Hawawezi kufuta fikra zetu zilizo vichwani mwetu

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,880
Hawawezi kufuta fikra zetu zilizo vichwani mwetu

Hotuba ya Mbunge wa Kigoma Mjini kwa Viongozi wa Matawi na Kata za Jimbo la Kigoma Mjini, Viongozi wa Majimbo yote ya Kigoma na Uongozi wa Mkoa wa ACT Wazalendo


Ukumbi wa ACT Wazalendo Ujiji, 1/4/2019

Ndugu Viongozi wa Chama kutoka matawi Jimbo la Kigoma Mjini, Viongozi wa Majimbo ya Mkoa wa Kigoma na Viongozi wa Mkoa

Machi 25, 2019, ACT Wazalendo tulipokea barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yenye kumbukumbu Na. HA. 322/362/20/98 ambayo; pamoja na mambo mengine, ilieleza juu ya kusudio la serikali kutaka kukifuta Chama cha ACT Wazalendo.

Machi 26, 2019 nilifanya mkutano na wanahabari makao makuu ya chama, kijitonyama, jijini Dar es salaam kuwajulisha wanachama pamoja na Watanzania juu ya barua husika pamoja na kutoa majibu ya hoja zote tatu ambazo Msajili wa Vyama vya Siasa alizitumia kwenye barua yake ya kuonyesha nia ya kufuta chama chetu. Sina sababu ya kuwachosha kwa kurudia Hotuba ile kwani naamini ninyi wote mliisikia. Kiufupi sababu zote 3 zilizotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama hazina mashiko. Chama chenu kupitia kwa Katibu Mkuu wake Mama Dorothy Semu kimejibu hoja zote kwa ushahidi.

  1. Hesabu za chama chetu za mwaka 2013/14 ( miezi 2 ya mwaka huo Ndio Chama kilikuwepo) ziliwasilishwa kwa Ukaguzi kwa CAG na Vitabu vya Hesabu zilizokaguliwa tuliziwasilisha kwa Msajili wa Vyama.
  2. Wanaoitwa wanachama wa Chama chetu waliochoma Bendera za CUF na kupandisha Bendera kwa maneno ya Mungu hawakuwa wanachama wetu na Chama hakina dhamana na watu ambao sio wanachama wetu.

Leo Jumatatu ya tarehe 1/4/2019 tumewasilisha maelezo yetu kwa Msajili wa Vyama. Lakini pia nimeona ni muhimu sana kukutana nanyi ili muelewe maana ya Tishio hili la Serikali kutaka kukifuta Chama chetu.

Uamuzi Huu wa Msajili Ukitekelezwa Utakewa na Athari Gani Hapa Kigoma?

Mimi, mbunge na mtoto wenu, Kabwe Z. Ruyagwa Zitto ni mwakilishi wenu wa Jimbo hili la Kigoma Mjini kupitia chama cha ACT Wazalendo, Meya wa Manispaa yetu ya Kigoma Ujiji anatoka chama hiki cha ACT Wazalendo, Madiwani 19 kati ya madiwani wote 26 wanatokana na ACT Wazalendo. Hivyo ACT Wazalendo ikifutwa mtakosa mbunge pamoja na kuvunjika kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji (maana madiwani 7 watakaobaki watashindwa kuunda 50% ya Baraza la Madiwani la kuongoza Manispaa yetu).

Jambo hilo lina maana kuwa sasa watu wa Kigoma Mjini na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla mtakosa mbunge wa kupaza sauti yenu bungeni, mtakosa mbunge wa kwenda kuhimiza kumalizwa kwa mradi wa maji uliocheleweshwa tokea mwaka 2015, mtakosa mbunge wa kupaza sauti juu ya uonevu wa watu wa uhamiaji dhidi yenu, mtakosa mpaza sauti juu ya utaifishwaji wa nyavu za wavuvi wetu kwenye Ziwa Tanganyika, mtakosa mpaza sauti juu ya kupotea kwa Diwani wa CCM na Mwenyekiti wa Halmashari ya Kibondo, ndugu Simon Kanguye, mtakosa mpaza sauti juu ya mauaji ya wafugaji wa Uvinza, mtakosa mpaza sauti juu ya kutupwa kwa zao la Michikichi huku Serikali ikitumia TZS 500 bilioni kuagiza mafuta ghafi ya Mawese kutoka Malaysia nk. Athari ni nyingi sana kwetu watu wa Kigoma.

Mkoa wetu umeachwa nyuma mno, umebaki kuwa mkoa pekee usiounganishwa na mtandao wa Barabara na mikoa mengine, tukiwa kwenye eneo muhimu la Kijiografia linalopakana na nchi mbili za Burundi na DRC Kongo lakini taratibu za uendeshaji uchumi na miundombinu zikituzuia kunufuaika na ujirani huo.

Mimi mbunge wenu nimetumia miaka hii minne ya kuwa mwakilishi wenu kushauri njia nzuri ya kututoa huku tuliko, nikishauri mapema hatua za kuchukua kwa mkandarasi wa maji aliyefilisika lakini anayebebwa na Serikali ili kuhakikisha mji wetu unakuwa na huduma ya uhakika ya maji, nikishauri namna njema ya kuondokana na matumizi ya Dola 220 milioni (TZS 500 bilioni) kununua mafuta ghafi ya mawese kutoka Malaysia kwa kuwekeza kwenye Kilimo cha Mawese hapa mkoani Kigoma, nikipigania upanuzi na uboreshaji wa bandari ya Kigoma ili kulikamata soko la Zambia na Kongo (70% ya mizigo yote ya bandari ya Dar es salaam), nk.

Licha ya Jumuiya ya Kimataifa kuelewa umuhimu wa Kigoma na kutoa fedha za Maendeleo yatakayochochea Maendeleo yetu, Serikali ya CCM imekuwa inavuta miguu kutekeleza miradi hiyo. Nitawapa mifano michache ya namna Serikali ya CCM inahujumu Mkoa wetu wa Kigoma.

  • Serikali ya Japan imeidhinisha mradi mkubwa wa kuboresha Bandari ya Kigoma wenye thamani ya dola za Marekani 40 milioni ( karibu Shs 100 bilioni ) Lakini mwaka Mzima sasa Wizara ya Fedha haitaki kusaini mkataba ili zabuni itangazwe na kazi ianze. Fedha hizi ni Msaada sio MKOPO.
  • Serikali ya Kuwait imeidhinisha Shilingi bilioni 35 kwa ajili ya Mradi wa Umwagiliaji wa Mto Luiche kwa ajili ya kilimo cha Mpunga, upembuzi yakinifu umekamilika na mkataba wa kutoa Fedha Upo tayari. Miaka 2 sasa Serikali imekalia kimya ikidai mkataba huo una masharti magumu ilhali ni hao hao Kuwait Fund waliotoa Fedha za Ujenzi wa Barabara ya Chaya-Nyahua kwa masharti hayo hayo kama ya Mradi wa Mto Luiche Lakini Huko masharti sio magumu!
  • Jumuiya ya Ulaya kupitia Benki yao ya European Investments Bank wameidhinisha Fedha dola milioni 20 Sawa na shilingi 50 bilioni kwa ajili ya Ujenzi wa Jengo la Abiria Katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma na kuupanua ili ndege kubwa zitue kwa ajili ya kuunganisha nchi za maziwa makuu na Mji wetu. Tangu mwaka 2018 Januari zabuni imetangazwa mpaka leo kazi haijaanza wakati Uwanja wa ndege wa Chato ambao haukuwa kwenye Bajeti ya Serikali wala mpango wa Maendeleo umejengwa na kukamilika.
Nimekuwa nafuatilia miradi hii muhimu sana kwetu kwa ukaribu Lakini Majibu ya Serikali ni kuzunguka zunguka tu. Hata miradi ambayo Fedha tayari zipo hazitolewi. Kwa Mfano mradi wa kuweka pavements kwenye mitaa yetu ili kutoa ajira kwa Vijana, Serikali imegoma kusaini mkataba wa mkandarasi mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi na usanifu. Serikali ya Ubelgiji Ndio yenye kufadhili kazi hii ambayo ingehusu kata 8 za Manispaa yetu. Sasa wanataka kufuta Chama chetu ili kuondoa Karaha ya kuwahoji hoji masuala Haya ya Maendeleo ya Watu wetu.

