Hasunga amsaidia Kigwangalla kunadi vivutio vya utalii

Makanyaga

JF-Expert Member
Sep 28, 2007
10,327
6,850
Wakati Dk Hamis Kigwangalla akiambatana na wasanii wa bongofleva kuhamasisha utalii wa ndani, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ametoka kivingine.

Kwa kutumia fursa ya Tanzania kuandaa mkutano wa kimataifa uliowakutanisha wadau wa korosho kutoka kila pembe ya dunia, Waziri Hasunga ameviuza vivutio vilivyopo nchini na kuwataka wajumbe waliohudhuria kuhakikisha hawaondoki nchini kabla hawajavitembelea.

“Fuvu la mtu wa kale liligundulika Tanzania hivyo wageni mliopo hapa mjione mpo nyumbani. Vitembeleeni vivutio vyetu vya utalii na kujifunza mambo mengi, mkutano wenu umeratibiwa vizuri kwa kuwapa nafasi ya kutembelea vivutio vilivyopo,” amesema Hasunga.

Hasunga ametoa hamasa hiyo leo alipokuwa anafungua mkutano wa mwaka wa Shirikisho la Wadau wa Korosho Afrika (ACA) unaotarajiwa kuhitimishwa kesho ukiwahusisha wawakilisha wadau kutoka pembe zote za dunia.

Waziri Kigwangalla anayesimamia maliasili na utalii anatumia njia tofauti kuhakikisha idadi ya wageni pamoja na Watanzania wanaovitembelea vivutio vilivyopo nchini inaongezeka. Mwaka jana Tanzania ilipokea wageni milioni 1.5 waliovitembelea.

Waziri ameishukuru ACA kwa kuuleta mkutano huo wa 13 nchini ikiwa ni mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 2008 na akawataka wahudhuriaji kutembelea vivutio vilivyopo kwani Tanzania ina hazina kubwa kuanzia Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa Ngorongoro na Serengeti hata maziwa makuu.

Akizungumza na wawakilishi 30 kutoka Benin ambao ni wengi zaidi wakifuatiwa na Ivory Coast yenye washiriki 29, Guinea Bissau (11) na, Msumbiji na Burkina Faso tisa kila moja amewataka kuongeza siku za kuwepo Tanzania ili waongeze uzoefu wao kwenye maeneo tofauti.

Kwenye mkutano huo, Tanzania inao washiriki 102 huku wengine wakitoka mataifa mengine ya Afrika pamoja na Vietnam, Ufaransa, Marekani, China na Ujerumani.

Hasunga ametumia fursa hiyo pia kukumbusha asili ya korosho kuwa ni Brazil lakini mpaka sasa haipo kwenye orodha ya nchi zinazoongoza kwa uzalishaji duniani ila akawataka wadau hao kutafuta namna nzuri itakayoifanya Afrika inayoongoza kwa uzalishaji wa zao hilo ibangue yenyewe badala ya kusafirisha korosho ghafi.

Tanzania ilianza uzalishaji mkubwa wa korosho miaka ya 1960 ilipovuna tani 8000 mwaka ambazo ziliongezeka hadi tani 100,000 mwaka 1970 na kuifanya kuwa ya pili Afrika ikiwa nyuma ya Msumbiji. Kwa sasa inashika nafasi ya nne ikiwa nyuma ya Nigeria, Ivory Coast na Guinea-Bissau.

Kutokana na tofauti ya hali ya hewa, Tanzania huvuma korosho zake miezi sita kabla ya nchi nyingine duniani hivyo kujiondoa kwenye ushindani na kujihakikishia bei nzuri kwa wakulima.

Kingine kinachoipa sifa korosho za Tanzania ni ukubwa, inaelezwa mbegu zake zina ukubwa unaofanana hivyo kuwa na thamani zaidi tofauti na kwingineko ambako ukubwa hutofautiana.

“Nawakaribisha wafanyabiashara mliopo hapa kuwekeza nchini kwani mazingira na sera zetu ni rafiki na miradi yetu inaweza kutekelezwa ndani ya muda mfupi hivyo kufanikisha malengo yenu kwa wakati,” amesema Hasunga.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom