SEHEMU YA PILI.
Shukuru na Rahabu wao mambo yao ni mazuri. Penzi lao kila uchao linazidi kuchanua. Kila mwisho wa juma wanapenda kwenda kutembelea sehemu tofauti tofauti. Shukuru na Othmani wanakaa chumba kimoja katika hosteli za Mkulima.
Ni majira ya saa tisa alasiri Rajabu amempitia mpenzi wake Shukuru ili wakatembee. Jumapili hii ni tulivu kabisa yenye jua kiasi. Nguo alizovaa Rahabu zimemkaa vizuri mithili ya mwanamitindo. Kafanya hivyo makusudi kuwachoma mioyo viforokwinyo ambao ni wabaya wake. Kila siku iendayo kwa Mungu hawaachi si tu kumsema bali kumwombea mabaya bali pia kumwingilia katika penzi lake. Japo hana ushahidi lakini wakati mwingine macho huwa yanaongea. Macho ya kina dada yamekuwa yakisema wazi kumtaka Shukuru.
Kwa jinsi Rahabu anavyompenda Shukuru wake hataki kabisa kuona hilo linatokea. Ndio maana yupo karibu na mtu wake akikaba hadi penalti. Anapofika kwenye mlango anabisha hadi.
"Hodi ndani ".
Rahabu anapoingia wote wanapigwa na butwaa. Ni kweli Rahabu ni mrembo wa nguvu kama sio haja. Lakini kwa namna alivyoupala leo amejiongezea 'credit'.
" Mbona hivyo jamani, hamnijui? " Rahabu anauliza.
" Tunakujua ila hongera sana, umependeza mno ndio maana tumekaa kimya kidogo kukuangalia " Othmani anajibu.
" Basi msinishangae, mkinishangaa nyinyi wengine itakuwaje? "
Baada ya mazungumzo kidogo Shukuru na Rahabu wanaafikiana waende Lakairo Hotel. Wanamuaga Othmani na kumwambia wataonana usiku.
******** ********** ***********
Usongo wa mawazo unamzidi Othmani baada ya rafiki yake kutoka na mpenzi wake wakiwa wamependeza na wenye furaha tele. Mawazo yanaanza kumsumbua. "Iweje Shukuru afanikiwe katika mapenzi yeye ashindwe?".
Anakumbuka likizo ya mwaka wa kwanza alivyomwomba Shukuru waende wote Dar es salaam. Shukuru hata Dar hakuwahi kufika kabla. Ni yeye ndie alimtembeza na kumwonyesha jiji. Alimtembeza maeneo yote muhimu Ikulu, Mlimani city, uwanja mkuu wa Taifa, soko la Kariakoo bila kusahau Bilicanas, San-siro, Travertine uwanja wa nyumbani wa mfalme na Jahazi yake na sehemu zingine. Lakini mbona yeye anachekelea ingali yeye akinuna.
Othmani anazidi kutafakari na kujiona kama mjinga. Anajidharau kutaka kumchukia rafiki yake bila sababu. Rafiki yake hajachangia kwa lolote linalofanya yeye kuangukia pua. Hiyo hali inajitokeza bila kupangwa. Anaanza kuyakemea mawazo yake, anaona ni mawazo mabaya yanayoweza kujenga chuki kati yao.
******** *********** ************
Shukuru na Rahabu wanapofika Lakairo Hotel wanaagiza vinywaji na utumbo wa kuchoma. Hotel hii inasifika sana kwa chakula Safi hasa mishikaki ya utumbo na samaki wa kuchoma. Wakiwa wanaendelea kunywa vinywaji anakuja bwana mmoja ambae anaonekana kiumri anatoka kwenye ujana, anaelekea kwenye utu uzima.
"Habari zenu jamani?" Anauliza.
"Nzuri " Shukuru anajibu.
" Samahani naomba niongee na wewe japo kidogo" Yule bwana anaongea
Shukuru anainuka na wanafuatana hadi pembeni.
"Samahani Kaka, yule dada nani yako? ".
" Yule ni rafiki yangu, tumekuja kujipumzisha"
"Hongera sana, anaonekana ni msichana mrembo "
" ahsante nashukuru "
" Wewe ni mwanaume kama mimi, naomba usijisikie vibaya kwa swali nililokuuliza "
" Hapana usijali " Shukuru anajibu.
Shukuru anarudi kwenye Meza yake na kukaa.
" Alikuwa anakwambia nini?" Rahabu anamuuliza Shukuru kwa hamu kubwa yenye kutaka kufahamu.
Kabla Shukuru hajajibu yule bwana anarudi kwenye meza yao na kusema "Nashukuru sana kuwafahamu, chukueni hiki kidogo mtaagiza mnachopenda". Ghafla yule bwana anatoa rundo la pesa na kuziweka mezani. Taratibu anaondoka na kuwaacha wakiwa wanashangaa.
Baada ya kupita sekunde kadhaa Shukuru anazichukua pesa na kuzihesabu. Haamini! ni laki tano. Anamueleza Rahabu namna alivyoongea nae. "Kuna nini nyuma ya hizi pesa?" Wote wanaanza kufikiri. Wanajifariji kwa kuamini hawajafanya lolote baya.
Baada ya dakika tano kupita wanaamua kukodi gari na kurudi chuo. Pamoja na kuianza siku yao vizuri wanaona wanaweza kuimaliza vibaya. Wote bado hawaelewi nia na dhamira ya yule bwana.