Wakiifuta ACT Wazalendo maana yake wanafuta nafasi yenu ya sauti yenu kupazwa bungeni. Madiwani wa Manispaa yenu ya Kigoma Ujiji wanasimamia miradi ya barabara zinazojengwa karibu kila kata ya Manispaa yetu kupitia mradi wa Benki ya Dunia, wakiifuta ACT Wazalendo maana yake watakuwa wanaondoa uwakilishi wenu kwenye usimamizi wa miradi hiyo.

Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 mlituchagua kihalali na kwa mujibu wa Sheria kuwa wawakilishi wenu kwenye nafasi za ubunge na udiwani kupitia chama cha ACT Wazalendo kwa muda wa miaka mitano, mliamua kutumia njia halali za kisheria kuchagua wawakilishi wa kupaza sauti zenu, kuwasemea mambo yenu. Tumetimiza wajibu wetu huo, lakini dola imekereka kwa kuwa tumepaza sauti sana, kwa kuwa tumewasemea mno, kwa kuwa Tanzania nzima imejua madhila yenu watu wa Kigoma, na kutengwa kwenu, wanataka kuwaziba sauti, wanataka kuwaondolea njia halali ya kupaza sauti yenu. Wanataka mtumie njia gani kuelezea kero zenu kama wanawaondolea njia halali iliyoko ya kisiasa?

Athari za Uamuzi wa Kuifuta ACT Wazalendo kwa Zanzibar na Taifa kwa Ujumla

Ni wiki mbili sasa tangu tumpokee kwenye chama chenu cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad, mshindi halali wa kura wa uchaguzi mkuu wa Urais wa Zanzibar wa mwaka 2015, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha CUF. Hakuja peke yake, amekuja pamoja na uliokuwa uongozi mzima wa CUF Zanzibar, Matawi zaidi ya 600 ya CUF Zanzibar pamoja na wanachama 125,000 waliojiunga kwa muda wa wiki hizi mbili kwa upande wa Zanzibar tu.

Wimbi hilo la waliokuwa wanachama na Viongozi wa chama cha CUF kujiunga na ACT Wazalendo limetokea pia kwa upande wa Tanzania Bara, maelfu ya wanachama wanachukua kadi katika Mikoa ya Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Mwanza, Morogoro, Pwani, Ruvuma, Tabora, Tanga nk. Chama chetu kimekuwa kikubwa mno, kimekuwa tishio mno. Ndio msingi wa hujuma za msajili wa vyama vya siasa kwetu.

Chama chetu sasa kimekuwa chama kikuu kwenye upande wa pili wa Muungano, Zanzibar na Serikali haipendi hilo na inataka kutufuta bila kufanya kosa lolote. Kama Serikali inamchukia Zitto Kabwe si wamshtaki mahakamani? Kama Serikali inamchukia Maalim Seif si wamkamate na kumfungulia mashataka? Kwanini ufute Chama Cha Siasa chenye maelfu ya Wanachama kwa makosa ya kubumba? Kwanini wazime haki yenu ya kikatiba ya kuamua kuwa kwenye Chama Cha Siasa mnachopenda? Wananchi wa Zanzibar umewanyanganya Chama chao, wamejiunga na ACT Wazalendo nacho pia kinafutwa, wafanye nini? Wamekuwa wakipaza Sauti Yao Kupitia Njia Halali za KiSiasa, Watawala Wanataka Kufuta Chama chao, Wakiapa kupambana kwa Njia Yeyote Ile watalaumiwa? Ninyi wanachama mtalaumiwa?

Chama chetu pia kimekuwa chama chenye nguvu zaidi katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, mikoa inayozalisha Korosho zaidi nchini. Sote tunajua madhila ya watu wa Korosho, chama chetu kilipaza sauti wakati walipokoseshwa pembejeo na Serikali, wakati walipoporwa Shs 200 bilioni zao za Exports Levy ya Korosho, na hata wakati Serikali ilipochukua korosho zao bila kuwalipa mpaka leo. Serikali ya CCM sasa inaogopa kuwa chama kilichopaza sauti juu ya korosho ndio sasa chama kikuu cha wakulima wa korosho. Tumesikia Rais Magufuli ana ziara ya kutembelea Mkoa wa Mtwara. Tunataraji kuwa Wakulima wote watakuwa wamelipwa. Pia Rais aeleze nini hatma ya hasara kubwa nchi imepata katika msimu wa Korosho uliopita. Nani atawajibika kwa hasara hiyo?

