SoC03 Hatua za kuchukuliwa ili kumaliza vitendo vya ukatili na vitisho kwa watumishi wa umma vijijini

Stories of Change - 2023 Competition

EDOGUN

JF-Expert Member
Jul 9, 2023
256
296
Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 2007 nilipopata ajira ya kudumu ya ualimu baada ya kuhitimu mafunzo ya astashahada ya ualimu kutoka chuo kimoja maarufu kilichopo wilayani Muleba.Nakumbuka nilipangiwa kufundisha katika shule moja ya msingi iliyopo wilaya moja inayopakana na nchi ya Burundi.

Siku niliyofika kuripoti shuleni hapo nilipatwa na mshangao mkubwa pale nilipokuta shule ikiwa na mwalimu mmoja tu.Pia,nilishangazwa sana na shule hiyo kutokuwa na nyumba hata moja tu ya mwalimu.Kibaya zaidi,hata nyumba za kupanga zenye hadhi kwa mtumishi wa serikali hazikuwepo kabisa kwa wakati ule hapo kijijini.

Licha ya mazingira hayo magumu niliyoyakuta,nilijitahidi kufundisha kwa bidii kwani nilijua kazi ya ualimu ni kazi ya wito.Nilitumia mbinu mbalimbali nilizofunzwa chuoni na kwa kiasi fulani nilifanikiwa kuwafanya wanafunzi wengi kuinuka kitaaluma.Nakumbuka mara nyingi tu nilitumia mpaka muda wangu wa ziada ili niweze kuinua hali ya taaluma shuleni hapo.

Kwa jinsi nilivyojitolea kufanya kazi kwa moyo wangu wote nilitarajia kuwa wazazi wa wanafunzi wangu wangefurahishwa sana na uwepo wangu hapo shuleni.Nakumbuka ilikuwa imepita miezi tisa toka nifike kijijini hapo nilipoanza kuona mabadiliko fulani yasiyokuwa mazuri kwa baadhi ya wanakijiji hasa wazazi wenye watoto walio darasa la saba.

Nilipokuwa nikiwasalimia wanakijiji pindi tukutanapo njiani au kwenye mikusanyiko mingine,wengi hawakuitikia salamu yangu na kuna nyakati nilipovipita vikundi vya wanakijiji niliona kama wakiteta jambo fulani hivi kuhusu mimi.

Niliishi na hali hiyo kwa muda kama wa mwezi mmoja hivi mpaka siku moja nilipopata ugeni wa ghafla nyumbani kwangu.Ugeni huo ulikuwa ni wa mwenyekiti wa kijiji aliyekuwa ameambatana na wazee wengine watatu ambao walikuwa ni maarufu sana kijijini hapo.

 Taarifa walizonipatia wageni hawa, kwa kiasi kikubwa ndizo zilizonifanya niijue hasa sababu halisi ya wanakijiji wengi kuonekana kama kutofurahia uwepo wangu hapo kijijini.

Wageni hawa walianza mazungumzo yao kwa kunieleza kuwa sifa za uchapakazi wangu zimeenea sana kijijini na hazijawafurahisha kabisa wanakijiji wengi.Wakanieleza kuwa katika kijiji chao, walimu wachapakazi kama mimi huonekana kama maadui wa kijiji kwani wanakijiji wengi huwa hawapendi watoto wao wafaulu kwenda shule za sekondari kwa sababu ni gharama sana kumsomesha mtoto sekondari.

Wanakijiji wengi wanaona ni bora kuwaozesha mabinti zao punde tu wamalizapo darasa la saba kuliko kutumia pesa nyingi kulipia ada na michango mingine,na kwa watoto wa kiume wanakijiji wengi huona ni bora tu kuwatafutia vibarua vya kuchunga ng'ombe kwa wanyarwanda kuliko kupoteza pesa kuwalipia ada.

Wageni hawa wakaendelea kunieleza kuwa,kwa mtazamo wa wanakijiji wengi,kutumia pesa kumsomesha mtoto sekondari ni sawa tu na kumpatia mbuzi pesa,hatazinunulia kitu chochote, hii ndio sababu kuu ya wanakijiji kubuni mbinu mbalimbali kwa miaka nenda rudi kuhakikisha wanakwepa kuwapeleka watoto wao shule za sekondari.Hata hali niliyoikuta, ya shule nzima kuwa na mwalimu mmoja tu haikuja kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya jitihada za miaka mingi zilizofanywa na wanakijiji kuhakikisha hali inabaki kuwa hivyo.

Mwisho,wageni hawa wakamalizia mazungumzo yao kwa kunisimulia kisa kimoja kilichonishangaza sana kama sio kunitisha kabisa.Wakanieleza kuwa,miaka kama minne iliyopita alifika muhudumu mmoja wa afya katika zahanati ya kijiji, muhudumu huyo kijana alifanya kazi kubwa sana kuwahudumia wagonjwa,na pia aliwaelimisha wanakijiji wengi mpaka wengine wakaacha kwenda kwa waganga wa kienyeji pindi wauguapo kama ilivyokuwa desturi ya wanakijiji kwa miaka mingi.

Wazee hawa wakaendelea kunieleza kuwa licha ya juhudi kubwa alizozifanya muhudumu huyo kuzipigania afya za wanakijiji, malipo yake ilikuwa ni kifo cha kutiliwa sumu kwenye kinywaji.Basi baada ya hayo mazungumzo marefu na hawa wazee maarufu kijijini,waliniaga na kuondoka huku wakinisihi sana kuyatafakari vizuri mambo yote waliyokuwa wamenieleza na niitumie elimu yangu kuangalia namna ya kuicheza vizuri midundo ya ngoma ninayopigiwa na wanakijiji.

Mambo waliyonieleza wazee hawa yaliniacha nikiwa na mawazo mengi yaliyochanganyika na hofu.
Kilichonitia hofu ni hicho kisa cha mwisho walichonisimulia,kisa cha tabibu kuuwawa eti kwa kosa la kuwahudumia vizuri wagonjwa.

Nilibaki nikitafakari peke yangu, kumbe inawezekana kabisa hata haya matukio tunayokuwa tukiyasikia au kuyashuhudia,ya baadhi ya wahudumu wa afya kutoa huduma mbovu kwa wagonjwa, walimu kutokufundisha vizuri au kuwa watoro,maafisa kilimo kutokuwaelimisha wanakijiji vizuri juu ya mbinu nzuri na za kisasa za kilimo,maafisa mifugo kutowaelimisha wafugaji juu ya mbinu bora za ufugaji na matukio mengine ya watumishi wa umma kufanya mambo yaliyo kinyume cha utumishi wa umma huenda wakati mwingine huwa hayapo kwa bahati mbaya bali huwa ni mbinu za watumishi hao ili kuweza kucheza vizuri mdundo wa ngoma wanayokuwa wanapigiwa na wanavijiji.

Hebu fikiria kitendo cha muhudumu wa afya kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu iwe ni kosa ambalo adhabu yake ni kifo au kitendo cha mwalimu kutekeleza majukumu yake kwa juhudi kubwa iwe ni kosa linaloweza kumfanya awe adui wa kijiji.

Kwa fikra zangu, mambo yafuatayo yanaweza kufanyika ili kupunguza au kukomesha matukio ya vitisho au ukatili kwa watumishi wa umma vijijini :


  • Wanakijiji waunde vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuimalisha usalama kwa watumishi wa umma na kijiji kwa ujumla.​
  • Watu wenye historia ya kufanya ukatili kwa watumishi wa umma wapewe onyo kutokurudia vitendo hivyo.​
  • Watumishi wa umma wenye uzoefu wa kazi kwa miaka mingi wapelekwe kwenye vijiji vyenye historia ya kuwa na matukio mengi ya vitisho na ukatili kwa watumishi wa umma.​
  • Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo wajenge miundombinu ya barabara, minara ya simu nk. katika maeneo yenye historia ya kuwa na jamii zisizotaka mabadiliko chanya ya maisha ili kuvutia watu wenye fikra chanya za maendeleo.​
  • Vituo vya polisi vijengwe hadi vijijini ili kudhibiti vitendo vya unyanyasaji kwa watumishi wa umma.
  • Watumishi wa umma kuripoti haraka vitendo vya vitisho toka kwa wanakijiji.
  • Serikali kufuatilia ukaribu sana taarifa za vitisho kwa watumishi wa umma.​
  • Serikali kuwapa elimu wazee wa mila ili waweze kuyapokea mabadiliko chanya ya maisha na sio kupambana nayo.​
  • Ziwepo namba za simu za bila malipo kwaajili ya kupokea taarifa za vitisho toka kwa watumishi wa umma.​
  • Viongozi wa dini watumiwe kutoa elimu kwa waumini wao kujiepusha na matukio ya kuwatisha au kuwadhuru watumishi wa umma.​
 
Asante Kwa kuonyesha upande ambao UPO na unakosa kuonwa Kwa uhalisia wake wa kikatili na uovu Wenye kututokomeza Wenyewe. Inasikitisha ila napata Tumaini kuona kuwa watanzania tunatambua uwepo wa hay MATUKIO.
 
Asante Kwa kuonyesha upande ambao UPO na unakosa kuonwa Kwa uhalisia wake wa kikatili na uovu Wenye kututokomeza Wenyewe. Inasikitisha ila napata Tumaini kuona kuwa watanzania tunatambua uwepo wa hay MATUKIO.
Shukrani mkubwa
 
Back
Top Bottom