Majuto alifanya hivyo. Baada tu ya kumaliza alisikia tumbo lake lina nguruma na mwili wote ulisisimka.
Alianza kujisikia wa tofauti kama vile amekuwa mwepesi zaidi. Mchawi akamwambia Majuto, " Hii dawa
imekufanya uwe mwepesi na kuanzia leo utaweza kuogelea bila ya kuzama". Majuto alifurahi sana na
kumshukuru mchawi kwa msaada wake. Kuonyesha shukurani yake Majuto aliitoa zawadi yake
aliyomletea na kumpa.
Wakati wa kuagana ulipofika Majuto alikuwa tayari kuondoka. "Asante sana mzee, sasa mimi nitarudi
kjijini kuendelea na maisha yangu", alisema Majuto. "Ngoja kidogo." Alisema mchawi. "Kwani wewe
usingependa nikuwezeshe pia kukamata samaki wengi zaidi? Kwanini nisikupe kifaa ambacho
kitakuwezesha kukamata samaki wengi sana?" Majuto hakuamini alichosikia. "Mzee, yaani kuna kifaa
ambacho kitaniwezesha kukamata samaki wengi zaidi?", alisema Majuto. "Ndio, nitakupa lakini itabidi
ukubaliane na masharti yangu kwanza", alisema mchawi. "Niambie tu na mimi nitayatekeleza", alisema
Majuto.
Mchawi aliondoka tena kuelekea uwani na kurudi na nyavu kubwa. Majuto hakuelewa ni nini kile
alichokuwa amekishika mchawi kwa kuwa hakuwahi kuona nyavu maishani mwake. Siku zote yeye na
wavuvi wenzake walikuwa wakitumia ndoano tu kuvulia samaki na hawakujua nyavu ni nini. Mchawi
akasema, "Hii ni nyavu. Iweke ndani ya maji kila jioni, utakapo rudi jioni utakuta samaki wengi sana
wamenasa kwenye matundu. Kazi yako itakuwa ni kuwaokota tu na kuwaweka ndani ya ngalawa yako."
Majuto hakuamini masikio yake. "Kweli hii ni siku ya furaha sana maishani mwangu. Lakini kwanini
unataka kunifanyia haya yote?" aliuliza Majuto. Mchawi alimjibu, "Hapo zamani niliwakosea watu wengi
na nilifanya mambo mengi mabaya. Ndio maana ilinibidi nikimbilie na kuishi mwenyewe huku milimani.
Lakini nimefikiria sana mambo niliyoyafanya na nimeyajutia ndio maana ninataka kuwasaidia watu.
Sitakuomba mengi, lakini kila utakapoenda ziwani kuvua samaki ninataka uchukue nusu ya samaki wote
uliowashika na kuwapa masikini na wazee wasiojiweza. Ukishindwa kuyatekeleza haya basi na wewe pia
hautafanikiwa" Majuto haikumbidi hata kufikiria sana na alijibu, "Mimi pia ninapenda sana kwasaidia
watu lakini tu sikuwa na uwezo. Sasa umeniwezesha na mimi pia nitawasaidia watu wengine zaidi ya
hata uliyoniambia."
Kwa maneno hayo waliagana, na Majuto alibeba nyavu aliyopewa na mchawi na kuelekea tena kurudi
nyumbani. Alikuwa na furaha kubwa sana na alikimbia upesi sana hadi kufika nyumbani kwake.
Hakuwaza hata kusimama na kusalimia familia yake na kuwaambia kuwa amerudi, alikimbia moja kwa
moja hadi kwenye ziwa na kujitupa kwenye maji. Na kweli mchawi alivyokuwa amesema Majuto
hakuzama. Alibaki tu juu ya maji akielea. Majuto alishangilia sana na kwenda kuwatangazia rafikiki zake