Tungetarajia Serikali ya CCM iwawajibishe Mawaziri Palamagamba Kabudi (Mambo ya Nje), Joseph Kakunda (Viwanda na Biashara) na Gavana wa Benki Kuu (BOT), Prof. Florens Luoga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Joseph Buchweshaija, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome, na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa, kwa kusaini mkataba wa kununua korosho na Kampuni ya kitapeli ya INDO Power Solutions bila hata kufanya uchunguzi wa kina (Due Diligence) juu ya kampuni hiyo, mpaka leo korosho hazijanunuliwa. Lakini Serikali imekaa kimya. Korosho zinapoteza ubora wake kwenye maghala. Hasara ya Mapato ya Fedha za Kigeni ya dola 500 milioni ( Sawa shs 1.2 trilioni ).

Badala ya Serikali kuhangaika na haya, Serikali ya CCM inahangaika kufuta chama kilichopaza sauti ya wakulima wa korosho kwa sababu wakulima hao wa korosho wameamua kujiunga kwa wingi kwenye chama cha ACT Wazalendo. Wanajua kuwa Ufukara waliowasabibishia wakulima wa korosho hautafutika kwa kuifuta ACT Wazalendo? Wanajua kuwa kwa kuwaondoa wakulima wa Korosho Chama kinachopaza sauti yao (ACT Wazalendo), wakulima hao wanaweza kutafuta njia mbadala ya kupaza sauti yao? Na njia hiyo inaweza isiwe halali na salama?

Ndugu Viongozi, tumekuwa pia Mwiba kwa Serikali Kuhusu uendeshaji wa Uchumi wetu. Tangu mwaka 2017 tumekuwa tukiionya Serikali kuwa namna inaendesha Uchumi lazima Uchumi wa Taifa utaanguka. Tumekuwa tukiihoji Serikali Kuhusu mzunguko wa fedha kuporomoka nchini na hivyo Uchumi kusinyaa. Serikali badala ya kuchukua tahadhari zetu kama ukosoaji wa kujenga ikaamua kutukamata na iliposhindwa kutufungulia mashtaka ikaamua kutunga sheria mpya ya takwimu ili kutuziba midomo. Sasa hali imekuwa mbaya zaidi. Hivi Karibuni itaibuka kashfa kubwa ya Serikali kudanganya takwimu za Pato la Taifa ( GDP ). Taasisi za Kimataifa kama IMF na Benki ya Dunia wamekuwa wakiitaka Serikali kutangaza takwimu za kweli ambazo kiwango Cha ukuaji wa Uchumi wetu ni kidogo sana kulinganisha na kile kinachosemwa na Serikali. Serikali inataka kutuziba tusiseme Hii kashfa kubwa na aibu kwa nchi yetu.

Ndugu Viongozi, Serikali ya CCM ya awamu ya 5 pia imevunja vunja misingi yetu ya Sera ya Mambo ya Nje. Miezi michache iliyopita vyama vya ukombozi kusini mwa Afrika vilikutana kule Namibia. Wakapaswa kutoa Tamko Kuhusu watu wanaoendelea kukandamizwa kama vile Sahara Magharibi na Palestine. Mwakilishi wa CCM kwenye mkutano ule Bwana Humphrey Polepole akakataa na kusema wao hawapo tena na watu hao. Kiingereza wanasema kuwa aliweka ‘Reservations’ kwenye tamko la pamoja. Hivi sasa nchi yetu inanuka mbele ya wenzetu Kusini mwa Afrika. Heshima ya nchi imeporomoka. Sisi kama ACT Wazalendo tumekuwa tukipigia kelele na kupaza sauti juu ya mambo Haya ndani na nje ya Bunge. Sasa watawala wamechoshwa na kelele zetu wanataka kutufuta.

