Hasara Ya Kula Mirungi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hasara Ya Kula Mirungi

Discussion in 'JF Doctor' started by X-PASTER, Jun 16, 2009.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Jun 16, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Mirungi au kama inavyojulikana kama Qaat au Qaadka huko Somalia, na Yemen huitwa au Al-Qaat; ingawa kwa matamshi ya huko hutamkwa 'Gaat'.

  Kadhalika Kenya kulingana na miji yake hujulikana kama; Miraa, Veve, Kijiti, Gomba n.k., na...

  Tanzania ni maarufu kwa majina; Mirungi, Gomba, Gati, Miti, Majani, Miraa n.k.

  Mirungi au (Catha edulis) Ni mmea au mti unaoota au kuoteshwa kwa wingi sana huko Ethiopia, Yemen na Kenya.

  Jani hilo ambalo Wataalam wameeleza kuwa ni halifahi kutafuna kama tutakavyoona mbele ya makala hii, ni jani lenye madhara mengi katika siha ya mwanadam na lenye kusababisha mengi katika madhara na maangamizi ya kimaadili na kijamii.

  Matumizi ya mmea huo ambao hakika kwa masikitiko makubwa, yameenea zaidi katika jamii zetu na haswa maeneo ya mijini na zaidi kwa wanaojulikana kama ‘Waswahili.'

  Ingawa neno ‘Waswahili' asli yake ni neno la Kiarabu 'Saahil' pwani, mwambao na 'Saahiliy' -ya pwani, au mkaazi wa pwani au mwambao, ila neno hilo au jina hilo hivi sasa limegeuka kimatumizi na kuashiria zaidi kwa wale watu zaidi wa mtaani, wasiopenda kutumika; kufanya kazi, wasio wakweli, wapenda starehe, wasio na elimu, wazembe n.k.

  Kwa wasio Waislam wao wanatumia jina hilo kuwaita nalo Waislam, na zaidi wakikusudia sifa hizo tulizozitaja hapo nyuma. Na kadhalika Waislam kadhaa huwaita wenzao hivyo wakimaanisha, wasio na ahadi, wasemao uongo, wasioaminika, wajanja wajanja, wajuaji, na wenye maneno mengi wasioshindika.

  Mirungi inakusanya ndani yake alkaloid iitwayo cathinone, amphetamine kama kichangamsho (stimulant) ambayo inasemekana husababisha msisimko, uchangamfu, kuwa na aina ya furaha ya kuwazika –kuhandasika- na huondosha hamu ya kula na kusababisha ukosefu wa usingizi.

  Mnamo mwaka 1980 WHO (Shirika la Afya Duniani) liliiweka Mirungi katika fungu la madawa ya kulevya ambayo inasababisha nafsi kutawaliwa nayo au kuwa na uraibu (addiction) kwa daraja ya kati hadi ile yenye nguvu.

  Mti huo umekuwa ukiandamwa na mashirika yenye kupinga madawa ya kulevya kama shirika liitwalo DEA (Drug Enforcement Administration).

  Shirika hilo katika mwaka 2006 Julai tarehe 26, shirika hilo katika operesheni iliyokuwa ikijulikana kama 'Somalia Express' ambayo katika upelelezi wake uliodumu kwa muda wa mwaka mmoja na nusu ambao ulihusisha wanachama 44 wa kundi lililokuwa likisafirisha tani 25 za Mirungi ambazo zilikuwa na thamani ya Dola milioni 10 za Kimarekani kutoka Somalia kupelekwa Marekani. Shitaka (Kosa) hilo lilihusisha utoroshaji mkubwa kabisa wa Mirungi katika Historia ya Marekani.

  [FONT=&quot]Biashara hiyo ambayo imeshamiri nchi za Afrika Mashariki ambapo hivi sasa Tanzania imepigwa marufuku, na pia kuenea katika nchi za Ulaya na Marekani.
  [/FONT]
   
 2. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #2
  Jun 16, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Mirungi imepigwa marufuku katika nchi mbalimbali za Scandinavia, lakini bado inajadiliwa Uingereza kama ni katika kifungu cha madawa ya kulevya au hapana!

  Ni mmea ambao umewekewa sheria kali au kupigwa marufuku nchi nyingi duniani.

  Mirungi imekuwa ni sehemu muhimu ya maisha ya watu wengi kuanzia Yemen, Ethiopia, Kenya, Tanzania na nchi ambazo watu wa nchi hizi wanaishi. Uingereza ambapo bado ulaji wa Mirungi haujapigwa marufuku; kila siku ndege inateremsha Mirungi kutoka Ethiopia na Kenya kwa wingi, na biashara yake imekuwa na nguvu kwa jamii ya Wasomali, Wayemen, Waethiopia na Watanzania wanaoishi katika nchi hiyo.

  Utagundua haraka sehemu au maeneo na nyumba zinazouzwa au kuliwa Mirungi kwa athari za uchafu wa vijiti vya Mirungi na majani yake yanayotupwa ovyo ovyo kila pahali na kuwa kero kubwa kwa wakazi wa jirani wa maeneo hayo na hata Manispaa au Serikali za Mitaa (Borough Councils) za maeneo hayo Uingereza.

  Kadhalika, kwa unafuu wake wa usafirishaji kwa ndege, majani hayo husafirishwa kuelekea sehemu zingine kama Wales, Rome, Amsterdam, Canada, Australia, New Zealand na Marekani.

  Ulaji wa Mirungi umekuwa ukiongezeka sana katika jamii mbalimbali hususan Yemen, Kenya na Tanzania na haswa walaji wa kiada –wakiwemo wanawake na hata watoto- na kusababisha kuongezeka mahitajio yake.

  Hii ni kwa sababu Mirungi ni kilevi cha kawaida katika jamii kama ilivyokuwa sigara ni kilevi kikubwa cha jamii ya Ulaya na Marekani hadi hivi karibuni baada ya kampeni za kila siku za kupiga vita. Ni kilewesho na uraibu ambao haujafikia daraja na uzito wa pombe. Haki ya uraibu huu umewatatiza Wasomi wengi wa Yemen na jamii zingine kufikia ufumbuzi wa kukata katika kuzima balaa hilo. Hata hivyo, kama tutakavyoona mbele ya makala hii, Wanasomii wengi wakubwa wa nchi mbalimbali duniani, wameeleza madhara yake.

  Kwa kujitetea, walaji Mirungi wanaamini kuwa majani hayo huwapatia nguvu, na uchangamfu na mliwazo wa furaha ‘Handasi au Nakhwa’ kwa lugha yao. “Hakuna Mirungi, hakuna nguvu, na hivyo hakuna kufanya kazi, Hakuna kufanya ngono (jimaa), kusoma, au chochote,” hivyo ndivyo wanavyodai.

  Pamoja na madhara yake na maonyo makali ya taasisi za tiba na mashirika ya Afya duniani, lakini inaelekea kumalizika matumizi ya Mirungi moja kwa moja, ni jambo linaloonekana litachukua miaka mingi sana na vizazi vingi huko Yemen na hata Afrika Mashariki. Yemen ni nchi ambayo uraibu huo umetawala hadi kufikia watu kulazimika kuwekea ‘nyakati maalumu’ za ulaji.

  Miaka kadhaa nyuma, Raisi wa nchi hiyo ‘Aliy ‘Abdullaah Swaalih aliwahi kueleza hadharani kuwa naye ni mlaji wa Mirungi lakini mwisho wa wiki; ingawa siku za mbeleni akaja kutangaza hadharani anajaribu kuachana nayo moja kwa moja. Mwaka 2002, wafanyakazi wote wa serikali ambao mwanzoni walikuwa wakila Mirungi kazini, walipigwa marufuku kuila kazini.

  Lakini leo hii, ulaji umeongezeka sana kuliko ulivyokuwa huko nyuma.

  Anasema mwandishi mmoja maarufu Yemen: “Mirungi (Qaat)… ni kileo cha watu wetu. Ni kiongozi wa kijani anayeongoza nchi yetu. Ni ufunguo wa kila kitu na ni makutano ya vikao na minasabati yote ya kijamii. Ni kitu kisichoelezeka kinachoeleza kila kitu”
   
 3. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #3
  Jun 16, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Historia Yake

  Inaaminika kuwa Ethiopia ndio asli yake kuanzia karne ya 15, na ikaenea katika milima ya Afrika Mashariki na Yemen. Ingawa vilevile kuna wanaoamini kuwa ilianzia Yemen katika karne ya 13 kabla ya kuenea hadi Ethiopia na nchi za jirani.

  Kutoka Ethiopia na Yemen, mti au mmea huo ulienea sehemu mbalimbali za Arabuni, Somalia, Sudan, Kenya, Tanzania, Uganda. Congo, Malawi, Zimbabwe, Zambia hadi Afrika ya Kusini.

  Baadhi hudai kuwa matumizi yake yanarejea miaka ya nyuma sana tokea wakati wa Wamisri wa kale ambao inasemekana walikuwa wakiitumia kama madawa ya jadi kwa baadhi ya magonjwa.

  Anaeleza mwandishi wa Kimalaysia... kuwa alipokuwa Yemen mwaka 1854, aliona ada na tabia ya utafunaji Mirungi huko Al-Hudaydah.

  Anaeleza: “Niliona jambo la ajabu katika mji huu –kila mtu anatafuna majani kama mbuzi anavyokula akameza na kisha kucheua kisha hutafuna tena kile alichokicheua. Kuna aina ya tawi, si pana sana kiasi cha urefu wa vidole viwili, ngumu kiasi, watu hutumia aina hii ya tawi au jani na kutia mdomoni na hutumiwa na viambatanishio vingine kuila, tawi hili hutiwa lote mdomoni na kutafunwa. Wanapokuwa wengi na kula kwa pamoja, utaona mabaki ya majani hayo yamerundikana mbele yao. Wanapotema mate, mate yao huwa ya rangi ya kijani. Kisha nikawauliza kuhusu hicho wanachokula: ‘Ni faida gani mnayopata kwa kula majani hayoWakajibu, ‘Hakuna chochote, ni jambo tulilolizoea lenye kutugharimu ambalo tumekulia nalo’.
  Wale wanaokula majani haya inawabidi watumie sana mafuta na asali, kwani wasipofanya hivyo wanaweza kuugua. Hayo majani hujulikana kama Kad (Mirungi).”
   
 4. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #4
  Jun 16, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Wasifu Na Kilimo Chake

  Mirungi ni mti unaoota polepole ambao unakuwa kwa urefu wa mita 1.5 hadi mita 20, kutegemea na eneo kijiografia na pia hali ya mvua ya eneo. Likiwa na majani ya kijani yaliyokoza ambayo yana urefu wa sentimeta 5 hadi 10 na upana wa sentimeta 1 hadi 4.

  Ina ladha ya uchachu mkali na utamu wa mbali kwa wakati mmoja.

  Hufungwa katika majani ya migomba ili kuhifadhi ubichi wake.
  Kawaida huvunwa asubuhi sana na kuuzwa mchana wake au usiku wake, kila inavyokaa sana hupunguza ubora wake kwa walaji na thamani yake. Na kwa sababu walaji wa Tanzania hutegemea zaidi Mirungi kutoka Kenya, huwa hawapati ule ubora unaotakikana kutokana na umbali na kutofika kwa haraka; ingawa walaji wa Arusha hupata haraka zaidi kwa ukaribu wake na Nairobi kuliko wale wa Dar na Zanzibar au miji ya bara ya mbali kama Mwanza na kwengineko.

  Kwa hivyo, majani ya Mirungi yanapoanza kukauka, kemikali ile kali ya aina ya cathinone inakauka pia na inabakia ile ambayo sio kali: cathine, na ndio maana mirungi inaposafirishwa inawekwa katika mifuko maalum ya plastiki au kufunikwa na majani ya migomba ya ndizi ili ihifadhike vizuri.

