Hii ni kwetu tunaomshabikia Clinton

Hii ni kwetu tunaomshabikia Clinton

john agrey

JF-Expert Member
Joined
Jan 24, 2015
Posts
1,280
Reaction score
2,080
Kwanini natamani Trump ambwage Clinton?


MIEZI michache iliyopita tukiwa tunajitayarisha kushiriki katika kipindi cha “Maoni” cha Redio Ujerumani (DW) niliwaambia washiriki wenzangu kwamba natamani Donald Trump awe mgombea wa urais wa chama cha Republican na baadaye amshinde Hillary Clinton, mgombea wa chama cha Democratic, katika uchaguzi ujao wa urais wa Marekani.

Baadhi ya wenzangu walicheka lakini mmoja ambaye ni profesa kutoka Tanzania anayesomesha Marekani alishtuka na akanijibu kwa kuniuliza swali: “Duh, unataka kuchukuwa nyundo umpe mwendawazimu?”

Pengine huyo profesa kimoyomoyo akiniona mimi pia kuwa ni mwendawazimu lakini heshima zake hazikumpa kunambia hivyo. Labda niseme tu kwamba huo wazimu kama ninao basi unaendeshwa na hoja na una mantiki yake.

Nafikiri dhana aliyonayo profesa ni kwamba Trump amepungukiwa na sukurubi mbili tatu kichwani na, kwa hivyo, akiibuka mshindi na kuwa rais atageuka kuwa tembo mkahawani. Atavunja kila kitu ndani yake: buli, sufuria, sahani, sinia na mabakuli. Atavikanyaga vyakula pamoja na wateja.

Mkahawa wenyewe ukiwa hii dunia yetu. Kwa mantiki ya profesa, kumchagua Trump ni sawa na kumpa uwezo wa kuiangamiza dunia.

Mchuano wa Novemba huko Marekani ni mchuano baina ya watu wawili ambao kimsingi hawatofautiani kiitikadi.

W.E. Du Bois, Mmarekani mweusi aliyekuwa msomi mashuhuri na mmoja wa waasisi wa Vuguvugu la Umajumui wa Afrika , aliwahi kuandika kwamba Marekani kuna “chama kimoja kiovu chenye majina mawili”. Alikusudia kwamba chama cha Democratic na kile cha Republican ni vyama vyenye mwelekeo mmoja, ingawa vina majina tofauti.

Malcolm X naye aliwahi kuwaelezea wana Democrat kuwa kama mbweha na wenzao wa Republican kama mbwamwitu. Wote, alisema, watakumeza tu.

Malcolm alikuwa akiwatahadharisha watu weusi wa Marekani kuwa katika maisha yao hakuna tofauti ya kimsingi baina ya utawala wa Democrat na ule wa Republican. Kwa hakika, hayo ni kweli si kwa weusi wa Marekani tu bali hata kwa Afrika nzima.

Hata hivyo, nadhani Malcolm X alikosea kidogo kwa sababu ingawa kweli serikali za vyama vyote hivyo viwili zinaweza zikatumeza wazimawazima, ipo tofauti baina yao kuhusu mchango wao kwa Afrika.

Tukizipima tawala za karibuni za Marekani na misimamo yao juu ya Afrika, tutaona kuwa utawala wa Republican chini ya George W. Bush uliifanyia mengi Afrika zaidi ya yaliyofanywa na utawala wa Barack Obama au ule wa Rais wa zamani Bill Clinton, mumewe Hillary. Hiyo ndiyo hakika ya mambo. Ndio maana kuna wasemao kuwa Bush alikuwa “Rais bora wa Afrika”.

Wanasema hivyo kwa sababu alianzisha Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) na aliidhinisha mabilioni ya dola za Marekani kugharimia mradi wa PEPFAR wa kupambana na virusi vya HIV na Ukimwi pamoja na mabilioni mengine ya kusaidia vita dhidi ya Malaria barani Afrika.

Kabla hajachaguliwa Rais 1992 Bill Clinton alifanya mambo ya kujitambulisha na watu weusi ambayo yaliwababaisha na kuwahadaa. Alipochaguliwa Rais walihisi kama wana mtu wao katika Ikulu ya Marekani, The White House. Mwandishi mashuhuri aliye mweusi Toni Morrison alithubutu kusema kwamba Clinton alikuwa “rais wetu wa kwanza aliye mweusi.”

Wamarekani weusi walimshangilia kwa vishindo wakitaraji kwamba atachukuwa hatua zitazonyanyua hali zao za maisha. Hakufanya hivyo. Matokeo yake ni kwamba hali zao zilizidi kudidimia na walizidi kuishi kwa dhiki.

