Hadithi: Mbio za sakafuni huishia ukingoni

Hadithi: Mbio za sakafuni huishia ukingoni

SEHEMU YA 16


ILIPOISHIA



Baada ya hapo ndipo mke wa Waziri Mkuu alipomsafisha Monica ile damu na kuliweka vizuri lile jaraha ili lisioneshe athari ya meno.



“Mimi naona tuweke plasta hapa watakaomuosha wataiondoa watajua alijiumiza mwenyewe” Mke wa Waziri Mkuu alishauriana na mume wake ambaye limkubalia.



Baada ya kuushughulikia mwili wa Monica ndipo Waziri Mkuu alipotoa taarifa ya kifo cha mwanawe usiku ule ule.



Viongozi wa serikali wakaanza kumiminika nyumbani kwa Waziri Mkuu. Raisi mwenyewe pia alifika usiku huo huo baada ya kupata habari ya kifo hicho.



Waziri Mkuu alikuwa akitoa maelezo ya uongo aliyokuwa ameyapanga na mke wake juu ya kifo cha binti yao.



Kwa vile kifo hicho kilikuwa kimetokea ghafla, watu wengi walipatwa na mshangao waliposikia taarifa ya Waziri Mkuu.



SASA ENDELEA



Asubuhi kulipokucha maombolezo yakaanza nyumbani kwa Waziri Mkuu. Wakati wote mke wa waziri Mkuu na Vero, binti yao wa kwanza, walikuwa sambamba na Sofia. hawakumpa nafasi ya kuwa peke yake kwa sababu yakutomuamini.



Hatimaye mwili wa Monica uliagwa kwa heshima za viongozi wa Serikali na wananchi waliofurika mchana kabla ya kusafirishwa kijijini kwao Morogoro kwa ajili ya mazishi.



Baada ya mazishi ya Monica ndipo Waziri Mkuu na mke wake walipokaa chini kulizungumzia suala la Sofia.



“Sasa itabidi uende naye Nairobi kama ambavyo tulipanga” Waziri Mkuu alimwambia mke wake.



“Niende naye lini?”



“Hatuna muda wa kupoteza, yasije yakatokea mengine. Utakwenda naye kesho kwa ndege”



“Umeshatayarisha mipango yote?”



“Mipango iko tayari. Kinachohitajika ni safari tu”



“Sawa”



Siku iliyofuata Sofia na mama yake wakapanda ndege kuelekea Nairobi nchini Kenya. Walitua katika uwanja wa Jommo Kenyatta wakapanda teksi iliyowapeleka katika hospitali ya magonjwa ya akili iliyokuwa nje kidogo ya jiji la Nairobi.



Siku ile ile vipimo vya akili ya Sofia vilichukuliwa na siku ile ile matokeo yake yalipatikana. Sofia aligunduliwa alikuwa mzima kabisa wa akili. Matokeo hayo yalimshangaza mama yake.



Akaona ampigie mume wake kumjulisha.



Waziri Mkuu alipoambiwa hivyo na mke wake naye alishangaa.



“Hawakugundua tatizo lolote?” akamuuliza.



“Ripoti yake inaonesha kuwa hana tatizo lolote la akili”



“Umewaeleza kuhusu vitendo ambavyo amevifanya”



“Siwezi kuthubutu kufanya hivyo”



“Ni kweli. Sasa jaribu kuchukua vipimo vya malaria”



“Itabidi twende katika hospitali nyingine. Hii ni ya magonjwa ya akili peke yake”



“Mnaweza kwenda”



Sofia na mama yake wakapanda tena teksi iliyowapeleka katika hospitali nyingine iliyokuwa katikati ya jiji.



Sofia alifanyiwa uchunguzi wa damu yake kuangalia vimelea vya malaria lakini jibu lililotoka ni kuwa Sofia hakuwa akiugua malaria.



Mama yake alimpigia tena simu mume wake akamjulisha kuhusu matokeo hayo.



“Mh! Ni mambo ya ajabu!” Waziri Mkuu akasema.



“Lingekuwepo moja kati ya malaria au ugonjwa wa akili tungeelewa”



“Sasa tuseme ana tatizo gani?”



“Tatizo lake halijulikani”



“Halijulikani lakini lipo. Lazima tatizo liwepo”



“Sisi tunalala leo tunarudi kesho”



Waziri Mkuu akanyamaza kimya.



“Mbona umenyamaza?”



“Ninafikiria. Tegemeo langu kubwa lilikuwa huyo mtoto atakutwa na matatizo kichwani mwake…”



“Hayakukutwa. Sasa unashaurije?”



“Basi mnaweza kurudi hapo kesho”



Usiku wa siku ile walilala katika hoteli moja jijini humo asubuhi yake wakapanda ndege kurudi Dar.



Waziri Mkuu alituma gari kwenda kuwapokea kiwanja cha ndege. Gari hilo liliwapeleka nyumbani. Siku iliyofuata Sofia na mama yake walikwenda kwao Morogoro.



Mke wa waziri Mkuu akaenda kwa mganga mmoja kijijini kwao na kumuelezea kuhusu matatizo ya mwanawe.



“Inawezekana ana matatizo lakini hatuwezi kuyajua mpaka nipige ramli” Mganga akamwambia.



“Tunataka tuyajue na uyatibu, piga ramli”



Mganga akapiga ramli yake ya kuchungulia tunguri. Alikuwa akichungulia kwenye tundu ya tunguri kisha anaeleza alichokuwa anakiona.



“Ramli yangu inanionesha mbali sana” Mganga akasema.



“Mbali, wapi?”



“Ramli inakwenda kwa baba yake”



“Amefanya nini?”



“Huyu ndiye amemdhuru mtoto…”



“Eti nini, baba yake ndio amemdhuru binti yetu? Amemdhuru kivipi?”



“Hebu nieleze wewe mke wake, kabla ya mumeo kuwa Waziri Mkuu alifanya nini?”



Mke wa Waziri Mkuu akabetua mabega.



“Sijui”



“Hakuna sehemu ambayo alikwenda kutambika au kufanya maombi?”



“Ndiyo nakumbuka. Alikwenda kwa bibi mmoja kijijini kwao wakaenda kwenye mzimu”



“Walikwenda kwenye huo mzimu kwa madhumuni gani?”



“Mh! Ni kwa mambo yao haya ya kisiasa”



“Yapi, hebu nieleze”



“Mimi aliniambia alikwenda kutambikiwa na kuweka nadhiri kwenye mzimu wa kwao kuwa endapo atateuliwa kuwa Waziri Mkuu atapeleka ng’ombe kwenye ule mzimu”



“Je alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu alitimiza nadhiri aliyoweka?”



“Mh! Sijui sasa…”



“Nenda kamuulize alipeleka yule ng’ombe?”



“Kwa hiyo kama hakupeleka linaweza kuwa ndio tatizo?”



“Ndio”



“Sasa ngoja nirudi Dar, niende nikamuulize Jibu atakalonipa nitakuja kukuambia”



“Utakuja lini tena?”



“Nitakuja kesho”



“Utanikuta”



Mke wa Waziri Mkuu akarudi Dar pamoja na Sofia. Wakati wa usiku akamueleza mumewe kuwa alikwenda kwa mganga wa kienyeji na kuelezwa aliyoelezwa.



Waziri Mkuu alipoyasikia maelezo ya huyo mganga akashituka. Mawazo yake yakarudi nyuma miaka kadhaa iliyopita, wakati huo akiwa Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais.



Chama chake kilikuwa kimeshinda uchaguzi. Rais alikuwa anasubiri kuapishwa ili aunde serikali yake. Kulikuwa na watu watatu waliokuwa wakitajika kupewa wadhifa huo, mmojawapo akiwa yeye.



ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 17


ILIPOISHIA



Kwa sababu ya kiherehere, aliamua kwenda kijijini kwao kuwaona wazee. Kulikuwa na bibi mmoja ambaye alikuwa mganga maarufu kijijini kwao akampeleka kwenye mzimu wa kwao na kumfanyia maombi ya kishirikina kwenye mzimu huo.



Akamuombea kupata uwaziri mkuu.



Baada ya maombi kukamilika, bibi huyo alimtaka Dastan Lazaro wakati huo akiwa si waziri mkuu, kuweka nadhiri kwenye mzimu huo kuwa endapo atateuliwa kuwa waziri mkuu atapeleka ng’ombe kwenye mzimu huo.



“Hilo ni sharti. Ukiteuliwa kuwa waziri mkuu kama unavyotaka, uje uchinje ng’ombe hapa” Bibi huyo alimsisitizia Lazaro.



“Hilo jambo dogo sana”



“Sawa. Kazi yetu imekwisha, turudi”



Waziri Mkuu alikumbuka kwamba alipoteuliwa kushika wadhifa huo alisahau kutimiza nadhiri aliyoiweka.



Kuna siku mke wake alimkumbusha. “Mume wangu unakumbuka kwamba uliniambia uliweka nadhiri kwenye mzimu kwamba utapaleka ng’ombe.?”



“Mke wangu huo ni ushirikina”



SASA ENDELEA



“Lakini si ulikwenda mwenyewe ukakubali kuweka nadhiri wewe mwenyewe”



“Nilimfuatisha tu yule bibi lakini sikuwa nikiamini”



“Kwa hiyo umeamua uache?”



“Unadhani naweza kufanya upuuzi ule? Si nitaharibu hata heshima yangu”



Dastan Lazaro akapuuza sharti alilopewa na mganga. Mzimu aliopelekwa ulikuwa maarufu na watu mbalimbali walikuwa wakifika kwenye mzimu huo kwa dharura zao za kishirikina.



Eneo hilo lilikuwa likikaribisha fisi waliokuwa wakifuata mizoga ya wanyama waliokuwa wakitolewa makafara kwenye mzimu huo. Kijiji kilipopanuka mzimu huo ukawa upo karibu na makazi ya watu, ndipo Waziri Mkuu alipoamuru uondolewe.



Magreda ya halmashauri yalipelekwa kwenda kuung’oa mzimu huo, ukawa haupo tena. Eneo hilo lilisafishwa likawa jeupe. Ziara za kuzuru mzimu huo zikawa hazipo tena. Baadaye mahali hapo palikuja kujengwa shule ya kijiji.



Baada ya Waziri Mkuu kuvuta kumbukumbu hiyo alimtazama mke wake.



“Mganga alikwambia uje uniulize kama nilitimiza ile nadhiri?” akamuuliza



“Ndio aliniambia nije nikuulize kisha niende nikamjibu”



“yeye alijuaje kama nilikwenda kuweka nadhiri kwenye mzimu ule?”



“Alijua baada ya kupiga ramli”



“Sio kwamba wewe ndio ulimueleza?”



“Hapana. Sikumueleza. Yeye ndiye alinieleza mimi”



“Alikuwa na maana kwamba kutotimiza ile nadhiri ndio kumemsababishia mtoto wetu matatizo aliyonayo?”



“Ndivyo alivyonieleza”



“Kivipi?”



“Alitaka kwanza nikampe jibu ndio atanieleza”



“Nenda kamwambie kwamba sikutimiza ile nadhiri. Sasa mtoto amedhurika kivipi?”



“Kesho nitakwenda kumueleza”



Asubuhi yake, mke wa Waziri Mkuu pamoja na Sofia wakaenda Morogoro. Wakiwa kijijini kwao Vicky, yaani mke wa Waziri Mkuu alimuacha Sofia nyumbani kwao, akaenda peke yake kwa yule mganga.



Alipofika alimueleza kuwa baada ya mume wake kuupata uwaziri mkuu hakutimiza ile nadhiri aliyoweka kwenye mzimu.



“Hilo ndilo lililoleta tatizo kwa binti yenu” Mganga akamwambia.



“Limeleta tatizo kivipi?”



“Ule mzimu uliahidiwa damu, yaani yule ng’ombe angechinjwa kwenye ule mzimu na mzimu ungepata damu. Sasa baada ya mume wako kutotimiza ahadi yake mzimu ule ulimuingia binti yenu, sasa unafyonza damu za watu”



Mke wa Waziri Mkuu alishituka.



“Kumbe ule uliompata mwanangu ni mzimu?” akauliza kwa mshangao.



“Ni mzimu”



“Kwani ulitaka ng’ombe wangapi?”



“Ng’ombe mmoja tu alioahidi mume wako”



“Sasa mbona ameshafyonza damu watu wawili?”



“Na utaendelea kufyonza watu zaidi”



“Kwanini sasa?”



“Ni kwa sababu mmeufanyia dharau. Mmeuahidi kitu halafu hamkutimiza”



“Si mimi, ni baba yake”



“Ndio unawakomoa nyote”



Vicky akatikisa kichwa kusikitika.



“Sasa hauna tiba?”



“Hauna tiba nyingine”



“Isipokuwa?”



“Mume wako atimize ile nadhiri yake?”



“Akitimiza ndio itakuwa tiba yake?”



“Ndio”



Vicky akarudisha jibu kwa mume wake.



“Mume wangu ulikosea sana kwenda kuweka nadhiri kwenye mzimu kisha ukapuuza”



“Mganaga amekwambiaje?”



“Ameniambia baada ya kuacha kupeleka yule ng’ombe, ule mzimu umemuingia mtoto wetu, sasa unafyonza damu za watu ukiwa mwilini mwake”



Waziri Mkuu akashituka.



“Mpaka lini?”



“Mpaka utimize ile nadhiri yako”



“Ngoja kesho nitakwenda kwa yule bibi niliyekwenda naye wakati ule. Tutakwenda kuyamaliza huko huko”



Siku iliyofuata Waziri Mkuu akaenda Morogoro. Alikwenda kijijini kwao na kufika nyumbani kwa yule bibi aliyekwenda naye kwenye ule mzimu.



“Yule bibi alikufa tangu mwaka jana?” Mwanamke mmoja alimwambia Waziri Mkuu alipomuuliza mwanamke huyo.



Waziri Mkuu akashusha pumzi ndefu.



“Kumbe yule bibi alikufa?”



“Alikufa, hatuko naye tena”



“Hivi hakuna mtu mwingine aliyechukua kazi zake?”



“Yule bibi hakuwa na mtoto wala mjukuu”



“Na wale wasaidizi wake wako wapi?”



“Msaidizi wake alikuwa mmoja tu na ndiye aliyetangulia kufa”



Waziri Mkuu hakuwa na jingine isipokuwa kuaga na kuondoka. Aliporudi nyumbani kwao alimuuliza ndugu yake kama alikuwa anamfahamu mganga yeyote wa kienyeji aliye hodari.



“Namfahamu”



“Kama namuhitaji unaeza kumleta hapa muda huu?”



“Naweza”



“Hebu nenda kamlete, nina shida naye”



Ndugu huyo wa Waziri Mkuu aliondoka na gari lake. Baada ya nusu saa tu alirudi akiwa na mtu mwingine ambaye alimpeleka kwa Wazi Mkuu.



“Mganga mwenyewe ndiye huyu” akamwambia



“Karibu sana” Waziri Mkuu alimwambia mganga huyo.



“Asante”



Ndugu wa Waziri Mkuu aliondoka na kuwaacha. Waziri Mkuu akamueleza mganga huyo tatizo la binti yake na jinsi walivyoambiwa na mganga wa awali kwamba tatizo hilo linatokana na nadhiri aliyoweka kwenye mzimu.



“Ni kweli kwamba uliweka nadhiri hiyo?” mganga akamuuliza Waziri Mkuu.