  Mirungi ni zao lenye kuwaingizia wakulima Yemen kipato kikubwa na ndio maana wengi wameanza kuacha kilimo cha kahawa, na hutumika asilimia 40 ya matumizi ya maji ya nchi nzima kwa kilimo chake, pamoja na uzalishaji wake kuongezeka kiasi cha asilimia 10 hadi 15 kila mwaka.

  Matumizi ya maji yamekuwa makubwa kiasi cha hifadhi ya maji ya San’aa mji mkuu wa Yemen kupungua na ikiendelea namna hii basi baada ya miaka kumi tu maji yatakauka na kwa hali hiyo imefikia serikali kugawa maeneo kwa kuwahamisha wakazi wa San’aa kwenda kuishi maeneo ya pwani ya Bahari nyekundu.

  Matumizi ya Mirungi aghlabu hutumika katika maeneo yanayolimwa zaidi na maeneo ya jirani na yale ambayo hufika Mirungi haraka ingali bado mpya mbichi na safi kwa sababu ya mzimuo wake. Kila inavyokaa mzimuo wake na upandishaji wa ‘handasi’/ ‘nakhwa’ yake hupungua.
   
 5. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #5
  Jun 16, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza ya kwamba zaidi ya masaa 14.6 milioni yanapotezwa kila siku katika ulaji wa Mirungi huko Yemen. Ripoti hiyo, iliotolewa katika tovuti ya WHO, inaonyesha ya kwamba asilimia 80 ya watu wazima (male adults) wanatafuna Mirungi kila siku kwa muda wa masaa matatu mpaka manne hadi matano wakati ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wamo pia katika tabia hii yenye hatari.

  Mirungi ni kileo kinachotumika sana kama ‘mkusanyiko wa kijamii’ katika maeneo mengi, na huwajumuisha zaidi wanaume ingawa baadhi ya sehemu na kwa miaka ya karibuni wanawake wamevamia sana uraibu huo haswa maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki kama Mombasa, Tanga na Dar-es-Salaam na mji kama Arusha ambao pia umekumbwa na ugonjwa huo kwa vijana wengi wa mjini.

  Na hupendelewa na madereva wa magari makubwa wanaosafiri safari ndefu, madereva wa abiria na hata wa magari ya kukodishwa kwa kuamini kuwa inawafanya wawe macho na makini. Vilevile hutumiwa na wanafunzi wakiamini kuwa inawafanya wasome muda mrefu na kukesha, kadhalika walinzi wa usiku huona inawasaidia kuwa macho usiku. Na baadhi ya watu hutumia kwa kisingizio cha kukesha kwa ajili ya kufanya ‘Ibaadah za usiku.
   
 6. Junius

  Junius JF-Expert Member

  #6
  Jun 17, 2009
  Joined: Mar 11, 2009
  Messages: 3,183
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 133
  Mkuu X-Paster,
  Inaelekea nchi kama za ulaya wanaichukulia kama sigireti uzito wake, hata hivyo, mbali na WHO kuguswa na athari za mirungi vp taasisi nyengine mfano za kiimani kuna matamko rasmi (fatwa) yaliyotoa msimamo wa kukubali au kukataa matumizi ya mirungi?
   
 7. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #7
  Jun 17, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Tutaona mkuu, ila kwa ufupi Mirungi haifai.
   
 8. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #8
  Jun 17, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Nchi kama Tanzania, imepigwa marufuku lakini serikali kwa kutofuatilia kwa karibu kumefanya kuwe kunaliwa hadharani na bila woga wowote. Hufuatwa sheria pale maaskari wanapotaka kupata chochote kutoka kwa walaji na ni nadra kusikia mla Mirungi katiwa ndani, na akitiwa ndani basi hutolewa mara moja bila kufikishwa mahakamani.