Nitazitaja hatua zake mbili tu zilizozidi kuwaumiza watu weusi. Ya kwanza ni kuacha kuzisaidia familia zenye watoto wenye kuwategemea wazee wao (AFDC). Msaada huo ulikuwa ukitolewa na serikali kuu ya Marekani tangu 1936 hadi 1996 uliposimamishwa na Rais Clinton.

Hatua ya pili ya Clinton iliyowaathiri watu weusi ni mageuzi aliyoyafanya ya Sheria ya Jinai. Watu, wengi wao weusi, walikuwa wakihukumiwa kufungwa gerezani kwa makosa madogodogo.

Matokeo yake ni kwamba Wamarekani weusi walikuwa wakiingizwa gerezani kwa mkururo. Idadi ya watu weusi waliotumbukizwa jela ilikithiri sana hata Julai mwaka jana Clinton mwenyewe alikiri kuwa alifanya kosa kuigeuza Sheria ya Jinai na sasa anasema anajuta kwa kuyafanya hivyo.

Hillary Clinton, mkewe, naye pia sasa anasema ilikuwa kosa kuifanyia mageuzi Sheria ya Jinai. Lakini wakati wote mumewe alipokuwa rais, Hillary aliziunga mkono sera zake zote za mambo ya ndani ya nchi, sera ambazo ziliufanya umasikini Marekani ukithiri.

Kwa ufupi, Rais Clinton, ingawa akisema maneno matamu ya kuwapumbaza Wamarekani weusi, hakuchukua hatua za kuwanyanyua kimaisha.

Juu ya hayo, 2008 wakati wa mchuano ndani ya chama cha Democratic kati ya Obama na Hillary Clinton wa nani awe mgombea wa urais wa chama hicho, mwanzo Wamarekani weusi wengi walimuunga mkono Clinton kushinda Obama.

Na mwaka huu Hillary alipochuana na Bernie Sanders kwa dhamira hiyohiyo Wamarekani weusi walimuunga mkono Clinton kwa wingi kushinda Sanders. Sijui kina Clinton wana uchawi gani unaowafanya Wamarekani weusi wawapende hivyo.

Ilipokuja zamu ya Obama kuwa Rais wa Marekani, Wamarekani weusi pamoja na Wamarekani wengine wenye siasa za wastani (za ulibirali) na hata Waafrika, walimuunga mkono kwa wingi na kwa dhati kwa sababu wakiamini alikuwa na nia njema. Aliahidi mengi yaliyokuwa mazuri. Haikuchukua muda naye pia akawavunja moyo. Kuna wasemao kwamba alimshinda George Bush katika kuyalinda maslahi ya mabepari wa Marekani pamoja na benki zao na mfumo wao wa unyonyaji. Aliyakinga mashirika yao ya kibiashara yasishitakiwe na wenye kuyatetea maslahi ya wafanyakazi.

Nje ya nchi Obama aliiendeleza ajenda ya Marekani ya kuidhibiti dunia. Mara tu baada ya kuwa rais alifunga safari na kwenda Misri ambako alitoa hotuba mwanana kabisa katika Chuo Kikuu cha Cairo, hötuba ambayo wengi waliamini ikiashiria msimamo mpya wa Marekani kuhusu Mashariki ya Kati, kuhusu nia mpya ya kupigania mfumo wa demokrasia ushamiri katika eneo hilo na kwingineko.

Wengi walidhania kwamba patakuwako ushirikiano wa aina mpya baina ya Marekani na ulimwengu wa Kiislamu. Obama alishangiliwa, alipewa heko kwa ahadi zake zilizoonekana kuwa ni za dhati.

Lakini hizo ahadi ziligeuka povu. Na hapo ndipo tulipogundua kwamba kulikuwa Obama wawili. Wa kwanza ni yule aliye akilini mwetu, yule tumpendaye, tunayejinasibisha naye na tuliyemtakia mema.

Wa pili ni Obama halisia. Huyu ni Obama aliyebana matumizi nchini na hivyo kuwaumiza watu wa chini, aliyefanya mageuzi ya mfumo wa fedha bila ya kuigusa ile mibepari mikubwa na namna wanavyozifanyia biashara fedha.

Kuhusu Afrika, Obama atakumbukwa kwa idadi ya majeshi iliyoyapeleka huko, kwa namna alivyoingilia Libya na pia kwa namna alivyoongeza vituo vya kijeshi vya Marekani barani humo.

Obama amefurutu ada kwa kuzidi kuliweka bara la Afrika chini ya kwapa za kijeshi za Marekani. Wiki iliyopita tu jarida la “Intercept” lililobobea katika ufichuaji wa nyaraka za siri za kijeshi na za kijasusi za Marekani lilifichua nyaraka zinazothibitisha kwamba Marekani inajenga kituo kipya cha droni nchini Niger.

Droni ni zile ndege za kijeshi zisizo na rubani zinazorushwa angani kuwaua watu wakiwa ardhini.

Marekani inajenga kituo hicho kwenye viunga vya mji wa Agadez katika jangwa la Sahara. Kitakuwa na zana za kisasa na kitagharimu dola milioni mia moja. Hicho hakitokuwa kituo cha kwanza cha aina yake huko Niger. Tayari Marekani ina miradi kadhaa ya kijeshi nchini humo na kwingineko Afrika, ikiwa pamoja na Djibouti katika kanda yetu ya Afrika ya Mashariki.

Itikadi yangu ya kisiasa ni mbingu na ardhi na ile ya Trump lakini hailingani pia na ya Clinton. Kama walivyoashiria Du Bois na Malcolm X, kiitikadi Trump na Clinton ni seti moja.

Wenye kumtetea Clinton wanasema kwamba anastahili awe rais kwa sababu ana uzoefu , hasa kwa kuushika wadhifa wake wa mwisho serikalini wa uwaziri wa mambo ya nje.

Wadhifa huo lakini umemtia dosari kwa kashfa zinazohusu Libya. Kadhalika utendaji kazi wakati katika wizara hiyo umemuonyesha kuwa ni mtu asiyeaminika. Anaweza, kwa mfano, akachochea uhasama wa bure baina ya Urussi na Marekani. Ni wazi kwamba hampendi Rais Vladimir Putin wa Urussi. Pia hampendi Rais Bashar al-Assad wa Syria na watawala wa Iran.

Clinton anapenda vita. Tusisahau kwamba aliunga mkono kujiingiza kijeshi Marekani Iraq na vita vya huko. Kuna wasiwasi kwamba endapo atachaguliwa rais atazidi kuchochea mapigano Mashariki ya Kati kwa kuiingiza nchi yake kijeshi Syria ambako tangu sasa kuna ushahidi wa kuwa Marekani inayasaidia makundi ya kigaidi, yakiwa pamoja na yale yenye mahusiano na mtandao wa al Qaeda na hata lile kundi lijiitalo al-Dawla al-Islamiya fi al-Iraq wa al-Sham (Dola ya Kiislamu katika Iraq na Sham au, kwa kifupi, Daesh).

Clinton anaweza pia akawapa nguvu wale wenye mipango ya kuupindua utawala wa sasa wa Iran.

Kwanza nilipokuwa nikiwatafakari Trump na Clinton na nilipofikia uamuzi wangu nikijifikiri kuwa ni Mwafrika pekee mwenye kutamani Trump ambwage Clinton. Baadaye nikagundua kwamba kuna Waafrika wengine wenye muelekeo kama wangu. Na wote niliozungumza nao ni wa mrengo wa kushoto.

Kuna wengine waliofikiri kuwa nafanya dhihaka, kuna walioguna wakiniona ni mwehu na kuna waliotaka kujua kwa nini nina msimamo huo.

Hoja yangu kubwa ni kwamba ataposhinda Trump, ikiwa atashinda, mpaka wa mapambano utakuwa dhahiri (The battle-line will be well-defined) nimekuwa nikiwaambia wenzangu. Hivi sasa kuna ubabaishaji mwingi na danganyadanganya zisizokwisha katika siasa za kimataifa.

Waliozoea kudanganyadanganya katika jukwaa la kimataifa ni wale wenye kujidai kufuata siasa za kiliberali. Kwa Marekani wanasiasa hao ni wa sampuli ya Hillary Clinton, mumewe Bill na Obama.

Hawa hujitia, kwa mfano, kupigania nchi zetu ziwe na mfumo wa kidemokrasia lakini watawala wetu wanapoikanyaga misingi ya kidemokrasi wao hutoweka hujui wamekimbilia wapi. Ila pakiwa na malsahi kwao. Pakiwa na utajiri mwingi au maslahi ya kistratejia basi hujishughulisha.

Lakini kule “pangu pakavu” kama Zanzibar , au hata Tanzania nzima kwa jumla, misimamo yao huwa ni ya kupiga kelele au ya kuchukua hatua hafifu zisizowadhuru watawala. Huu ndio ukweli. Na ukweli huo ndio unaozidi kuwapa jeuri watawala wetu wafanye watakalo kwa sababu wanajua ya kuwa hizo kelele si za dhati na kwa hivyo haziwezi kubadili mambo kwa haraka.

Wenye kumponda Trump wanasema kwamba yeye si mtu makini na pengine hazimtoshi. Zaidi ya hayo ni mbaguzi wa kikabila, wa kidini na wa kijinsia. Kwa vile si makini, kuna hatari kwamba akipata madaraka anaweza akaiangamiza dunia, yaani kwa kugeuka yule tembo wa mkahawani.

Trump ni mwanasiasa tofauti na kina Clinton. Ni mtu mwenye kujiona, mwenye kujipenda, anayeona hakuna aliye bora kushinda yeye. Isitoshe, ni kidhabu, mwongo wa kutupwa.

