Hii ndiyo zawadi kubwa ambayo Serikali inaweza kuwapa Watanzania

wanzagitalewa

Senior Member
Jan 25, 2018
128
84
Kuna idadi kubwa ya watu wanaochukizwa na mfumo wetu wa mahakama. Mtazamo wao kuhusu mfumo wamahakama ni kuwa ni taasisi yenye watendaji wanaofanya kazi kwa kujivuta, wasioendana na kasi ya serikali wanayoitumikia na wala haikerwi na rushwa.

Watanzania wengi watakubaliana na watu wenye mtazamo huo hapo juu kuhusu mahakama, mimi nikiwa mmoja wao. Ni kero kubwa na huzuni kwa taifa kushindwa kuwashughulikia wahusika wa rushwa, huku kesi zikicheleweshwa pasi na kuwa na sababu za msingi.

Napata wakati mgumu pia kuelewa pale ninaposikia kuwa, baadhi ya mafisadi wameingia makubaliano na serikali, tena kwa uhuru. Je! Hatukupaswa kuiachia mahakama kuchukua hatua juu ya hili? Kwamba mtu anaweza kuvunja sheria, kisha akapatana tu na kiongozi fulani wa serikali na kesi ikaondolewa? La haula!

Mimi bado ni miongoni mwa watu wachache ambao wana imani katika vita dhidi ya rushwa. Bado naamini kuwa tunaweza kutatua changamoto zinazoikumba jamii, na imani yangu ni kuwa ili tufanikiwe, mfumo wetu wa kisheria ni lazima uwe nguzo muhimu katika vita hii.

Pasi na mashaka bado nina amini kuwa kila mmoja ana nafasi katika vita dhidi ya rushwa. Haitatokea tu kwa njia za kimuujiza. Matatizo yetu hayatamalizika kutoka kwenye serikali moja kwenda nyingine. Mafanikio ya nchi yetu hayataletwa na mabadiliko ya viongozi bali taasisi madhubuti.

Tatizo langu ni moja, vita dhidi ya rushwa imeanza kuonekana kama ni kitu cha kutengenezwa. Kila siku tunasikia kupitia vyombo vya habari kuwa TRA imekamata watu sehemu fulani. Tunasikia kila siku hatua mbalimbali zinazochukuliwana TAKUKURU dhidi ya watuhumiwa wa rushwa.

Haya yote ni mambo mema, lakini sasa inaonekana kuwa serikali imeanza kuwa na upendeleo katika vita hii kwasababu hatua zinazochukuliwa zimekuwa haziko bayana.

Utafiti wa Afrobarometer umethibitisha kuwa Watanzania wana mashaka sana na utajiri wa wafanyabiashara pamoja na malengo yako. Watanzania wapo katika nafasi kubwa zaidi ya kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuikwepa mahakama, mashtaka na kulipa kodi. Hatupaswi kuliacha hili liendelee. Hii ni kutokana na kuamini jamii yetu si ya misingi ya haki tena bali kila mtu kwa nguvu zake.

Mtanzania wa kawaida atakuwa tayari kuunga mkono vita dhidi ya rushwa endapo vita hiyo italeta mabadiliko chanya katika maisha yake. Hadi hapo kutakapokuwa na matokeo yanayoonekana, vita dhidi ya rushwa inabaki nadharia na kiini macho.

Hatupaswi kutoa nafasi kwa wenye hila kutumia rushwa kuweza kuachiwa huru. Kufanya hivyo kutaharibu jitihada zote zenye tija ambazo zimefanywa katika vita dhidi ya rushwa. Matajiri hawapaswi kupewa nafasi ambayo itawafanya waonekana kana kwamba wapo juu ya sheria. Tukiifika hapo, mfumo wetu wa sheria utakuwa hauna maana na nchi yetu itaenda sehemu mbaya.

Kama kweli wapo watu ambao wanakamatwa kwa rushwa, ufisadi au uhalifu na wenye ushahidi lakini wanapewa nafasi ya kufanya makubaliano na serikali nje ya mfumo wa mahakama, hatua hiyo inamshushia heshima Rais na jitihada zote alizofanya. Moja ya zawadi kubwa za uongozi wowote nchini itakuwa ni kushughulikia rushwa na kuitibu ipasavyo. Maafisa serikali ambao wanawaacha matajiri kuendelea kupeta mitaani licha ya makosa waliyoyafanya wakumbuke kuwa wao ni wasaliti na sumu kwa taifa pale wanapochukua zawadi zinazotolewa na wala rushwa.

Serikali haipaswi kuamini makubaliano yoyote yaliyofanywana maafisa hao wakiwa wamejifungia vyumbani ambapo mahakama haikushirikishwa. Hii ni hadaa kwa wananchi na najisi kwa mahakama.



Talewa Nyaronyo

Mara, Tanzania
 
Back
Top Bottom