hawakuwahi kurudi nchini. Nonda Shaabani aliondoka Yanga mwaka 1995 kisha akaenda Vaal Professional ya Afrika Kusini. Kuanzia hapo alienda kutamba Uswisi, Ufaransa, England, Italia na Uturuki.

Mwingine ni Mbwana Samatta. Fahari yetu. Alipoondoka hapa nchini akaenda Congo akafunga mabao mengi kisha akaibukia safari Ulaya. Sidhani kama Mayele ana safari ya Ulaya kutokana na umri wake kusogea kwa kiasi kikubwa lakini kuna uwezekano akazurura kwa wakubwa wa Afrika kama akiendelea kucheka na nyavu kama alivyofanya akiwa nchini na katika michuano ya CAF.
Kila la kheri kwake.

CREDIT: MWANASPOTI
 
Back
Top Bottom