Tatizo la wanachama wa Simba ni kukata wajihi (uso) ili kuunga pua, badala ya kukata pua ili waunge wajihi. Matokeo yake ni kukosa vyote, pua na wajihi. Friends of Simba wana nafasi yao ndani ya Simba, kubwa kuliko zote ikiwa ni 'fitna za soka.' Fitna zenyewe haziishii kwenye kusaka ushindi tu, bali hata kwenye kuamua nani acheze mechi ipi, kocha awe nani, nani awe kiongozi, mwamuzi gani achezeshe mechi ipi, n.k. Kuwateua kuwa viongozi maana yake ni kuifanya timu kuongozwa na 'fitna' hizo badala ya kusimamia timu, usajili, n.k. Kwa hivyo kazi waliyokuwa wakiifanya walipokuwa FOS ya kuuchagiza uongozi unapoonekana kuboronga inakosa wa kuifanya. Huko kwenye uongozi wanaendekeza uleule u-FOS: kumsajili kocha huku wakijua hawamwamini ili kuja kumfukuza ndani ya mwezi mmoja, kuwalaumu wachezaji waliomlalamikia kocha huyo kwamba eti wamezoea kudekezwa lakini walipoambiwa wao ukweli siku moja tu na kocha huyohuyo wakamtimua kwa hoja ya kutoendana na utamaduni wa Simba, kumfanyisha kazi kocha na wachezaji bila ya vibali na bila ya kujali mpaka ilipokaribia mechi na mtani wao - tena kwa kuzinduliwa na wadau wao walioko Uhamiaji, kukubali kudanganywa na wao wakajidanganya kwamba Kwizera ni mchezaji bora wa Ligi ya Ivory Coast bila ya kujiuliza kuwa kama ni hivyo kwa nini asiwaniwe na timu za Ulaya (angalau ya Mashariki), kushindwa kujiuliza kwamba kama Kiongera alikuwa ni mzuri kama alivyovumishwa kwa nini asingekuwa na mkataba wa muda mrefu na timu yoyote huko kwao Kenya,kumsajili Okwi na kumwacha Musoti bila ya ridhaa ya mwalimu, kuipeleka timu SA kwa wiki moja ya maandalizi huku ikipoteza siku 3 kati ya hizo kwa safari yenyewe huku wachezaji wengine wakishindwa kabisa kujiunga nayo lakini bado wakachezeshwa kwenye mechi iliyokusudiwa, kuwafukuza uanachama watu kwa sababu tu wana mawazo tofauti na wao huku wakisingizia Katiba (kana kwamba Katiba hiyo haina kifungu cha kusamehe au kuonya), kumtuhumu mchezaji kwa kuendekaza dhana za kishirikina, n.k.
Simba ni timu kubwa. Inahitaji kuchukua hatua kubwa na ngumu ili kuondokana na udogo inayoendelea nao. Nina wasiwasi majukumu ya kuiongoza Simba yamewazidi kimo FOS. Sisemi Katiba ibadilishwe ili Dalali agombee, la hasha!