Hitimisho

Nimewaeleza kwa ufupi nini kinatukabili ili muweze kujua kuwa hatufutwi kwa sababu ya Hesabu zetu au hao wanaoitwa wanachama wetu kuchoma Bendera za Chama kingine. Wanataka kutufuta kwa sababu wanakiogopa Chama chetu. Wanataka kutufuta kwa sababu wanamwogopa Maalim Seif ambaye amebeba matumaini ya Wazanzibari katika kutetea Muungano wa Haki na Usawa na Zanzibar yenye Maendeleo makubwa. Wanataka kutufuta kwa sababu ya kuwazima watu wa Kusini ambao tumekuwa nao bega kwa bega. Wanataka kutufuta kwa sababu tumekuwa mwiba kwao katika kuwahoji namna wanaendesha Uchumi wa nchi yetu. Sababu walizotoa kwenye Barua zao ni Geresha tu na sisi tumeshajibu Geresha zao.

Kama nilivyoeleza hapo juu, tumejibu Barua ya Msajili. Lakini pia tumechukua hatua mbalimbali ili kuzuia hili lisitokee. Tumewasiliana na Mwenyekiti wa Nchi za SADC, Rais wa Namibia Komred Geingob na pia Rais wa Afrika Kusini Komredi Cyril Ramaphosa. Pia tumewasiliana na Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye ni Mwenyekiti wa EAC na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. Wote tumewaomba wazungumze na Rais mwenzao ndugu Magufuli kindugu kabisa kuwa asiminye Demokrasia na kufuta Chama chetu. Tumeonana na Mabalozi wa Nchi za Afrika na nchi za Ulaya kuwaeleza hali halisi na kuwaomba waingilie kwa namna wanaona inafaa. Sisi tunaamini kuwa kitendo Cha Serikali ya Tanzania kutaka kutufuta ni kitendo Cha lengo la kuvuruga amani ya nchi yetu. Tumeomba marafiki zetu Afrika na nje ya Afrika waongee na Serikali yetu ili waachane na mpango huo. Pia tumejipanga kwa hatua za kisheria ili kulinda haki yetu ya kikatiba ya kuwa na Chama Cha Siasa. Kwa hiyo Viongozi tumeyafanya hayo yote ili kulinda Chama chenu.

Kama dhamira yao ni kutufuta basi watatufuta sio kwa sababu hatujafanya lolote kulinda haki yetu.

Lakini Viongozi wenzangu, Serikali itafuta shabaha zetu ndani ya mioyo yetu? Itafuta mawazo yetu ndani ya vichwa vyetu? Wamesahau kuwa “ unaweza kufuta taasisi, unaweza kuua watu Lakini huwezi kuua mawazo ya kimapinduzi”? Nataka msimame imara kuhami Chama chetu.