  Huko Somalia, waliposhika madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na kuleta amani ambayo haikuwahi kuonekana Somalia, Baraza La Juu La Mahkama Ya Kiislam, walipiga marufuku kuliwa mwezi wa Ramadhaan na kusababisha maandamano na upinzani huko Kismayo. Na mwaka huo huo katika mwezi wa Novemba, Kenya ilipiga marufuku ndege kwenda Somalia wakitaja ni sababu za kiusalama, hali ambayo ilisababisha upinzani kutoka kwa walimaji Mirungi. Mbunge wa Ntonyiri, Meru ambayo ndio eneo lenye kutegemewa sana Afrika Mashariki kwa ulimaji wa Mirungi, alieleza kuwa imetengwa ardhi maalum ya kulimia Mirungi, ambapo tani 20 zenye thamani ya Dola Laki 8 ($800, 000) husafirishwa kila siku kuelekea Somalia na hivyo kizuizi cha serikali kitailetea taifa madhara ya kiuchumi na kipato kama hicho kwa siku.
   
 9. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #9
  Jun 17, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Aina Zake
  Alenle (yenye majani mapana mengi, na ni ghali sana) – Yemen, Ethiopia na Kenya

  Kangeta – Kenya
  Giza (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ndogo) – Kenya

  Mbaga (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ya aina duni ambayo aghlabu ni ya bei ya chini -japo kuna baadhi ya mashamba machache sana hutoa aina yenye afadhali- na huliwa na wasiomudu kununua aina za ghali) – Tanzania

  Madhara Yake
  “Familia nyingi zinateketea, wake kukimbia waume zao, waume kutojali familia zao; hawataki kufanya kazi, jamii kujaa wavivu waombaji, wazazi na wakwe kulea wajukuu wasiongaliwa na wazazi wao, ulaghai na maasi kuzidi, ‘Ibaadah kupuuzwa, uchumi kuporomoka…”

  Naam, tukiyaunganisha maneno hayo na tunavyoona hali ya walaji, hakika yana ukweli mtupu usiopingika kwa wanaojua hali hiyo katika jamii.
  Tutajaribu kuyaorodhesha madhara mbalimbali yanayosababishwa na ulaji Mirungi.
   
 10. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #10
  Jun 17, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Madhara Ya Kidini Na Kimaadili
  1. Kupitwa na vipindi vya Swalah au kutokuswali kabisa;

  2. Swawm haikamiliki – katikati ya mchana wa Ramadhaan watu huhangaika kutafuta Mirungi na kucheza bao, keramu, dhumna, kutazama mipira na sinema. Jambo la kwanza baada ya futari, watu huanza kusaga Mirungi. Hakuna Swalah za usiku, hakuna ‘Ibaadah nyingine yoyote, hata Swalah ya Alfajiri huwapita walaji wengi kwa sababu Shaytwaan wa Mirungi huwaambiwa wakalale muda mchache tu kabla ya Swalah ya Alfajiri! Kuamka kwao ni mchana au Alasiri, Ramadhaan inakuwa haina uzito wowote kwa maisha ya mla Mirungi;

  3. Mchanganyiko baina ya wanaume na wanawake;

  4. Uongo – hii ni kawaida kwa wengi ili wafikie malengo ya kupata wakitakacho; ima kudanganya wengine kwa kuwakopa pesa za kununulia Mirungi na kisha hawarejeshi madeni hayo. Na pia wanapokopa husingizia matatizo makubwa waliyonayo wao au jamaa zao kama maradhi, matibabu, ada za shule, n.k. ili waweze kukubaliwa kupata mikopo hiyo. Aghlabu wanapokopa hawasemi ukweli kuwa wanataka pesa za kununulia Mirungi; maana hakuna atakayewakopesha;

  5. Usengenyaji – vikao vingi vya walaji huwa ni mazungumzo ya kidunia, mipira, filamu, kujadili mambo ya siasa, jamii, na kujadili maisha ya watu, maingiliano ya kindoa, na wao kwa wao kutoa siri zao za ndani na kutaja maovu yao waliyowahi kuyafanya;

  6. Uropokaji, uchache wa adabu, ujuaji wa kila kitu, mlaji akiongelea siasa basi hakuna mwanasiasa kama yeye, akija kwenye mpira wa miguu na hususan ligi ya Uingereza, basi hakuna anayeichambua ligi hiyo kama yeye… na mtihani mkubwa na msiba ni kuwa hata mas-ala ya Diyn wao pia ni wataalam wakioongelea Taariykh na kwanini fulani aliuliwa na wangapi waliritadi baada ya Mtume na kwanini fulani walikuwa hawastahiki Ukhalifa walimdhulumu fulani n.k.!

  7. Upungufu wa hayaa;

  8. Kupoteza muda mkubwa katika vikao hivyo;

  9. Kuomba omba – wengi huwa hawana uwezo wa kununua Mirungi kukidhi mahitaji ya uraibu wao, na hivyo kuwapelekea kuwa waombaji kwa wengine ima wa pesa za kununulia au uombaji wa Mirungi kwa walaji wenzao;

  10. Maasi – baadhi ya vikao vya Mirungi hutawaliwa na kutazamwa sinema za uchi ili kusukumia handasi zao. Hali hiyo ya uchafu wa maadili na kujitumbukiza katika uharamu, huwakutanisha wazee kwa vijana na matokeo kupoteza heshima baina yao, na pia nyumba hizo kupoteza hadhi katika jamii na nyakati nyinginezo kuwatukanisha wake za wenye nyumba hizo kwa machafu yanayoendelea hapo. Baadhi ya nyumba waume wamepoteza wake zao kwa marafiki zao kutokana na maingiliano huru yasiyo na mipaka baina ya wake kwa waume;

  11. Kuharibiwa itikadi zao – mji kama Arusha, vijana wengi wamebadili itikadi zao za Diyn baada ya kujiunga na uraibu huo na kushiriki vikao vyake. Ndani ya vikao hivyo kuna kundi la wakongwe ambao wameweza kuwashawishi vijana kutoka katika itikadi waliyozaliwa nayo na kujiunga na itikadi ya kukufurisha na kulaani watu wema waliopita.

  Imefikia hali ya kusikitisha sana kwa kuona kundi kubwa la watu likiwa limekaa barazani likicheza Dhumna (Domino) na huku Swalah ya Jama’ah ikiadhiniwa, kuqimiwa, na kuswaliwa ubavuni mwao kwenye Msikiti na wala hawana wasiwasi tena wakifanya zogo na kelele na kuzipigisha kete zao kwa nguvu kana kwamba wanashindana na sauti ya Mnadi Swalah. Maskini na wao wanajiona wako sawa kabisa kwenye haki! Na wanapo tanabahishwa waache lahwu zao na waende kuswali, husema kuwa wao wanajumuisha Swalah kutokana na Itikadi yao. Ukweli wengi hata kuswali hawaswali;

  12. Haki za kifamilia kukiukwa – haki za kinyumba; waume wanakuwa hawatoa haki zao ima kwa kukesha nje ya nyumba zao, au kwa kudhoofika nguvu zao za kiume na pia kumaliza haraka wanapofanya tendo la ndoa na hivyo kusababisha wake kukosa haki za msingi;

  13. Talaka kuzidi – kwa sababu tulizotaja katika kipengele kilichotangulia, wake wengi hushindwa kuvumilia katika ndoa zao na kuamua kudai talaka;

  14. Haki za watoto hazitekelezeki – kwa kuwa walaji wengi hawafanyi kazi, na wanaofanya kazi hutumia gharama nyingi kwenye ulaji, hivyo hakupatikani matumizi nyumbani au matumizi kubanwa na haki kutotimizwa. Walaji wengine hulelewa watoto wao na wakwe zao au wazazi wao;

  15. Kutoka nje ya ndoa – baadhi ya walaji wanakuwa si waaminifu kwenye ndoa zao, kadhalika baadhi ya wake wanashindwa kuvumilia kuwa wapweke kila mara kwa kuwa waume zao hukesha nje ya nyumba zao, na wakirudi ni usingizi, wakiamka ni kutafuta Mirungi, na hivyo hupelekea wake hao kukosa uvumilivu na kwa kuzidiwa kwao na matamanio yao –na kwa uchache wa Iymaan- kunawapelekea wao kuyahamisha matamanio yao pengine.

  16. Walaji wa uraibu huu hukesha kuorodhesha mambo watakayoyafanya siku ifuatayo, pasi na kuyatekeleza, na kuendelea katika hali hiyo kila mara bila ya mafanikio yoyote.

  17. Wengine husingizia eti wanakesha kwa ajili ya ‘Ibaadah, lakini ni aina gani ya ‘Ibaadah inayofanyika wakati mashavu yametuna kwa kujaa majani hayo?
   
 11. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #11
  Jun 17, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Madhara Ya Kiafya
  Matatizo na madhara ya Mirungi yaligunduliwa mwanzo katika mwaka 1935 na League Of Nations, Mwaka 1970 taasisi ya tiba ikaitenga madhara ya cathinone yanayopatikana katika Mirungi ambayo kikemikali inafanana na amphetamine, na hivyo katika mwaka 1971 ikaorodheshwa na United Nation kuwa ni miongoni mwa madawa ya kulevya.

  Bwana mmoja kutoka Canada ajulikanaye kama Mathew Bryden aliyekuwa akifanya kazi na mashirika ya msaada kwa miaka mitatu huko Somalia anasema, “Watumiaji wengi wa Mirungi wamejikuta wakipambana na msisimko wake ili waweze kupata usingizi au hata kufanya kazi kisawasawa". Wanaelekea kwenye pombe au madawa ili kupata mapumziko au kupunguza hali ya wasiwasi.

  “Hali ilivyo Mogadishu ni watu kutawaliwa na nguvu za Mirungi, madawa au pombe,” Bwana Bryden anaendelea, “Unakuwa umevurugikiwa kabisa. Ima uharibikiwe kikamilifu au upoteze mwelekeo wa hali halisi

  Utumiaji wa Mirungi husababisha madhara mbalimbali kiafya kama:

  1. Magonjwa ya vidonda vya tumbo (ulcers);

  2. Ukosefu wa haja kubwa (constipation) ;

  3. Utumiaji wa muda mrefu husababisha kuharibu utendaji kazi wa ini, na pia kusababisha ubadilikaji rangi meno, kudhoofika, na fizi kuuma na harufu ya mdomo;

  4. Upungufu wa msukumo wa kufanya jimaa (sex drive). Na pia kuwahi kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu;

  5. Kupatwa na ugonjwa wa futuru/future/ bawasiri/ baasili – nyama inayoota kwenye utupu wa nyuma;

  6. Upungufu wa usingizi;

  7. Humpelekea mlaji kutawaliwa nayo (Addiction);

  8. Walaji wengi huvuta na sigara, hata yule aliyekuwa havuti kabla ya kuanza kula Mirungi, hujikuta akizama kwenye uvutaji, na madhara huwa maradufu;

  9. Madhara ambayo bado kinamama walaji Mirungi hawajayagundua ni kwamba mtoto anayezaliwa na mama mlaji Mirungi mara nyingi hukataa kunyonya titi la mama yake kwa sababu ladha ya maziwa inabadilika kwa ajili ya utumiaji wa madawa (pesticides) unaotumiwa na wakulima wa Mirungi kama inavyoeleza utafiti uliofanyika na Chuo Kikuu Cha Aden (Aden University). Utafiti huo unazidi kueleza ya kwamba aina ya madawa yanayotumiwa na wakulima ni zaidi ya 118 (na nyingi katika hizo ni katika zile zilizokatazwa kisheria [illegal pesticides]) na ambazo zinasababisha asilimia 70 ya ugonjwa wa saratani (cancer) huko Yemen.

  10. Utafiti mwengine kule Ethiopia unatueleza ya kuwa mtoto wa mama mwenye kula Mirungi kwa wingi huwa hana uzito wa kawaida wakati wa kuzaliwa.

  11. Ukosefu wa hamu ya kula chakula na mengi mengine.

  12. Madhara Ya Kiuchumi Na Kijamii

  13. Kuwa na taifa la wavivu wapenda starehe wasiotumika;

  14. Jamii ya Kiislamu iliyo chafu kimaadili na isiyosimamisha ‘Ibaadah;

  15. Harakati za kunyanyua uchumi kuwa duni, harakati na juhudi zinazopatikana huwa ni za kuwazika na kutajika tu. Anapokuwa mtu ameshakhazin fundo lake la Mrungi kwenye shavu lake linalovimba kama pulizo kwa kujaa ‘taksima’, hapo atakuwa anatoa mipango na mikakati mizito mizito ya kujenga maghorofa, kuanzisha miradi ya mamilioni…lakini yote ni mipango inayopangwa na ‘Handas’ na ‘Nakhwa’, baada ya kutemwa gomba, mipango yote iliyokuwa ikipangwa huyeyuka na kuwa kama ngano za Alinacha….hapo tena husubiriwa siku ya pili ya kusagwa na mipango yake mingine ya mamilioni ya kuwazika;

  16. Kulala mchana kutwa – kukosekana harakati na michakato ya utafutaji rizki.

  17. Kuzidi kwa omba omba – bila shaka ikiwa watu hulala mchana mzima na hawahangaiki kufanya kazi, kinachotarajiwa ni kuzidi kwa wanyanyua mikono na wainamisha vichwa wanaoongea kwa huzuni kama waliofiwa wakati wanatupa makombora yao ya maombi;

  18. Vijana wa mjini hawataki kuajiriwa – kwa sababu wanajiona ni ma-alwatwan, kwa hiyo –kwa mtazamo wao- haiwezekani kwao kutumwa au kuajiriwa! Matokeo yake uchumi wa wakazi wa mjini kuporomoka na mwisho wake ni wao kukodisha nyumba zao kwa wageni (wanaotoka miji ya mbali) zikawa maduka, na mwisho wake hufikia kuuza hizo nyumba zao ambazo wamerithi kutoka kwa wazee wao waliokuwa wakihangaika na kuchapa kazi;

  19. Huwapelekea baadhi yao kujidunisha na kuwatumikia mabwana wakubwa si kwa lingine ila kwa ajili ya kilo ya Mirungi.
   
 12. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #12
  Jun 19, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Djibouti:
  Tani kumi za Mirungi hupelekwa kila siku kwa ndege kutoka Ethiopia kuelekea Djibouti. Katika uwanja wa ndege, hakuna mgeni anayengojewa kwa hamu kama mgeni huyo (Mirungi).

  Zaidi ya magari 300 yanakuwa tayari kwenye kiwanja cha ndege kumpokea “mgeni” huyo wa thamani. Wafanya biashara wa Mirungi wanaitwa ‘Masultani wa Qaat.’

  Ilitokea siku moja watu walishikwa na kiwewe kiwanja cha ndege walipopata habari ya kwamba huenda Mirungi isiwasili siku hiyo kwa sababu fulani fulani. Ilitokea fujo katika nchi na ilikuwa ni siku ya huzuni na watu waligoma kuondoka kiwanja cha ndege.

  Punde si punde, ndege iliwasili na watu walipopata habari hiyo, basi walikumbatiana kwa furaha na kupeana mikono kama vile ni Siku Kuu.

  Djibouti imekataa kupiga marufuku mirungi kwa sababu inaingiza serikalini kila mwaka faida ya zaidi ya dollar 15,000,000 - Kwa hivyo, umefanya mkataba wa Kiserikali baina ya Djibouti na Ethiopia kuhusu kutochelewesha Mirungi hata siku moja.
   
Loading...