Hii ndiyo Katiba ACT, pakua na isome hapa.

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,282
Kwa muda mrefu hasa wanajamvi wamekuwa wakihangaika kupata katiba ya ACT, na mara zote tulikuwa tunawaambia katiba yetu iko katika mchakato wa kufanyiwa mabadiliko, hatimaye mchakato huo ulihitimishwa tarehe 28 baada ya mkutano mkuu kuridhia mabadiliko hayo.

Hvyo sasa leo nawawekea katiba ya chama chetu kama ilivyofanyiwa mabadiliko tarehe 28/3/2015, hapa utaweza kuisoma au ukiamua utaweza kuiakua sababu chini kabisa nimeambatanisha faili ambalo unaweza kuliweka kwenye kifaa chako au kopyuta yako na ukaweza kuisoma katiba yetu kwa utaratibu na kuielewa.

Alliance for Change and Transparency

(ACT-Wazalendo)

Chama cha Wazalendo

KATIBA

TOLEO LA 2015

Kama ilivyoidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Jumamosi Tarehe 28 Machi 2015
Ukumbi wa Kadinali Rugambwa, Dar es Salaam.


DIBAJI

KWA KUWA tumeamua kupambana dhidi ya rushwa, ufisadi, uzembe na uvivu;

NA KWA KUWA tumeamua kuhakikisha kuwa maliasili ya Nchi yetu Tanzania ni mali ya wananchi wote na kwamba lazima itumike kutokomeza umasikini nchini kwetu na kuleta maendeleo sawia na endelevu ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa;

NA KWA KUWA tumeamua kujenga Chama cha siasa chenye lengo la kuchochea ujenzi wa Taifa la Kujitegemea, lisilo na unyonyaji wala ubaguzi wa rangi, dini, kabila, jinsia, maumbile, hali ya kipato na kwa kuzingatia misingi ya haki kwa watu wake wote;

NA KWA KUWA tumeamua kushiriki katika ujenzi wa Umoja wa Afrika ili kuwaenzi waasisi wa ukombozi wa Mwafrika na kujenga bara lenye sauti yenye nguvu na ushawishi katika jamii ya mataifa ulimwenguni;
NA KWA KUWA tumeamua kupigania demokrasia, umoja, utu, uadilifu, uwajibikaji, uzalendo kwa Taifa;
NA KWA KUWA kwa nia moja tumeamua kujenga Chama chenye kufuata misingi ya Ujamaa wa Kidemokrasia (Democratic Socialism), na misingi asili iliyoasisi Taifa letu (Unyerere) ikiwemo Azimio la Arusha ; na
NA KWA wajibu tulio nao wa kujenga, kukuza na kuendeleza demokrasia na utamaduni wa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania;

HIVYO BASI; Sisi Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha Wazalendo (ACT) uliofanyika Dar es salaam leo tarehe 28 Machi 2015, tumepitisha
KATIBA MPYA ya Chama chetu itakayojulikana kama KATIBA YA ACT YA MWAKA 2015.

SURA YA KWANZA

JINA, MAKAO MAKUU, ALAMA, ITIKADI, LUGHA, MISINGI NA MALENGO YA CHAMA

SEHEMU YA I

JINA, MAKAO MAKUU, ALAMA, ITIKADI NA LUGHA

1. Jina la Chama
Jina la Chama litakuwa ni ALLIANCE FOR CHANGE AND TRANSPARENCY
(ACT) na chama kitajulikana kwa Kiswahili kama CHAMA CHA WAZALENDO.

2. Makao Makuu ya Chama
(1) Makao Makuu ya Chama yatakuwa ni Dar es Salaam
(2) Kutakuwa na ofisi ndogo ya Makao Makuu Zanzibar na Mwanza.

3. Alama za Chama
(1) Alama za Chama zitakuwa ni:
i. Rangi za Chama ambazo ni Zambarau na Nyeupe;
ii. Bendera ya Chama ambayo itakuwa ni ya rangi ya Zambarau ama Nyeupe ikiwa na nembo ya chama katikati ya bendera;
iii. Nembo ya Chama
iv. Wimbo rasmi wa Chama
v. Vazi rasmi la Chama.
(2) Halmashauri Kuu ya Chama itatengeneza na kufafanua muundo na yaliyomo
ndani ya Nembo ya Chama, Wimbo rasmi wa Chama na Vazi rasmi la Chama
kupitia Kanuni za uendeshaji Chama zitakazotungwa na Halmashauri Kuu ya
chama. Halmashauri Kuu itakuwa na uwezo wa kubadili alama za chama kutokana na mahitaji ya wakati.

4. Itikadi na Falsafa ya ACT:
(1) ACT inaamini katika msingi ya Ujamaa wa Kidemokrasia (Democratic Socialism).
Misingi mikuu ya ujamaa wa Kidemokrasia ni:
i. Undugu;
ii. Usawa;
iii. Uhuru;
iv. Heshima kwa kila mtu; na
v. Demokrasia
(2) Falsafa ya ACT ni UNYERERE, ikiwa ni dhamira ya kurudisha, kuhuisha na kupigania misingi mama iliyoasisi Taifa la Tanzania, kama ilivyoainishwa katika Azimio la Arusha na kwa mazingira ya Tanzania ya sasa.
(3) Shabaha kuu ya ACT ni kupigania na kusimamia uwajibikaji na uwazi nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla na kwamba mabadiliko ni ajenda ya kudumu.
(4) Chama kinazingatia elimu, uadilifu, uwajibikaji, kujitegemea na bidii katika kazi kama njia kuu za kujikomboa dhidi ya umaskini, ujinga, maradhi na rushwa, ambavyo ndio maadui wakuu wa Taifa la Tanzania na Afrika kwa ujumla.

5. Lugha rasmi ya chama
(1) Lugha rasmi ya chama itakuwa ni Kiswahili.
(2) Bila kuathiri ibara ndogo ya (1) ya ibara hii hapo juu, lugha ya Kiingereza
inaweza kutumika sambamba na lugha ya Kiswahili inapobidi.
(3) Nyaraka zote muhimu, ikiwemo Katiba hii, zitaandikwa katika lugha ya Kiswahili na kutafsiriwa katika lugha ya Kiingereza.
(4) Chama kitaweka mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa mawasiliano mbadala zikiwemo lugha za alama kwa kadri ya mahitaji.

SEHEMU YA II

MISINGI NA MALENGO YA CHAMA


6. ACT itaongozwa
1) ACT itaongozwa na Misingi Kumi (10).
2) Misingi hii imewekwa kwa ajili ya kutekeleza Itikadi ya Ujamaa wa Kidemokrasia na Falsafa ya unyerere katika ubora wake.

3) Katiba hii ya ACT ipo kwa ajili ya kuilinda misingi hii muhimu ya chama na hivyo kipengele chochote cha Katiba hii kitakachokiuka mmoja wa misingi hii, kitakuwa batili.

4) Misingi kumi ya ACT ni:
i) Uzalendo
ii) Usawa
iii) Kupinga na Kupiga Vita ubaguzi
iv) Uadilifu
v) Uwazi
vi) Uwajibikaji
vii) Demokrasia
viii) Uhuru wa Mawazo na Matendo
ix) Utu
x) Umoja

5) Misingi hi itafafanuliwa katika nyaraka mbalimbali zitakazotolewa na Chama kwa mujibu wa Katiba hii na Kanuni za uendeshaji wa Chama.

7. Malengo
ACT itapambana kuhakikisha kwamba inashinda uchaguzi na kuunda serikali ili kutekeleza malengo yafuatayo:
i) Kuhakikisha kwamba serikali inatumia raslimali yote ya nchi kwa ajili ya kuondosha umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, na kuleta maendeleo ya nchi kwa ujumla;
(ii) Kupigania na kulinda uongozi bora na Utawala wa Sheria;
(iii) Kujenga, kukuza na kuendeleza demokrasia raslimali na serikali inayowajibika kwa umma wa Watanzania;
(iv) Kuhakikisha usawa mbele ya Sheria kwa raia wote wanaume kwa wanawake bila kujali kabila, rangi, imani za kidini, itikadi, utamaduni ama hadhi ya mtu kiuchumi na kijamii;
(v) Kuendeleza na kudumisha Demokrasia na utamaduni wa mfumo wa vyama vingi vya siasa;
(vi) Kuchochea, kuimarisha na kulinda uzalendo, uadilifu, uwajibikaji na uwazi kama misingi mikuu katika uongozi wa nchi;
(vii) Kuchochea na kuendeleza mapambano katika kulinda haki za watoto, wanawake na watu wenye ulemavu;
(viii) Kupigania haki na heshima ya wafanyakazi, wakulima, wafugaji na wajiasiliamali katika ngazi zote;
(ix) Kudhibiti soko huria ili kuhakikisha kuwa haliathiri haki za utu za wafanyakazi na walaji wenye kipato cha chini;
(x) Kulinda na kuendeleza mazingira bora kwa vizazi vya leo na vijavyo;
(xi) Kuhakikisha kuwa idhini, mikataba na ushirikiano wa kikanda barani Afrika ambavyo Tanzania ni mwanachama kama vile Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) vinaendana na misingi mikuu ya kidemokrasia na kuendeleza kuheshimu utawala wa sheria Afrika;
(xii) Kuhimiza ushirikiano na mahusiano na vyama vingine vinavyoamini katika demokrasia jamii Afrika na duniani kote;na
(xiii) Kuunga mkono na kusukuma mbele juhudi za kuundwa kwa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki na kupigania umoja wa Afrika.

SURA YA PILI

UANACHAMA NA UONGOZI
SEHEMU YA I
UANACHAMA

8. Uanachama wa ACT utakuwa wazi kwa raia wote
(1) Uanachama wa ACT utakuwa wazi kwa raia wote wenye umri wa kupiga kura bila kubagua jinsia, kabila, dini, au hali yoyote.
a) Kila raia atakayekuwa ameandikishwa kuwa mwanachama wa ACT atapewa kadi ya uanachama itakayoonyesha pamoja na habari nyingine, jina lake, anuani, saini yake na saini ya afisa wa Chama aliyemwandikisha.
b) Kikundi cha watu kinaweza kujiunga na ACT kama kikundi kwa umoja wao, na kwamba kikundi hicho kinakubali itikadi na misingi ya kuanzishwa kwa ACT.
(2) Sifa mahsusi za mtu anayetaka kujiunga uanachama wa ACT:
i. Awe raia wa Tanzania;
ii. Awe ana umri wa kupiga kura kwa mujibu wa Sheria za Tanzania;
iii. Awe anakubaliana na itikadi, falsafa na misingi ya ACT;
iv. Awe na akili timamu;
v. Awe na moyo na utayari wa kukitumikia Chama na kueneza itikadi, falsafa na misingi yake.
vi. Aonyeshe uzalendo na upendo wa kuitumikia nchi yake; na
vii. Asiwe Mwanachama wa chama kingine cha siasa baada ya kujiunga na ACT.
(3) ACT itakuwa na aina zifuatazo za wanachama:
i. Wanachama wa Kawaida
Ni wanachama wote waliojiandikisha na kulipa ada ya ACT na kuzingatia masharti ya Katiba hii.
ii. Wanachama Vikundi
Ni wanachama wanaotokana na jumuiya, taasisi, mashirika au vikundi mbalimbali ambavyo vimeamua kujiunga na Chama kupitia umoja wao.
iii. Wanachama wanafunzi
Hawa ni wanachama ambao hawajatimiza umri wa kupiga kura na ambao wanajiandaa kujiunga na Chama siku za usoni

9. Ada ya Uanachama
(1) Kila mwanachama atawajibika kulipa ada za uanachama kama itakavyoainishwa kwenye Kanuni za Uendeshaji Chama zitakazotungwa na Halmashauri Kuu ya Chama.
(2) Bila kuathiri Sheria zinazohusu vyama vya siasa nchini, pamoja na misingi na masharti ya Katiba hii, kila mtu au kundi la watu wanaokubaliana na misingi, malengo, sera na mipango ya Chama wanaweza kutoa ada ya kundi la uanachama.
(3) Kutakuwa na kiingilio kwa kila mwanachama na kundi lolote litakalotaka kujiunga na Chama itakavyoainishwa kwenye Kanuni za Uendeshaji Chama zitakazotungwa na Halmashauri Kuu ya Chama
(4) Utaratibu wa ulipaji wa kiingilio na ada vitafafanuliwa katika kanuni za Uendeshaji Chama.
10. Haki za mwanachama wa ACT
(1) Kila mwanachama wa ACT atakuwa na haki ya:
i. Kushiriki shughuli zote za Chama kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa;
ii. Kusikilizwa na kuuliza maswali kuhusu maendeleo na mwenendo wa Chama;
iii. Kuchagua na kuchagliwa kuwa kiongozi ndani ya Chama;
iv. Kuwasilisha pendekezo au maelezo kwenye kikao chochote cha Chama, hadi katika ngazi ya Halmashauri Kuu;

v. Kukosoa kiongozi yeyote ndani ya vikao vya Chama;
vi. Wajumbe wanaweza kuitisha kikao chochote endapo tu asilimia sabini na tano ya wajumbe wa kikao hicho watatia saini kuhitaji kikao hicho kiitishwe;\
vii. Bila kuathiri yaliyomo katika kipengele (f) hapo juu, wajumbe wanaohitaji kikao hicho lazima waonyeshe kuwa viongozi katika ngazi husika wameshindwa kuitisha vikao hivyo zaidi ya mara tatu kwa mujibu wa katiba na utaratibu wa kuitisha vikao vya namna hiyo utafafanuliwa kwenye kanuni za Chama.
(2) Kila mwanachama wa ACT atakuwa na wajibu wa:
a) Kujifunza na kupanua uelewa kuhusu itikadi, falsafa na misingi ya ACT;
b) Kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba ACT inashinda katika chaguzi mbalimbali zitakazoitishwa nchini kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi;
c) Kuzingatia nidhamu ya ACT;
d) Kushiriki kikamilifu katika shughuli za Chama na kutekeleza kwa vitendo sera na maamuzi ya Chama;
e) Kushiriki kikamilifu katika kukomesha vitendo vyovyote ndani na nje ya Chama vinavyoweza kuhatarisha uhai na maslahi ya Chama;
f) Kueneza itikadi, falsafa na misingi ya ACT kwa umma, na kujifunza mahitaji ya umma kwa wakati na kuhakikisha kwamba yanazingatiwa katika sera za Chama;
g) Kuwa mfano na sura ya ACT kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na umakini; na
h) Kulipa ada na kuchangia mchango wowote kwa mipango maalumu na shughuli za ACT kama itakavyokuwa imeamuliwa na vikao vya Chama.

11. Kukoma Uanachama
i. Mwanachama atakoma kuwa mwanachama ikiwa:
ii. Atajiuzulu mwenyewe kwa hiari yake kwa kuandika barua kwa Katibu wa ngazi yake au Katibu Mkuu kwa kueleza kusudio la kuacha kuwa mwanachama na kurudisha kadi ya uanachama;
iii. Kujiunga na chama kingine cha siasa;
iv. Kufukuzwa uanachama kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa katika Katiba hii; au
v. Atapoteza sifa za uanachama kama zilivyoainishwa katika Katiba hii.
(2) Mwanachama anaweza kusimamishwa uanachama ili kupisha uchunguzi kuhusu mwenendo wake utakaofanywa na Kamati ya Uadilifu katika ngazi husika.
(3) Mwanachama anaweza kufukuzwa kwenye Chama kwa sababu zinazotokana na mwenendo usiofaa kwa mujibu wa masharti na Kanuni za Katiba hii, na mara baada ya kufukuzwa, uanachama wake utakoma.

(4) Pamoja na sababu nyingine kama zilivyoelezwa katika katiba hii na kanuni zitakazotungwa na Halmashauri Kuu, mwanachama yeyote ambaye atasaidia, kushawishi, kujiunga, kutoa tamko la kuunga mkono chama kingine
au mgombea wakati Chama kimeweka mgombea kwenye uchaguzi wowote
kwa mujibu wa Sheria ya Nchi atakuwa amepoteza uanachama wa ACT.

(5) Hakuna mwanachama atakayesimamoshwa au kufukuzwa uanachama hadi pale ambapo mashart yaliyoainishwa katika Katiba hii na Kanuni za Uendeshaji Chama yatakapokuwa yamefuatwa.
(6) Uamuzi wa kumsimamisha uanachama ama kumfukuza mwanachama yeyote hautakuwa na nguvu hadi pale uamuzi huo utakapokuwa umewasilishwa kwa mwanachama husika kwa maandishi.
(7) Bila kuathiri ibara ndogo ya (6) ya ibara hii, mwanachama ambaye atakataa kupokea taarifa ya maandishi juu ya uamuzi wa kusimamishwa au kufukuzwa uanachama uliochukuliwa dhidi yake, atahesabika kwamba ameshawasilishiwa taarifa hiyo kwa mujibu wa ibara ndogo ya (6) na uamuzi wa kumsimamisha au kumfukuza uanachama utakuwa na nguvu.

(8) Kila mtu ambaye amekoma kuwa mwanachama atalazimika kurudisha mali za Chama zilizo chini yake. Hata hivyo, ada, michango na mali zingine ambazo atakuwa amechangia alipokuwa mwanachama hazitarudishwa

(9) Pale mwanachama atakapokuwa amepoteza uanachama wake kwa njia yoyote ile anaweza kuomba tena uanachama wa ACT na anaweza kukubaliwa kuwa mwanachama tena kwa mujibu wa Katiba hii, labda tu pale ambapo Halmashauri Kuu ya ACT itakuwa imeamua vinginevyo.

12. Orodha ya Uanachama
(1) Kutakuwa na rejesta ya orodha ya wanachama wote katika kila Tawi,
Kata na katika kila Jimbo la Uchaguzi, na rejesta hii itahuishwa kila baada ya miezi sita. Makatibu wa Chama katika ngazi husika watatuma orodha ya wanachama kwa ngazi inayofuata kwa ajili ya kumbukumbu za Chama katika kila ngazi.
(2) Katibu wa Chama Mkoa atatunza orodha ya wanachama wote kwenye mkoa wake na atapokea orodha ya wanachama wote walioandikishwa kila jimbo katika mkoa wake.
(3) Sekretariati ya Chama Makao Makuu itatunza rejesta ya wanachama wote nchi nzima.

13. Ahadi tano za kila mwanachama wa ACT
Kila mwanachama wa ACT atatoa ahadi tano zifuatazo:
i) Nitapambana dhidi ya dhuluma, fitina, unafiki uongo, rushwa na ufisadi kwa uwezo wangu wote;
ii) Nitapambana dhidi ya umasikini na nitasimamia utajiri wa nchi yangu kwa faida ya wote;
iii) Nitashiriki kujenga Taifa lenye kujitegemea, lisilo na unyonyaji, ubaguzi na lenye misingi ya Haki;
iv) Nitashiriki kujenga Umoja wa Afrika; na
v) Nitapigania kuwepo kwa demokrasia ndani na nje ya Chama changu.
vi) Nitajielimisha kila mara na nitatumia elimu yangu kwa manufaa ya jamii na Tanzania kwa ujumla


SEHEMU YA II
UONGOZI
14. Sifa za Kiongozi
Sifa, mwenendo na maadili ya Kiongozi wa ACT
1) Sifa, mwenendo na maadili ya viongozi wa ACT vimeainishwa kwa kina kwenye Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Viongozi wa ACT.
2) Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Viongozi zimeambatanishwa kama Nyongeza ya kwanza na ni sehemu ya Katiba hii.

15. Aina za Viongozi
(1) Kutakuwa na aina zifuatazo za Viongozi ndani ya ACT:
i. Viongozi wa kuchaguliwa na mikutano mikuu ya kila ngazi;
ii. Viongozi wa kuchaguliwa au kuteuliwa na vikao vya uongozi katika ngazi mbalimbali za Chama;
iii. Viongozi watakaoteuliwa na Kiongozi Mkuu wa chama kwa mujibu wa Katiba hii
iv. Watendaji/waajiriwa/watumishi katika Chama;
v. Viongozi wa Ngome za Chama watakaochaguliwa au kuteuliwa kwa mujibu wa katiba hii na kanuni za ngome zao; na
vi. Viongozi wanaotokana na nafasi zao kama zilivyoainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama vile Diwani, Mbunge, Waziri, Waziri Mkuu, Rais, n.k.
(2) Kila kiongozi aliyechaguliwa au kuteuliwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa
Chama atashika wadhifa wake kwa kipindi cha miaka tano.
(3) Halmashauri Kuu inaweza kuitisha uchaguzi wakati wowote kabla ya muda wa miaka mitano kwisha kama itaona inafaa na ni kwa manufaa ya Chama na/au Taifa na viongozi ambao muda wao wa uongozi utafupishwa kwa mujibu wa ibara ndogo hii watahesabika kwamba wamekaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano
(4) Kiongozi aliyechaguliwa au kuteuliwa baada ya Uchaguzi Mkuu, atashika wadhifa wake hadi kipindi cha Uchaguzi Mkuu alichochaguliwa/teuliwa kwisha na anaweza kugombea au kuteuliwa kwa kipindi kingine cha miaka mitano ambacho kitakuwa ndio ukomo wake wa kugombea au kuteuliwa kushika nafasi hiyo.
(5) Kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena, mradi awe ametimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi. Isipokuwa mwanachama yeyote wa ACT atakuwa kiongozi kwa vipindi visivyozidi viwili katika nafasi moja ya uongozi katika ngazi husika.
(6) Ibara hii itahusu pia viongozi wa NGOME za ACT-Vijana, Wazee na Wanawake.
(7) Kwa muktadha wa ibara ndogo ya (5) ya ibara hii, Kiongozi aliyechaguliwa/kuteuliwa kushika wadhifa kwa kuziba nafasi iliyoachwa wazi atahesabiwa kwamba amekaa kwenye wadhifa wake kwa kipindi cha miaka mitano ikiwa amedumu kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi

16. Haki za Kiongozi
Pamoja na haki za mwanachama zilizoanishwa katika Katiba hii, Kiongozi wa
ACT pia ana haki zifuatazo:
i) Haki ya kukiwakilisha Chama katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiserikali;
ii) Kuandaa na kupendekeza programu mbalimbali za Chama ili kuleta ustawi katika Chama;
iii) Haki ya kujitetea au kutoa taarifa juu ya jambo au mashtaka yoyote juu yake na ana haki ya kukata rufaa kwenye vikao vya juu iwapo hajaridhika na uamuzi uliotolewa na kikao cha chini; na
iv) Haki ya kupata habari au taarifa zote zilizojadiliwa na kutolewa uamuzi na wanachama au uongozi wa juu katika kumbukumbu za vikao vinavyomhusu.

17. Ukomo wa Uongozi
(1) Mwanachama wa ACT-Tanzania atakoma kuwa Kiongozi wa Chama:
i) Kwa kujiuzulu kwa hiari yake;
ii) Kwa kuachishwa uongozi au kufukuzwa uanachama;
iii) Kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa masharti ya Katiba; Kanuni au maadili ya Chama;
iv) Kwa kufariki dunia;
v) Kupatwa na matatizo ya akili;
vi) Muda wa uongozi kumalizika;
vii) Kupatikana na hatia mahakamani kwa kosa la jinai linalokidhalilisha chama.
(2) Kamati ya Uongozi ya kila ngazi au Halmashauri Kuu kwa ngazi ya Taifa itaziba kwa muda nafasi yoyote ya kiongozi aliyechaguliwa na Mkutano Mkuu wa ngazi husika.
(3) Nafasi wazi za uongozi walioteuliwa zitazibwa na vikao husika kwa kufanya uteuzi mpya katika muda usiozidi miezi sita tangu nafasi kuwa wazi.
(4) Muda wa uongozi wa muda kwa mujibu wa kifungu ibara ndogo ya (2) hapo juu hautazidi miezi kumi na miwili (12) na ndani ya kipindi hicho uchaguzi mpya ufanyike kuziba nafasi iliyoachwa wazi.
(5) Bila kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (4) hapo juu, hakutafanyika uchaguzi rasmi wa kuziba nafasi kama kumebakia miezi sita tu au chini ya hapo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa kawaida wa Chama unaofuata kufanyika.
18. Kukasimu Madaraka
(i.) Kamati ya Uongozi ya kila ngazi au Kamati Kuu Taifa zinaweza kukasimu baadhi ya madaraka kwa Sekretarieti yake kwa azimio la wingi wa kura za wajumbe wa kikao
(ii.) Halmashauri Kuu inaweza kukasimu baadhi ya madaraka yake kwa Kamati Kuu kwa azimio la wingi wa kura za wajumbe
(iii.) Mkutano Mkuu unaweza kukasimu kwa Halmashauri Kuu baadhi ya madaraka yake, lakini kwa azimio maalumu kwa ajili hiyo.


SURA YA TATU

NIDHAMU NA UTATUZI WA MIGOGORO KATIKA CHAMA

19. Kuteuliwa kwa Kamati ya Uadilifu
(1) Kila Kata itakuwa na Kamati ya Uadilifu ya Kata itakayoteuliwa na Mkutano Mkuu wa Kata. Kamati ya Uadilifu ya Kata itaundwa na wajumbe wasiopungua watatu (3) na wasiozidi watano (5), kwa kuzingatia kuwa kutakuwa na angalau mjumbe mmoja (1) mwanamke kama Kamati itakuwa na wajumbe watatu (3), au angalau wajumbe wawili (2) wa kike kama Kamati itakuwa na wajumbe watano (5). Hakuna afisa au kiongozi wa Chama katika ngazi ya Kata atakayeruhusiwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Kata.
(2) Kila jimbo litakuwa na Kamati ya Uadilifu ya Jimbo itakayoteuliwa na Mkutano Mkuu wa Jimbo. Kamati ya Uadilifu ya Jimbo itaundwa na wajumbe wasiopungua watatu (3) na wasiozidi watano (5), kwa kuzingatia kuwa kutakuwa na angalau mjumbe mmoja (1) mwanamke kama Kamati itakuwa na wajumbe watatu (3), au angalau wajumbe wawili (2) wa kike kama Kamati itakuwa na wajumbe watano (5). Hakuna afisa au kiongozi wa Chama katika ngazi ya Jimbo atakayeruhusiwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Jimbo.
(3) Kila mkoa utakuwa na Kamati ya Uadilifu ya Mkoa itakayoteuliwa na Mkutano Mkuu wa Mkoa. Kamati ya Uadilifu ya Mkoa itaundwa na wajumbe wasiopungua watatu (3) na wasiozidi watano (5), kwa kuzingatia kuwa kutakuwa na angalau mjumbe mmoja (1) mwanamke kama Kamati itakuwa na wajumbe watatu (3) au angalau wajumbe wawili (2) wa kike kama Kamati itakuwa na wajumbe watano (5). Hakuna afisa au kiongozi wa Chama katika ngazi ya Mkoa atakayeruhusiwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Mkoa.
(4) Kutakuwa na Kamati ya Uadilifu ya Taifa, ambayo itakuwa ni moja kati ya Kamati za Kudumu za Chama, na itaundwa na wajumbe watakaochaguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya ACT kwa mapendekezo ya Kamati Kuu.
i) Kamati ya Uadilifu ya Taifa itakuwa na wajumbe wasiopungua watano (5) na wasiozidi tisa (9).
ii) Mwanachama yeyote mwaminifu na mwenye uelewa wa Chama na siasa za nchi na dunia anaweza kuomba ujumbe wa Kamati ya Uadilifu.
iii) Halmashauri Kuu ya Taifa itateua wajumbe wa Kamati ya Uadilifu wasiopungua watano (5) na wasiozidi tisa (9), kwa kuzingatia kuwa kutakuwa na angalau wajumbe wawili (2) wanawake kama Kamati itakuwa na wajumbe watano (5), au angalau wajumbe watatu (3) wanawake kama Kamati itakuwa na wajumbe wanaozidi watano (5). Hakuna afisa au kiongozi wa Chama katika ngazi ya Taifa atakayeruhusiwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Taifa.

iv) Halmashauri Kuu itachagua Mwenyekiti wa Kamati ya Uadilifu ya Taifa kwa mapendekezo ya Kamati Kuu kwa kuzingatia kuwa Mwenyekiti atakuwa mtu mwenye angalau Shahada ya Sheria ya Chuo Kikuu kinachotambulika na mamlaka husika nchini.
(5) Hakuna chombo kitakachokuwa na mamlaka ya kuivunja Kamati ya Uadilifu ya Taifa, isipokuwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa idadi ya zaidi ya nusu ya kura zote za wajumbe waliohudhuria na kupiga kura.
(6) Muda wa wajumbe wa Kamati ya Uadilifu utakuwa miaka minne, lakini wanaweza kuteuliwa tena baada ya muda wao kwisha na kuwepo kwake kutazingatia masharti mengine ya Katiba hii.

20. Mamlaka ya Kamati za Uadilifu
(1) Kamati ya Uadilifu ya Kata itakuwa na mamlaka juu ya masuala yote ya kinidhamu na kimaadili kwa wanachama na viongozi katika ngazi ya Kata na ngazi za chini yake isipokuwa wale waliotajwa katika ibara ndogo za (2) na (3).
(2) Kamati ya Uadilifu ya Jimbo itakuwa na mamlaka kuhusu masuala yote ya kinidhamu kwa viongozi katika ngazi ya Jimbo na wawakilishi wa chama (wenyeviti na wajumbe) kwenye serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji na halmashauri za miji midogo. Kamati hii haitakuwa na mamlaka kwa viongozi waliotajwa katika ibara ya (3) na (4). Kamati ya uadilifu ya Jimbo kitakuwa ndicho chombo cha rufaa na mapitio kwa masuala ya kinidhamu katika ngazi ya Kata na uamuzi wake utakuwa ni wa mwisho.
(3) Kamati ya Uadilifu ya Mkoa itakuwa na mamlaka ya masuala yote ya kinidhamu yanayohusu viongozi wa ngazi ya Mkoa isipokuwa waliotajwa kwenye ibara ndogo ya (4), pamoja na wawakilishi wa chama (madiwani) kwenye Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya. Pia kitakuwa chombo cha rufaa na mapitio kwa masuala ya kinidhamu katika ngazi ya Jimbo na uamuzi wake utakuwa wa Mwisho.
(4) Kamati ya Uadilifu ya Taifa itakuwa na mamlaka ya kinidhamu kuhusu maafisa na viongozi katika ngazi ya Taifa, pamoja na viongozi na wanachama wengine waandamizi wakiwemo wabunge, wajumbe wa Kamati za Kudumu na wajumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu, pamoja na masuala yote ya kinidhamu yatakayoelekezwa kwake na vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.
(5) Kamati ya Uadilifu Taifa ndicho kitakachokuwa chombo cha Rufaa kwa masuala ya kinidhamu kutoka ngazi ya Mkoa.
(6) Halmashauri Kuu itakuwa ndiyo ngazi ya rufaa ya kitaifa na uamuzi wake utakuwa wa mwisho.

21. Kazi ya Kamati za Uadilifu
(1) Kamati za Uadilifu zitakuwa na kazi zifuatazo:
i) Kufanya uchunguzi kamili, kwa imani na weledi na bila upendeleo, kuhusu tuhuma zilizowasilishwa dhidi ya mwanachama, mjumbe, afisa, mwakilishi au kiongozi wa Chama katika ngazi husika;
ii) Kutoa taarifa kwa maandishi kuhusu matokeo ya uchunguzi na sababu na mazingira yaliyosababisha kufikia hitimisho;
iii) Kutoa adhabu yeyote kwa mujibu wa Katiba hii isipokuwa kusimamisha au kufukuza uanachama au uongozi;
iv) Kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu kwa ngazi ya Taifa au Kamati ya Uongozi kwa ngazi ya Mkoa na Jimbo kwa adhabu ambazo haina mamlaka nazo;
v) Kamati Kuu kwa ngazi ya Taifa au Kamati ya Uongozi kwa ngazi ya Mkoa na Jimbo itayapitia mapendekezo ya Kamati ya Uadilifu na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu kwa ngazi ya Taifa au Halmashauri ya Mkoa au Jimbo kwa ngazi hizo kwa maamuzi ya mwisho;

vi) Kikao katika ngazi husika kitapokea na kutoa maamuzi ndani ya siku kumi na nne (14) kuhusu mapendekezo ya Kamati ya Uadilifu kwa kukubali mapendekezo yote, kurekebisha au kukataa na itatoa maamuzi yake na sababu za maamuzi hayo kwa wote walioathirika; na

vii) Kikao katika ngazi husika kitatoa maelekezo na maamuzi yanayolenga kuimarisha nidhamu ndani ya Chama, ikiwemo kusimamisha au kufukuza uanachama.
viii) Uamuzi wa kikao husika utaanza kutekelezwa mara moja kama hapatakuwa na rufaa ndani ya siku 14 tangu maamuzi yatolewe.
(2) Namna na mchakato wa Kushughulikia Mashauri ya Nidhamu na uadilifu
itaelezwa kwenye Kanuni za Uendeshaji Chama zitakazotungwa na
Halmashauri Kuu ya Chama.
(3)Mwanachama, mjumbe, mwakilishi au kiongozi yeyote ambaye hakuridhishwa
na maamuzi ya kikao kilichotoa maamuzi ya kinidhamu atakata rufaa kwa
mamlaka ya rufaa ndani ya siku kumi na nne (14) tangu maamuzi yatolewe.
(4) Maamuzi ya Mamlaka ya Rufaa yatakuwa ya mwisho.

22. Makosa Yanayoweza Kusababisha Hatua za Kinidhamu
(1) Makosa yafuatayo yanaweza kusababisha hatua za kinidhamu kwa mwanachama, afisa, mjumbe, mwakilishi au kiongozi wa Chama:
i) Kukiuka miiko na maadili ya uongozi kama yalivyoainishwa katika Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Viongozi ambazo zimeambatanishwa kama Nyongeza ya Kwanza na ni sehemu ya Katiba hii;
ii) Kukataa kutekeleza wajibu na/au majukumu ya kikatiba;
iii) Kufanya fujo au kutoa vitisho dhidi ya mwanachama au kiongozi mwingine;
iv) Kughushi au kutoa taarifa za uwongo kuhusu mahesabu au madai ya uwongo kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia isiyo halali;
v) Kuharibu mali ya Chama kwa makusudi;
vi) Kupinga Itikadi, falsafa, misingi, katiba au sera za Chama katika majukwaa ya kisiasa;
vii) Kusababisha mgawanyiko ndani ya Chama;
viii) Kufanya kitendo chochote ambacho kinagharimu na/au kuharibu taswira ya Chama au taifa katika umma;
(2) Kuthibitika kutenda kosa lolote hapo juu au linalofanana na hayo kutahesabiwa kuwa ni utovu wa nidhamu na kutasababisha kutolewa adhabu stahiki zikiwemo:
i. Karipio;
ii. Karipio kali;
iii. Onyo;
iv. Onyo kali;
v. Faini;
vi. Kusimamishwa kugombea nafasi ya uongozi kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja;
vii. Kusimamishwa uanachama; au
viii. Kufukuzwa uanachama.


SURA NNE

MUUNDO WA CHAMA NA VIKAO

23. ACT-Tanzania ni Chama cha kitaifa
(1) ACT-Tanzania ni Chama cha kitaifa, na kitakuwa na uwakilishi katika kila
ngazi katika muundo wa uchaguzi wa nchi kama ifuatavyo:
a) ACT Tawi
b) ACT Kata
c) ACT Jimbo
d) ACT Mkoa
e) ACT Taifa
(2) Uundaji wa ngazi moja ya Chama utafanyika baada ya kuwa na muundo na uongozi katika ngazi za chini kwa angalau asilimia 40 . Mfano, ili kuunda ngazi ya Kata ni lazima kuwe na angalau asilimia 40 ya matawi yenye uongozi katika kata husika.
(3) Kwa kuzingatia Ibara ndogo ya (1) hapo juu, ngazi ya juu ya Chama itateua Kamati ya muda itakayokuwa na wajibu wa kuratibu shughuli za Chama na kuwaunganisha wanachama katika eneo lisilo na uongozi wa kikatiba mpaka wanapofikia uwezo wa kuwa na uongozi wa kikatiba.

24. Ngazi ya ACT Tawi
(1) Ngazi ya ACT Tawi itaundwa katika eneo la kijiji, Mtaa au Sheia kwa
Tanzania Zanzibar
(2) Idadi ya chini ya Wanachama wa ACT Tawi itakuwa ni watu ishirini (20)
(3) Viongozi wa ACT Tawi watakuwa ni:
(i.) Mwenyekiti wa ACT Tawi;
(ii.) Katibu wa ACT Tawi;
(iii.) Katibu wa Mawasiliano na Uenezi wa ACT Tawi;
(iv.) Mwekahazina wa ACT Tawi
(v.) Katibu wa Mipango na Chaguzi
(vi.) Wenyeviti wa NGOME za ACT Vijana, Wanawake na Wazee katika Tawi;
(vii.) Makatibu wa NGOME za ACT Vijana, Wanawake na Wazee katika Tawi; na
(viii.) Wajumbe wanne wa Kamati ya Uongozi watakaochaguliwa na Mkutano mkuu wa Tawi, wanaume wawili na wanawake wawili.
(4) Vikao vya ACT Tawi vitakuwa ni:
i. Mkutano Mkuu wa Tawi - Ndicho Kikao Kikuu kupita vyote kwenye ngazi ya tawi na wajumbe wake ni viongozi wote wa ACT Tawi na wanachama wote kwenye tawi;
ii. Kamati ya Uongozi – Ni chombo cha utendaji cha Mkutano Mkuu wa Tawi na wajumbe wake ni viongozi wote waliotajwa kwenye ibara ndogo ya (3) ya ibara hii pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji/Mtaa anayetokana na ACT na mwakilishi wa wenyeviti wa vitongoji na mwakilishi wa wajumbe wa serikali ya kijiji/Kamati ya Mtaa.
iii. Sektretarieti ya Tawi – Ni kikao cha utendaji wa kazi za siku kwa siku kwenye ofisi ya tawi mwenyekiti wake akiwa ni Katibu wa tawi, katibu wa kikao ni Katibu mwenezi wa tawi na wajumbe ni Mwekahazina wa tawi, Katibu wa Mipango na chaguzi tawi na makatibu wa ngome za vijana, wanawake na wazee kwenye tawi.
(5) Kazi za Mkutano Mkuu wa ACT Tawi
i) Kuchagua viongozi wa ACT-Tawi kama walivyotajwa katika ibara ndogo ya (3) hapo juu, isipokuwa kwamba viongozi wa ngome kwenye tawi watachaguliwa kwa mujibu wa miongozo ya ngome zao;
ii) Kupiga kura ya maoni na kupendekeza wagombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji;
iii) Kujadili taarifa ya Kamati ya Uongozi ya ACT Tawi na kutoa maamuzi au maelekezo ya utekelezaji;
iv) Kupokea maamuzi na maagizo ya vikao vya juu vya Chama na kutoa maelekezo kwa Kamati ya Uongozi ya ACT Tawi kwa utekelezaji;
v) Kujadili utekelezaji wa itikadi, falsafa, sera na mipango ya Chama inayohusu masuala ya jamii katika eneo la kijiji, mtaa ama Sheia;
vi) Kutoa mwongozo na maelekezo kwa wawakilishi wa Chama walio kwenye Serikali ya Kijiji au Kamati ya Mtaa;
vii) Kujadili na kuzingatia taarifa za utendaji wa NGOME za ACT Vijana, Wanawake na Wazee katika Tawi na kutoa maelekezo; na
viii) Kuidhinisha programu za Chama katika eneo lao.
(6) Kazi za Kamati ya Uongozi ya ACT Tawi
i) Kuendesha shughuli za kila siku za Chama katika eneo lake;
ii) Kuandaa Mkutano Mkuu wa ACT Tawi na ajenda zake;
iii) Kuhamasisha wananchi kujiunga na Chama kwa kueneza itikadi, falsafa, sera na madhumuni ya Chama;
iv) Kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea kwenye serikali za mitaa, vijiji na vitongoji;
v) Kuendesha na kusimamia Kampeni za Uchaguzi wa wagombea wa Chama katika Uchaguzi wa Kiserikali;
vi) Kusimamia na kuweka kumbukumbu za mali, mapato na matumizi ya ngazi husika;
vii) Kusimamia utekelezaji na uzingatiaji wa maadili ya Chama; na
viii) Kuhakikisha Chama kinashika hatamu kwenye uchaguzi wa Tawi na kinapata kura nyingi za mwenyekiti wa kijiji/mtaa, Ubunge na Urais katika ngazi ya Tawi.
(7) Kazi za Sekretarieti ya ACT Tawi:
i. Kuandaa Kikao cha Kamati ya Uongozi ya Tawi na agenda zake;
ii. Kusimamia uendeshaji wa shughuli za kila siku za Chama katika Tawi;
iii. Kuandaa mikakati na kuishauri Kamati ya Uongozi ya Tawi juu ya kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za kiserikali;
iv. Kuhamasisha wananchi kujiunga na Chama kwa kueneza itikadi, falsafa, sera na madhumuni ya Chama;
v. Kutekeleza maamuzi ya vikao vya Tawi na ngazi za juu vya Chama;
vi. Kuweka kumbukumbu sahihi za wanachama na wafuasi wa Chama katika madaftari ya wanachama na wafuasi vijana wa Chama kwa mujibu wa Kanuni za Chama;
vii. Kuandaa taarifa mbalimbali za Chama katika Tawi na kuziwasilisha kwenye ngazi za juu kwa mujibu wa Kanuni za Chama.
(8) Kazi za Mwenyekiti wa ACT Tawi
i) Atakuwa Mwenyekiti wa mikutano na vikao vyote vya ACT Tawi;
ii) Atakuwa msemaji mkuu wa Chama katika ACT Tawi;
iii) Atakuwa ndiye mwenezi na mhamasishaji mkuu wa siasa ya Chama katika eneo lake;
iv) Katika mikutano anayoongoza, zaidi ya kuwa na kura yake ya kawaida, atakuwa pia na kura ya uamuzi endapo kura za wajumbe wanaoafiki na wasiofiki zitalingana; na
v) Atahakikisha kuwa Chama kinashinda ngazi ya Tawi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
(9) Kazi za Katibu wa ACT Tawi
i) Atakuwa Katibu wa mikutano na vikao vyote vya ACT Tawi;
ii) Atawajibika kuandaa na kutoa taarifa ya kila mwezi kuhusu utendaji wa shughuli za Chama katika Tawi;
iii) Atakuwa Mtendaji Mkuu wa ACT Tawi;
iv) Atakuwa Mdhibiti Mkuu wa mali za Chama katika Tawi;
v) Atatunza daftari la wanachama wote waliopo katika eneo lake;
vi) Ataitisha vikao vya tawi vya Kamati ya Uongozi na Mkutano Mkuu kwa maelekezo ya Sekretariat na Kamati ya Uongozi;
vii) Atakuwa ndiye mwajibikaji mkuu wa masuala yote yahusuyo fedha na mali za Chama katika eneo lake; na
viii) Kuhakikisha kuwa Chama kinashinda ngazi ya Tawi katika uchaguzi wa kiserikali.

25. Ngazi ya ACT Kata/Wadi
(1) Ngazi ya ACT Kata/Wadi itaundwa katika eneo la kiutawala la Kata/Wadi
katika Serikali za Mitaa.
(2) Vikao vya Chama vya ACT Kata/Wadi vitakuwa ni:
i) Mkutano Mkuu wa ACT Kata/Wadi;
ii) Kamati ya Uongozi ya ACT Kata/Wadi; na
iii) Sekretariat ya Kata/Wadi.
(3) Viongozi wa Chama ngazi ya ACT- Kata/Wadi
i) Mwenyekiti wa Chama Kata/Wadi;
ii) Katibu wa Chama Kata/Wadi;
iii) Katibu wa Mawasiliano na Uenezi wa Chama wa Kata/Wadi;
iv) Mwekahazina wa Chama Kata/Wadi;
v) Katibu wa Mipango na Chaguzi wa Kata/Wadi;
vi) Wenyekiti NGOME za ACT Vijana, Wanawake na Wazee Kata/Wadi;
vii) Makatibu NGOME za ACT Vijana, Wanawake na Wazee Kata/Wadi; na
viii) Wajumbe wanne wa kuchaguliwa wa Kamati ya Uongozi ya ACT Kata / Wadi watakaochaguliwa na mkutano mkuu wa Kata/Wadi, wanaume wawili na wanawake wawili.
(4) Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ACT-Kata/Wadi:
i) Wajumbe wote wa kamati ya uongozi ya ACT Kata/Wadi;
ii) Wenyeviti wote wa ACT Tawi kwenye Kata/Wadi;
iii) Makatibu wote wa ACT Tawi kwenye Kata/Wadi;
iv) Katibu Mawasiliano na Uenezi, Katibu wa Uchaguzi na Mwekahazina wa kila tawi ndani ya Kata/Wadi;
v) Wenyeviti wote wa Ngome za Vijana, Wanawake na Wazee wa matawi kwenye kata/wadi;
vi) Makatibu wote wa Ngome za Vijana, Wanawake na Wazee wa matawi kwenye kata/wadi;
vii) Diwani, Diwani wa Viti Maalum, Mbunge/Mwakilishi anayeishi katika Kata;
viii) Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Wenyeviti wa Kamati za Mitaa wanaotokana na ACT kwenye kata;
ix) Wawakilishi wawili wa kila ACT-Kijiji/mtaa waliochaguliwa na Mkutano Mkuu.
(5) Kazi za Mkutano Mkuu wa Kata/Wadi
i) Kuchagua viongozi wa ACT Kata kama walivyoorodheshwa kwenye ibara ndogo ya (3) ya ibara hii, isipokuwa viongozi wa ngome watachaguliwa kwa mujibu wa miongozo ya ngome zao;
ii) Kupiga kura ya maoni katika kuchagua mgombea udiwani katika kata husika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Kanuni za ACT;
iii) Kujadili taarifa za Kamati ya Uongozi ya Kata/Wadi na kutoa maamuzi au maelekezo kwa utekelezaji;
iv) Kupokea maamuzi na maagizo ya vikao vya juu na kutoa maelekezo ya utekelezaji kwa Kamati ya Uongozi;
v) Kuzingatia, kujadili na kuweka miongozo ya utekelezaji wa Itikadi, Falsafa, Misingi na Sera za Chama katika Kata/Wadi;
vi) Kujadili na kutoa mapendekezo kwa ngazi za juu, kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayojitokeza katika Kata/Wadi, ambayo yanahitaji hatua za kichama ngazi za juu;
vii) Kuidhinisha Programu ya Chama katika Kata/Wadi;
viii) Kuchagua wajumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Kata; na
ix) Kujadili taarifa za utendaji wa NGOME za ACT Vijana, Wanawake na Wazee katika Kata/Wadi.
(6) Mkutano Mkuu wa ACT Kata utakutana mara mbili (2) kwa mwaka. Mikutano maalum/dharula inaweza kuitishwa wakati wowote na Kamati ya Utendaji kadri itakavyolazimu.
(7) Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Kata/Wadi:
i) Mwenyekiti wa ACT-Kata/Wadi;
ii) Katibu wa ACT-Kata/Wadi;
iii) Katibu Mwenezi wa ACT-Kata/Wadi;
iv) Katibu wa Mipango na Chaguzi Kata/Wadi;
v) Mweka hazina wa Kata/Wadi
vi) Wenyeviti wa NGOME za ACT Vijana, Wanawake na Wazee ngazi ya Kata/Wadi;
vii) Wajumbe wawili wa kuchaguliwa wa Kamati ya Uongozi ya Kata/Wadi;
viii) Diwani wa kuchaguliwa na wa viti maalum wanaotokana na ACT kwenye kata/wadi husika;
ix) Wawakilishi watatu (angalau mmoja awe mwanamke kama yupo) wa wenyeviti wa Mitaa, vijiji na vitongoji na wajumbe wa serikali na kamati za vijiji/mitaa.
(8) Kazi za Kamati ya Uongozi ya Kata/Wadi.
i) Kufanya uteuzi wa awali wa wagombea nafasi za uenyekiti, ujumbe na ujumbe viti maalum wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji;
ii) Kupokea na kujadili majina ya wagombea wa Chama katika uchaguzi wa Madiwani na kupeleka kwa Mkutano Mkuu wa ACT Kata/Wadi kwa kupigiwa kura ya maoni;
iii) Kuandaa Mkutano Mkuu wa Kata/Wadi na agenda zake;
iv) Kuandaa mikakati na kusimamia uendeshaji wa shughuli za Chama katika Kata;
v) Kusimamia uchaguzi wa viongozi wa Chama katika matawi;
vi) Kuandaa mikakati na kusimamia kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za kiserikali ndani ya kati/wadi;
vii) Kuhamasisha wananchi kujiunga na Chama kwa kueneza itikadi, falsafa, sera na madhumuni ya Chama;
viii) Kutekeleza maamuzi ya vikao vya juu vya Chama;
ix) Kuweka kumbukumbu sahihi za uanachama na ufuasi wa Chama katika madaftari ya wanachama na wafuasi vijana wa Chama kwa mujibu wa kanuni za Chama;
x) Kuandaa taarifa mbali mbali za Chama Kata/Wadi na kuziwasilisha kwenye ngazi ya Jimbo kwa mujibu wa Kanuni za Chama;
xi) Kuweka katika majalada maalum kumbukumbu za vikao na nyaraka nyingine za mawasiliano katika Chama;
xii) Kufuatilia utendaji kazi wa viongozi wa kiserikali katika Kata/Wadi waliotokana na Chama na kutoa ushauri au maelekezo kwa kadri inavyowezekana;
xiii) Kusimamia na kuweka kumbukumbu za mali, mapato na matumizi ya Kata husika;
xiv) Kufuatilia utendaji na utekelezaji wa maelekezo ya Chama kwa viongozi wawakilishi wa Chama katika mabaraza ya Serikali za Mitaa;
xv) Kutoa msaada kila inapobidi kwa viongozi wawakilishi wa Chama katika mabaraza ya Serikali za Mitaa;
xvi) Kutayarisha na kusimamia programu za Chama katika ngazi husika;
xvii) Kusimamia utekelezaji na uzingatiaji wa maadili ya Chama; na
xviii) Kusimamia utendaji wa NGOME za ACT Vijana, Wanawake na Wazee katika Kata.
(9) Kamati ya Uongozi ya ACT-Kata itakutana mara nne kwa mwaka yaani kila baada ya miezi mitatu. Vikao maalum/dharula vinaweza kuitishwa kadri itakavyolazimu.
(10) Wajumbe wa Sekretariet ya Kata/Wadi watakuwa ni:
i) Katibu wa Kata /Wadi – Mwenyekiti;
ii) Katibu wa Mawasiliano na Uenezi Kata/Wadi – Katibu;
iii) Mweka hazina wa kata/wadi;
iv) Katibu mipango na chaguzi; na
v) Makatibu wa ngome za vijana, wanawake na wazee kwenye kata/wadi.
(11) Kazi za Sekretarieti ya ACT Kata/Wadi:
(i) Kuandaa Kikao cha Kamati ya Uongozi ya Kata/Wadi na agenda zake;
(ii) Kusimamia uendeshaji wa shughuli za kila siku za Chama katika kata/wadi;
(iii) Kuandaa mikakati na kuishauri Kamati ya Uongozi ya Kata/Wadi juu ya kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za kiserikali;
(iv) Kuhamasisha wananchi kujiunga na Chama kwa kueneza itikadi, falsafa, sera na madhumuni ya Chama;
(v) Kutekeleza maamuzi ya vikao vya Kata/Wadi na ngazi za juu vya Chama;
(vi) Kuweka kumbukumbu sahihi za wanachama na wafuasi wa Chama katika madaftari ya wanachama na wafuasi vijana wa Chama kwa mujibu wa Kanuni za Chama;
(vii) Kuandaa taarifa mbalimbali za Chama katika Tawi na kuziwasilisha kwenye ngazi za juu kwa mujibu wa Kanuni za Chama.
(12) Kazi za Mwenyekiti wa Kata/Wadi:
i) Atakuwa na madaraka ya kuangalia mambo yote ya Chama katika Kata/Wadi yake;
ii) Atakuwa Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Chama wa Kata au Wadi na Kamati ya Uongozi ya Kata au Wadi;
iii) Katika Mikutano anayoiongoza, zaidi ya kuwa na kura yake ya kawaida, Mwenyekiti wa Chama wa Kata/Wadi pia atakuwa na kura ya uamuzi endapo kura za wajumbe wanaoafiki na wasioafiki zitalingana;
iv) Atakuwa msemaji na mhamasishaji mkuu wa Chama katika Kata/Wadi; na
v) Atahakikisha Chama kinashinda uchaguzi wa udiwani na kupata kura nyingi za Urais na Ubunge katika eneo lake.
(13) Kazi za Katibu wa Kata/Wadi:
i) Atakuwa Katibu wa vikao vyote vya kikatiba vya Chama katika Kata/Wadi;
ii) Atakuwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Chama katika Kata/Wadi;
iii) Atakuwa ndiye Mkuu wa mipango ya Chama katika Kata /Wadi;
iv) Atatunza orodha ya ACT Matawi, idadi ya ACT Matawi na wanachama waliopo kwa kila ACT Tawi lililoko katika Kata/Wadi yake;
v) Atatunza kumbukumbu za mali za Chama zisizoondosheka na zinazoondosheka zilizopo katika au chini ya ofisi ya Chama ya Kata/Wadi hiyo;
vi) Atawajibika na kutoa taarifa za kila mwezi kuhusu utendaji wa shughuli za Chama katika Kata/Wadi kwa ngazi ya Jimbo;
vii) Atakuwa ndiye mdhibiti Mkuu wa mali za Chama katika Kata/Wadi;
viii) Atawajibika kuandaa na kuitisha mikutano yote ya vikao halali vya Chama vya Kata/Wadi kwa maelekezo ya secretariat na Kamati ya Uongozi na kwa kushauriana na Mwenyekiti wake wa Kata/Wadi;
ix) Atafuatilia na kuratibu masuala ya ulinzi na usalama wa Chama katika Kata/Wadi yake;
x) Atafanya kazi yoyote itakayokuwa imetajwa penginepo katika Katiba hii; na
xi) Atahakikisha Chama kinashinda ngazi zote za udiwani na kupata kura nyingi za Urais na Ubunge.

26. ACT Jimbo
ACT Jimbo itaundwa kwenye eneo la Jimbo la Uchaguzi wa Ubunge/Uwakilishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na litaundwa kwa mujibu wa Katiba
na Kanuni za Chama.
(1) Vikao vya Chama vya ACT Jimbo vitakuwa ni:
i) Mkutano Mkuu wa ACT Jimbo;
ii) Kamati ya Uongozi ya ACT Jimbo; na
iii) Sekretarieti ya ACT Jimbo.
(2) Viongozi wa ACT-Jimbo
i) Mwenyekiti wa Jimbo;
ii) Katibu wa Jimbo;
iii) Katibu wa Mawasiliano na Uenezi wa Jimbo;
iv) Mweka Hazina wa Jimbo;
v) Katibu Mipango na Chaguzi Jimbo;
vi) Wenyeviti wa NGOME katika Jimbo;
vii) Makatibu wa NGOME katika Jimbo; na
viii) Wajumbe wanne wa kuchaguliwa wa Kamati ya Uongozi Jimbo watakaochaguliwa na mkutano mkuu wa Jimbo, wanaume wawili na wanawake wawili.

(3) Kwa wilaya zenye majimbo zaidi ya moja, Viongozi wa jimbo ambalo ndio Makao Makuu ya wilaya watakuwa ndio wawakilishi wa Chama wilaya kwa mambo yote ya kiserikali yanayohusu chama katika wilaya husika. Ikiwa kiongozi yeyote wa jimbo la makao ya wilaya hayupo, atawakilishwa kwenye shughuli za serikali ya wilaya na kiongozi mwenye cheo hicho hicho kutoka kwenye jimbo lisilo makao makuu ya wilaya.

(4) Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ACT Jimbo
i) Wajumbe wote wa Kamati ya Uongozi ya ACT Jimbo;
ii) Wenyeviti wote wa Kata/Wadi katika jimbo;
iii) Makatibu wote wa Kata/Wadi katika jimbo;
iv) Makatibu wa Uenezi, Makatibu wa Mipango na Wekahazina wote wa Kata/Wadi katika Jimbo;
v) Wenyeviti wa Ngome zote za Kata/Wadi katika Jimbo;
vi) Makatibu wa Ngome zote za Kata/Wadi katika Jimbo;
vii) Madiwani na Madiwani wa Viti maalum wanaotokana na ACT katika Jimbo.
(5) Kazi za Mkutano Mkuu wa ACT-Jimbo
i) Kuchagua Viongozi wa ACT Jimbo waliotajwa katika ibara ndogo ya (2) hapo juu, isipokuwa katibu wa Jimbo atachaguliwa kwa kupendekezwa kwa Kamati Kuu ambayo ndiyo itafanya uteuzi wa mwisho;
ii) Bila kuathiri kipengele cha (i) hapo juu, viongozi wa ngome zote watachaguliwa kwa mujibu wa miongozo ya ngome husika;
iii) Kupokea, kujadili na kupitisha taarifa ya utendaji na mapato na matumizi ya Jimbo;
iv) Kupokea na kuzingatia mikakati ya ushindi wa ACT katika chaguzi za kiserikali ndani ya Jimbo;
v) Kuzingatia na kutoa maelekezo ya utekelezaji kwa Kamati ya Uongozi ya Jimbo juu ya maamuzi na maagizo ya vikao vya juu;
vi) Kujadili taarifa za Kamati ya Uongozi ya Jimbo na kutoa maamuzi au maelekezo kwa utekelezaji;
vii) Kujadili na kuweka miongozo ya utekelezaji wa Itikadi, Falsafa, Misingi na Sera za Chama katika Jimbo;
viii) Kutoa mwongozo na maelekezo kwa wawakilishi wa Chama katika vyombo vya maamuzi vya kiserikali;
ix) Kuzingatia na kutoa mapendekezo kwa ngazi za juu, juu ya masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayojitokeza katika Jimbo na yanayohitaji hatua za kichama ngazi za juu;
x) Kuidhinisha Programu ya Chama katika Jimbo;
xi) Kupiga kura ya maoni ya wagombea wa Ubunge/uwakilishi katika Jimbo husika; na
xii) Kuchagua wajumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Jimbo. (6) Mkutano Mkuu wa Jimbo utafanyika mara mbili kwa mwaka. Mikutano maalum/dharula inaweza kuitishwa wakati wowote na Kamati ya Uongozi ya Jimbo kadri itakavyolazimu.
(6) Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya ACT Jimbo:
(ii) Mwenyekiti wa Jimbo;
(iii) Katibu wa Jimbo;
(iv) Katibu wa Mawasiliano na Uenezi wa Jimbo;
(v) Mweka Hazina wa Jimbo;
(vi) Katibu Mipango na Chaguzi Jimbo;
(vii) Wenyeviti wa NGOME katika Jimbo;
(viii) Makatibu wa NGOME katika Jimbo;
(ix) Wajumbe wanne wa kuchaguliwa wa Kamati ya Uongozi Jimbo;
(x) Mbunge na/au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi katika jimbo husika;
(xi) Meya na/au Naibu Meya anayetokana na ACT ikiwa anaishi ndani jimbo husika;
(xii) Mwakilishi wa Madiwani wote wanaotokana na ACT katika jimbo
(xiii) Wenyeviti na Makatibu wa Kamati mbalimbali zilizoundwa katika ngazi ya jimbo;
(xiv) Wajumbe wote wa Kamati Kuu wanaoishi katika Jimbo watakaoingia kama waalikwa lakini watakuwa hawana haki ya kupiga kura.
(7) Kazi za Kamati ya Uongozi ya ACT Jimbo
i. Kuandaa agenda za Mkutano Mkuu wa Jimbo;
ii. Kuandaa mikakati na kusimamia uendeshaji wa shughuli za kila siku za Chama katika Jimbo;
iii. Kusimamia misingi mikuu ya ACT katika jimbo husika;
iv. Kusimamia uchaguzi wa ndani ya chama katika kata/wadi;
v. Kupanga mipango ya kampeni za uchaguzi katika jimbo;
vi. Kuhakikisha chama kinaenea kwenye jimbo lote;
vii. Kupanga na kuandaa mkutano mkuu wa Chama jimbo;
viii. Kufanya uteuzi wa awali wa wagombea udiwani kwenye kata/wadi zilizo katika jimbo;
ix. Kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa nafasi mbalimbali katika ngazi ya Mitaa, vijiji na vitongoji;
x. Kuunda Kamati ndogo kadri itakavyoona inafaa; na
xi. Kujaza kwa muda nafasi za uongozi zilizowazi katika jimbo.
(8) Vikao vya Kamati ya Uongozi ya jimbo vitakutana angalau mara nne (4) kwa mwaka na vinaweza kuitishwa kwa dharula pale panapokuwa na uhitaji kufanya hivyo.
(9) Wajumbe wa Sekretariati ya ACT Jimbo
i. Katibu wa ACT Jimbo (Mwenyekiti);
ii. Katibu wa Mawasiliano na Uenezi Jimbo (Katibu)
iii. Mweka Hazina wa ACT Jimbo;
iv. Katibu wa Mipango na Chaguzi Jimbo
v. Makatibu wa NGOME katika Jimbo; na
vi. Makatibu wa Kamati mbalimbali katika Jimbo;
vii. Makatibu wa NGOME katika Jimbo;

(10) Kazi za Sekretarieti ya Jimbo
i. Kupokea taarifa ya majina ya wagombea udiwani katika Kata zilizo ndani ya Jimbo na kura walizopigiwa za maoni;
ii. Kuandaa kikao cha Kamati ya Uongozi ya Jimbo na agenda zake;
iii. Kuandaa mikakati na kuendesha shughuli za kila siku za Chama katika Jimbo;
iv. Kuandaa mikakati itakayopitishwa na Kamati ya Uongozi ya Jimbo kwa ajili ya kusimamia kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za kiserikali;
v. Kuhamasisha wananchi kujiunga na Chama kwa kueneza itikadi, falsafa, sera na madhumuni ya Chama;
vi. Kutekeleza maamuzi ya vikao vya Kamati ya Uongozi na Mkutano mkuu Jimbo;
vii. Kuweka kumbukumbu sahihi za wanachama na wafuasi wa Chama katika madaftari ya wanachama na wafuasi vijana wa Chama kwa mujibu wa Kanuni za Chama;
viii. Kuandaa taarifa mbalimbali za Chama katika Jimbo na kuziwasilisha kwenye ngazi za juu kwa mujibu wa Kanuni za Chama;
ix. Kuweka katika majalada maalum kumbukumbu za vikao na nyaraka nyingine za mawasiliano katika Chama;
x. Kuweka kumbukumbu za mali, mapato na matumizi ya Jimbo; na
xi. Kazi nyingine zozote watakazoagizwa na Kamati ya Uongozi ya Jimbo.
(11) Sekretariati ya Jimbo itakutana mara moja kila mwezi na inaweza
kukutana kwa dharula au vikao maalum kadri itakavyoona inafaa au
kwa maagizo ya vikao vya juu.
(12) Kazi za Mwenyekiti wa ACT-Jimbo
i) Atakuwa na wajibu wa kusimamia mambo yote ya Chama katika Jimbo;
ii) Atakuwa ndiye msimamizi mkuu wa mikakati ya ushindi wa Chama katika chaguzi za serikali ndani ya Jimbo, na utendaji wake utapimwa kutokana na, pamoja na mambo mengine, ufanisi wa Chama katika chaguzi za kiserikali ndani ya Jimbo;
iii) Atakuwa Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu na Kamati ya Uongozi ya Jimbo;
iv) Katika mikutano anayoiongoza, zaidi ya kuwa na kura yake ya kawaida, Mwenyekiti wa Chama wa Jimbo atakuwa na kura ya uamuzi endapo kura za wajumbe wanaoafiki na wasioafiki zitalingana;
v) Atakuwa msemaji na mhamasishaji mkuu wa shughuli za kila siku za Chama katika Jimbo; na
vi) Atahakikisha chama kinashinda uchaguzi wa Ubunge na kupata kura nyingi za Urais.
(13) Kazi za Katibu wa Jimbo
i) Atakuwa Katibu wa mikutano na vikao vya Kamati ya Uongozi na Mkutano Mkuu wa Jimbo;
ii) Atakuwa mwenyekiti wa vikao vya Sekretarieti ya Jimbo;
iii) Atakuwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Chama katika Jimbo na atafanya kazi chini ya Kamati ya uongozi ya Jimbo;
iv) Atakuwa ndiye Mkuu wa mipango ya Chama katika Jimbo;
v) Ataitisha na kuongoza vikao vya viongozi watendaji wakuu wa Chama katika Jimbo kwa madhumuni ya kushauriana, kuandaa agenda ya vikao vya Jimbo na kuchukua hatua za utekelezaji wa maamuzi ya Chama;
vi) Ataitisha vikao vya Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu wa Jimbo kwa maelekezo ya Sekretariat na Kamati ya Uongozi na kwa kushauriana na Mwenyekiti wa Jimbo;
vii) Atatunza orodha ya Kata/Wadi, Matawi na wanachama wa Jimbo lake;
viii) Atatunza kumbukumbu za mali za chama zisizoondosheka na zinazoondosheka zilizopo katika au chini ya ofisi ya Chama ya Jimbo lake;
ix) Atakuwa mdhibiti mkuu wa mali za Chama za Jimbo;
x) Atawajibika kutoa taarifa za utendaji wa shughuli za Chama katika Jimbo kila mwezi kwa ngazi ya Mkoa;
xi) Atafuatilia na kuratibu masuala ya ulinzi na usalama wa Chama katika Jimbo lake; na
xii) Kufanya kazi yoyote itakayokuwa imetajwa penginepo katika Katiba hii.

27. Ngazi ya ACT Mkoa
Ngazi ya ACT Mkoa itaundwa katika kila eneo la Nchi la kiutawala la Mkoa.
(1) Vikao vya ACT-Mkoa
i) Mkutano Mkuu wa Mkoa;
ii) Kamati ya Uongozi ya Mkoa; na
iii) Sekretariet ya Mkoa.
(2) Viongozi wa ACT-mkoa
i. Mwenyekiti wa ACT Mkoa;
ii. Katibu wa ACT Mkoa;
iii. Mweka hazina wa ACT Mkoa;
iv. Katibu wa Mawasiliano na Uenezi wa ACT Mkoa;
v. Katibu wa Mipango na Uchaguzi wa Mkoa;
vi. Wenyeviti wa Ngome za Vijana, Wanawake na Wazee Mkoa;
vii. Wajumbe wanne wa kuchaguliwa wa Kamati ya Uongozi Mkoa watakaochaguliwa na Mkutano mkuu wa Mkoa, wanaume wawili na wanawake wawili.
(3) Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ACT Mkoa:
i. Wajumbe wote wa Kamati ya Uongozi ya Mkoa;
ii. Wenyeviti na Makatibu wa majimbo yote yaliyomo kwenye mkoa;
iii. Makatibu wa uenezi, mipango na wekahazina wa majimbo yote yaliyomo kwenye mkoa;
iv. Wajumbe wanne wa kamati za uongozi za majimbo wa kuchaguliwa, wanaume wawili na wanawake wawili;
v. Wabunge na wabunge wa viti maalum wanaotokana na ACT kwenye mkoa; na
vi. Wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu wanaoishi katika Mkoa.
(iv.) Mkutano Mkuu wa ACT Mkoa utafanyika mara moja kwa mwaka. Mkutano Mkuu Maalumu au wa dharula unaweza kuitishwa wakati wowote kwa mahitaji maalumu na/au ya dharula.
(v.) Kazi za Mkutano Mkuu wa ACT Mkoa
i. Kuchagua Viongozi wa ACT Mkoa waliotajwa katika ibara ndogo ya (2) hapo juu, isipokuwa katibu wa Mkoa atachaguliwa kwa kupendekezwa kwa Kamati Kuu ambayo ndiyo itafanya uteuzi wa mwisho;
ii. Bila kuathiri kipengele cha (i) hapo juu, viongozi wa ngome zote watachaguliwa kwa mujibu wa miongozo ya ngome husika;
iii. Kupokea, kujadili na kupitisha taarifa ya utendaji na mapato na matumizi ya Mkoa;
iv. Kupokea na kuzingatia mikakati ya ushindi wa ACT katika chaguzi za kiserikali ndani ya Mkoa;
v. Kuzingatia na kutoa maelekezo ya utekelezaji kwa Kamati ya Uongozi ya Mkoa juu ya maamuzi na maagizo ya vikao vya juu;
vi. Kujadili taarifa za Kamati ya Uongozi ya Mkoa na kutoa maamuzi au maelekezo kwa utekelezaji;
vii. Kujadili na kuweka miongozo ya utekelezaji wa Itikadi, Falsafa, Misingi na Sera za Chama katika Mkoa;
viii. Kutoa mwongozo na maelekezo kwa wawakilishi wa Chama katika vyombo vya maamuzi vya kiserikali kwa mambo yanayohitaji msimamo wa chama kimkoa;
ix. Kuzingatia na kutoa mapendekezo kwa ngazi za juu, juu ya masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayojitokeza katika Jimbo na yanayohitaji hatua za kichama ngazi za juu;
x. Kuidhinisha Programu ya Chama katika Mkoa;
xi. Kuchagua wajumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Mkoa.
(6) Mkutano Mkuu wa Mkoa utafanyika mara moja kwa mwaka. Mikutano
maalum/dharula inaweza kuitishwa wakati wowote na Kamati ya Uongozi ya
Mkoa kadri itakavyolazimu.
(7) Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya ACT Mkoa:
i. Mwenyekiti wa Mkoa;
ii. Katibu wa Mkoa;
iii. Katibu wa Mawasiliano na Uenezi wa Mkoa;
iv. Mweka Hazina wa Mkoa;
v. Katibu Mipango na Chaguzi Mkoa;
vi. Wenyeviti wa NGOME katika Mkoa;
vii. Makatibu wa NGOME katika Mkoa;
viii. Wajumbe wanne wa kuchaguliwa wa Kamati ya Uongozi Mkoa;
ix. Wawakilishi wawili wa wabunge na/au wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika mkoa husika;
x. Mwakilishi wa mameya/wenyeviti na mwakilishi wa manaibu Meya/makamu wenyeviti wa halmashauri wanaotokana na ACT katika mkoa; na
xi. Wenyeviti na Makatibu wa Kamati mbalimbali zilizoundwa katika ngazi ya Mkoa.
(8) Kazi za Kamati ya Utendaji ya Mkoa
i) Kuratibu shughuli za chama katika Mkoa;
ii) Kufanya uteuzi wa awali wa wagombea ubunge/uwakilishi katika mkoa;
iii) Kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani kwenye mkoa;
iv) Kutoa ushauri na misaada ya kiutendaji kwa uongozi wa ACT-Jimbo katika Mkoa;
v) Kuratibu shughuli za kampeni za wagombea Urais na Ubunge katika mikoa na mgawanyo wa majukumu kijimbo;
vi) Kuratibu na kuunganisha shughuli za NGOME za Chama katika Mkoa;
vii) Kuwa kiunganishi cha Chama na shughuli za kiserikali katika Mkoa;
viii) Kuratibu na kutoa taarifa kwa Chama ngazi ya Taifa juu ya hali ya kisiasa, kijamii na kiutawala ndani ya Mkoa;
ix) Kuandaa mikakati na kusimamia uendeshaji wa shughuli za kila siku za Chama katika Mkoa;
x) Kusimamia misingi mikuu ya ACT katika Mkoa husika;
xi) Kusimamia uchaguzi wa ndani ya chama katika Majimbo;
xii) Kupanga mipango ya kampeni za uchaguzi katika Mkoa;
xiii) Kuhakikisha chama kinaenea kwenye Mkoa wote;
xiv) Kupanga na kuandaa mkutano mkuu wa Chama Mkoa na agenda zake;
xv) Kuunda Kamati ndogo kadri itakavyoona inafaa; na
xvi) Kujaza kwa muda nafasi za uongozi zilizowazi katika Mkoa.
(9) Kikao cha kawaida cha Kamati ya Uongozi ya Mkoa kitafanyika mara nne kwa mwaka. Vikao maalum / dharula vinaweza kuitishwa na Sekretariet wakati wowote kadri itakavyohitajika.
(10) Wajumbe wa Sekretariati ya Mkoa
i) Katibu wa Mkoa (Mwenyekiti);
ii) Katibu wa Mawasiliano na Uenezi Mkoa;
iii) Mweka Hazina wa ACT Mkoa;
iv) Katibu wa mipango na uchaguzi;
v) Makatibu wa NGOME za ACT Mkoa; na
vi) Makatibu wa Kamati mbalimbali zilizoundwa katika mkoa.

(11) Kazi za Sekretariati ya Mkoa
i. Kupokea taarifa ya majina ya wagombea ubunge katika majimbo yaliyo ndani ya Mkoa na kura walizopigiwa za maoni;
ii. Kuandaa kikao cha Kamati ya Uongozi ya Mkoa na agenda zake;
iii. Kuandaa mikakati na kuendesha shughuli za kila siku za Chama katika Mkoa;
iv. Kuandaa mikakati itakayopitishwa na Kamati ya Uongozi ya Mkoa kwa ajili ya kusimamia kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za kiserikali;
v. Kuhamasisha wananchi kujiunga na Chama kwa kueneza itikadi, falsafa, sera na madhumuni ya Chama;
vi. Kutekeleza maamuzi ya vikao vya Kamati ya Uongozi na Mkutano mkuu Mkoa;
vii. Kuweka kumbukumbu sahihi za wanachama na wafuasi wa Chama katika madaftari ya wanachama na wafuasi vijana wa Chama kwa mujibu wa Kanuni za Chama;
viii. Kuandaa taarifa mbalimbali za Chama katika Mkoa na kuziwasilisha kwenye ngazi za juu kwa mujibu wa Kanuni za Chama;
ix. Kuweka katika majalada maalum kumbukumbu za vikao na nyaraka nyingine za mawasiliano katika Chama;
x. Kuweka kumbukumbu za mali, mapato na matumizi ya Mkoa; na
xi. Kazi nyingine zozote watakazoagizwa na Kamati ya Uongozi ya Mkoa.
(12) Sekretariati ya Mkoa itakutana mara moja kila mwezi na inaweza
kukutana kwa dharula au vikao maalum kadri itakavyoona inafaa au
kwa maagizo ya vikao vya juu.
(13) Kazi za Mwenyekiti wa Chama Mkoa.
i) Atashughulikia au atakuwa na madaraka ya kuangalia mambo yote ya Chama katika Mkoa;
ii) Atakuwa Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Chama wa Mkoa, na Kamati ya Uongozi ya Mkoa;
iii) Katika mikutano anayoiongoza zaidi ya kuwa na kura yake ya kawaida, Mwenyekiti wa Chama wa mkoa atakuwa pia na kura ya uamuzi endapo kura za wajumbe wanaoafiki na wasioafiki zitalingana; na
iv) Atakuwa msemaji na mhamasishaji mkuu wa Chama wa Mkoa.

(14) Kazi za Katibu wa Chama wa Mkoa:
ii) Atakuwa mtendaji mkuu wa shughuli zote za Chama katika mkoa na atafanya kazi chini ya uongozi wa Kamati ya Uongozi ya Chama mkoa;
iii) Atakuwa ndiye msimamizi mkuu wa mipango ya Chama katika Mkoa;
iv) Ataitisha na kuongoza vikao vya viongozi watendaji wakuu wa Chama katika mkoa kwa madhumuni ya kushauriana, kuandaa agenda za Kamati ya Uongozi ya Mkoa na kuchukua hatua za utekelezaji wa maamuzi ya Chama;
v) Kutunza orodha ya Majimbo, Kata/Wadi, Matawi, na wanachama wa mkoa wake;
vi) Kutunza kumbukumbu za mali za Chama zisizohamishika na zinazohamishika zilizopo katika au chini ya ofisi ya Chama ya mkoa huo;
vii) Atakuwa mdhibiti mkuu wa mali za Chama wa mkoa;
viii) Atawajibika kutoa taarifa za kila mwezi kuhusu utendaji wa shughuli za Chama katika mkoa kwa ngazi ya Kamati Kuu Taifa;
ix) Atakuwa na wajibu wa kuandaa na kuitisha mikutano yote ya vikao vya Chama mkoa kwa maelekezo ya sekretarieti na Kamati ya Uongozi Mkoa kwa kushirikiana na Mwenyekiti wake;
(a) Atafuatilia na kuratibu masuala ya ulinzi na usalama wa Chama katika mkoa wake; na
(b) Atafanya kazi yoyote itakayokuwa imetajwa penginepo katika Katiba hii.

28. ACT Zanzibar
(1) Kutakuwa na Kamati Maalum ya Kamati Kuu kwa upande wa Zanzibar.
(2) Wajumbe wa Kamati Maalum ya Chama Zanzibar watakuwa ni:
i) Makamu Mwenyekiti Zanzibar (Mwenyekiti wa Kamati);
ii) Naibu Katibu Mkuu Zanzibar (Katibu wa Kamati);
iii) Wajumbe wa Kamati Kuu watokao Zanzibar;
iv) Manaibu Katibu Taifa wa Ngome za Vijana, Wanawake na Wazee;
v) Wenyeviti wa Mikoa Zanzibar ; na
vi) Maofisa katika idara mbalimbali za Ofisi ndogo ya Makao Makuu Zanzibar watakuwa wajumbe wasio na kura.
(3) Kazi za Kamati Maalumu Zanzibar:
i) Kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu juu ya masuala mbalimbali yahusuyo Zanzibar;
ii) Kusimamia utendaji wa Sekretarieti ya ofisi ya Makao Makuu Zanzibar;
iii) Kupendekeza mambo ya kisera yahusuyo Zanzibar;
iv) Kuleta mapendekezo kwa Kamati Kuu juu ya uteuzi wa wagombea ubunge na uwakilishi kwa upande wa Zanzibar kabla ya Kamati Kuu kufanya uteuzi wa mwisho;
v) Kuteua maafisa wa idara mbalimbali za Ofisi ndogo ya Makao Makuu Zanzibar;
vi) Kuratibu shughuli za chama Tanzania visiwani;
vii) Kutoa ushauri na misaada ya kiutendaji kwa uongozi wa ACT katika Mikoa ya Zanzibar;
viii) Kuratibu shughuli za kampeni za wagombea Urais na Urais wa Zanzibar katika eneo lote la visiwani;
ix) Kuratibu na kuunganisha shughuli za NGOME za Chama Visiwani;
x) Kuwa kiunganishi cha Chama na shughuli za kiserikali katika Zanzibar;
xi) Kuratibu na kutoa taarifa kwa Chama ngazi za juu kuhusu hali ya kisiasa, kijamii na kiutawala Zanzibar;
xii) Kuandaa mikakati na kusimamia uendeshaji wa shughuli za kila siku za Chama visiwani;
xiii) Kusimamia misingi mikuu ya ACT visiwani;
xiv) Kuhakikisha chama kinaenea Zanzibar yote;
xv) Kupendekeza majina ya wagombea urais na makamu wa Rais Zanzibar; na
xvi) Kufanya uteuzi wa awali wa mgombea uspika na naibu spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
(4) Kwa shughuli za kiutendaji Zanzibar, patakuwa na Sekretarieti ya Ofisi ndogo
ya Makao Makuu Zanzibar yenye wajumbe wafuatao:¬
i) Naibu Katibu Mkuu Zanzibar (Mwenyekiti);
ii) Manaibu Makatibu wa Taifa wa Ngome za Vijana, Wanawake na
wazee;
iii) Maofisa wa idara mbalimbali zilizopo Ofisi ndogo ya Makao Makuu
Zanzibar; na
(5) Kazi za Sekretarieti ndogo Zanzibar:
i) Utekelezaji wa kazi za kila siku za chama Zanzibar;
ii) Utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Kamati Kuu yanayohusu Zanzibar; na
iii) Uandaaji wa agenda na nyaraka kwa ajili ya vikao vya Kamati Maalum Zanzibar.
29. ACT-Taifa
(1) ACT-Taifa ni eneo lote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na litaundwa kwa kuzingatia masharti ya Kanuni za Chama zilizotungwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.
(2) Viongozi Wakuu wa Chama Taifa watakuwa ni:
i) Kiongozi wa ACT Taifa;
ii) Mwenyekiti wa ACT Taifa;
iii) Makamu Mwenyekiti wa ACT Taifa upande wa Zanzibar;
iv) Makamu mwenyekiti ACT Taifa upande wa Bara;
v) Katibu Mkuu wa ACT Taifa;
vi) Naibu Katibu Mkuu ACT Taifa upande wa Zanzibar; na
vii) Naibu Katibu Mkuu ACT Taifa upande wa Bara.
(3) Vikao vya Chama Taifa:
i) Mkutano Mkuu Taifa – ndicho kikao cha juu kabisa katika ACT na
ndicho chenye maamuzi ya mwisho kuhusu jambo lolote ndani ya
chama;
ii) Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia Taifa;
iii) Halmashauri Kuu ya Taifa;
iv) Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa; na
v) Sekretarieti ya Kamati Kuu.
(4) Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ACT watakuwa wafuatao:
i. Wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya Taifa;
ii. Wenyeviti na Makatibu wa Majimbo;
iii. Wawakilishi 15 wa ngome za chama taifa kwa wawakilishi watano kila ngome;
iv. Wawakilishi 12 wa wanafunzi wa vyuo vikuu waliochaguliwa na umoja wao kwa mujibu wa Kanuni zitakazowekwa na Ngome ya Vijana, kwa masharti kwamba angalau theluthi moja ya wajumbe hawa watakuwa wanawake;
v. Wawakilishi watatu wa ACT Nje watakaochaguliwa na wanachama walio nje ya nchi kwa sharti kwamba angalau mmoja awe mwanamke;
vi. Wawakilishi watano wa Wabunge na wawakilishi wanaotokana na ACT;
vii. Wawakilishi watano wa Madiwani wanaotokana na ACT; na
viii. Mjumbe mmoja atakayewakilisha kila mwanachama kikundi.
(5) Kazi za Mkutano Mkuu wa Chama Taifa:
i) Kuchagua Kiongozi wa ACT Taifa;
ii) Kuchagua Mwenyekiti wa ACT Taifa;
iii) Kuchagua Makamu Mwenyekiti wa ACT Taifa (Tanzania Bara);
iv) Kuchagua Makamu Mwenyekiti wa ACT Taifa (Zanzibar);
v) Kujadili taarifa za Halmashauri Kuu na kutoa maamuzi na maelekezo kwa utekelezaji;
vi) Kuteua mgombea wa Urais na mgombea mwenza wake kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
vii) Kujadili na kuridhia Itikadi, Falsafa, Misingi na Sera za Chama kisha kuweka mikakati na miongozo ya utekelezaji;
viii) Kujadili na kuridhia programu ya Chama kwa kuzingatia mapendekezo ya Halmashauri Kuu;
ix) Kupokea na kujadili taarifa ya Bodi ya wadhamini wa Chama juu ya mali na raslimali za Chama;
x) Kuidhinisha Ilani (Manifesto) ya Chama kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu;
xi) Kujadili na kuthibitisha mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ya Chama; na
xii) Kujadili na kufanyia maamuzi agenda nyingine yoyote iliyoletwa kwake na Halmashauri Kuu au Kiongozi Mkuu wa chama.
(6) Mkutano Mkuu Taifa utakutana mara moja katika kipindi cha miaka mitano. Mkutano Mkuu maalum/dharula unaweza kuitishwa wakati wowote ukiwepo ulazima kwa utaratibu utakaowekwa na Kanuni
(7) Kutakuwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa Kidemokrasia (National Democratic Congress) ambao ni mkutano wa Wanachama wa ACT. Mkutano huu:
i. Wajumbe wa mkutano huu ni wanachama wote wa ACT-Tanzania, wadau, wafadhili na wananchi wote kwa ujumla watakaopenda kuhudhuria;
ii. Utafanyika mara moja kwa mwaka kwa mikoa kupokezana na unaweza kuitishwa mara nyingi zaidi kama kuna hitaji la kufanya hivyo;
iii. Mkutano Mkuu wa Wanachama utakuwa ndio jukwaa la Kiongozi wa Chama kutoa mwelekeo wa kisera wa Chama na jukwaa la wanachama wote kuhoji utendaji wake.
iv. Mkutano Mkuu wa wanachama utajadili hali ya siasa na uchumi ya Nchi, Afrika na dunia kwa kila mwaka.
v. Mkutano Mkuu wa Wanachama litakuwa jukwaa la majadiliano lakini hautakuwa na maamuzi yoyote.
vi. Mambo yote yaliyojitokeza na kupendekezwa katika majadiliano ya Mkutano Mkuu wa Wanachama yanayohitaji maamuzi ya vikao mbalimbali yatawasilishwa katika vikao husika vya chama kwa maamuzi na yanayohitaji utekelezaji tu, yatawasilishwa kwa vyombo vya utekelezaji kwa ajili hiyo.

(8) Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya ACT Taifa:
i. Wajumbe wote wa Kamati Kuu;
ii. Wenyeviti wote wa Mikoa;
iii. Makatibu wote wa Mikoa;
iv. Makatibu wa Ngome taifa
v. Wawakilishi tisa wa Ngome za Vijana, Wanawake na Wazee kwa kila ngome kuwakilishwa na wajumbe watatu;
vi. Wawakilishi watano wa wabunge na wawakilishi wanaotokana na ACT;
vii. Wawakilishi watatu wa wanafunzi wa elimu ya juu watakaochaguliwa kwa utaratibu utakaoelezwa kwenye mwongozo wa Ngome ya Vijana;
viii. Wawakilishi watatu wa madiwani wanaotokana na ACT; na
ix. Wajumbe kumi na tano (15), ambapo angalau wajumbe watano (5) watakuwa wanawake, waliochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa.

(9) Kazi za Halmashauri Kuu ya Chama ya Taifa:
i. Kupendekeza wagombea wa Urais na Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwasilisha mapendekezo yake katika Mkutano Mkuu wa Taifa;
ii. Kuteua mgombea Urais wa Zanzibar;
iii. Kuchagua Katibu Mkuu wa Chama;
iv. Kuchagua wajumbe wanane kuingia kwenye Kamati Kuu;
v. Kusikiliza na kutoa maamuzi juu ya rufaa za uchaguzi na za kinidhamu kwa mujibu wa Katiba hii;
vi. Kujadili mikakati ya uendeshaji wa shughuli za Chama kwa kipindi kati ya Mkutano Mkuu na kuifanyia maamuzi panapostahili;
vii. Kuthibitisha mikakati na raslimali za kuendesha kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za Serikali hususani Uchaguzi Mkuu na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa;
viii. Kuandaa ratiba na Kanuni za Uchaguzi wa ndani ya chama kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama;
ix. Kutunga na kuzifanyia marekebisho Kanuni za kuendesha shughuli za Chama;
x. Kujadili taarifa za Kamati Kuu na kutoa maamuzi na maelekezo kwa utekelezaji;
xi. Kusimamia utendaji kazi wa Kamati Kuu;
xii. Kupendekeza kwa Mkutano Mkuu masuala yote ya Katiba ya Chama na mabadiliko yake;
xiii. Kujadili rasimu ya Ilani (Manifesto) ya uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwasilisha mapendekezo yake kwa Mkutano Mkuu kwa maamuzi;
xiv. Kuteua Wadhamini wa Chama;
xv. Kuthibitisha miongozo ya NGOME za Vijana, Wanawake na Wazee;
xvi. Kujadili na kuidhinisha majina ya wagombea wa nafasi za Kiongozi Mkuu, Mwenyekiti na Makamu Wenyeviti.
(10) Halmashauri Kuu ya Taifa itakutana angalau mara mbili kila mwaka. Vikao maalum/dharula vinaweza kuitishwa kadri itakavyolazimu kwa mujibu wa kanuni za Chama.
(11) Kiongozi wa Chama ataendesha vikao vya Kamati ya Uongozi wa Kitaifa ambayo itakutana kadri inavyoona inafaa. Inapotokea Kiongozi wa Chama hayupo, Mwenyekiti ataendesha vikao vya Kamati ya Uongozi wa Kitaifa.


(12) Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa watakuwa:¬
i. Kiongozi wa ACT;
ii. Naibu Kiongozi wa ACT, kama yupo;
iii. Mwenyekiti wa ACT Taifa;
iv. Makamu wenyeviti Taifa;
v. Katibu Mkuu Taifa;
vi. Manaibu Katibu wakuu Taifa;
vii. Wenyeviti wa Ngome za Vijana, Wanawake na Wazee Taifa;
viii. Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Chama Taifa;
ix. Makatibu wa Kamati za Kudumu za Chama Taifa;
x. Wajumbe wanane waliochaguliwa na Halmashauri Kuu kuingia Kamati Kuu kwa kuzingatia kuwa wajumbe sita watatoka bara na ambao angalau wawili (2) watakuwa wanawake, na wajumbe wawili (2) watatoka Tanzania Zanzibar na ambao angalau mjumbe mmoja (1) atakuwa mwanamke;
xi. Wajumbe watano walioteuliwa na Kiongozi wa Chama kwa mujibu wa Katiba hii
xii. Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar au Makamu wa Rais wa Zanzibar aliyetokana na ACT;
xiii. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Spika wa Baraza la wawakilishi waliotokana na ACT;
xiv. Waziri Mkuu au Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na Kiongozi wa Kambi ya upinzani kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar;
xv. Washauri wa chama Taifa, na
xvi. Mwenyekiti na Katibu wa Bodi ya Wadhamini.
(13) Kazi za Kamati Kuu ya Chama Taifa:
i. Kuunda Kamati za kudumu Makao Makuu ya chama;
ii. Kuteua washauri wa chama wasiozidi 3 kwa mapendekezo ya Kiongozi baada ya kushauriana na Mwenyekiti;

iii. Kuteua Wajumbe na Makatibu wa Kamati za kudumu za Chama Makao Makuu;
iv. Kuidhinisha wasemaji wa kisekta (wenyeviti wa kamati za kudumu za chama) kama walivyopendekezwa na Kiongozi wa Chama;

v. Kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu juu ya rufaa za uchaguzi na kinidhamu;
vi. Kuandaa na kutoa Mapendekezo kwa Halmshauri Kuu, Mikakati ya kuendesha shughuli za Chama kwa kila mwaka na kwa kipindi cha miaka mitano;
vii. Kuandaa na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu, Mikakati ya kupata mahitaji ya raslimali za kuendesha kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za kiserikali;
viii. Kuandaa na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu juu ya ratiba na maelekezo ya uchaguzi wa ndani ya chama;
ix. Kupitia na kutoa kwa Halmashauri Kuu mapendekezo ya haja ya kuzifanyia marekebisho au maboresho Kanuni za Chama ama Katiba ya Chama;
x. Kujadili taarifa za Sekretarieti ya Kamati Kuu na kutoa maamuzi na maelekezo kwa utekelezaji;
xi. Kusimamia utendaji kazi wa Sekretarieti ya Kamati Kuu;
xii. Kufanya mapitio ya Sera za Chama na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu kwa kuzingatia matokeo ya Utafiti uliofanywa na Sekretarieti ya Kamati Kuu;
xiii. Kusimamia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu;
xiv. Kuwa kiungo na kudumisha mahusiano mema kati ya Chama na vyama vingine vya siasa nchini, Afrika Mashariki na nchi nyingine;
xv. Kuteua kamati au tume za kushughulikia masuala maalum ya kichama kwa muda maalum;
xvi. Kuteua wakaguzi wa mahesabu ya Chama kwa kila mwaka;
xvii. Kuthibitisha uteuzi wa wagombea Uspika, Ubunge na Uwakilishi;
xviii. Kuandaa agenda za Halmashauri Kuu na Mapendekezo ya agenda za Mkutano Mkuu;
xix. Kuandaa hoja za kupelekwa Bungeni na Wabunge wa Chama;
xx. Kuratibu utendaji wa ofisi ndogo ya Makao Makuu Zanzibar;
xxi. Kusimamia utendaji kazi wa NGOME za Vijana, Wanawake na Wazee; na
xxii. Kuthibitisha Uteuzi wa Manaibu Katibu wakuu wa Tanzania bara na visiwani kutokana na mapendekezo ya Kiongozi wa Chama atakayependekeza majina ya manaibu katibu wakuu kwa kushauriana na Mwenyekiti Taifa na Katibu Mkuu Taifa.

(14) Kamati Kuu itakutana mara nne (4) kwa mwaka. Vikao maalum/dharula vinaweza kuitishwa kadri itakavyolazimu kwa mujibu wa kanuni za Chama.
(15) Kutakuwa na kamati za kudumu za Utendaji Makao Makuu ya Chama
zitakazoundwa na Kamati Kuu, ie.
i. Kamati ya Fedha na Raslimali;
ii. Kamati ya Mawasiliano na Uenezi;
iii. Kamati ya Mipango na Mikakati;
iv. Kamati ya Chaguzi na Kampeni;
v. Kamati ya Katiba na Sheria;
vi. Kamati ya Utafiti na Sera;
vii. Kamati ya Uadilifu ya Taifa;
viii. Kamati ya ACT - Amani
ix. Kamati ya Mambo ya Nje.

(16) Kamati Kuu inaweza kuunda Kamati zingine kama itakavyoona inafaa kwa
ufanisi wa Chama.

(17) Kutakuwa na Kikosi cha Amani cha Chama kitakachoitwa ACT-Amani kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa ambapo katika ngazi hii ya Taifa kitakuwa chini ya Kamati ya ACT- Amani. Kazi ya kikosi itakuwa ni kuhakikisha ulinzi na usalama wa wanachama, viongozi na mali za Chama.
(18) Muundo na kazi za Kamati zitaainishwa katika Kanuni za uendeshaji
zitazotungwa na Halmashauri Kuu.
(19) Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chama Taifa:
i. Katibu Mkuu – Mwenyekiti wa Sekretarieti;
ii. Naibu Katibu Mkuu Bara;
iii. Naibu Katibu Mkuu Zanzibar;
iv. Makatibu wa Kamati zote Makao Makuu; na
v. Makatibu wa NGOME zote za Chama Taifa.
(20) Katibu wa Mawasiliano na Uenezi atakuwa ndiye msemaji wa Chama na ndiye
Katibu wa secretariet ya Kamati Kuu.
(21) Kazi za Sekretariati ya Kamati Kuu ya Chama Taifa
i) Utekelezaji wa kazi za kila siku za uendeshaji shughuli za Chama;
ii) Utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Kamati Kuu;
iii) Kuajiri watumishi wa makao makuu; na
iv) Uandaaji wa agenda na nyaraka kwa ajili ya vikao vya Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu.
(22) Kutakuwa na Kamati ya Uongozi ya Kitaifa itakayoundwa na:
a) Kiongozi wa Chama
b) Mwenyekiti wa Chama
c) Naibu Kiongozi wa Chama (kama yupo)
d) Makamu Wenyeviti wa Chama
e) Katibu Mkuu
f) Wajumbe wasiozidi wawili watakaoteuliwa na Kiongozi wa Chama
(23) Kazi ya Kamati ya Uongozi wa Kitaifa itakuwa ni kushauriana kuhusu mambo mbalimbali ya chama lakini sio kikao cha maamuzi
(24) Bila kuathiri masharti ya Katiba hii, Kamati ya Uongozi wa Kitaifa inaweza kufanya maamuzi kwa jambo lolote ambalo ni la dharura na ambalo kusubiri kwake vikao vya kawaida vya chama kunaweza kuathiri taswira, uhai na/au ustawi wa chama.

(25) Kazi na sifa za Kiongozi wa Chama
i) Atakuwa kiongozi mkuu wa Chama na Mwenyekiti wa kikao cha Mkutano Mkuu wa kidemokrasia
ii) Atakuwa mkuu wa siasa, mshauri na mwelekezaji kwa viongozi wote na maafisa wa ACT pamoja na vikao vya chama;

iii) Kuteua wajumbe watano wa Kamati Kuu baada ya kushauriana na kukubaliana na Mwenyekiti wa Chama Taifa na uteuzi kuthibitishwa na Kamati Kuu kwa mujibu wa Katiba hii;
iv) Kuteua wasemaji wa kisekta ambao pia watakuwa ni wenyeviti wa Kamati za Makao Makuu;
v) Kuteua Naibu Kiongozi wa Chama kwa kushauriana na Kamati ya Uongozi atakapoona haja hiyo;
vi) Kiongozi wa Chama anaweza kuteua mwanachama mwingine mwenye mchango maalumu kuingia katika vikao vya chama kwa kushauriana na Mwenyekiti na Katibu Mkuu kama ataona kuna haja ya kufanya hivyo kwa maslahi ya chama;

vii) Kupendekeza majina ya washauri wa chama baada ya kushauriana na Mwenyikiti;
viii) Atakuwa ndiye mtoa tamko rasmi kuhusu masuala ya sera na mtazamo wa Chama katika mambo ya kitaifa na kimataifa;
ix) Atakuwa mtoa habari mahususi kwenye Mkutano Mkuu, Halmashauri Kuu na Kamati Kuu kuhusu hali ya kisiasa nchini na masuala mengine ya kitaifa na kimataifa;
x) Ataendesha vikao vya Kamati za Kisekta ili kutengeneza misimamo ya kisera ya chama na kuwasilisha mapendekezo ya kisera katika vikao vya chama kwa maamuzi
xi) Iwapo Kiongozi wa Chama hayupo kwa sababu yoyote ile na pale ambapo hakuna Naibu Kiongozi wa Chama, basi Mwenyekiti wa Chama atamteua moja ya wasemaji wa kisekta kuwa Kaimu Kiongozi wa Chama;
xii) Iwapo kiti cha Kiongozi wa Chama kitakuwa wazi kwa sababu ya kujiuzulu, kuondoka katika Chama, kuvuliwa uongozi au uanachama, maradhi yenye kuondoa uwezo wa kufanya kazi au kifo, Naibu Kiongozi wa Chama au kama na yeye hayupo basi aliyechaguliwa kutoka miongoni mwa wasemaji wa kisekta, atashikilia nafasi yake kwa sharti kwamba Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa utaitishwa katika muda usiozidi miezi kumi na miwili tangu kuwa wazi kwa kiti hicho kwa ajili ya kuchagua Kiongozi wa Chama, mwingine.

xiii) Mtu atakayechaguliwa kuwa Kiongozi wa Chama lazima awe na sifa za kuwa mbunge
xiv) Endapo Kiongozi wa Chama atashindwa katika uchaguzi wowote wa kiserikali, Halmashauri Kuu ya Taifa itabidi ikutane katika kipindi kisichozidi miezi sita tangu kufanyika kwa uchaguzi huo ili kujadili mazingira ya kushindwa kwake na kupiga kura ya siri ya kuamua kama Kiongozi wa Chama anastahili kuendelea na nafasi yake au la. Kiongozi wa Chama ataendelea na nafasi yake endapo zaidi ya nusu ya wajumbe watapiga kura ya kuwa na imani naye.

(26) Halmashauri Kuu ya Taifa inaweza kumsimamisha Kiongozi wa Chama kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa. Hata hivyo, kura ya imani haitapigwa hadi kuwe na hoja maalumu kwa ajili hiyo na ambayo imeungwa mkono na zaidi ya theluthi moja ya wajumbe wote wa Halmashauri Kuu.

(27) Kiongozi wa Chama ataweza kuondolewa kwenye madaraka baada ya mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa litakaloungwa mkono na zaidi ya nusu ya kura za wajumbe halali
waliohudhuria na kupiga kura.
(28) Kazi za Mwenyekiti wa Chama Taifa :
i) Atakuwa mlinzi mkuu wa sera zilizopendekezwa na kupitishwa au jambo lolote litakaloamuliwa na kupitishwa na vikao vya chama;
ii) Atahakikisha kuwa ngazi zote za chama zinatekeleza maamuzi yaliyotolewa na vikao;
iii) Atahakikisha kuwa ngazi zote zinafanya kazi ndani ya mipaka ya katiba, kanuni, sera na maamuzi yoyote yaliyoagizwa na vikao vikuu vya chama;
iv) Atafuatilia na kuratibu masuala ya ulinzi na usalama katika Chama Taifa;
v) Atakuwa mwenyekiti wa mikutano yote ya chama ya kitaifa isipokuwa vikao vya utendaji na Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia wa Wanachama;
vi) Atafanya shughuli nyingine za Chama kama atakavyoelekezwa na vikao vya Chama
vii) Atapendekeza kwa Kamati Kuu majina ya watu wanaofaa kuteuliwa kuwa Manaibu Katibu wakuu kwa kushauriana na Kamati ya Uongozi ya Kitaifa
viii) Katika mikutano anayoiongoza zaidi ya kuwa na kura yake ya kawaida atakuwa pia na kura ya uamuzi endapo kura ya wajumbe wanaoafiki na wasioafika zitalingana

(29) Iwapo Mwenyekiti wa Chama hayupo kwa sababu yoyote ile basi Makamu
Mwenyekiti kutoka Bara atakuwa Kaimu Mwenyekiti wa Chama kama
Mwenyekiti anatoka Zanzibar, au Makamu Mwenyekiti kutoka Zanzibar kama
Mwenyekiti anatoka Bara. Na kama huyo Makamu Mwenyekiti aliyetajwa
kwanza naye hayupo, basi makamu mwenyekiti aliyebakia atakaimu nafasi ya
uenyekiti.
(30) Iwapo kiti cha mwenyekiti wa Chama kitakuwa wazi kwa sababu ya kujiuzulu, kuondoka katika Chama, kuvuliwa uongozi au uanachama, maradhi yenye kuondoa uwezo wa kufanya kazi au kifo, Mkutano Mkuu maalumu wa Taifa utaitishwa katika muda usiozidi miezi kumi na mbili tangu kuwa wazi kwa kiti
hicho ili kuchagua Mwenyekiti mwingine. Katika muda huo, Halmashauri Kuu ya chama itateua Mwenyekiti wa muda kuziba nafasi hiyo kwa muda.

(31) Halmashauri Kuu ya Taifa inaweza kumsimamisha Mwenyekiti wa Chama kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa. Hata hivyo, kura ya imani haitapigwa hadi kuwe na hoja maalumu kwa ajili hiyo na ambayo imeungwa mkono na zaidi ya theluthi moja ya wajumbe wote wa Halmashauri Kuu.
(32) Mwenyekiti wa Chama ataweza kuondolewa kwenye madaraka baada ya mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa litakaloungwa mkono na zaidi ya nusu ya kura za wajumbe halali
waliohudhuria na kupiga kura.
(33) Kazi za Makamu Wenyeviti wa Chama Taifa
a. Watakuwa wasaidizi wakuu wa Mwenyekiti wa Chama na watafanya kazi zozote za Chama watakazopewa na Mwenyekiti wa Chama Taifa;
b. Watakuwa washauri wakuu wa Ngome za chama katika maeneo yao (Bara na Zanzibar)
c. Watakuwa wajumbe maalumu katika vikao vyote vya Ngome za chama kitaifa;
d. Makamu Mwenyekiti Zanzibar ndiye atakuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Zanzibar;
e. Watamshauri Mwenyekiti katika majukumu yake ya kila siku kwa maeneo yao;
f. Watakuwa wahamasishaji wa chama katika maeneo yao; na
g. Watakaimu nafasi ya mwenyekiti kama hayupo kwa mujibu wa Katiba hii
h. Halmashauri Kuu inaweza kumsimamisha Makamu Mwenyekiti kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye na ambayo itaungwa mkono na zaidi ya nusu ya wajumbe wote waliohudhuria kikao cha Halmashauri Kuu wakati hoja hiyo inatolewa.
(34) Kazi za Katibu Mkuu wa Chama Taifa
i) Atakuwa Katibu wa mikutano ya chama katika ngazi ya Taifa;
ii) Atakuwa ndiye msimamizi mkuu wa shughuli zote za utendaji za Chama;
iii) Ataitisha na kuongoza vikao vya sekretariet ya Kamati Kuu ya Chama kwa madhumuni ya kushauriana, kuandaa agenda za Kamati Kuu na kuchukua hatua za utendaji wa maamuzi ya Chama;
iv) Atakuwa na uwezo wa kuajiri, kuachisha kazi na kusimamia nidhamu ya watumishi wote wa kwa kushauriana na sekretarieti ya Chama kwa mujibu wa Katiba, Kanuni, taratibu za Chama na sheria za nchi;
v) Atakuwa na wajibu wa kuandaa na kuitisha mikutano yote ya vikao vya Chama katika ngazi ya Taifa kwa kushauriana na Kiongozi wa Chama na Mwenyekiti wa Chama, na kuchukua hatua za utekelezaji wa maamuzi ya Chama;
vi) Atakuwa mdhibiti mkuu wa mali za Chama zinazohamishika na zisizohamishika; na
vii) Atafanya kazi yoyote itakayokuwa imetajwa penginepo katika Katiba hii na/au kwa maelekezo ya vikao vya Chama.
viii) Halmashauri Kuu itakuwa na uwezo wa kumuondoa Katibu Mkuu kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani na kama kura hiyo itaungwa na zaidi ya nusu ya wajumbe waliohudhuria mkutano wa Halmashauri Kuu ambapo hoja hiyo imetolewa.
(35) Kazi za Manaibu Katibu Wakuu wa Chama Taifa
i) Kutakuwa na Naibu Katibu Mkuu atakayeishi na kufanya kazi zake Zanzibar na mwingine ataishi na kukaa Tanzania Bara. Isipokuwa kwa kuishi kwao hivyo hakutapunguza upeo wa madaraka yao ya kushughulikia kazi za Chama kwa Tanzania nzima;
ii) Naibu Katibu Mkuu wa Chama atakayefanya kazi Zanzibar ndiye atakuwa na wajibu wa kuandaa na kuitisha mikutano ya Kamati maalumu ya Halmashauri Kuu ya Chama Taifa Zanzibar;
iii) Mmoja wao atamsaidia Katibu Mkuu kukaimu kiti chake wakati Katibu Mkuu hayupo;
iv) Manaibu Katibu Mkuu wa Chama watakuwa ndio wasaidizi wakuu wa Katibu Mkuu wa Chama na watafanya kazi zozote za Chama watakazopewa na Katibu Mkuu wa Chama;
v) Watakuwa Makatibu wasaidizi wa vikao vyote vya Chama wakimsaidia Katibu Mkuu;
vi) Watamsaidia Katibu Mkuu kusimamia shughuli, taratibu na Kanuni zote za Kiutawala za Chama za kila siku;
vii) Watakuwa wajumbe wa vikao vyote ambavyo Katibu Mkuu wa Chama Taifa anashiriki kwa wadhifa wake;
viii) Naibu Katibu Mkuu Bara ndiye atakuwa mkuu wa utawala na itifaki wa Chama;
ix) Watafanya kazi nyingine zozote za Chama zitakazokuwa zimetajwa penginepo katika Katiba hii na/au kwa maelekezo ya Vikao vya Chama.

(36). Akidi katika vikao vyote
1. Akidi katika vikao vyote itakuwa ni asilimia 50 ya wajumbe wote wanaopaswa kuhudhuria kikao husika.
2. Bila kuathiri ibara ndogo ya (1) ibara hii, kamati kuu yaweza kupunguza idadi ya wajumbe watakaopaswa kuhudhuria vikao mbalimbali kwa wakati fulani kwa asilimia zisizozidi hamsini kwa azimio litakaloungwa mkono na asilimia 75 ya wajumbe wa Kamati Kuu.
3. Ikiwa wajumbe walioalikwa wamealikwa kwa kupunguza idadi kwa mujibu wa ibara ndogo ya (2) ya ibara hii, basi akidi kwenye vikao hivyo itakuwa asilimia 75 ya wajumbe wanaopaswa kuhudhuria.



SURA YA TANO

NGOME ZA CHAMA NA JUMUIA YA WABUNGE WA ACT

31. NGOME ni vitengo au jumuiya za Chama
1) NGOME ni vitengo au jumuiya za Chama ambazo zitaundwa na vijana, wanawake na wazee ambao ni wanachama wa ACT.
2) Kutakuwa na Ngome za Vijana, Wanawake na Walezi.
3) NGOME za chama zitakuwa na jukumu kuu la kueneza itikadi, falsafa, misingi na sera za chama kwa makundi yao husika (Vijana, Wanawake na Walezi).
4) Kanuni za uendeshaji wa Ngome zitatungwa na Ngome husika na
kuidhinishwa na Halmashauri Kuu kabla ya kuanza kutumika.
5) Kanuni na miongozo ya Ngome lazima zizingatie misingi ya Katiba hii. Pale
ambapo kuna mgongano wa kitafsiri kati ya Katiba hii na Kanuni za Ngome, Tafsiri ya Katiba ndiyo itakayotamalaki.

32. Kutakuwa na jumuiya ya wabunge wa ACT
Kutakuwa na jumuiya ya wabunge wa ACT itakayoundwa na wabunge wote wa ACT kwa mujibu wa Katiba hii na Kanuni za Chama. Jumuiya itaunda utaratibu wake wa kuijiendesha bila kuathiri masharti ya Katiba hii na kanuni za uendeshaji kazi za chama.

SURA YA SITA
MAPATO NA MALI ZA CHAMA:

33. Mapato ya Chama
(1) Mapato ya Chama ni:
i) Ada na viingilio vya wanachama.
ii) Michango ya hiari ya wanachama na wafuasi wa Chama.
iii) Michango ya hiari ya watu wa ndani na nje wanaounga mkono Chama.
iv) Misaada kutoka kwa vyama rafiki vya kisiasa vya ndani na nje ya nchi.
v) Misaada na ruzuku kutoka ndani na nje ya nchi.
vi) Mapato yanayotokana na hisa na miradi halali ya Chama.
(2) Mali za Chama ni:
i) Mali zozote zinazohamishika na zisizohamishika.
ii) Hisa za Chama katika miradi ya kiuchumi.
iii) Mali za NGOME Taasisi zingine katika Chama.

34. Kutakuwa na bodi ya wadhamini wa Chama
1) Kutakuwa na bodi ya wadhamini wa Chama yenye wajumbe wasiopungua
saba (7) na wasiozidi tisa (9) itakayoteuliwa na Halmashauri Kuu.
2) Mali zote za kudumu, vitega uchumi na dhamana zote zitawekwa chini ya
jina lililosajiliwa la Bodi ya Wadhamini.
3) Bodi ya wadhamini itateuliwa kila baada ya miaka mitano ya Uchaguzi Mkuu
wa viongozi wa Chama.
4) Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini watateuliwa na Kamati Kuu na kuidhinishwa na Halmashauri Kuu.
5) Mwenyekiti na Katibu wa Bodi ya Wadhamini watachaguliwa na wajumbe wenyewe kutoka miongoni mwao.
6) Wajumbe wa Kamati Kuu hawatateuliwa katika Bodi ya Wadhamini, isipokuwa Mwenyekiti na Katibu wa Bodi ya Wadhamini watakaoingia kwenye kamati kuu kwa nafasi zao.
7) Kanuni za Chama zitaainisha taratibu za mikutano ya Bodi ya wadhamini.
35. Ukaguzi wa Hesabu za Chama
(1) Kutakuwa na Kanuni za Fedha za Chama zitakazoidhinishwa na Halmashauri
Kuu. Kanuni hizi zitaainisha utaratibu wa fedha ndani ya Chama.
(2) Kutakuwa na Idara ya Ukaguzi wa ndani wa Hesabu za Chama.
(3) Hesabu za Chama zitakaguliwa kila mwaka na Kampuni ya Wakaguzi wa Nje
itakayoteuliwa na Kamati Kuu.
(4) Hesabu za Chama zitatawasilishwa katika vikao vya Chama na kwa Msajili wa
Vyama ili azifikishe kwa vyombo vingine kwa mujibu wa Sheria ikiwamo ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Serikali.
(5) Mweka Hazina atatoa taarifa kwa umma kuhusu taarifa ya fedha ya Chama kila baada ya muda maalum kama itakavyoamriwa na Halmashauri Kuu.

SURA YA SABA

MAMBO YA JUMLA KUHUSU KATIBA

36. Marekebisho ya Katiba
1) Mapendekezo ya mabadiliko yoyote ya Katiba yatafanywa na Hamashauri Kuu ya Taifa kabla ya kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa.
2) Mapendekezo yoyote ya mabadiliko ya Katiba yatajadiliwa katika ngazi za chini za Chama kabla ya Halmashauri Kuu kuandaa Rasimu ya mapendekezo kwa Mkutano Mkuu.
3) Mkutano Mkuu ndio pekee wenye mamlaka ya kubadili Katiba.
4) Mapendekezo ya marekebisho ya Katiba yatafikishwa katika ngazi ya Jimbo si chini ya siku 60 kabla ya tarehe ya Mkutano Mkuu unaohusika kujadili mabadiliko.
5) Kamati za Jimbo zitatakiwa kurejesha maoni yake na ya wanachama angalau marekebisho ya katiba.

37. Kanuni za Uendeshaji Chama
(1) Halmashauri Kuu itatunga Kanuni mbalimbali za uendeshaji wa Chama kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
(2) Kukitokea mgongano kati ya kipengele cha Katiba na kile cha Kanuni, kipengele cha Katiba kitatamalaki.
(3) Halmashauri Kuu itakuwa na mamlaka ya kuzifanyia marekebisho Kanuni za Chama ili kwenda na mahitaji na wakati.
(4) Kamati Kuu itatunga mwongozo wa uendeshaji wa vikao vya Chama.

38. Kuvunjwa kwa Chama
(1) Chama kitavunjwa rasmi endapo robo tatu (3/4) ya wajumbe wote watakaohudhuria Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa ulioitishwa kwa madhumuni ya kuvunjwa kwa Chama watapitisha hoja hiyo. Mkutano huo utatangaza rasmi kuvunjwa kwa Chama na kusimamishwa kwa shughuli zote za Chama.

(2) Katika tukio la kuvunjwa kwa Chama, Bodi ya Wadhamini wa Chama itahodhi mali zote za chama na kipaumbele kitakuwa ni kulipia madeni yote ya Chama. Endapo kutakuwa na salio lolote la mali ya Chama baada ya kulipa madeni yote, salio hilo litawasilishwa au kukabidhiwa kwa Taasisi yoyote ambayo shughuli zake zinaakisa misingi iliyoanzisha chama hiki kama itakavyoamuliwa na Bodi ya Wadhamini.

(3) Katika tukio la kuvunjwa kwa Chama kwa nia ya kuungana na Chama kingine cha Siasa, Bodi ya Wadhamini wa Chama itahodhi mali yote ya Chama na kuitumia mali hiyo kulipia madeni yote ya Chama. Endapo kutakuwa na salio lolote la mali ya Chama baada ya kulipa madeni ya Chama salio hilo litatumika kufuatana na azimio la kuvunja Chama ili kuungana na Chama kingine.


Kuanza Kutumika kwa Katiba Hii:
Katiba hii itaanza kutumia Tarehe 28 Machi 2015, baada ya kupitishwa na Mkutano Mkuu wa Chama Taifa.

 
NYONGEZA YA KWANZA

KANUNI ZA MWENENDO NA MAADILI YA VIONGOZI WA ACT

SEHEMU YA I:

MASHARTI YA JUMLA

Ibaya ya 1: Dhumuni la Maadili ya Uongozi
Dhumuni la Kanuni hizi za mwenendo na maadili ya viongozi ni kuweka viwango vya tabia na mienendo ya viongozi wa chama ili kuwafanya wawe na uwezo wa kimaadili kuiongoza jamii katika namna ya utii wa sheria na misingi ya ACT.
Ibara ya 2: Wanaohusika na Kanuni hizi za Mwenendo na Maadili
Kanuni hizi zitawahusu viongozi wote wa chama ndani ya ACT katika ngazi zote, wagombea katika uchaguzi wowote ule wanaogombea kwa tiketi ya ACT na mwanachama yeyote wa ACT-Tanzania anayeshikilia nafasi ya uongozi katika taasisi ya umma.
Kanuni hizi pia zitakuwa ni rejea na nyongeza ya Katiba ya ACT.

SEHEMU YA II:
SIFA ZA KIONGOZI
Ibara ya 3: Kiongozi wa ACT:
1) Awe Mzalendo;
2) Asiidhalilishe nchi yake Tanzania na Watanzania;
3) Awe na mtazamo wa kimaendeleo na mbunifu;
4) Awe mwadilifu;
5) Awe na maadili ya kiutamaduni, mwenendo na awe ni mtu wa kuchangamana na watu;
6) Awe na mapenzi ya dhati kwa chama na mweledi;
7) Asiwe amewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai linalohusiana na kukosa uaminifu;
8) Asiwe amewahi kunyang’anywa haki ya kiraia na/au ya kisiasa, isipokuwa kama alirudishiwa haki hiyo baada ya kuthibitika kutokuwa na kosa;
9) Awe na umri wa miaka 18 au zaidi;
10) Ajue kusoma na kuandika; na
11) Asiwe amewahi kufungwa jela kwa kipindi kinachozidi miezi sita bila parole kwa kosa linalohusiana na kukosa uaminifu.

SEHEMU YA III:
MAADILI YA VIONGOZI

Ibara ya 4: Sheria na Kanuni ambazo kiongozi wa ACT anapaswa kuzitii
Kiongozi wa ACT atatii Katiba ya Nchi, Sheria za Nchi, Katiba ya ACT na kanuni zake pamoja na Nyongeza hii ya Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Viongozi.
Ibara ya 5: Mwenendo bora wa Kiongozi
Kiongozi wa ACT atapaswa kuwa na viwango vifuatavyo vya kiuongozi:
1) Uzalendo na kuweka maslahi ya taifa mbele badala ya maslahi binafsi;
2) Kuzijua na kuziheshimu haki za binadamu na kuwahimiza wanachama na viongozi wengine kufanya hivyo;
3) Kujielimisha wakati wote
4) Kufanya kazi zake kwa kuzingatia misingi ya Demokrasia, Uwazi na Mashauriano;
5) Kuwa tayari kupokea na kuwasikiliza wote wanaomuijia;
6) Kukuza utamaduni wa mashirikiano na kuwawezesha wanachama kutekeleza wajibu wao;
7) Kuwataka wanachama kuheshimu maelekezo halali na kusimamia utekelezaji wa shughuli zilizoainishwa;
8) Kuheshimu ratiba ya kazi, muda na kuwasilisha ripoti panapohitajika;
9) Kuchapa kazi kwa bidii, umakini na weledi
10) Kuwafanya wanachama watambue mipango na programu za chama na kwa nafasi yake, kiongozi awe mfano wa kuigwa katika kutekeleza mipango na programu hizo;
11) Awe mtetezi wa Umoja wa Taifa na Afrika;
12) Kupinga na kupigana dhidi ya ubaguzi wa aina zote;
13) Kutangaza mali zake kwa mujibu wa sheria hii ya miiko na maadili ya Viongozi;
14) Kujitahidi kuwa mkweli katika kutimiza wajibu wake na katika jambo lingine lolote linalohusu mwenendo kwa hiari ama kwa kuombwa;
15) Asiwe mtu wa kujali maslahi yake binafsi dhidi ya maslahi ya umma;

SEHEMU YA IV:

MWENENDO NA MATENDO YASIYORUHUSIWA

Ibara ya 6: Matendo ya Ubaguzi na Utengano
Katika kutekeleza majukumu yake, kiongozi hataruhusiwa kumpendelea mtu yeyote kwa misingi ya udugu/urafiki, ukabila, familia, ukoo, udini, jinsia, mkoa ama kufanya tendo lolote litakalopelekea ubaguzi na kuwatenga watu katika madaraja.

Ibara ya 7: Makatazo mengineyo
Kiongozi pia hataruhusiwa kufanya yafuatayo:
1. Kushindwa kulipa deni linalotokana na dai ama mkataba halali; kutoa ama kupokea rushwa, kutaka kuabudiwa na kupewa upendeleo, utapeli, utakatishaji fedha na makosa mengine yanayohusiana na rushwa;
2. Kuweka maslahi ya mataifa ya nje mbele badala ya maslahi ya Tanzania;
3. Kutenda ama kuunga mkono tendo lolote linalolenga kukidhalilisha chama na/au nchi yetu;
4. Kutumia vibaya mali za chama na za taifa yeye mwenyewe ama kwa makusudi kuwaacha wanachama kufanya hivyo; kujibinafsisha mali au mchango uliotolewa kwa ajili ya chama na/au taifa, mradi ama tawi analosimamia;
5. Matumizi ya maneno na matendo yanayolenga kushusha hadhi, kudhalilisha utu, kumsimamisha ama kumfukuza mwanachama ama kiongozi mwingine kinyume na katiba ya chama na kanuni za uendeshaji chama;
6. Kutumia udikteta na ukandamizaji;
7. Kutumia madaraka vibaya kwa kuwanyanyasa watu na kuvunja sheria;
8. Kujimilikisha ngazi/idara/kitengo cha chama anachoongoza;
9. Na mwenendo wowote ambao unaweza kushusha uadilifu, kazi ama nafasi aliyonayo kama itakavyotafsiriwa na Halmashauri Kuu kwa mujibu wa Katiba ya ACT, Katiba ya Tanzania na sheria za nchi.
SEHEMU YA V:
MASUALA KINZANI YANAYOHUSIANA NA KAZI

Ibara ya 8: Masuala Kinzani
Inapotokea kiongozi ana wajibu wa kufanya maamuzi kwenye jambo lolote ambalo ana maslahi binafsi nalo, atatakiwa kuwataarifu viongozi wa juu yake ama mkuu wa taasisi iliyomwajiri ama kumteua na kuwataka radhi kwamba hatafanya uamuzi huo. Maslahi binafsi yaweza kutokana na nafasi yake au sababu nyingine yoyote iwe ni mchango wake mwenyewe ama kitu alichochangia na wengine ama ni mshauri tu.
Ibara ya 9: Viongozi kutofanya biashara
Kiongozi wa kuchaguliwa au kuteuliwa kwenye vyombo vya serikali kuanzia ngazi ya jimbo na kuendelea, hataruhusiwa kumiliki, kufanya ama kuendesha biashara ya binafsi. Ikitokea kiongozi wa namna hiyo ana biashara ya binafsi, mbali ya kuitangaza hadharani, atatakiwa kuiweka biashara yake chini ya menejimenti binafsi na kutangaza hilo hadharani.


SEHEMU YA VI:
KUTANGAZA MALI BINAFSI ZA KIONGOZI

Ibara ya10: Tangazo la mali binafsi za kiongozi
Kila kiongozi wa ACT wa kuchaguliwa ama kuteuliwa kwenye ngazi ya Jimbo au zaidi atawasilisha tangazo la mali zake binafsi, zilizo ndani ama nje ya nchi, kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu.
Fomu ya tangazo la mali ikionyesha mali halisi za kiongozi itawasilishwa ofisini kwa Katibu Mkuu si zaidi ya tarehe 30 Juni ya kila mwaka, kwa viongozi ambao bado wako madarakani na katika kipindi kisichozidi siku 15 tangu wamalize muda wao kwa viongozi waliomaliza muda wao wa uongozi. Viongozi wapya waliochaguliwa watatakiwa kuwasilisha tangazo la mali ofisini kwa Katibu Mkuu wa chama katika kipindi cha mwezi mmoja tangu walipoingia madarakani.

Kiongozi yeyote ambaye fomu yake ya tangazo la mali haikukubaliwa, atatakiwa kuwasilisha nyingine ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Na kama fomu ya tangazo la mali haikukubaliwa kwa mara ya pili na kwa sababu ambazo amefahamishwa yeye mwenyewe, Ofisi ya Katibu Mkuu itaandaa taarifa na kuiwasilisha kwa chombo/mamlaka iliyomchagua/kumteua huyo kiongozi kwa ajili ya hatua stahiki dhidi ya kiongozi mhusika. Taarifa ya Mali na Madeni ya Viongozi itawekwa wazi kwenye tovuti ya chama na daftari la mali na madeni litakuwa wazi kwenye ofisi ya Katibu Mkuu.

Ibara ya 11. Viongozi kutangaza mali kabla hawajamaliza muda wao
Kila kiongozi aliyeko madarakani kwa kuchaguliwa ama kuteuliwa kwenye ngazi ya Jimbo au zaidi na ambaye ametangaza mali zake kwa mujibu wa ibara ya 10 ya nyongeza hii, atalazimika kutangaza mali zake miezi sita kabla ya kipindi chake cha uongozi kumalizika. Baada ya hapo ofisi ya Katibu Mkuu itafanya uchunguzi juu ya tangazo hilo na kuweka hadharani ripoti.
Ikiwa uchunguzi utaonyesha kwamba kuna uvunjifu wa maadili, mali ilinunuliwa kwa njia haramu, rushwa ama wizi, kiongozi ataondolewa kwenye nafasi yake na kupelekwa kwenye vyombo vya nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.


SEHEMU YA VII:
ADHABU NA MAREJEO MENGINE

Ibara ya 12: Adhabu kwa kiongozi mwenye hatia
Bila kuathiri sheria nyingine za nchi, kiongozi yeyote atakayevunja masharti ya nyongeza hii ya kanuni za mwenendo na maadili, atakabiliwa na mojawapo ya adhabu zifuatazo:
1. Onyo kwa maandishi;
2. Karipio kwa maandishi;
3. Kuachishwa uongozi; na
4. Kuachishwa uongozi kutakakofuatiwa na uchapishaji wa sababu za kuachishwa kwenye magazeti ikiwa ni kwa maslahi ya umma.
Kiongozi atakayeng’ang’ania kukaa kwenye nafasi ambayo ameondolewa ama kusimamishwa, ataondolewa uanachama.
Ibara ya 13: Haki ya Kujitetea
Kiongozi yeyote aliyepatikana na hatia kwa mujibu wa Maadili na Miiko iliyoainishwa katika nyongeza hii atakuwa na haki ya kusikilizwa.

Ibara ya 14: Rufaa
Kiongozi yeyote atakayeadhibiwa adhabu yoyote iliyomo kwenye nyongeza hii ya mwenendo na maadili ya viongozi, anaweza kukata rufaa kwa ngazi ya juu inayofuata kwa maandishi akielezea utetezi wake ama maelezo mengine kwenye kosa ambalo kwalo uamuzi ulichukuliwa. Utetezi huo uifikie ngazi ya rufaa ndani ya siku 14 baada ya kutaarifiwa.
Mchakato wa rufaa hautasimamisha utekelezaji wa uamuzi uliokwishachukuliwa isipokuwa kama mrufani ameomba hivyo na baada ya mamlaka ya rufaa kujiridhisha kwamba mamlaka ya chini ilikosea katika uamuzi wake ama kwamba ilipotoshwa wakati ikichunguza na kuchukua uamuzi huo.


SEHEMU YA VIII:


MASHARTI MENGINEYO NA MASHARTI YA MPITO

Ibara ya 14: Chombo chenye wajibu wa utekelezaji wa kanuni hizi za mwenendo na maadili
Kamati ya Uadilifu ya kila ngazi ndiyo itakuwa na wajibu wa kutekeleza kanuni hizi za mwenendo na maadili ya viongozi isipokuwa pale itakapokuwa imeelezwa vinginevyo. Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama itahakikisha kunakuwepo utengamano katika utekelezaji wa kanuni hizi za mwenendo na maadili na Katiba ya Chama.
Kila ripoti ya mwaka ya Katibu Mkuu itaonyesha nini kimeonekana katika utekelezaji wa kanuni hizi za mwenendo na maadili ya viongozi.
Masharti yote yaliyotangulia yanayokinzana na kanuni hizi za asili yanabatilishwa rasmi.
Ibara ya 15: Kuanza kutumika kwa Kanuni hizi
Kanuni hizi za mwenendo na maadili ya viongozi zimepitishwa rasmi kuwa nyongeza ya katiba ya chama na Mkutano Mkuu wa Taifa wa ACT jijini Dar es salaam na kuanza kutumika leo tarehe 28 Machi 2015.
 

Attachments

  • ACT Katiba Kama Ilivyopitishwa na Mkutano Mkuu 29Machi15.docx
    283.5 KB · Views: 238
(4) Pamoja na sababu nyingine kama zilivyoelezwa katika katiba hii na kanuni zitakazotungwa na Halmashauri Kuu, mwanachama yeyote ambaye atasaidia, kushawishi, kujiunga, kutoa tamko la kuunga mkono chama kingine au mgombea wakati Chama kimeweka mgombea kwenye uchaguzi wowote kwa mujibu wa Sheria ya Nchi atakuwa amepoteza uanachama wa ACT. Kanuni hiyo ingekuwapo CHADEMA ingetosha kabisa kumvua uanachama ZZK wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010 maana alijipambanua hadharani kumuunga mkono Kafulila wakati akigombea ubunge hali CHADEMA imemsimisha mgombea wake
 
Jina la Chama litakuwa ni ALLIANCE FOR CHANGE AND TRANSPARENCY (ACT) na chama kitajulikana kwa Kiswahili kama CHAMA CHA WAZALENDO. ALLIANCE FOR CHANGE AND TRANSPARENCY kwa kiswahili ndo CHAMA CHA WAZALENDO hivi mbona tafsiri ya kiingereza na kiswahili haviendani kabisa, hivyo utata umeanza kwenye jina la chama, na kama jina la chama lipo katika kiingereza ni uzalendo upi mnao?
 
Katiba ya Iran hii. Eti kutakuwa na kiongozi mkuu wa chama aka supreme leader ambaye ndiye Mmiliki wa chama na Mali zake zote
 
(4) Pamoja na sababu nyingine kama zilivyoelezwa katika katiba hii na kanuni zitakazotungwa na Halmashauri Kuu, mwanachama yeyote ambaye atasaidia, kushawishi, kujiunga, kutoa tamko la kuunga mkono chama kingine au mgombea wakati Chama kimeweka mgombea kwenye uchaguzi wowote kwa mujibu wa Sheria ya Nchi atakuwa amepoteza uanachama wa ACT. Kanuni hiyo ingekuwapo CHADEMA ingetosha kabisa kumvua uanachama ZZK wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010 maana alijipambanua hadharani kumuunga mkono Kafulila wakati akigombea ubunge hali CHADEMA imemsimisha mgombea wake


Mbowe pia almuunga mkono Nimrod Mkono
 
(4) Pamoja na sababu nyingine kama zilivyoelezwa katika katiba hii na kanuni zitakazotungwa na Halmashauri Kuu, mwanachama yeyote ambaye atasaidia, kushawishi, kujiunga, kutoa tamko la kuunga mkono chama kingine au mgombea wakati Chama kimeweka mgombea kwenye uchaguzi wowote kwa mujibu wa Sheria ya Nchi atakuwa amepoteza uanachama wa ACT. Kanuni hiyo ingekuwapo CHADEMA ingetosha kabisa kumvua uanachama ZZK wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010 maana alijipambanua hadharani kumuunga mkono Kafulila wakati akigombea ubunge hali CHADEMA imemsimisha mgombea wake
Katiba lazima izingatiwe.
 
Back
Top Bottom