Asante sana

Zitto Kabwe
Ujiji, Kigoma
1/4/2019
 
Sisi wengine tunapenda kuona demokrasia iki stawi nchini, tukiamini kuwa ushindani mara zote huwalazimisha wahusika kuwa bora zaidi ili kuweza ku "survive" kwenye ushindani ambapo matokeo yake kwa ujumla ni kujengeka kwa jamii inayojifikirisha na kuwajibika hivyo kujenge nchi imara.​
Jambo ambalo tunapaswa kufahamu ni kuwa, Tanzania hatuna tatizo la chama bali tuna tatizo la watu. Tuna tatizo la watu ambao wanaongozwa na unafiki, tuna tatizo la idadi kubwa ya watu ambao wanaongozwa na ushabiki, tuna tatizo kubwa la watu ambao hawana wanachosimamia "seriously", kwa hiyo atakachokuambia leo na kesho ni tofauti. Tuna tatizo la idadi kubwa ya walaghai na pia tuna tatizo kubwa la watu wengi wanaopenda kunufaika kwa hila au hata kudhuru wengine ikiwezekana.Hii ipo tu miongoni mwa watu, na watu hao hao ndio wanaojiunga au kuhama kutoka chana kimoja hadi kingine.​
Viongozi wa ACT , tumieni uwezo wenu wote wa kiakili na muda wenu kujenga "Spirit". Msitegemee kufanya siasa za upepo kwa sababu upepo unavyokuja ndivyo unavyoondoka.Kwa kuwa Watanzania ndio hawa hawa wanaohama kutoka chama kimoja kwenda kingine, kwa kuhama tu hakuwafanyi wawe bora na hivyo kuwa na mchango wa maana zaidi au kuleta mabadiliko kwenye nchi, bali kwa kufanyika kazi ya ziada kuwafanya wawe watu bora kuliko ilivyokuwa jana.​
Kaeni chini mtambue ni vitu gani mnaamini na mnasimamia na mtasimamia bila kujali shida au raha (kwa kuwa tu mnaamini juu ya vitu hivyo). huu ndio msingi pekee unaoweza kuwasaidia kuwa na mafanikio ya kudumu na endelevu (wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kushindwa kwenye hili).​
Bila kulifanyia kazi jambo hili, mtajikuta mnaunganishwa na msingi wa unafiki na ushabiki (kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa vyama vingine tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe nchini), misingi ambao kusema kweli si imara na historia haioneshi kama ilishawahi kusaidia kuleta mafanikio yoyote ya maana kokote duniani. Jengeni misingi, aminini juu ya misingi hiyo, na simameni humo kwani kitu chochote endelevu huanzia kwenye imani. "Believe, live the belief and Succeed!".
Kwa jinsi ilivyo, watanzania Tunafahamiana. Wanasiasa wanafahamiana vilevile. Kama mtu ni mnafiki anafahamika, kama hana anachosimamia zaidi ya kupigania madaraka anafahamika lakini pia kama ana simamia misingi muhimu ana/atafahamika. Hakuna mtu atakayepata ujasiri wa kuwadhuru kwa namna yoyote watu ambao wataamini kwelikweli na kujidhihirisha kwenye kusimamia mambo ya msingi bila double standard wala unafiki. Ifahamike kuwa hata sasa, kitu kinachofanya inakuwa vigumu kupata uungwaji mkono wa maana hata kama chama/kiongozi wa chama anafanya jambo la maana au kadhulumiwa, ni kwa sababu wananchi wanakuwa hawana uhakika kama muhusika yuko serious au anaigiza na baadae hawezi kubalidika.​
Pia, mnashauriwa kufundisha na kujenga idadi kubwa ya viongozi wenye mawazo na fikra nzuri. Ukiwa na mtu mmoja au wawili wenye mawazo ya aina fulani (haijalishi ni mazuri kiasi gani), ni rahisi kwa watu wasiopenda mawazo hayo (kwa sababu yoyote ile) kuwa "target " watu hao na mawazo yao kuishia hapo hapo (Hata kama mawazo hayo ni mazuri kama mawaridi). Kwa hiyo kiongozi mzuri, ambaye anadhani ana mawazo mazuri, anatakiwa ahakikishe anawaandaa viongozi wengine wengi wenye mawazo mazuri kama yake au zaidi, ili kutawanya "RISK" Ili hata kama siku moja mtu mmoja anakuwa hayupo kwa sababu fulani, "spirit" inakuwa ipo. Kumbuka wanadamu leo tupo ila huwezi kujua kesho, kwa hiyo usikumbatie vitu (vizuri)peke yako bali sambaza (fundisha, shawishi,elimisha). mawazo yanayoweza kuleta mafanikio ni yale ambayo yanasambazwa na kuaminiwa kwa watu wengi zaidi kuwa ni mawazo sahihi na yanapaswa kusimamiwa.​
 
Labda kwa formality! Lakini kwa Kagame ni westage of resources mkuu wangu sana Erythrocyte
najua , lakini ukipeleka malalamiko kwenye balozi huwa wanauliza kama ulipita na humu kwenye hizi jumuiya zetu

Mimi ni miongoni mwa wadau waliomuonya sana Zitto kutobaki bungeni kwa ajili ya hotuba ya Magufuli kipindi Maalim ameporwa ushindi
 
Vipi Hon. Zitto mtasimamisha mgombea jimbo la Arumeru?
 
Bado hujasema figisu anazofanyiwa yule mwekezaji wa kiwanda cha sukari.
Halafu kuna watu CCM wanasema wanayaleta maendeleo ya viwanda.
Umma utashinda juu ya haya madhila ya CCM
 
Zitto tuko pamoja na wewe kwenye hizi harakati bila kumsahau jabari la siasa Africa mashariki Maalim Seif.

Nina ombi moja tu kwako mkanye huyu Home boy wako Abdul Nondo hajabarehe bado JF ni kina kirefu kwake, yeye si msemaji wa ACT anachokifanya humu anakuvuruga wewe kwa makusudi au kwakutojujwa.

Mkanye kijana huyu is not too late.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom