Happy birthday Yericko Nyerere

Happy birthday Yericko Nyerere

Joined
Oct 5, 2015
Posts
90
Reaction score
483
HAPPY BIRTHDAY KAMARADE YERICKO JOHANNES NYERERE.

Na. Christopher Cyrilo

Siku moja, wakuu wa mashirika ya intelijensia wa CIA ya Marekani, MSS ya China na KGB ya Urusi walikutana kujadili mambo yao. Ghafla kukazuka ubishi juu ya nani ni zaidi ya mwingine kati yao. Ubishi ulikuwa mkubwa sana kiasi cha kushindwa kufikia muafaka, ndipo umoja wa mataifa ukaingilia kati ili kumaliza ubishi.
Ikaamuliwa kuwe na shindano maalum la kutafuta bingwa wa kukusanya taarifa kati ya CIA, MSS na KGB.

Kamati maalum ya umoja wa mataifa ikaandaa shindano; kila taasisi ilitakiwa kumtafufa panya mmoja aiyefichwa katika misitu mikubwa ya Amazon, huko nchini Brazil.

Basi wakaanza CIA, wakaweka makamera karibu kila kona ya msitu, wakawashawishi wanyama wengine, pamoja na panya wengine wawasaidie kutoa taarifa za panya huyo kwa dau nono, wanyama hao waliwekwa maeneo tofauti ambayo panya angeweza kutembelea. Baada ya mwaka mmoja wa sughuli hiyo, panya hakupatikana - CIA wakahitimisha kwamba; Panya huyo hayupo ndani ya misitu ya Amazon"

Shughuli ikahamia kwa MSS ya Uchina. Tofauti na CIA, vijana wa MSS waliamua kuishawishi serikali ya Uchina iwaalike panya wote waishio katika misitu ya Amazon kwenda kutembelea China. Huko mjini Beijing, panya walikaribishwa kwa heshima kubwa, wakafanywa kuwa ndugu, kisha mmoja mmoja wakaitwa 'chemba' na kuhojiwa, huku wakiombwa taarifa zinazoweza kusaidia kumpata panya wa Umoja wa mataifa, bila mafanikio. Panya wakarudi Amazon wakiwa tayari ndugu wa wachina na kila taarifa walizopata walizifikisha kwa wachina, wakati mwingine bila kuombwa.
Baada ya mwaka mmoja, panya hakupatikana. MSS walighafirika sana, wakaamua kuchoma moto msitu wote wa Amazon, halafu wakatangaza kwamba msitu umeungua na chanzo cha moto bado hakijafahamika, na shughuli za kumtafuta panya huyo zikasitishwa.

Zamu ya KGB. Baada ya msako mkali uliofanywa na maafisa wa KGB, ukigusa kila pembe ya msitu- bado panya hakupatikana. Baadaye, KGB walikamata nguruwe na kuanza kumpa kipigo cha mbwa mwizi ili atoe siri juu ya alipo panya huyo, nguruwe wa watu hakuwa anajua chochote, lakini alipokea kipigo kikali karibu kufa. Mwishowe, Nguruwe akaanza kulia;- "Mimi ndio panyaa mnayemtafutaa..mimi ndio panyaaa..hata baba yangu na mama yangu walikuwa panyaa...mnisamehee.."

Basi maofisa wa KGB wakatoka msituni na Nguruwe, wakatangaza kuwa Panya wa umoja wa mataifa amepatikana..na yeye mwenyewe amekiri hadharani.

Funzo.
Hadithi hii fupi inaweza kuchekesha lakini inatoa funzo kubwa kwenye kazi za vyombo vya ulinzi na usalama, hususani eneo la ukusanyaji taarifa. Watu wengi sana wameteswa bila hatia kwa sababu ya kuhisiwa tu kuwa wahalifu hali kwamba wahalifu wakibaki salama.

Katika hadithi hii, Taswira ya KGB imekuwa hasi kutokana na vitendo vyao vya kutesa watu wasio na hatia, hata kuwabambikiza kesi ili tu ionekane wamefanikisha kazi yao. Bahati nzuri kwa Urusi, KGB ilifutwa na kuanzishwa FSB ambayo iliboreshwa na kuanza kufanya kazi kwa weledi. Bahati mbaya, utamaduni wa KGB ulirithiwa na mataifa machanga yaliyo amua kufuata itikadi za kijamaa na kikomunisti, Tanzania ikiwemo. Vyombo vya ulinzi na usaama katika mataifa haya machanga bado vinaendeleza utamaduni wa kale wa KGB, kufanya maamuzi ya kuumiza wengine bila taarifa sahihi. Watu wengi wameumizwa; Mathalani, wiki mbili zilizopita wanausalama wa Tanzania walivuka mpaka wa Namanga na kuingia nchini Kenya, wakamteka mfanyabiashara aliyeitwa Mohammed Bashir na kumsafirisha hadi Arusha, kisha kutoka Arusha mjini hadi 'eneo maalum', kilometa 20 zaidi. Wakati wa safari hiyo mfanya biashara Mohammed Bashir alikuwa akipokea kipigo cha mbwa mwizi. Wanausalama saba wa Tanzanian walimpiga kwa kutumia kitako cha bunduki, ngumi na makofi, wakiamini mtu waliye naye anaitwa Jamal, ambaye anasadikiwa kuwa gaidi na muhusika wa biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Bashir mwenyewe anadai aliteswa kwa muda wa masaa 12. Baadaye iligundulika kuwa, Bashir aliyekamatwa si gaidi wala sio msafirishaji haramu wa binadamu. Wanausalama wa Tanzania walimtesa Bashir huku wakimlazimisha akubali kuwa yeye ndiye Jamal, na kila alipokataa, mateso yaliongezeka.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Bashir aliachiwa baada ya wanausalama kugundua walimteka mtu asiye mlengwa.

Tasnia ya intelijensia, katika eneo la ulinzi na usalama inataka weledi mkubwa ili kuepuka kuumiza watu wasio na hatia. Sanaa ya kukusanya taarifa, kuzipembua na kupata ukweli au karibu na ukweli, ni sanaa ngumu inayohitaji maarifa na uadilifu pia. Ubabe na kutojali hisia za wengine huharibu zaidi. Kwa mfano, Bashir hakuwa muhalifu, lakini kwa mateso aliyopewa, hawezi kutoa taarifa za uhalifu kwa watu waliomtesa, na pengine akipata fursa ya kulipiza kisasi, au kusaidia maadui wa watu waliomtesa anaweza kufanya hivyo. Vitendo vya kutesa watu wasio na hatia kwa kifupi vinachochea uasi kwa jamii dhidi ya vyombo vya usalama, na kuibua uhalifu zaidi. Si ajabu katika jamii ambayo vyombo vya usalama vimejipa ukuu juu ya haki za binadamu, hutokea wanajamii wakawasaidia wahalifu dhidi ya vyombo vya usalama.
Dunia imebadilika, kukamata mtu asiye mlengwa pengine ni kitu kinachotokea duniani kote, lakini kumtesa mtu bila uhakika, ni jambo la aibu, ni ishara ya kukosa ukomavu katika kupambana na uhalifu, ni ishara ya uchanga wa tasnia ya intelijensia, ni utamaduni wa kale, ni mbinu za kishamba na kizamani.

Mateso hupatiwa 'magaidi' haswa, ambao wamethibitika, si watuhumiwa wa ugaidi. Magaidi huteswa ili kufichua siri zinazohitajika ambazo zitasaidia kuokoa maisha ya wengi. Magaidi hao mara nyingi wamekwisha kuharibu au kupoteza maisha ya wengi, kwa hivyo mateso ni kitu wanachostahili. Lakini kumtesa mtu kwa tuhuma, au kwa kudhani, ni ujinga mkubwa. Tumeiga mambo haya, na tuliowaiga wamekwisha achana nayo.

Nimtakie heri ya siku ya kuzaliwa, Kamarade Yericko Nyerere, andiko hili liwe ujumbe kwa rafiki zake wale. Nitaitumia siku ya leo kurejea maeneo fulani ndani ya kitabu cha Ujasusi wa kidola na kiuchumi.
Happy birthday bro! Yericko Nyerere
 

Attachments

  • IMG-20190404-WA0000.jpg
    IMG-20190404-WA0000.jpg
    15 KB · Views: 38
Back
Top Bottom