Hadithi za Esopo

Hadithi za Esopo

IMG_20181002_140915_623.jpeg



KISA CHA KIJANA NA UPUPU_______ 14

Hapo zamani kulikuwa na Kijana mmoja mtukutu ambaye alipenda sana kuchezea mimea na wadudu. Siku moja akiwa kwenye kichaka jirani na nyumbani kwake, aligusa Upupu kwa mkono wake wa kuume, nao ukaanza kumwasha. Ukamletea karaha na maumivu makali.


Akaamua kukimbilia nyumbani kwake haraka huku akiendelea kujikuna na machozi yakimlengalenga. Alimfuata Mama yake bustanini na kumwambia kwa sauti ya kudeka akisema,

“Mama, Ingawa upupu unanichomachoma na kuniletea maumivu makali kiasi hiki, mie niliugusa taratibu na kwa unyenyekevu. Sijui ni kwa nini unaniumiza hivi”

“Kuugusa taratibu ndiyo haswa sababu iliyopelekea ukuchome, na kukuumiza.” Mama yake alimwambia. “Siku nyingine mwanangu, ukitaka kuugusa Upupu, ukamate na uufinye kwa nguvu, nao utakuwa laini na mororo kiganjani mwako, na wala hautokuchoma na kukuumiza hata kidogo.”
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg



KISA CHA POPO, NDEGE NA WANYAMA_________15

Hapo zamani za kale kulitokea mgogoro mkubwa sana kati ya Ndege na Wanyama, na vita kati yao ilinukia. Ilionekana kana kwamba juhudi zote za mapatano ziligonga mwamba. Wakati majeshi hayo mawili yakijikusanya kujiandaa kwa mapigano ya umwagaji damu, Popo alisita kuchagua upande wa kujiunga nao kivita.

Jeshi la Ndege lilipita karibu na kitulio chake na kumwambia; “Twende nasi vitani ee Popo ndege mwenzetu.”

Popo alikataa na kusema, “Mimi ni mnyama. Wala si ndege kama ninyi”

Baadaye jeshi la Wanyama nalo lilipita chini ya kitulio chake, walipomwona walimwita na kumwambia; “Twende nasi vitani ee Popo myama mwenzetu.” Popo alikataa tena na kujibu, “Mimi ni Ndege. Wala si mnyama kama ninyi.”

Basi kukawa na ngurumo za kutisha za wanyama shupavu kama vile simba duma na tembo; na ndege shupavu kama tai na furukombe. Anga lote lilijaa vitisho na harufu ya damu. Majike wenye ndama na majike wenye makinda walihisi kiyama chao kimefika.

Kwa bahati sana, katika dakika za mwisho mwisho kuelekea vita, muafaka ulifikiwa kati ya pande mbili hizo na vita vikaepukwa. Kukawa na amani badala ya mapigano. Kuona hivyo, Popo naye alitamani kuwa sehemu ya shamrashamra hizo. Alikwenda kwa Ndege akitaka kujiunga nao katika furaha na cherekochereko za kushangilia amani, wakamfukuza.

Akaamua kuondoka akaenda kwa wanyama huku akitabasamu na kutegemea kushiriki nao furaha ile ya amani. Nao walimfukuza kwa hasira hata akalazimika kukimbia wasije wakamdhuru kwa kumjeruhi au kumtoa roho kabisa.

“Ah,” Popo alijisemea kimoyomoyo, “sasa nimeng’amua,”
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg



KISA CHA KIJANA MWINDA SENENE___________16

Kijana mmoja mdogo alikuwa akidaka Senene kwenye majani yaliyomea kando ya shamba lao. Ilikuwa ni mapema wakati wa asubuhi, hata umande ungali haujavukizwa. Baada ya nusu saa tu alifanikiwa kuwadaka Senene wengi sana. Wakati akijiandaa kurudi nyumbani, alitupa macho huku na huko na kumwona Nge akiwa amejipachika katikati ya majani mawili. Basi yule Kijana kwa haraka yake hakuweza kutambua kuwa yule ni Nge na badala yake alimfananisha na Senene. Akanyoosha mkono wake ili amkamate, aongezee idadi ya kitoweo.


Nge naye akaunyoosha mwiba wake tayari kwa kung’ata na kumuasa yule Kijana, akasema;

“ee Kijana mwenye uchu na ulafi, laiti ungelithubutu hata kunigusa tu, ungejuta, kwani ungelinikosa mimi na pia hao Senene wote uliokwisha kuwapata!”
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg



KISA CHA SIMBA NA PAPA____________17

Siku moja Simba alikuwa akirandaranda ufukweni mwa bahari, akamwona Papa akichomoza kichwa chake juu ya uso wa bahari katikati ya mawimbi. Alizama na kuibuka tena… akazama na kuibuka tena… Simba alivutiwa naye na kumwona kuwa anafaa kuwa rafiki kwani ni mkubwa na mwenye nguvu kama yeye.


Alimwita karibu naye akasogea.

Baada ya kusalimiana Simba akamshauri mwenzake kuwa ipo haja ya kufanya makubaliano ya ushirikiano na urafiki baina yao, akimchagiza kuwa kati ya wanyama wote wa mwituni, wao Simba na Papa ndiyo wapaswao kuwa maswahiba haswa. Kwani mmoja wao ni mfalme wa wanyama wote wa nchi kavu ilhali mwingine ni mtawala wa viumbe wote wa baharini.


Papa alilipokea wazo hilo la Simba kwa mikono miwili. Wakakubaliana.

Punde akatokea Mbogo, na Simba, kwa kuwa alikuwa na njaa alimtamani na kuanza kupambana naye. Simba alipoona analemewa aliamwita rafikiye Papa aje nchi kavu kumsaidia.

Papa, ingawa alikuwa na nia ya dhati ya kumsaidia, hakuweza kufanya hivyo kwani hakuwa na namna yoyote ya kuweza kutoka majini.


Simba akamshutumu na kumdhihaki Papa kuwa ni muasi na asiye mwaminifu.

Papa akamjibu; “Hapana rafiki yangu, wala sistahili mzigo huo wa lawama toka kwako, yakupasa umlaumu muumba, ambaye, pamoja na kunipa ukuu na utawala majini, ameninyima kabisa uwezo wa kuishi juu ya nchi kavu.”
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg



KISA CHA MBWEHA NA MBU______________18

Siku moja, baada ya kutembea kwa muda mrefu, Mbweha aliukuta mto mdogo wenye kina kifupi cha maji. Maji yalikuwa masafi na maangavu kabisa na mandhari ya bonde lile kwa ujumla ilikuwa ya kuvutia kutokana na uoto na magugu yaliyonawiri vizuri pembezoni. Akayatamani maji kwa uzuri wake japo hakuwa na kiu kabla, akayanywa, kisha akatulia kidogo kwa tafakuri.


Hapohapo akapata wazo la kwenda ng’ambo ya mto kumtembelea rafiki yake ambaye hawakuwahi kuonana kwa takribani miezi kenda. Na kwa kuwa ilikuwa muda wa jioni aliona ni vyema zaidi kwani katika mila za kimbweha, kulala kwa rafiki huchukuliwa kama heshima kubwa na ishara ya urafiki wa kweli. Akajitoma majini na kuvuka.



Baada ya kufika ng’ambo ya mto Mbweha alijikuta akiunasisha mkia wake kwenye magugu kizembe, na kila alivyofanya jitihada za kujinasua ndo kwanza alijinasisha zaidi. Mwisho akawa hana uwezo wa kwenda wala kusogea.

Kundi la Mbu lilipita eneo lile na kuona tatizo lililomkabili, wakashauriana na kutua wote kwa pamoja kwenye mwili wake, wakamnyonya na kujipatia mlo wa damu pasipo bughudha ya mkia wake.


Nungunungu, akiwa hana hili wala lile, naye akapita mahali pale na kuona matatizo mawili yanayomkabili Mbweha. Alimhurumia sana, akamfuata na kumwambia: “Pole ee jirani yangu, naona upo kwenye mapitio mabaya, je nikusaidie kupunguza maswaibu yako kwa kuwafukuza hao Mbu wakunyonyao damu yako?”

Mbweha aliguna na kumjibu,


“Asante sana kwa kunijali na kwa nia yako ya kutaka kunitatulia tatizo moja kati ya mawili haya, rafiki Nungunungu,” alisema, “ila naona ni heri usiwafukuze hawa Mbu.”

“Kwa nini, wanakutesa na kukunyonya halafu hutaki niwaondoe!?”

“Sikiliza rafiki,” alijibu Mbweha, “Mbu hawa wameninyonya sana na kwa sasa wamekwishashiba, matumbo yao yamejaa damu yangu; endapo utawafukuza hawa, Mbu wengine wenye njaa kali watakuja kuchukua nafasi yao, waninyonye upya na pengine kuniua kabisa.”
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg



KISA CHA BABU KIZEE NA KIFO___________19

Babu kizee mmoja aliajiriwa kufanya kazi ya kukata magogo ya miti msituni. Siku moja akiwa anarejea nyumbani jioni alibebeshwa mzigo wa kuni aupeleke mjini ukauzwe. Mzigo ule ulikuwa mzito sana kwake.

Baada ya mwendo wa kitambo kirefu alichoka akawa hoi kabisa. Alisononeka kwa ufukara wake unaopelekea apate mateso ya kufanya kazi mzito mchana kutwa, na jioni kutwikwa mizigo mizito katika umri kama ule.

Mwishowe aliamua kuutupa chini mzigo ule, akaketi kando ya njia, akajiinamia na kuomba kwa dhati kabisa “Kifo” kimchukue aepuke suluba na mateso ya kubeba mzigo ule.

Kwa bahati nzuri ombi lake lilisikika na kutekelezwa bila ucheleweshaji; alipoinua uso wake baada ya kumaliza kuomba, alimwona “Kifo” amesimama mbele yake tayari kwa kazi, akiwa amekuja kuitika ule wito wake.

Kifo akauliza, “nimesikia wito wako ee mzee, je unataka nini hata ukaniita nikujie?”

Mzee akajibu haraka, “nilihitaji unipe msaada wa kuuinua mzigo huu wa kuni, unitwike mabegani kwangu niendelee na safari.
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg



KISA CHA AYALA NA MZABIBU_________20

Ayala, baada ya kukimbizwa na kuandamwa na wawindaji toka mbali, alichoka sana na kujua sasa mwisho wake umefika. Wawindaji walipomkaribia alifanya hila, akachupa kuume na kujibanza kwenye mvungu wa majani makubwa ya

Mzabibu. Wawindani nao kwa haraka waliyokuwa nayo (na hulka ya kuwahi ni kupata) hawakuweza kuing’amua hila yake, wakampita palepale bila kumwona.

Baada ya muda mfupi, kwa kudhani kuwa hatari haipo tena, Ayala aliinuka na kuanza kuyanyofoa nyofoa yale majani ya Mzabibu. Mwindaji mmoja aliyekuwa nyuma ya wenzake alisikia kwa mbali ule mchakato wa majani, akageuka kuangalia nyuma walikotoka, akamwona yule Ayala chini ya Mzabibu. Akachomoa mshale, akauweka kwenye upinde, akapiga na kumchoma Ayala tumboni.

Ayala, wakati akitapatapa karibia kukata roho, alikoroma na kusema; “Nimepata tijara nistahiliyo, kwani sikupaswa kabisa kuyatendea vile majani ya Mzabibu ambao punde uliokoa maisha yangu.”
 
Tutaendeleaaa hadithi ziko nyingi na nitazipost zote kulingana na muda nitakaopata__________!
 
Tunaendelea hivi punde wakuuu
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg



KISA CHA MAKSAI NA WACHINJA NG'OMBE_________21

Maksai, hapo zamani za kale, waliazimia kufanya hila ya kuwashambulia ghafla na kuwaangamiza Wachinja ng’ombe wote, kwa kuwa walikuwa wanaendesha biashara inayoteketeza jamii yao. Azimio hilo lilipitishwa kwa wingi mkubwa wa kura na maandalizi ya utekelezaji wake yakaanza mara moja.

Siku ya siku ilipofika walikusanyika ili waweze kutekeleza azma hiyo ya mauaji ya kushtukiza. Walinoa pembe zao vizuri kujiandaa kwa mapambano. Hamasa ilikuwa kubwa, na vijana walichagizwa kukaa mstari wa mbele.

Lakini miongoni mwao kulikuwako Maksai mmoja ambaye alikuwa mzee sana kwa umri (na wingi wa mashamba aliyokwishalima katika maisha yake) akawaasa kwa kuwaambia: “Ni kweli, Wachinja ng’ombe hawa wanatuchinja na kutuua, lakini tusisahau kuwa wanafanya hivyo kwa ujuzi na taaluma ya hali ya juu, na hivyo hutuepusha na maumivu yasiyo ya lazima. Endapo tutawashambulia na kuwaangamiza, tutaangukia mikononi mwa wafanyabiashara wasio na ujuzi wa kuchinja, na tutaanza kuuawa kwa nyundo na mashoka, kwa mateso na maumivu makali. Itakuwa ni kifo mara mbili zaidi: kwani hakika nawaambieni, ingawa tutawaangamiza Wachinja Ng’ombe wote, bado binadamu wataendelea kuhitaji nyama ya ng’ombe daima.”
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg


KISA CHA MJAKAZI NA NYOKA__________22

Hapo zamani za kale, kulikuwapo Nyoka mkubwa mwenye sumu kali, ambaye aliweka makazi yake kwenye shimo pembezoni mwa baraza ya nyumba ya Mjakazi mmoja. Siku moja usiku wa manane yule Nyoka alimng’ata mtoto mchanga wa Mjakazi, mwili wake ukabadilika rangi kuwa mweusi tii, akafa.

Kukawa msiba na simanzi isiyo kifani.

Wakati akiomboleza kifo cha mwanae kwa uchungu, mtu huyo aliapa kulipiza kisasi kwa kumuua Nyoka huyo pindi atakapopata wasaa.

Siku iliyofuata, majira ya jioni, Nyoka yule alitoka shimoni ili kwenda kujitafutia chakula. Ndipo Mjakazi alimwona akitambaa kwenye kiambaza kuelekea ndani, akachukua shoka na kumwendea kwa hasira ili ammalize. Na kwa kuwa

alinyanyua shoka na kutaka kumshambulia kwa papara, alikikosa kichwa na kiwiliwili na badala yake akamkata ncha ya mkia tu.

Nyoka akafanikiwa kujiokoa na kurudi ndani ya shimo.

Baada ya siku kadhaa kupita, Mjakazi yule akalemewa na hofu ya kuwa yeye pia yu hatarini kung’atwa na yule Nyoka. Akapata wazo la kuanzisha mchakato wa kumrubuni nyoka waafikiane kuishi kwa amani. Akamtengea mikate na chumvi kando ya shimo lake, na maji ya kunywa, ikiwa ni ishara ya kuomba urafiki.

Yule nyoka, huku akitoa mlio wa tahadhari na kitisho, alimwambia: “ndugu, kamwe hakuwezi kuwa na amani ya kweli kati yako nami; kwani kila nitakapokuona nitakumbuka nilivyopoteza mkia wangu, nawe kila unionapo utakumbuka kifo cha mwanao.”
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg


KISA CHA MWANAKONDOO NA MBWA MWITU_______23

Mbwa mwitu alimkimbiza Mwanakondoo, ambaye ili kujiokoa alikimbilia ndani ya hekalu moja la ibada. Mbwa mwitu hakuweza kuingia hekaluni, badala yake alisimama nje akapaza sauti kumwita akimwambia, “Ni heri uje kwangu, maana humo ulimokimbilia Padre akikukamata atakuchinja na kukufanya dhabihu.”

Mwanakondoo akamjibu, “Ni heri nitolewe kafara ndani ya hekalu la Mungu kuliko kuja kwako nikaliwa nawe.”
 
IMG_20181002_140915_623.jpeg

Mbweha na Beberu_________25

Siku moja Mbweha alitumbukia kisimani kwa bahati mbaya, na ingawa kisima chenyewe hakikuwa na kina kirefu sana, alijikuta akishindwa kutoka nje tena. Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu bila mafanikio, hatimaye akatokea Beberu mwenye kiu kali. Beberu alidhani kuwa Mbweha ametumbukia kwenda kunywa maji kukidhi kiu yake, na hivyo akauliza kama maji yalikuwa safi au la.


“Ni safi na matamu kupita maji yote kwenye nchi hii,” alijibu Mbweha yule mjanja, “jirushe utumbukie ujionee mwenyewe. Maji ni mengi yanatutosha sote na tutasaza.”


Beberu mwenye kiu mara moja alijitosa kisimani na kuanza kuyafakami maji. Mbweha naye kwa haraka sana alimdandia Beberu mgongoni akachupa kwenye ncha za pembe za Beberu na kutoka zake nje ya kisima.

Yule Beberu mpumbavu akang’amua kuwa amejiingiza matatizoni, akaanza kumbembeleza Mbweha amsaidie kumtoa kisimani. Lakini Mbweha tayari alikwishaanza kutokomea zake mitini.


“Laiti ungalikuwa na akili kama ulivyo na ndevu, rafiki,” alimwambia huku akikimbia zake, “ungalikuwa makini na kujaribu kung’amua kwanza njia utakayoitumia kutokea kisimani kabla hujatumbukia.”
 
So do i. Nilivyokuwa mdogo nilikuwa napenda kuhadithiwa hadithi. Nyengine zilikuwa za wanyama
 
Wadau nadhani kila mtu anazifaham hizi hadithi za abunuasi, leo hii nimeleta hii maada ili mnisaidie maana ya neno ambalo mheshimiwa alitamka siku zilizopita. Alisema halafu mtu atuletee afu ulela ulela na mwishoni akatamka neno esopo. Mi nahitaji kujua maana ya neno esopo, je hili neno lipo kwenye hadithi za abunuasi? Na lina maana gani?
Fyekelea mbaliii
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom