Happy Birthday

Verifier

JF-Expert Member
Aug 14, 2019
457
1,503
Hongera ndugu yangu kwa kumbukizi ya siku yako ya kuzaliwa! Mungu afanikishe ndoto zako na zaidi akujalie afya nzuri na maisha marefu yenye furaha na mafanikio! Furahia siku yako!

Naikumbuka vema hadithi ya maisha yako ndugu yangu kwa hakika umepitia mengi. Historia ya maisha yako ilianzia mwaka 1977 wakati pendo zito la marehemu baba yako na mama yako lilipozaa matunda na kukuleta wewe duniani mwaka huo wa 1977. Bahati mbaya marehemu baba yako hakuwa bado amekamilisha taratibu za ndoa kabla ya kukupata wewe japo alikuwa akiishi na mama yako kama mke wake. Jambo hili halikuwa limewafurahisha wazazi na ndugu za mama yako.

Mwaka 1978, Tanzania iliingia vitani na Uganda, hivyo kwa vile marehemu baba yako alikuwa ni askari wa Jeshi la Wananchi ilimbidi aende mstari wa mbele kulitetea taifa lake. Bahati mbaya, mauti yalimkuta akiwa katika kazi ya kulipigania taifa lake. Hukumjua baba yako zaidi ya kumuona katika picha! Ndipo masaibu yako yalipoanza.

Baada ya kifo cha baba yako, mama yako alikosa pa kwenda kwani kwao walimkataa. Hakuwa na jinsi aliamua kukutelekeza kwa bibi yako ukiwa na miezi tisa. Bibi yako alichukua jukumu la kukulea na kukunyonyesha maziwa wake. Bibi na babu walikulea japo mahitaji ya muhimu ilikuwa ni vigumu kuyapata. Wajomba zako japo walikuwa na uwezo hawakukusaidia!

Ulisoma shule kwa kuungaunga, leo unaenda kesho huendi kutokana na ufukara uliopitilza. Chakula kilikuwa shida kwako, kushina na kulala njaa ilikuwa ni kawaida kwako. Uliona bora utoroke nyumbani uende kuishi mtaani ili upate ahueni. Mvua, jua lilikuwa lako huko mtaani. Mateso yalikithiri. Wenzako mtaani walikupiga na kukunyanyasa lakini ulivumilia. Uliathirika kisaikolojia, kimwili na kihisia.

Mungu si athumani, alitokea Mzee mmoja aliyuguswa na masaibu yako na akaamua kukusaidia kwa kukupeleka kwa wataalamu wa saikolojia. Aliongea na Bibi na Babu yako wakakubali kukupokea tena baada ya kukaa miaka miwili mtaani! Mzee huyu alichukua jukumu la kukupeleka kujifunza ufundi wa magari katika gereji ya rafiki yake. Kutokana na bidii yako uliweza kujua ufundi na udereva kwa haraka sana. Kutokana na heshima, bidii, uaminifu na uchapa kazi wako, mweye gereji alikupenda akaamua kukupeleka Nairobi kusomea lugha ya Kiingereza kisha akakuajiri kuwa dereva katika kampuni yake ya utalii.

Leo hii ndugu yangu umefungua kampuni yako ya utalii, una magari yako ya utalii na umeajiri watu. Umewajengea bibi na babu yako nyumba. Yule mzee aliyekutoa mtaani amekuwa ndiye baba yako. Wale ndugu zako waliokuktaa zamani wanaomba msaada kwako na wewe bila hiyana unawasaidia. Watoto wako watatu wanasoma katika shule nzuri kwani hutaki wapitie uliyopitia wewe! Mke wako anasimamia mashamba na mifugo ambao mnayo.

Hongera ndugu yangu, furahia kumbukizi ya siku yako ya kuzaliwa leo. Nimepokea kwa mikono miwili mwaliko wako wa kukusindikiza kwenda kutoa zawadi katika kituo cha watoto wa mitaani siku ya leo, nitakuja.

Nimeamua kuandika hii historia ya kweli ya rafiki yangu iwe fundisho kwetu sote.

Have a fruitful and blessed day!
 
Very touching story...Happy birthday to him 🎂🍾🍷
Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu na huo moyo wake mzuri aendelee kusaidia wengi zaidi.
 
Back
Top Bottom