Hali ya kisiasa nchini ni tulivu - JPF

EMT

Platinum Member
Jan 13, 2010
14,483
15,308
Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na Tafiti za Kukuza Utawala Bora Afrika (JPF), imesema hali ya kisiasa nchini ni tulivu na yenye amani tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Wabunge na Rais, Oktoba mwaka jana, kinyume madai ya baadhi ya viongozi wa serikali na chama tawala kwamba kuna baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikiandaa maandamano yenye lengo la kuvuruga amani nchini.

Aidha, taarifa ya taasisi hiyo imebainisha kuwa suala la kuandikwa upya kwa katiba ya nchi ni jambo lisilokwepeka kwa sasa, na kuwataka wananchi wote kupinga haki yao ya kutoa maoni ya katiba kupelekwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa.
Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Praygod Mmassy, alisema utafiti umeonyesha kuwa vyama vyote vimetekeleza wajibu wao kisheria tangu kipindi hicho.

Mmassy alisema hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kulegea kwa hali ya amani na utulivu kutokana na maandamano ambayo yamekuwa yakifanywa na vyama vya siasa kwani vimekuwa vikifanya hivyo kwa kutumia fursa yao kisheria. "Hakuna chama wala kiongozi yeyote wa chama cha siasa mwenye nia au malengo ya kuihujumu au kuiondoa madarakani serikali kwa kutumia vita au maandamano kama ilivyodaiwa na viongozi wakuu wa serikali na wale wa chama tawala," alisema Mmassy.

Aliongeza, kimsingi madai yote yaliyotolewa na serikali na viongozi wa chama tawala yameshindwa kuthibitika au kuthibitishwa na viongozi wa serikali, chama tawala, viongozi wa vyama vya upinzani, viongozi wa dini, viongozi wa idara na asasi za serikali na zile za kiraia.

"Madai ya Chama cha Mapinduzi (CCM), yamebaki kuwa porojo na hadithi za kutunga zilizokuwa na lengo la kuwatisha wananchi na kuhujumu chama cha Chadema kwa propaganda hizo ili wananchi wasikiunge mkono chama hicho na maandamano yao ya amani," alisema zaidi.

Kuhusu madai ya katiba, Mmassy alisema wananchi wote Tanzania Bara wana wajibu wa kushiriki katika kuandika katiba mpya ya Tanganyika au Tanzania bara, kwa vile Zanzibar wameshaandika yao. "Jambo la msingi ni sisi kuwa na katiba yetu huru itakayotupa nafasi ya kushiriki bila kikwazo, na baada ya hapo tunaweza kuwashirikisha wenzetu wa Zanzibar kuandika kwa katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Mmassy ameshauri wananchi wote kushirikishwa katika zoezi hilo, na kumtaka rais kufuata utaratibu mzuri katika mchakato huo ikiwa ni pamoja na kuitisha kongamano la kitaifa la wadau wote kuamua juu ya hoja hiyo. "Ni vyema rais akaitisha kongamano ili wananchi waamue kama ipo sababu ya kuandikwa katiba mpya, au ile ya zamani ifanyiwe marekebisho, au kama Tanzania Bara iwe na katiba yake au la," alisema.

Aidha, alisema ni wajibu wa serikali kupeleka bungeni mswada wa kutunga sheria ili kulitambua kongamano hilo la kitaifa na kulitangaza ndilo litakalokuwa na mamlaka ya kusimamia utaratibu wa kuandikwa kwa katiba.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom