Hadithi tamu - ahadi ya ndotoni

23
SASA ENDELEA...

"Tumekuwa watu wa kipigo kila kukicha ili turudishe mali zako."
"Kipigo! Toka kwa nani?"
"Mumeo, tena amekuwa akitufuata ndotoni na kutusumbua turudishe mali zako zote bila kuacha kitu chochote."

"Ina maana bila kupata kipigo msingenirudishia mali yangu?"
"Hapana Jeska...ooh samahani Lakashina tulikutafuta muda mrefu bila mafanikio, lakini sasa hivi mali zote zimekatika, sasa hivi maisha yetu yamekuwa ya kubahatisha."

"Sasa mimi niwafanyeje?"
"Muombe mumeo atusamehe au atupe muda tuitafute."
"Mmh, mimi sina neno labda mwenyewe."
"Basi mwambie umetusamehe ili atuache."
"Nitamwambia akirudi."

"Amekwenda wapi?"
"Sijui."
"Atarudi lini?"
"Sijui."

"Lakashina mtumie ujumbe hata kwa njia ya simu kumueleza umetusamehe ili kutupunguzia mateso."
"Mume wangu sijawahi kumuona na simu hata siku moja, na muda huu hayupo."
"Basi akija nitamueleza kuwa umetusamehe."
"Mmh! Sawa."

Baada ya simu kukatwa Lakashina alijikuta akijawa na mawazo juu ya kauli za baba zake wadogo waliomdhulumu mali yake. Moyoni alikuwa radhi kuwasamehe, aliamini mali ile isingewafikisha popote. Lakini alikumbuka kauli ambayo hakujua ni ya nani iliyomuelekeza awashe simu na kuikubali mali yake yote na asiwaonee huruma hata kidogo.

Lakashina aliamini kama ni mali yake, alikuwa na uwezo wa kusamehe hata kuigawa kwa mtu aliyempenda. Hakuona umuhimu wa kung'ang'ania kulipwa mali asiyokuwepo. Akiwa katika lindi la mawazo simu yake iliita, aliipokea.

"Asalamu aleykum," Lakashina alisalimia.
"Waleyku musalam," sauti nzito ilijibu upande wa pili na kumfanya Lakashina ashtuke na simu kumponyoka, lakini sauti ilisikika kama ameweka ‘loud speaker'.
"A..a..abee."

"Lakashina nani kakuita, acha kujitia hofu usipokuwa na kosa."
"Sa...sa...wa," alijibu kwa kutetemeka.
"Lakashina."
"Abee."

"Tuliza moyo wako kabla hatujazungumza lolote."
"Nimetuliza," Lakashina alisema huku akijiweka vizuri kwenye kochi na kufuta mikono usoni kujipa ujasiri.
"Lakashina," Sauti ile nzito ilimwita tena.
"Abee."

"Umetulia?"
"Ndiyo."
"Vizuri, umewasikia baba zako wadogo?"
"Ndiyo."

"Wamesema wataleta lini mali yako yote?"
"Mmh, wameomba niwaombee msamaha kwa vile mali yote hawana kwa sasa."
"Lakashina hakuna kitakachobadilika mali yako inatakiwa mara moja."
"Wamesema tuwape muda."

"Ha...ha...ha...he...he...he...ee," sauti ilicheka sana mpaka ikamkera Lakashina.
"Lakashina," sauti ilimwita baada ya kicheko.
"Abee."

"Unataka tugombane?"
"Hapana."
"Sasa nisikilize, nakuomba hiyo mali iletwe mara moja, mbona wao hawakukusubiri mpaka upate akili ndipo wakudhurumu...Lakashina," sauti ilijirudia kama mwangwi.

"Hii ni amri na siyo ombi, nataka uwakaripie wakuletee mali yako mara moja, kila kitu walichochukua warudishe. Hawakukuonea huruma wakati unamatatizo kwa nini unawasamehe. Kilio chako ndicho kilichofanya niitafute mali yako na kukupa maisha mazuri. Kama hutafanya hivyo adhabu yao itakurudia wewe."

Sauti ile ilinyamaza ghafla na kumfanya Lakashina azidi kuchanganyikiwa, sauti ya adhana ndiyo iliyoufanya moyo wake utulie. Alinyanyuka na kwenda kutia udhu kwa ajili ya swala ya adhuhuri. Alipomaliza kuswali alirudi sebuleni kujipumzisha simu iliita tena moyo ulimpasuka, aliichukua na kuzungumza.

"Asalamu aleykum."
"Lakashina, mama wewe pekee wa kuiokoa familia yako, bila huruma yako tunateketea wote," sauti ya upande wa pili iliyoambatana na kilio pili ilikuwa ya baba yake mdogo.

Lakashina alishindwa awajibu nini, huruma ilimjaa moyoni lakini onyo alilopewa muda mfupi lilimtisha kwa kuhofia maisha yake. Alijikuta akiporomokwa na machozi na kukosa la kuwaeleza baba zake wadogo.
 
24
SASA ENDELEA...
Lakashina huruma ilimjaa moyoni jinsi baba zake wadogo walivyokuwa wakilalamika mateso waliokuwa wakipata kutoka kwa mumewe. Pamoja na kulazimishwa kuchukua mali zake bado aliona kuna umuhimu wa kusimama yeye kama yeye kuwatetea baba zake wadogo.

Alikumbuka siku moja ndotoni aliyaona maisha ya tabu ya baba zake wadogo baada ya kumdhulumu mali yake. Alijikuta akiwahurumia wao badala ya kuwachukia na asubuhi alipoamka alikosa raha kabisa.

Alijifikiria kama ni kweli baba zake wadogo ndivyo walivyo, kwa muda ule hakukuwa na haja ya kuwalazimisha warudishe mali zaidi ya kuwasamehe.

Akiwa bado anabubujikwa na machozi huku upande wa pili wa simu ukiendelea kuomba msaada wake kuwaokoa na mateso. Aliwasikia wakisema;

“Mama siku hizi hatulali ni mateso mtindo mmoja ili turudishe mali yako, japo tunajua tuna kazi ya kurudisha vitu vyote.

Basi mtupe muda, nasema laana yako kwetu ilikuwa kubwa kwani baada ya kukufukuza haikupita muda tukaanza kugombana wenyewe kwa wenyewe na kufikia uamuzi wa kuuza sehemu kubwa ya mali, hata pesa tulizogawana iliyeyuka bila kufanya jambo lolote la maana.

“Lakashina tunakuomba utusamehe tunajua tulikutenda, lakini hakuna tulichopata toka kwenye mali ya wazazi wako zaidi ya dhambi na mateso.”

Maneno yale yalizidisha kuumiza moyo wa Lakashina kuona jinsi gani dhuluma ilivyo na malipo mabaya. Machozi yalimtoka bila kizuizi kila alipotaka kuzungumza alikosa maneno zaidi ya kuendelea kulia.

Ghafla sauti ya upande wa pili ilibadilika na kuwa nzito, haikuwa ngeni tena masikioni kwake wala hakuishangaa, aliisikiza ina ujumbe gani tena.
“Lakashina...Lakashina,” sauti ilijirudia kama mwangwi zaidi ya mara tatu.

“Moyo wako unaonekana kabisa unataka kuniudhi, sitaki ubadili uamuzi wangu.”
“Siwezi...siwezi.”
“Lakashina huwezi nini?”
“Nasema siwezi.”

“Sikia Lakashina najua kabisa unataka kuwahurumia baba zako wadogo viumbe wasio na huruma, kama huwezi niachie hiyo kazi mimi watarudisha tu.”

“Watatoa wapi?” Lakashina alijikaza na kujibu.
“Hiyo hainihusu, watapata mateso mpaka wanaingia kaburini.”
“Hapana...hapana.”

“Hapana nini?”
“Nasema tena hapana.”
“Huwezi kuzuia hasira zangu huenda zikakurudia wewe.”
“Sawa...sawa na zinirudie, lakini nakuomba uwaache kama mateso uliyowapa yanatosha na mali hawajarudisha.”

“Hapana Lakashina hata siku moja mwanamke hana kauli kwa mumewe.”
“Ha! Kumbe ni wewe mume wangu Lakashi?”
“Si muhumu kujua.”
“Kama si muhimu kujua nakuomba uachane nao mara moja.”

“Unanishurutisha?”
“Ndiyo, kama mali zako chukua niache na maisha yangu ya mateso,” Lakashina alijibu kwa ujasiri mkubwa.
“Lakashina ujasiri huo umeutoa wapi?”
“Si muhimu kujua.”

“Lakashina,” sauti nzito ilimuita, lakini hakuitikia aliendelea kulia kuonesha hasira zake zipo kwa yule mtesaji asiye na chembe ya huruma.
“Lakashina umekasirika?”

Hakumjibu aliendelea kulia kilio cha kwikwi, kifua kikiwa kimefura kwa hasira, alijiegemeza kwenye kochi. Mkono laini uliokuwa ukimpapasa shingoni ukifuatiwa na manukato aliyoyazoea yalimfanya anyanyue uso. Alishtuka kumuona mumewe Lakashi katika uso wa tabasamu.

“Laazizi unalilia nini?”
“Unajua, unajua Lakashi,” Lakashina alilia kilio cha kwikwi.
“Kuhusu nini?”
“Mimi nani yako?”
“Mke wangu.”

“Kwa nini hutaki kunisikiliza?”
“Kuhusu nini?”
“Baba zangu wadogo.”

“Ni hilo tu mpenzi?”
“Ni hilo, pia ni maisha gani ya kutishana.”
“Nani kakutisha?”

“Sijui nani kanipigia simu amesema kama nikiwasamehe basi nitamtambua.”
“Asikutishe, mwenye mamlaka juu yako ni mimi mumeo na si mwingine.”

“Na aliyekuwa akizungumza ni nani?”
“Achana naye ila nakuahidi baba zako hawataguswa tena na ikiwezekana nitawabadilishia maisha yao.”
“Asante mpenzi,” Lakashina alitabasamu na kumkumbatia mumewe kwa furaha.

Aliposhtuka alijikuta amelala kitandani peke yake na kujiuliza yaliyotokea ilikuwa ndoto au kama kweli mume wake kipenzi yupo wapi ila harufu ya manukato ilitawala chumba kizima.
 
Back
Top Bottom