“Ni kweli niliiweka lakini sikuwahi kuitimiza kwa sababu ya shughuli kuwa nyingi”



itaendelea
 
SEHEMU YA 18

ILIPOISHIA



“Ungeweza kuitimiza nadhiri yako na hilo tatizo lingeondoka lakini sasa kuna tatizo jingine”



“Tatizo gani?”



“Ule mzimu haupo tena, ni afadhali kama ungehamishwa na kupelekwa sehemu nyingine lakini aliondolewa kabisa. Na hivi sasa haupo tena”



Waziri Mkuu akakumbuka amri ya kuuondoa mzimu huo kwenye kijiji hicho aliitoa yeye baada ya kuona kijiji kilikuwa kimepanuka na watu walikuwa wakifanya vitendo vya kishirikina waziwazi na kusababisha fisi waliokuwa wakifuata mizoga ya wanyama kuhatarisha maisha ya watu.



“Ni bora ningeuacha” Waziri Mkuu akajiambia kimoyo moyo.



“Sasa kama huo mzimu haupo haitawezekana kutimiza ile nadhiri?” akauliza huku akiizuia sauti yake isioneshe hofu.



“Haitawezekana. Mzimu wenyewe haupo. Hiyo nadhiri utaitimiza wapi?”



Waziri Mkuu akamkumbuka mwanawe.



“Sasa mwanangu atapona vipi?”



“Hilo swali ni vigumu kukujibu, ungemfuata yule mganga wa kwanza uliyekwenda naye kwenye huo mzimu”



SASA ENDELEA



“Nimeambiwa huyo mganga amekwishakufa”



Mganga akatikisa kichwa kusikitika.



“Hilo suala litakuwa gumu sana”



“Una maana gani, una maana kwamba mwanangu hatapona”



Mganga aliendelea kutikisa kichwa.



“Kupona itakuwa vigumu sana”



Waziri mkuu alitoa macho ya taharuki.



“Unasemaje?”



“Mheshimiwa kwa upande wangu, sina uwezo wa kukusaidia” Mganga akasema huku uso wake ameuinamisha chini akiyakwepa macho ya mheshimiwa.



“Unadhani nani anaweza kunisaidia?”



“Sijui lakini unaweza kujaribu kwa waganga mbalimbali”



“Loh! Itakuwa ni kazi!”



“Hakuna njia nyingine ya kufanya isipokuwa kuhangaika tu, kujaribu huku na huku”



“Namsikitikia sana mwanangu na ninajuta kuweka ile nadhiri”



“Na ni kwanini uliweka nadhiri halafu ulishindwa kuitimiza katika muda wake?



“Kusema kweli sikudhani kama yangekuwa makubwa kiasi hiki”



“Umedharau kitu ambacho hukijui. Ni bora usingekwenda kuweka nadhiri ile”



“Yaani ninajuta..!”



Palipita kimya cha karibu nusu dakika kabla ya mganga huyo kuinuka na kumuaga Waziri Mkuu aliyekuwa amechanganyikiwa



“Mheshimiwa naona nikuage…ninakwenda zangu”



“Ehe! Ndio unakwenda?” Waziri Mkuu akamuuliza baada kuzinduka kwenye mawazo.



“Naona niende, kuna kazi zinaningoja”



Waziri Mkuu naye akasimama. Hisia za uheshimiwa zilikuwa zimeshamtoka.



“Sasa utanisaidiaje?”



“Labda nijaribu kukuulizia kwa wataalamu wengine.



“Basi jaribu kufanya hivyo, nitakupa zawadi yako. Utakuwa unawasiliana na huyu ndugu yangu anayeishi hapa”



“Sawa. Kama nikifanikiwa kupata mtu anayeweza kulitatua hilo tatizo nitamfahamisha”



“Asante sana”



Wakapeana mikono kuagana.



Mganga akatoka. Waziri Mkuu alirudi kwenye kochi akaketi na kukiinamisha kichwa chake.



Ndugu yake akaingia na kuketi kando yake. Waziri Mkuu akamtazama.



“Nina matatizo makubwa ndugu yangu, inabidi nikueleze lakini hii iwe ni siri yako” akamwambia.



“Itakuwa ni siri yangu, ni matatizo yapi kaka?”



Waziri Mkuu akamueleza tatizo la mwanawe na jinsi waganga walivyomueleza kuwa lilitokana na mizimu.



“Niliwahi kuweka nadhiri kwenye ule mzimu ulioondolewa halafu sikutimiza nadhiri ile” alimwambia.



“kwa hiyo huo mzimu ndio umemuingia binti yetu?”



“Ndivyo ninavyoambiwa na wataalamu na inaweza kuwa ni kweli kwa sababu vipimo vyote vya hospitali vimeonesha kuwa Sofia hana matatizo”



“Sasa huwezi kuitimiza hiyo nadhiri kwa sasa?”



“Haiwezekani kwa sababu ule mzimu haupo tena”



“Huyu mganga niliyemleta amekushauri nini?”



“Ameshindwa”



“Tutatafuta waganga wengine, wapo wengi”



“Basi nitafutie, itabidi nirudi Dar muda huu lakini ukimpata nipigie simu nitakuja mimi au mke wangu”



“Hakuna tatizo kaka, nitafanya kazi hiyo”



Waziri Mkuu akarudi Dar. Asubuhi ya siku iliyofuata kabla ya kutoka kwenda ofisini kwake ndugu yake akampigia simu.



“Asubuhi njema kaka” Sauti kutoka simu ya upande wa pili ikasikika.



“Na kwako pia. Mmeamka salama huko?”



“Sisi tumeamka salama, sijui nyinyi huko?”



“Huku pia tumeamka salama. Umeshughulikia lile suala langu?”



“Nimelishughulikia jana ile ile na nimepta mtu ambaue ataweza kutusaidia”



Waziri Mkuu alijisikia kupata nguvu ndani ya kiwiliwili chake.



“Kweli eh!” akauliza.



“Sasa sijui utakuja lini huku?”



“Umemueleza hali halisi ilivyo?”



“Nimemueleza kila kitu na nimemueleza kuwa ule mzimu kwa sasa haupo tena. Ameniambia uje”



“Atakuja mke wangu pamoja na huyo binti”



“Atakuja lini?”



“Atakuja leo hii”



“Saa ngapi?”



“Sijaua saa lakini watakapokuja nitakufahamisha”



“Sawa, basi nawasubiri”



Wakati ule mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa chumbani kwake akatoka haraka na kwenda sebuleni ambako mke wake alikuwa akizungumza na Sofia.



“Hebu njoo chumbani” akamwambia.



Mke wake alimuacha Sofia akamfuata mume wake chumbani.



“Kuna nini?”



“Stambuli amenipigia simu ameniambia yule mtaalamu atakayeweza kuyashughulikia haya matatizo amepatikana, sasa nataka uende Morogoro na Sofia baada ya kumaliza kazi zako”



“Naweza kuacha kazi zote ili niende naye”



“Basi fanya hivyo, mimi naenda ofisini”



“Wewe nenda, tukitoka nitakupigia simu”



“Sawa”



Dakika chache baadaye akiwa ofisini kwake Waziri Mkuu akapigiwa simu na mke wake.



“Ndio tunatoka”



“Sawa. Nataka huyo dereva wako asijue kitu”



“Hatajua”



“Unijulishe kitakachoendelea”



“Nitakujulisha”



Mke wa waziri Mkuu alifika Morogoro katika kijiji alichotoka mume wake.



Shemeji yake Stambuli baada ya kumkaribisha nyumbani alimwambia asubiri ili aende akamchukue huyo mganga aliyezungumza naye.