Kwao Marekani kumefanywa uchambuzi wenye kuonyesha kuwa katika kila dakika tano anazozungumza lazima aseme uongo japo mara moja. Asiposema uongo katika muda huo basi atasema jambo lisilo sahihi. Atapotosha.

Kwa ufupi, Trump ni mtu wa ajabu. Endapo atamshinda Clinton na kuwa Rais tujiandae kumsikia akitamka maneno yanayoweza kuifanya midundo ya nyoyo zetu ikose nidhamu mara baada ya mara.

Kuna maraisi wawili duniani ambao kuna kila dalili, kwa kiwango fulani, kuwa atafanana nao wa kuendesha serikali kibabe, ingawa yeye atazuiliwa na sheria na taasisi za kidemokrasia za Marekani. Mmoja ni Rais wa Philippines Rodrigo Duterte, mwengine nakuachia wewe uagulie ni nani.

Kuna Wamarekani wengi wenye kuamini kuwa endapo ataibuka na kuwa rais, Trump atakuwa tishio kwa amani ndani ya Marekani. Na wana hofu kwamba nje ya Marekani ataivunjia heshima nchi yao.

Trump ni mtu asiyejua kusema. Hata hivyo, uzuri wake ni kwamba ayasemayo ni mambo anayoyaamini. Kwa hivyo, ni rahisi kuujua msimamo wake. Ni afadhali mara elfu kuwa na adui kama huyo kushinda yule mwenye msimamo usiofahamika, mwenye kubabaishababaisha au yule mwenye kusema hivi na akafanya kinyume na hivyo.

Chanzo: Raia Mwema
 
You are very right brother:Trump for president
Bila ya kumung'unya maneno,Hilary Clinton ni kizabizabina,warmonger.
Ana laana ya damu za watu huyo mama ,lakini ndio yupo upande wa wale wanaoitwa elites wa huko USA ,kwa hiyo piga ua yy ndiye rais.
 
Bila ya kumung'unya maneno,Hilary Clinton ni kizabizabina,warmonger.
Ana laana ya damu za watu huyo mama ,lakini ndio yupo upande wa wale wanaoitwa elites wa huko USA ,kwa hiyo piga ua yy ndiye rais.
tusubiri uchaguzi
 
hivi sijui nipo peke yangu ila kwa yale macho ya yule mama siamini kama hajawahi kupaa usiku asee,, ana macho ya wamama wachawi wale.. jicho ukiliangalia kwa nje linatabasam ila ukiliangalia kwa ndani sana limejaa chuki, unafiki na uchawi wa kiwango cha juu sana sipati picha yule awe mama ako wa kambo,,, kama hakuna yoyote anaemuona hivyo basi mnisamehe bure
 
Huyu mama akiingia madrakani tujiandae na endless wars,maana sera yake kubwa niusalama na kutokomeza makundi ya kigaidi,na kuzichapa nchi asizozipenda na alisha zitaja
 
Kuna haja ya kufanya summarisation.....kuandika maneno machache yenye ujumbe wa kueleweka.
Si unajuaga akili za waandishi wa magazeti ya kibongo. wenyewe huwa wanaandikaga tu ilimladi wajaze ukurasa.
 
Kweli Mkuu...tasnia ina changamoto kubwa sana.
Na inabidi wawe wanajifunza kwamba mtu unapo kuwa unaongea sana ndipo unapojipa nafasi kubwa ya kuongea utumbo inamaana hata kwenye uandishi ipo hivyo. Na kama wataendelea na kuangagalia wameandika makaratasi manapi? bila kuangali humo ndani wameandika nini? Itafika hatua hayo magazeti yatakosa wateja.
 
Na inabidi wawe wanajifunza kwamba mtu unapo kuwa unaongea sana ndipo unapojipa nafasi kubwa ya kuongea utumbo inamaana hata kwenye uandishi ipo hivyo. Na kama wataendelea na kuangagalia wameandika makaratasi manapi? bila kuangali humo ndani wameandika nini? Itafika hatua hayo magazeti yatakosa wateja.
Kwenye magazeti sina shida nako,...Tatizo ni hapa JF, wanatakiwa kutambua kwamba hbr ni nyingi za kusoma na muda ni kidogo.Kwa hiyo wawe short and clear.
 
Trump hafai kuwa Raisi wa marekani. Bora wabaki na utawala walionao wa Obama kwa Hilary kuwa Raisi kwa miaka 4 ili wapate nafasi ya kuchagua Raisi mwengine. Huyu jamaa ni matatizo kwa wamarekani na dunia kwa ujumla.
 
Paragraph ya tatu toka mwisho. Umeniacha hoi kwenye mmoja wa marais dikteka ambaye umewaachia wasomaji wamtaje wenyewe
 
Back
Top Bottom