Aliondoka kwa gari lake kuelekea alikokuwa akiishi mganga huyo ambako kulikuwa kijiji cha pili



Alipofika alimkuta mganga huyo akihudumia mtu. Akamsubiri hadi alipomaliza, alimfuata na kumwambia kuwa mke wa Waziri Mkuu pamoja na binti yao mwenye matatizo walikuwa tayari wamefika nyumbani kwake.



Mganga huyo kwa heshima ya kumhudumia binti wa Waziri Mkuu alijiandaa haraka haraka akajipakia kwenye gari ya Stambuli wakaondoka.



Walipofika kwa mke wa Waziri Mkuu, Stambuli aliwapisha. Sofia pia hakutakiwa kusikiliza yale mazungumzo.



ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 19


ILIPOISHIA



“Tatizo la binti yenu ni kubwa lakini kwangu mimi ni dogo sana” Mganga huyo alimwambia mke wa Waziri Mkuu.



“Kwa hiyo utaweza kulishghulikia?” Mke wa Waziri Mkuu akamuuliza kwa matumaini.



“Ninaweza kulishughulikia na binti yenu akawa mzima kabisa”



“Tutafurahi kwa sababu ni tatizo lililotusumbua sana. Utahitaji nini na nini?”



“Nitahitaji ng’ombe watatu na shuka nyeusi, yaani kaniki, ziwe vipande vitatu”



“Hivyo vitu vitapatikana. Na wewe mwenyewe utahitaji kiasi gani?”



“Mimi mtanifikiria wenyewe, siwezi kukwambia nataka kima fulani”



“Tuambie tu”



Mganga akatikisa kichwa.



SASA ENDELEA



“Siwezi kuwatajia kima, nyinyi wenyewe ndio mtanifikiria. Mtakachonipa nitashukuru”



“Sawa. Sasa tunataka uishughulikie hiyo kazi. Binti mwenyewe si umemuona”



“Nimemuona. Atapona tu. Sasa hivyo vitu vitapatikanaje?’



“Nitamtuma shemeji sasa hivi”



“Sasa kama utamtuma shemeji yako, nataka nikwambie kuwa hiyo kazi tutaifanya usiku”



“Usiku saa ngapi?”



“Saa mbili usiku”



“Utaifanya wapi”



“Porini, kwenye mzimu mwingine”



“Kwenye mzimu mwingine itafaa”



“Mzimu ni mzimu, mizimu yote ina asili moja na inasikizana. Kama ule wa kwanza umeondolewa, mzimu mwingine unaweza kufaa. Tofauti ni kuwa utatakiwa ulipe na adhabu, yaani badala ya ng’ombe mmoja wawe watatu kama nilivyokuagiza. Ule mzimu wenyewe utapata ng’ombe wawili na ule mzimu tutakaoutumia utapata ng’ombe mmoja”



“Kumbe wale waganga wa kwanza walishindwa nini?”



“Ujuzi. Ujuzi unatofautiana. Mimi kazi hii ni ya kurithi kwa baba yangu na baba yangu aliirithi kwa babu yangu. Na tangu baba yangu anashirikiana na babu, mimi nilikuwa nao pamoja. Sijisifu lakini nashukuru wazee hao wameniachia ujuzi wa kutosha”



“Sawa. Nimekuelewa. Sasa ngoja nimuite shemeji nimpatie hizo pesa za hao ng’ombe watatu na hizo shuka nyeusi. Wewe utamuagiza pa kuwapeleka ngombe hao”



“Sawa. Muite”



Mke wa Waziri Mkuu alimuita shemeji yake kwa kumpigia simu. Stambuli akafika pale muda ule ule.



“Kumbe hukuwa mbali?”



“Nilikuwa karibu tu”



Akamueleza mazungumzo yake na yule mganga kisha akampa shilingi milioni mbili kwa ajili ya kununua ng’ombe watatu na vipande vitatu vya kaniki.



“Hao ng’ombe nikishawanunua niwapeleke wapi?” Stambuli akauliza.



“Tutatoka pamoja nitakwenda kukuonesha mahali pa kuwapeleka” mganga akamwambia.





“Sawa. Kwa hiyo shemeji atasubiri hapa hapa hadi saa mbili usiku?”



“Itabidi nisubiri hapa hapa, siwezi kurudi Dar kisha nije tena hapa. Lakini nitashauriana na mheshimiwa. Kama kutakuwa na mabadiliko nitawambia”



Stambuli na mganga huyo walipotoka mke wa waziri akampigia mume wake na kumueleza mazungumzo yake na mganga huyo.



“Basi wewe endelea kukaa huko huko. Ikiwezekana unaweza kulala huko huko” Waziri Mkuu akamwambia mke wake.



“Na huyu dereva wangu itakuwaje?’



“Kama utaamua kulala, mwambie aende akatafute chumba kwenye hoteli yoyote Morogoro mjini akufuate kesho hapo kijijini.



“Sawa. Nitaangalia itakavyokuwa”



“Hiyo shughuli ikikamilika utanijulisha”



“Sawa”

************





Mnamo saa mbili usiku, watu saba walikuwa kwenye msitu chini ya mti mkubwa uliokuwa umezungukwa na kichaka.



Alikuwa Mke wa waziri Mkuu na Sofia. Pia alikuwepo Stambuli na mganga wao pamoja na wasaidizi wake wawili.



Ng’ombe watatu weusi walikuwa wamefungwa kando ya kichaka hicho.



Kaniki moja ilitandikwa ndani ya kichaka. Kaniki nyingine alivalishwa Sofia na kaniki ya tatu aliivaa mganga mwenyewe.



Sofia alikuwa amekalia ile kaniki iliyotandikwa chini. Mganga aliyekuwa ameshika mwengo wa uganga alikuwa akimzunguka huku akitabana maneno ya kiganga.



Wasaidizi wake wawili walikuwa wamesimama karibu yake wakingoja kupewa amri yoyote.



Stambuli na mke wa Waziri Mkuu walikuwa wamesimama pembeni wakitazama.



Baada ya mganga kumzunguka sofia mara saba huku akitabana maneno, aliwaagiza wasaidizi wake wamchinje ng’ombe wa kwanza mbele ya miguu ya Sofia.



Ng’ombe alichinjwa, sofia akarambishwa damu mbichi ya ng’ombe.



“Meza!” Mganga alimwambia Sofia alipomuona ameiweka ile damu mdomoni.



Sofia akaimeza.



Alipakwa damu nyingine kwenye miguu na nyingine kwenye chembe cha moyo kisha akaambiwa ainuke.



Ngombe wa pili akachinjwa na kuachwa. Ngombe wa tatu aliachwa akiwa mzima.



“Mizimu itakuja kumchukua wenyewe usiku” Mganga aliwambia Stambuli na mke wa Waziri Mkuu na kuongeza.



“Kazi imekwisha, sasa tunaweza kwenda zetu”



“Ninataka kukuuliza” Mke wa waziri akamwambia mganga huyo.



“Uliza”



“Huyu binti atakwenda kulala hivyo hivyo pamoja na damu?”



“Ndio. Asioge leo. Ataoga kesho asubuhi”



“Sawa”



Mke wa waziri Mkuu akamtazama Stambuli.



“Hatutarudi Dar leo, tutalala hapa hapa kijijini” akamwambia.



“Mtaondoka kesho asubuhi?’



“Tutaondoka kesho asubuhi”



“Sawa” Stambuli alimwambia mke wa Waziri Mkuu kisha mwanamke huyo akamgeukia mganga aliyemshughulikia mwanawe.



“Ndio kusema kwamba mwanangu ameshapona matatizo yake?” akamuuliza.



“Mwanao ameshapona, hatakuwa na matatizo tena. Mzimu umeshapata ulichokuwa unakitaka” Mganga alimwambia. Kauli ambayo ilimpa matumaini mama yake Sofia.



“Sasa ndio tunaondoka, sijajua nikupe kiasi gani?”



“Utakachotaka wewe”



“Nimetumia pesa nyingi leo” Mke wa Waziri Mkuu alisema huku akifungua pochi yake. Akaongeza.



“Nimebakisha pesa kidogo….”



Alitia mkono kwenye pochi akatoa kitita cha noti.



“Kwa sasa nitakupa laki mbili ili nibakishe pesa za kunirudisha Dar kesho asubuhi ila pesa zingine nitazituma kwa shemeji atakuja kukupa. Sawa?”



“Hakuna tatizo”



Mganga alizipokea laki mbili alizopewa.



“Asante sana”



Wakaagana.



Waliporudi nyumbani mke wa Waziri Mkuu akampigia mume wake.



“Ndio tumerudi kutoka kwenye huo uganga” akamwambia.



“Imekuwaje?’ Waziri Mkuu akamuuliza kwenye simu.



“Ameshafanyiwa”



“Kwa hiyo kazi imekwisha?”



“Imekwisha na tumeamua kulala huku huku”



“Mganga amesemaje, yale matatizo hayatajirudia?”



“Amenihakikishia kwamba Sofia amepona kabisa”



“Kwa hiyo mtarudi asubuhi?”



“Tutarudi asubuhi”



“Nilikwambia umwamie dereva aende akatafute hoteli ya kulala Morogoro”



“Ameshaondoka, hayuko hapa”



“Huyo mganga ametaka kiasi gani?”





itaendelea
 
SEHEMU YA 23


ILIPOISHIA

“Enhe ameambiwa anaitwa nani?”

“Latifa kama sikosei”

“Sasa aliuawa na nani?”

“Ndiyo haijajulikana”

“Basi ndio hivyo”

“Inaelekea hapo shuleni kwenu kuna matatizo”

“Matatizo kama yapi?’

“Kama wanafunzi wameanza kuanguka chooni na kufa, huoni kama ni matatizo?’

Sofia akanyamaza kimya.

“Baba yako ameshauri tukusimamishe masomo kwa muda mpaka hali itakapokuwa nzuri”

“Una maana hali ya pale shule?”

“Ndiyo”

“Baba ana wasiwasi kuwa naweza kufa?”

“Hatujui lakini inawezekana?”

“Kwani mnahisi ni kitu gani?”

SASA ENDELEA

“Ni kama miujiza tu ambayo haielweki kwa sababu tumeambiwa kwamba huyo mwanafunzi alifyonzwa damu”

“Sawa” Sofia akasema kwa sauti iliyonywea kisha akauliza.

“Kwa hiyo kuanzia kesho sitakwenda shule?”

“Hutakwenda?”

“Inabidi kuwe na taarifa”

“Taarifa itapelekwa”

“Sawa”

Siku iliyofuata Sofia akapelekwa kijijini kwa mama yake. Kwa mara nyingine tena aliendelea kuaguliwa na waganga mbali mbali na kuwekewa ulinzi mkali saa ishirini na nne. Hata baada ya waganga kumuhakikishia mama yake Sofia kuwa matatio ya Sofia yamekwisha, baba yake alitaka aendeleaa kukaa hapo kijijini ili kumtazamia hali yake.

****************

Maria rafiki yake Sofia alikuwa akiishi na kaka yake ambaye ni daktari eneo la sinza jijini Dar. Dk Deo alikuwa akimiliki hospitali yake mwenyewe eneo la Mikocheni ambayo ilikuwa maalum kwa kuunga mifupa iliyovunjika.

Deo alikuwa daktari bingwa wa mifupa ambaye alikuwa amejipatia sifa ndani na nje ya nchi kutokana na uwezo wake wa kuunga mifupa iliyoshindikana kuungika katika hospitali nyingine.

Awali alikuwa daktari wa jeshi, akaamua kuacha kazi na kufungua hospitali yake mwenyewe ambayo ilikuwa ikipokea wagonjwa wa mifupa kutoka mikoani na nje ya nchi.

Ilikuwa na idadi kubwa ya wagonjwa waliotoka Kenya, Uganda,Malawi. Congo DRC, Rwanda na Burundi.

Ilikuwa hospitali kubwa iliyokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa zaidi ya mia tatu. Mbali ya yeye Dk Deo, alikuwa ameajiri madakatari wengine kwa ajili ya kumsaidia kazi pamoja na kutibu magonjwa mengine.

Mke wa Dk Deo alikuwa ameshafariki dunia kwa ajali ya gari miaka kadhaa iliyopita. Hakuwahi kuoa tena na alikuwa akiishi na mdogo wake Maria pamoja na watumishi wawili wa nyumbani kwake.

Kulikuwa na kipindi ambapo Maria aliugua malaria akalazwa katika hospitali ya kaka yake. Wanafunzi wenzake mbali mbali walikuwa wanakwenda kumjulia hali.

Sofia aliporudishwa jijini baada ya kuaguliwa na waganga mbalimbali huko kijijini kwao, alipata habari kuwa Maria alikuwa amelazwa katika hospitali ya kaka yake iliyoko mikocheni.

Alimwambia mama yake na wakapanga kumtembelea pamoja na mheshimiwa Waziri Mkuu.

Ilikuwa siku ya jumapili, mara tu waliporudi nyumbani kutoka kanisani wakapanda gari moja kuelekea Mikocheni. Kwa heshima yake waziri mkuu na kwa cheo chake, alitanguliwa na gari la polisi kwa ajili ya kumuwekea ulinzi.

Gari la Waziri Mkuu lilipofika hospitali ya Dk Deo, Waziri Mkuu, mke wake na Sofia walishuka na kuingia katika lango la hospitali. Walikwenda moja kwa moja katika chumba alichokuwa amelazwa Maria. Muuguzi aliyewapeleka aliwafungulia mlango wakaingia ndani.

Maria alikuwa amelala kitandani akionekana kuwa taabani.

“Maria unajionaje?” Waziri Mkuu akamuuliza Maria.

Maria alikuwa akitazama lakini hakuweza kujibu.

“Hali yake bado si nzuri” muuguzi akamwambia Waziri Mkuu kisha akaongeza.

“Subiri nikamuite dokta ambaye ni kaka yake aje akupe maelezo”

“Nenda katuitie tunakusubiri” Waziri Mkuu alimwambia muuguzi huyo.

Wakati muuguzi anatoka, Sofia akamfuata. Muuguzi huyo alikwenda katika ofisi ya Dk Deo akafungua mlango na kuingia.

Dk Deo hakuwemo.

Wakati muuguzi huyo anageuka ili atoke, Sofia naye akaingia mle ofisini. Macho yake yalikuwa yameshabadilika rangi na kuwa mekundu. Alimshika muuguzi huyo ambaye baada ya kushikwa na sofia alihisi mwili wake ukilegea.

Sofia alifungua mdomo wake na kukita meno yake kwenye shingo ya muuguzi huyo ambaye alifungua mdomo wake ili apige kelele lakini sauti haikutoka.

Sofia baada ya kumpiga meno alianza kumfyonza damu.

Katika chumba alichokuwa amelazwa Maria, dakika ziliendelea kupita. Waziri Mkuu alitazama saa yake na kuona zilikuwa zimeshapita dakika kumi na tano. Ingekuwa ni muuguzi peke yake wanayemsubiri, Waziri Mkuu asingepata wasiwasi lakini Sofia naye alikwenda huko huko.

Amekwenda wapi muda wote huo?

Na amefuata nini?

Waziri Mkuu akatoka. Mke wake naye akamfuata.

Wakati wanatoka, walimuona Dk Deo akitoka katika chumba kilichokuwa jirani na ofisi yake. Wakati huo huo wakamuona Sofia akitoka katika ofisi ya Dk Deo. Walikutana kando ya mlango. Sofia hakuonekana kumjali Dk Deo japokua walikuwa wakifahamiana. Alimpita kama vile hakumuona akaelekea kwenye mlango wa kutokea nje ya jengo hilo.

Dk Deo alisita, akawa anamtazama Sofia kwa nyuma huku uso wake ukionesha mshangao.

Alikuwa kama anajiuliza huyu ni Sofia binti wa Waziri Mkuu au siye. Na amefuata nini ofisini kwangu?

Dk Deo akaingia ofisini kwake. Sofia alikuwa ameuacha wazi mlango wa ofisi yake.

Dk Deo alipoingia ofisini humo alishituka alipomuona muuguzi wake yupo chini akiwa na jeraha linalovuja damu kwenye shingo yake.

Dk Deo alichutama na kumtazama muuguzi wake huyo.

“Mage Mage!” alimuita huku akimshika kichwa.

Mage alikuwa kimya. Macho yake yalikuwa wazi lakini hayakuwa yakiona chochote.

Waziri Mkuu na mke wake walikuwa wameshafika kwenye usawa wa mlango wa ofisi ya Dk Deo. Walimuona Dk Deo akichunguza lile jaraha kwenye shingo ya Mage.

Mara moja walimuona daktari huyo akiinuka kwa kasi. Waziri Mkuu na mke wake walijua kuwa alikuwa anamfuta Sofia aliyekuwa ametoka humo ofisini.

“Dokta unafanya nini?” waziri Mkuu akamuuliza kwa mshituko.

Hapo Ndipo Dk Deo alipoona kuwa kulikuwa na mheshimiwa mbele ya mlango.

“Kuna tatizo limetokea!” akasema kwa taharuki.

“Tatizo gani?”

“Huyu muuguzi wangu sijui amepatwa na tatizo gani. Ameanguka chini na ameshakufa lakini kwenye shingo yake ana jeraha la kung’atwa na meno na linatoa damu”

“Amefanya nini?” Waziri Mkuu akamuuliza kimtego.

“Sijajua ila kuna binti yako, rafiki wa mdogo angu nimemuona ametoka katika ofisi yangu katika hali ambayo si ya kawaida, amenitia wasiwasi sana”

“Unataka useme nini Dokta wakati tumekuona ulichofanya, wewe umemdhuru muuguzi wako halafu unataka kusingizia watu waliotembelea wagonjwa”

“Hapana, Sofia alitoka ofisini mwangu muda huu huu mwenyewe nikiwa sipo”

“Acha uongo! Tumeona kila kitu ulichofanya. Ulikuwa unamfyonza damu muuguzi wako!”

“Mhehimiwa siijafanya hivyo, nimemkuta muuguzi huyu tayari yuko katika hali hii na sijajua amepatwa na nini”

“Tafadhali simama hapo hapo!”

Waziri Mkuu alitoa simu yake ya mkononi akawapigia polisi waliokuwa katika gari la polisi lililokuwa linaongoza gari lake.

“Hebu njooni humu ndani mara moja! aliwambia.

Polisi hao walipofika aliwaaamuru wamkamate Dk Deo.

“Amemdhuru muuguzi wake mbele ya macho yetu, huyu ni dokta hatari kweli kweli”

Polisi hao walimkamata Dk Deo.

“Tokeni naye nje” akawambia kisha akapiga simu tena makao ya polisi.

Alimpigia Mkurugenzi wa Upelelezi akamtaka afike katika hospitali ile iliyokuwa Mikocheni.

“Kuna tukio limetokea”

“Tukio gani mheshimiwa?” Sauti ya Mkurugenzi wa upelelezi ikasikika kwenye simu.



ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 24


ILIPOISHIA



Waziri Mkuu akamueleza kwamba kuna muuguzi ameuawa na daktari wake.

“Sawa mheshimiwa, tunakuja”

Waziri Mkuu alipomaliza kuzungumza na mkurugenzi wa upelelezi alitoka nje ya hospitali hiyo akiwa amefuatana na mke wake.

Walikuta Dk Deo amepakiwa katika gari la polisi huku mmoja wa polisi hao akiwasiliana kwa radio Call na polisi wenzake.

Wasiwasi wa Waziri Mkuu na mke wake ulikuwa kwa Sofia, hawakujua lipotoka katika ofisi ya Dk Deo alikwenda wapi.

Lakini walipokwenda kwenye gari lao walimkuta amejipakia katika siti ya nyuma na alikuwa amelala. Kwenye mdomo wake wa chini alikuwa na chembechembe za damu.

SASA ENDELEA

Mke wa Waziri Mkuu alifungua mlango wa gari akajipakia. Alifungua mkoba wake akatoa kitambaa na kuifuta midomo ya Sofia kisha alikikunja kitambaa hicho na kukirudisha kwenye mkoba.

Waziri Mkuu hakuingia kwenye gari. Alibaki nje ya gari akihaha huku na huku. Baadhi ya wauguzi na madaktari walikuwa wakitoka na kuingia ndani ya hospitali hali iliyoonesha taharuki.

Hakukuwa na yeyote miongoni mwao aliyefahamu nini kimetokea.

Muda usio mrefu, magari matatu ya polisi na makachero yakawasili. Gari la kwanza lilikuwa la mkurugenzi wa Upelelezi. Gari la pili lilikuwa na mchanganyiko wa makachero na polisi na gari la tatu lilitoka kituo kikuu cha polisi baada ya polisi walokuwa wakifuatana na Waziri Mkuu kuwapigia radio call.

Polisi na makachero hao waliokuwa zaidi ya kumi walishuka na kusogea alipokuwa amesimama Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alimueleza Mkurugenzi wa upelelezi kuhusu tukio lililokuwa limetokea akimuhusisha Dk Deo kumshambulia muuguzi wake.

“Polisi wamemkamata, yuko kwenye hili gari” alimwambia huku akimuonesha gari hilo.

Akaongeza. “Muuguzi aliyemfanyia unyama huo yuko ofisini kwake”

Mkurugenzi wa Upelelezi alisogea kwenye gari hilo akamtazama Dk Deo kisha alimwambia atoke kwenye gari. Alipotopka alimwambia.

“Twende ukatuoneshe huyo muuguzi wako”

“Lakini mimi sijamfanyia kitendo chochote kibaya, nilimkuta ofisini kwangfu akiwa ameshajeruhiwa” Dk Deo alijitetea.

“Muongo mkubwa. Nilimuona kwa macho yangu akimpopotoa” Waziri Mkuu alisema.

Mkurugenzi wa Upelelezi akampiga kibao Dk Deo kabla ya kumwambia.

“Twende ukatuoneshe huyo muuguzi wako”

Kabla ya Dk Deo kuinua hatua alitandikwa kibao kingine na kusukumwa. Mkurugenzi wa Upelelezi alikuwa amemshika kiunoni.

Wakati Dk Deo akiwapeleka ofisini kwake, Waziri Mkuu alifuata nyuma.

Walipofika ofisini humo, Waziri Mkuu aliwaonesha yule muuguzi aliyekuwa amelala chini. Ile damu iliyokuwa ikimvuja shingoni sasa ilikuwa imeganda.

“Huyo achukuliwe apelekwe hospitali ya Muhimbili kufanyiwa

uchunguzi” akawambia.

Baada ya polisi kumkagua na kumpiga picha, walimbeba na kutoka naye. Alipakiwa kwenye gari mojawapo la polisi. Dk Deo alipakiwa kwenye gari jingine.

Makachero kadhaa pamoja na polisi walibaki pale hospitali na kuanza kuwahoji madaktari wengine na wauguzi kuhusu kilichokuwa kimempata mwenzao.

Mwili wa muuguzi huyo ulipelekwa hospitali ya Muhimbili. Dk Deo alipelekwa kituo kikuu cha polisi. Waziri Mkuu, mke wake pamoja na Sofia waliondoka na kurudi nyumbani.

Walimuacha Sofia aende akalale chumbani mwake. Waziri Mkuu na mke wake wakakaa sebuleni.

“Kama nisingetumia mbinu ile ya kumsingizia yule dakatari, leo Sofia angebainika kuwa ndiye mfyonza damu na angekamatwa kutokana na ushahidi wa yule dokta” Waziri Mkuu alimwambia mke wake.

“Angekamatwa kwa sababu ingeonekana wazi kuwa ndiye aliyemfyonza damu. Aliondoka naye kule chumbani akangoja alipoingia mle ofisini akamshika…”

“Hili sasa limekuwa balaa!”

Mke wa Waziri Mkuu akatikisa kichwa.

“Sijui kama mwanangu atarejea katika hali yake ya kawaida!” alisema na kuongeza.

“Juhudi kubwa zimefanyika lakini bado hali inatia mashaka, sijui tufanye nini?’

“Sijui mke wangu, nimechanganyikiwa! Yaani nimelazimika kuokoa jahazi kwa kumbambikia yule daktari kosa la Sofia”

“Kwani atashitakiwa?’

“Lazima ashitakiwe kwa mauaji, najua tutapambana sana mahakamani lakini nitatumia kila mbinu kuhakikisha haepuki ile tuhuma”

“Sasa Sofia tutampeleka wapi?”

“Tutamrudisha kijijini akae huko huko chini ya uangalizi. Tutakodi watu wa kuwa naye wakati wote kuhakikisha hafyonzi watu. Ile damu inaweza kumuua. Damu nyingine si salama”

Ili kumkandamiza zaidi Dk Deo, Waziri Mkuu alimpigia simu Waziri wa Mambo ya Ndani akamueleza kuhusu lile tukio akidai alimshuhudia kwa macho yake Dk Deo akimfyonza damu muuguzi wake hadi kumuua.

Baada ya kumpigia Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri Mkuu alimpigia Mkuu wa Jeshi la Polisi.

“Nimeshapata taarifa mheshimiwa na hivi sasa tunalifanyia uchunguzi tukio hilo” Mkuu wa Jeshi la Polisi alimwambia Waziri Mkuu mara tu alipomdokeza kuhusu tukio hilo.

“Kama mmeanza kufanya uchunguzi ni vizuri. Yule mtu ni katili sana”

“Kumekuwa na matukio ya ufyonzwaji damu hapa nchini, tutachunguza kuona kama ni yeye aliyehusika”

“Itakuwa ni yeye, wasomi wengine wanafanya kazi zao kwa kutegemea ushirikina”

“Hilo suala tunalifanyia kazi mheshimiwa”

“Tunataka haki itendeke na mhakikishe kwamba anapelekwa mahakamani mara tu uchunguzi wenu ukikamilika”

“Asante mheshimiwa”

Wakati huo hospitali ya Dk Deo ilikuwa imezingirwa na makachero na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi. Mwili wa muuguzi aliyefyonzwa damu na Sofia ulifanyiwa uchunguzi haraka haraka katika hospitali ya Muhimbili na matokeo ya uchunguzi huo yalitolewa kwa polisi.

Uchunguzi huo mbali ya kuthibitisha kifo cha muuguzi huyo ulieleza kuwa kifo hicho kilitokana na marehemu kufyonzwa damu nyingi mwilini mwake kupitia katika jereha lililokuwa kwenye shingo yake ambalo lilitokana na kuumwa meno ya binaadamu.

Taarifa hiyo ya madaktari ndio iliowapa polisi taharuki. Ile dhana kwamba Dk Deo ndiye mfyonza damu za binaadamu iliwafanya polisi wamng’ng’anie kama ruba.

Mbali ya hospitali yake kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi, makachero walianza kuwahoji madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo.

Madaktari na wauguzi wote waliohojiwa walieleza kuwa hawakuliona tukio hilo linalodaiwa kufanywa na Dk Deo.

Pia walieleza kwamba hawaamini kuwa Dk Deo anafyonza watu damu.

Baada ya kutoridhishwa na maelezo ya madaktari na wauguzi hao, makachero walianza kuwahoji wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo.

Wagonjwa hao pia hawakuwa na maelezo ya kuwatosheleza polisi kuhusiana na tuhuma zilizokuwa zinamkabili Dk Deo. Mkurugenzi wa Upelelezi akaja na dhana nyingine. Aliwataka makachero hao kuifanyia upekuzi hospitali hiyo kwa hofu kwamba Dk Deo anaweza kuwa ananunua viungo vya binaadamu ambavyo anavitumia katika shughuli zake za kishirikina.

Upekuzi huo ulifanywa lakini hakukuwa na kiungo chochote kilichopatikana.

Dk Deo mwenyewe alihojiwa kwa saa kadhaa. Alichokuwa akikieleza kilikuwa hakikubaliwi na polisi ambao tayari walishajenga hisia kwamba Dk Deo ni mfyonza damu.

Dk Deo alieleza kwamba wakati tukio hilo linatokea hakuwepo ofisini. Lakini wakati anarudi ofisini mwake alimuona Sofia binti wa Waziri Mkuu akitoka ofisini mwake.

“Nilipoingia ofisini mwangu nikamuona muuguzi wangu akiwa chini huku akitokwa na damu shingoni. Nilipomchunguza vizuri nikagundua kuwa alikuwa na jeraha ambalo sikuweza kujua ni la kitu gani.

“Nikaondoka pale pale kumfuata yule msichana aliyetoka mle ofisini ili nimuulize nini kilitokea ndio hapo nilipomuona Waziri Mkuu na mke wake wamesimama mbele ya mlango wakinitazama. Waziri Mkuu akaanza kunishutumu kuwa nimemfyonza damu muuguzi wangu jambo ambalo si kweli”

“Sofia binti wa Waziri Mkuu alikuwa amefuata nini ofisini kwako?” Thabit kembo, mmoja wa makachero waliokuwa wakimhoji Dk Deo alimuuliza.

“Sijui”

“Je wewe ulikutana na Waziri Mkuu alipofika hospitalini kwako?’

“Sikukutana naye na wala sikuwa na taarifa kuwa waziri Mkuu anakuja hospitalini kwangu”

“Baada ya Waziri Mkuu kukwambia kwamba amekuona umemfyonza damu muuguzi wako, alichukua hatua gani?’

“Aliita polisi wanikamate na hakunipa nafasi ya kujitetea”



ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 26

ILIPOISHIA

Sofia akatikisa kichwa kusikitika.

Pakapita ukimya wa sekunde kadhaa.

“Sasa wewe nenda zako kajisomee. Hao polisi wakifika utaitwa”

“Sawa baba. Watakuja muda huu?’

“Muda wowote kutoka sasa”

“Haya, mimi nakwenda”

Sofia akanyanyuka na kuondoka. Akili yake ilikuwa imeshachanganyikiwa. Tangu alipoanza kufyonza watu alikuwa akisikia harufu ya damu midomoni mwake mara tu anaporejewa na akili yake.

Alipomfyonza mpishi wa nyumbani kwao alisikia harufu ya damu midomoni mwake. Alipomfyonza dada yake alisikia harufu ya damu midomoni mwake. Alipomfyonza mwanafunzi mwenzake alisikia harufu ya damu midomoni mwake na alipomfyoza muuguzi wa hospitali ya Dk Deo pia alisikia harufu ya damu.

SASA ENDELEA

Ingawa hakuwa na kumbukumbu zozote kichwani mwake za kumfyonza mtu damu lakini hali ile ilimpa maswali mengi.

Alikuwa akijiuliza kwanini linapotokea tukio kama lile, yeye anasikia harufu ya damu midomoni mwake?

Mawazo yake yalikwenda mbali zaidi, akajiuliza ni kwanini alikatizwa masomo baada ya tukio la kufyonzwa damu kwa mwanafunzi mwenzake? Kwanini alipelekwa kijijini na kuaguliwa? Kwanini wakati fulani alipelekwa Nairobi kupimwa akili yake?

Maswali yote hayo yalipitita akilini mwa Sofia bila kuwa na majibu.

Akaingia chumbani mwake na kuendelea kujisomea.

Baada ya saa moja makachero wawili wakawasili nyumbani kwa Waziri Mkuu.

Kachero Kembo na Inspekta Alex walikaribishwa sebuleni kwa Waziri Mkuu.

Wakaeleza dhumuni lao kuwa ni kupata maelezo kutoka kwa Waziri Mkuu, mke wake na mwanawe kuhusiana na tukio lililotokea katika hospitali ya Dk Deo, asubuhi ya siku ile.

Waziri Mkuu akawafahamisha kuwa walikuwa tayari kutoa maelezo.

Thabit Kembo alifungua jalada alilokuwa nalo mikononi akaandika tarehe ya siku ile kisha akaandika jina la Waziri Mkuu.

“Mheshimiwa tutaanza na wewe” kembo akamwambia baada ya kuandika.

“”Anza”

“Tunaomba utueleze nini kilitokea katika hospitali ya Dk Deo leo asubuhi”

“Sisi tulifika pale hospitali kumjulia hali rafiki wa mwanangu na mwanafunzi mwenzake ambaye anaumwa”

“Mwanao huyo anaitwa nani?” Kembo akamuuliza.

“Anaitwa Sofia”

“Na huyo mgonjwa mliyekwenda kumjulia hali ni nani?”

“Anaitwa Maria, ni mdogo wake Dk Deo”

“Dk Deo huyu ambaye amehusika na hili tukio?”

“Ndio”

“Endelea”

“Nataka uelewe kwamba tulikwenda pale kama raia wa kawaida kumjulia hali mgonjwa”

“Ndiyo”

Waziri Mkuu akaendelea kueleza jinsi walivyomuona mgonjwa huyo wakiongozwa na muuguzi mmoja wa hospitali hiyo ambaye hakuwa akimfahamu jina lake.

Akaendelea kueleza baada ya kumuona mgonjwa walihitaji kupata maelezo kutoka kwa daktari anayemtibu kwa vile mgonjwa mwenyewe bado hakuwa na hali nzuri na hakuweza kutoa maelezo.

“Muuguzi tuliyekuwa naye alitoka mle chumbani kwenda kumuita daktari lakini alichelea sana kurudi kiasi kwamba tuliamua kutoka kumfuata” Waziri Mkuu aliendelea kueleza.

“Wakati huo mlikuwa watu wanagapi?’

“Nilikuwa mimi, mke wangu na mwanangu Sofia”

“Endelea kueleza, baada ya kutoka nini kilitokea?”

“Tulipofika katika mlango wa ofisi ya Dk Deo, tuliukuta mlango ukiwa wazi. Tukamuona Dk Deo akiwa ndani ya ofisi yake amemshikilia yule muuguzi huku meno yake yakiwa kwenye shingo ya muuguzi huyo na pale shingoni palikuwa panatoka damu” Waziri Mkuu alieleza.

“Ulihisi alikuwa anamfanya nini?”

“Nilihisi kama alikuwa anamfyonza damu”

“Baada ya hapo nini kilitokea?’

“Yule muuguzi alianguka chini, ndipo nilipomuuliza Dk Deo unafanya nini? Akaanza kubabaika. Hakujua kuwa kulikuwa na watu wanamuona?”

“Baada ya kumuuliza hivyo na kubabaika, ulichukua hatua gani?’

“Nilipiga simu polisi, polisi wakafika na kumchukua”

Kembo alimaliza kuandika maelezo ya Waziri Mkuu kisha alimwambia.

“Dk Deo baada ya kuhojiwa alitupa maelezo tofauti”

“Aliwambia uongo gani?” Waziri Mkuu akamuuliza huku macho yake yakimeta kwa taharuki.

“Alitueleza kwamba, yeye hakuwako ofisini kwake lakini wakati anarudi ofisini kwake alimkuta Sofia akitoka mle ofisini…”

“Huo ni uongo mtupu, Sofia tulikuwa naye sisi” Waziri Mkuu akadakia.

“Alitueleza kwamba licha ya kwamba yeye na Sofia walikua wanajuana lakini Sofia hakumsemesha chochote, alimpita kama vile alikuwa hamjui. Alipoingia ofisini kwake ndipo alipomkuta yule muuguzi amelala chini huku damu ikitoka kwenye shingo yake…”

“Yule dakatari ni muongo sana tena hafai kabisa. Sisi tumemuona waziwazi akifanya unyama wake halafu anamsingizia mwanangu! Mwanangu alifuata nini ofisini kwake wakati tulikuwa naye sisi?” Waziri Mkuu alifoka.

“Sawa. Tutachukua pia maelezo kutoka kwa Sofia lakini kabla ya yeye ni vizuri pia tupate maelezo ya mama yake kwa vile alikuwepo katika tukio”

“Sawa”

Kembo akamgeukia mke wa waziri Mkuu.

“Tupe maelezo yako, nini ulikishuhudia hapo hospitali asubuhi”

Mke wa Waziri mkuu alieleza kama alivyoeleza mume wake. Kembo baada ya kumaliza kuandika alitaka aitwe Sofia.

Mama yake ndiye aliyekwenda kumuita. Alimkuta Sofia amepitiwa na usingizi. Akamuamsha na kumwambia kuwa maafisa wa upelelkezi wameshafika kuchukua maelezo ya tukio lililotokea katika hospitali ya Dk Deo.

“Haya mama nakuja” sofia akamwambia.

Mke wa Waziri Mkuu aliporudi sebuleni Sofia alikuwa nyuma yake.

“Kaa kwenye kochi” Waziri Mkuu alimwambia.

Sofia akakaa.

“Hujambo?” Kembo akamsalimia.

“Sijambo, habari ya kazi?’

“Nzuri, za masomo?’

“Pia ni nzuri”

“Sawa. Sisi ni maafisa wa idara ya polisi ya upelelezi. Tunahitaji maelezo yako kuhusiana na tukio lililotokea leo asubuhi kwenye hospitali ya Dk Deo. Uko tayari kutueleza nini kilitokea?’

“Niko tayari”

“Sawa, anza kutueleza”

“Kuna rafiki yangu ambaye amelazwa pale hospitali akiugua malaria. Leo asubuhi tulikwenda kumsalimia…”

“Mlikwenda nani na nani?’

“Mimi, baba na mama”

“Mlipofika mlimuona huyo mgonjwa?”

“Ndio tulimuona”

“Alikuwa na hali gani?”

“Kwa kweli hali yake haikuwa nzuri, alikuwa hawezi hata kuzungumza”

“Endelea kueleza”

“Yule muuguzi aliyetupeleka alikwenda kumuita daktari ili atupe maelezo kuhusu mgonjwa”

“Ndiyo”

Hapo Sofia alisita akawa anafikiria alivyofundishwa na baba yake.

Kitendo hicho kilimuudhi Waziri Mkuu akamkazia macho Sofia.

“Eleza kilichotokea baada ya hapo” akamwambia.

“Ndio naeleza baba. Yule muuguzi hakurudi tena” Sofia akasema huku akiendelea kufikiri.

“Mlichukua hatua gani?” Kembo akamuuliza.

“Na sisi tukatoka kumfuata daktari”

“Mlimfuata wapi?”

“Ofisini kwake”

“Je mlimkuta?”



ITAENDELEA
 
Ushirikina ni mbaya sana...

Na ni kazi sana kuficha siri kwa muda mrefu ambayo ipo na inatokea ndani kwako...

Soon Sofia mtoto wa waziri mkuu atajulikana...


Cc: mahondaw
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom