Hadithi: Jini Mweusi

SEHEMU YA 68

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Aliamua kukimbia kupitia Mlandizi, huko, akapitia misukosuko mingi na mwisho wa siku akajikuta kwenye kijiji kimoja ambapo baada ya wanakijiji kumuona, wakaanza kujificha. Huku akijiuliza nini kinaendelea, akatokea kijana aliyekuwa na picha yake mkononi, Dickson akashtuka.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Umefikia wapi?” ilisikika sauti ya kamanda IGP Mayala.
“Bado, ila nimefanikiwa kupita alipopita, naona hivi karibuni nitampata,” alisema Fredrick.
“Basi sawa. Hakikisha anapatikana, huku mambo yapo ovyo na wananchi wamecharuka sana,” alisikika IGP.
“Sawa mkuu!”

Mpelelezi Fredrick alikuwa akizungumza na IGP Mayala katika simu. Zilipita siku kadhaa hakuwa amemtafuta kumwambia ni kitu gani kilikuwa kimeendelea tangu alipoanza safari ya kumtafuta Dickson ambaye alikuwa akichanja mbuga kuelekea jijini Mwanza kwa kupitia pori kwa pori.

Kuna kipindi aliwaona wanyama wakali kama simba, ngiri na wanyama wengine, akapanda juu ya mti na kutulia na hali ilipokuwa shwari, akateremka na kusonga mbele. Alitembea mpaka alipofika katika mto mmoja, ulikuwa mkubwa na hakukuwa na sehemu ya kuvukia hivyo alichokifanya ni kusubiri kwanza. “Au nipige mbizi?” alijiuliza.


Alikuwa amesubiri hapo kwa zaidi ya dakika arobaini na tano, hakukuwa na mtu yeyote aliyetokea na mtumbwi na kitu alichokifikiria ni kuingia ndani ya mto huo na kupiga mbizi kuelekea upande wa pili. Alipotaka kufanya hivyo, moyo wake ulikuwa mzito mno, hakuelewa ni kwa sababu gani lakini aliutii sana moyo wake kuliko maamuzi yake, hivyo akataka kusubiri zaidi.

Hiyo ilikuwa ni saa mbili asubuhi lakini mpaka inafika saa nne, hakukuwa na mtu yeyote aliyejitokeza mahali hapo kitu kilichomfanya kuanza kujiandaa kuuvuka mto huo kwa kupiga mbizi mpaka upande wa pili.
“We kijana unafanya nini hapo?” ilisikika sauti kutoka kwa mwanaume mmoja aliyesimama nyuma yake, alipogeuka, macho yake yakatua kwa mzee mmoja aliyekuwa na ndevu nyingi, mkononi alishika panga.
“Nataka kwenda upande wa pili.”
“Kwa kuogelea?”
“Ndiyo!”
“Una hatari sana kijana, wewe ni mgeni mahali hapa? Hujui hatari juu ya huu mto? Hujaambiwa kwamba jana tu mamba wameua familia nzima huku mtoni?” aliuliza mzee huyo, Dickson akashtuka.
“Unasemaje?”
“Hebu sogea huku, hata hapo uliposimama, kuna hatari kubwa,” alisema mzee huyo, Dickson akamsogelea.
Hapo ndipo mzee yule akamwambia Jackson kuhusu mto huo, ulikuwa ni hatari sana, ulimaliza watu wengi kijijini hapo kutokana na mamba waliokuwa humo ndani. Jackson alipoambiwa hivyo, moyo wake ulisisimka, kijasho chembamba kikamtoka na hapo ndipo alipokumbuka kwamba moyo wake haukupenda kabisa kuvuka kwa kuogelea.
“Unakwenda wapi?” aliuliza mzee huyo.
“Nataka niende mbele zaidi, kuna sehemu nakwenda,” alijibu.
“Basi sawa. Kama unataka kuvuka, nitakusaidia, sina mtumbwi ila nitakupa dawa, utajipaka kisha kuvuka bila tatizo lolote,” alisema mzee huyo.
“Mmh!”
“Unaamini katika dawa za asili?”
“Siamini, ila kama unataka kuniaminisha, hakuna tatizo,” alijibu Dickson, hapohapo mzee huyo akamchukua na kuondoka naye kwenda nyumbani kwake, huko, akachukua dawa fulani na kumpaka mwili mzima na kumwambia aende akauvuke mto ule kwa kupiga mbizi.
Kwanza hakuamini, ila kwa sababu aliambiwa tena kwa kutolewa mifano ya watu waliowahi kuuvuka mto huo baada ya kujipaka dawa hiyo, hakuwa na jinsi, akakubaliana naye, alipofika mtoni, akaanza kuingia taratibu. Alipopiga macho pembeni, akagundua kulikuwa na mamba waliokuwa pembezoni mwa mto wakimtazama, alipoingia mtoni tu, nao mamba wakaingia pamoja naye.
* * *
Dickson alitulia, alijisogeza pembeni kidogo na kumwangalia mtu aliyekuwa amemnyooshea bunduki ile, alikuwa mzee wa makamo ambaye kwa kumtazama tu alionekana kuwa miongoni mwa watu wenye roho mbaya, mmoja wa watu waliopitia mafunzo ya kijeshi.
Dickson akamuomba mzee huyo asimpige risasi kwani hakuwa mtu mbaya, alifika hapo porini kwa sababu alikuwa na matatizo makubwa hivyo alihitaji msaada wake. Mzee yule akamwangalia vizuri Dickson, hakukubaliana na maneno yake, alivyomwangalia vizuri, jinsi sura yake ilivyokuwa mbaya, akapata uhakika kwamba mtu huyo hakuwa mtu mzuri hata kidogo, alikuwa miongoni mwa majambazi waliokuwa wakiitetemesha nchi kwa kuteka mabasi. Akamsogelea.

“Nyie ndiyo mliomuua mke wangu! Lazima nilipe kisasi na nitawatafuta wenzako wote,” alisema mzee yule, tayari alikigusa kitufe cha kuruhusu risasi itoke katika bunduki hiyo na kumuua Dickson ambaye jasho lilikuwa likimtoka tu.
“Mimi siyo mtu mbaya mzee wangu, naomba unisaidie, nimetoka kukimbizwa na Savimbi, walitaka kuniua pia,” alisema Dickson huku akitetemeka pale chini alipokuwa.
Mzee huyo aliposikia jina la Savimbi, akatulia kwanza, huyo ndiye mtu aliyekuwa akimtafuta kwa udi na uvumba na ndiye aliyemuua mke wake, akajikuta akishusha mkono uliokuwa na bunduki na kumkazia macho Dickson.
“Savimbi yupo wapi?” aliuliza huku akionekana kuwa na hasira.
“Yupo humuhumu porini, wamenikimbiza, walitaka kuniua,” alijibu Dickson.

Hiyo ndiyo ilikuwa salama yake. Mzee huyo akaiweka bunduki yake vizuri kisha kumuinua Dickson mahali pale na kuondoka naye. Huko, alimwambia wazi kile kilichokuwa kimetokea mpaka kuanza kumtafuta huyo Savimbi.
Alisema kwamba mkewe aliuawa na mtu huyo alipokuwa akitoka Mara kwenda Dakawa, mkoani Morogoro. Njiani basi lao lilitekwa na majambazi saba waliokuwa na silaha nzito waliowalazimisha abiria wafanye ngono wao kwa wao, waliokataa waliwamininia risasi na kuwaua kama wanyama bila huruma.

“Mke wangu alikataa, hivyo wakamuua,” alisema mzee huyo.
Wakati mzee huyo akizungumza, alionekana kuwa na hasira dhidi ya majambazi hayo.
“Pole sana…”
“Ahsante! Wewe ni nani na unakwenda wapi?” aliuliza mzee huyo.
“Naitwa Fabian, naelekea Mwanza kwa miguu!”
“Mwanza kwa miguu?”
“Ndiyo!” alijibu Dickson, mzee huyo akabaki akiwa na mshangao na kujiuliza kwa nini asitumie usafiri na kuamua kuhatarisha maisha yake kwa kupita porini kulikowa na hatari nyingi!

Je, Dickson atasalimika kutoka mikononi mwa mzee huyo?
 
SEHEMU YA 69

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Aliamua kukimbia kupitia Mlandizi, huko, akapitia misukosuko mingi na mwisho wa siku akajikuta amefika kwa mzee ambaye anamwambia kwamba angemsaidia kufika Mwanza Mjini ila si kwa miguu kama aliyotaka yeye.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Mzee yule aliyeitwa Saidi akashangaa, hakuamini alichokisikia kwamba kijana huyo, Dickson alikuwa njiani kuelekea Mwanza, tena kwa miguu. Alimwangalia mara mbilimbili, hakuamini, alimuonea huruma kwani kutoka hapo Dakawa, Morogoro mpaka Mwanza ilikuwa mbali mno. Njia nzima ya kwenda Mwanza haikuwa salama, hapo walikuwa Dakawa ambapo ilikuwa ndani ya Mbuga ya Wanyama ya Mikumi, hivyo kutoka hapo na kusonga mbele ingekuwa safari ndefu ambayo ingehatarisha maisha yake.

Hakuwa na jinsi, alifikiri kwamba mtu huyo hakuwa na nauli ya kupanda basi, alitaka kumsaidia kiasi fulani cha nauli lakini hakuona kama kuna haja ya kufanya hivyo kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa na usafiri wake, Land Rover Defenders iliyochoka, hivyo kwa kutumia usafiri huo, alitegemea kumfikisha salama mpaka Morogoro Mjini.
“Nitakusaidia kufika Morogoro Mjini,” alisema mzee Saidi.
“Kivipi?”
“Nina usafiri wangu, wala usijali kuhusu hilo,” alisema mzee huyo.
“Hapana! Acha tu niendelee na safari, natumaini nitafika salama,” alisema Dickson.
“Hapana! Njia hii ni hatari sana, kuna wanyama wakali, kuna watu wengi walishawahi kuliwa na simba, chui, sipendi wewe ukutane nao, naomba nikusaidie, hata kama huna nauli, nitakupa mimi,” alisema mzee Saidi, alimuonea huruma Dickson, maisha yake yalikuwa porini tu, hata kumfahamu, hakumfahamu.

Hakutaka kumuona Dickson akiondoka kwa miguu kuelekea Mwanza, alijua hatari iliyokuwepo njiani, kulikuwa na watu wengi walikuwa wakiuawa, kulikuwa na wanyama wakali, hata wafanyakazi wa mbugani nao hawakutaka kabisa kutembea mbugani pasipo gari, walijua hatari iliyokuwepo. Baada ya kumbembeleza sana Dickson, hatimaye akakubaliana naye kwamba wapande gari lake na kuelekea Morogoro Mjini ambapo huko angechukua basi na kuelekea Mwanza. Hakukuwa na muda wa kupoteza, walichokifanya ni kuingia ndani ya gari hilo na moja kwa moja safari kuanza. Njiani, walikuwa wakizungumza mambo mengi, kwa Dickson, japokuwa alijitahidi sana kuuweka uso wake kuwa kwenye tabasamu pana lakini bado hakuwa na amani kabisa.

Morogoro Mjini palikuwa kama Dar es Salaam, kulikuwa na magazeti mengi, mitaani watu walijaa na huko pia picha zake zilibandikwa kila kona kwamba alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba, awe hai au amekufa, bado alihitajika.
Kutoka hapo Dakawa mpaka Morogoro Mjini walitumia saa kadhaa ndipo wakafika ambapo kitu cha kwanza kabisa, Dickson akahitaji kofia kubwa ya Marlboro kwa kisingizio cha kuwa na tatizo kichwani mwake ambapo kama angepigwa sana na jua basi damu zingemtoka puani.

“Nina tatizo la kutoka damu puani, ngoja ninunue kofia,” alisema Dickson, alikuwa akimwambia mzee Saidi. Hilo halikuwa tatizo, kofia ikanunuliwa na kupewa. Kidogo akawa na amani, aliishusha kiasi kwamba sura yake haikuwa ikionekana vizuri. Kabla ya kwenda Msamvu, wakapitia katika mgahawa mmoja kwa ajili ya kupata chakula cha mchana kabla ya Dickson kuanza safari ya kwenda Dodoma na kuunganisha mpaka Mwanza.

“Hivi huko Mwanza unakwenda kufanya nini?” aliuliza mzee Saidi.
“Nani? Mimi?” aliuliza Dickson japokuwa alilisika sana swali hilo.
“Ndiyo!”
“Nakwenda kuishi huko. Nilikuja Dar mwaka juzi, lengo kubwa lilikuwa ni kutafuta maisha lakini mambo yamekuwa magumu sana, Dar hakuna maisha kama nilivyokuwa nikifikiria kabla, nilidhani kwamba kama ningepata maisha mazuri ndani ya miezi michache lakini hakuna kitu. Sasa si bora nirudi nyumbani nikavue sato na sangara tu,” alisema Dickson.

“Daah! Pole sana. Umechukua uamuzi mzuri sana, kama vijana wengine wangekuwa na uamuzi kama huo, ingekuwa safi sana. Ngoja nikwambie kitu Fabian, vijana wengi wamekuwa hawajiamini, wanahisi kwamba wakienda mjini ndipo watapata maisha mazuri, hakuna kitu kama hicho, wangapi wapo mjini na hawana maisha mazuri? Wapo, tena wengi tu. Nyie kama vijana inabidi mtumie fursa ambazo zipo kila kona, hata vijijini, kote kuna fursa,” alisema mzee Saidi.

Wakati wanazungumza hayo, watu walikuwa wakiingia na kutoka katika mgahawa huo, muda mwingi Dickson alikuwa mtu wa kuangalia chini tu, hakutaka kugundulika kwani kama watu wangejua kuwa alikuwa yeye angekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Dakika ziliendelea kwenda mbele, wateja waliendelea kumiminika ndani ya mgahawa huo. Dickson akaanza kukosa amani, kitendo cha wateja wengi kujaa humo ndani kilimfanya kuona angekamatwa muda wowote ule. Alichokifanya ni kula haraka ili arudi garini.

“Unakwenda wapi?” aliuliza mzee Saidi mara baada ya kumuona Dickson akiwa amesimama.
“Garini! Nimeshamaliza kula.”
“Sawa! Nenda, nitakuja, ngoja nimalize kula,” alisema mzee Saidi aliyekuwa akila taratibu sana.
Dickson akaondoka ndani ya mgahawa ule na kurudi garini. Alipokuwa akitembea, muda wote macho yake yalikuwa chini kama mtu aliyekuwa akitafuta kitu fulani, picha zake zilisambazwa kila kona, alipoziona, moyo wake ukapiga paaa! Sehemu hiyo haikuwa salama katika maisha yake hata mara moja, alipofika ndani ya gari, akatulia.
Huku nyuma, mzee Saidi aliendelea kula, hakuwa na wasiwasi wowote ule, alichokijua ni kwamba mtu aliyekuwa amemsaidia alikuwa mwema ambaye kwa namna moja au nyingine alihitaji msaada wake.

Alipomaliza, akamuita mhudumu kisha kumlipa. Wakati alipokuwa akitoka, macho yake yakatua katika picha moja iliyobandikwa mlangoni, alitaka kuipita pasipo kuiangalia lakini kitu cha ajabu kabisa kilichotokea, akajikuta akivutiwa kuiangalia picha ile. Alichokiona, hakuamini.

Ilikuwa ni picha ya Dickson, mwanaume aliyekuwa akitafutwa baada ya kufanya mauaji jijini Dar es Salaam, mwanaume aliyekuwa amewaua wanawake wengi na wengine kuwazika, mzee Saidi hakuamini, akasogea karibu kuiangalia picha ile, kweli alikuwa Dickson, mwanaume yuleyule aliyemwambia atangulie garini.

“Kumbe ni muuaji! Milioni ishirini kwa atakayefanikisha kupatikana, haiwezekani, siamini macho yangu,” alisema mzee Saidi, hakuamini, kiasi kilichokuwa kimewekwa kilikuwa kikubwa mno, alikitaka sana hivyo hata kumkamata Dickson hakukuwa na tatizo lolote lile.

Akaondoka hapo mgahawani na kuwahi kule garini, alitaka atakapofika, amdhibiti na kama akishindwa basi apige kelele, wananchi wakusanyike na hatimaye kumkamata. Wakati akielekea kule alipoegesha gari lake, alijiona kama anachelewa kufika, alitamani apate mbawa apae kwani furaha aliyokuwa nayo moyoni, haikuelezeka.
“Amekwisha…” alijisemea mzee Saidi. Tayari mbele yake akajiona kuwa na mamilioni katika akaunti yake benki.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 70

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.
Aliamua kukimbia kupitia Mlandizi, huko, akapitia misukosuko mingi na mwisho wa siku akajikuta amefika kwa mzee ambaye anamwambia kwamba angemsaidia kufika Mwanza Mjini ila si kwa miguu kama aliyotaka yeye.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Dickson hakuwa na amani kabisa, kila alivyokaa ndani ya gari lile, mwili ulimsisimka, alikuwa na hofu moyoni mwake kana kwamba pale alipokuwa hakukuwa salama hata mara moja. Alibaki akiangalia huku na kule, alihisi labda kulikuwa na mtu aliyekuwa amemuona na kumgundua, ila kila alipopitisha macho yake, kila mtu alikuwa bize na mambo yake.
Hakujua sababu iliyomfanya kuwa na hofu namna ile, alijitahidi kuuletea moyo wake amani lakini haikuja kabisa. Akahisi lazima kungekuwa na kitu, hisia zake zilikuwa na maana kubwa mno, alichokifanya ni kutoka kwanza ndani ya gari.

“Ni lazima niondoke, haiwezekani hali kuwa hivi,” alisema huku akiteremka kutoka garini.
Wakati akiwa amesimama nje ya gari lile na kuangalia upande wa pili kutoka katika mgahawa ule uliokuwa kama hatua thelathini kutoka gari lilipokuwa limeegeshwa, akamuona mzee Saidi akija kule alipokuwa huku uso wake ukionesha furaha ya ajabu.

Hakutaka kujiuliza ni kitu gani kilitokea, alijua fika kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilimfanya mzee huyo kuwa katika hali hiyo, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo, tena kwa mwendo wa haraka na kwenda kujificha sehemu, katika moja ya magari yaliyokuwa yameegeshwa mahali hapo.

Macho yake yalikuwa yakimwangalia mzee Saidi kule ndani ya gari alipokuwa. Kwa muonekano tu, mzee huyo alionekana kuchanganyikiwa, kitendo cha kumkosa Dickson ndani ya gari lile kilimchanganya mno, hakuamini kama kweli furaha aliyokuwa nayo ilikuwa ikienda kupotea kirahisi namna ile, hakukubali, akateremka na kuanza kumwangalia huku na kule, japo amuone na kuanza kumuitia mwizi na watu wamkamate, hakufanikiwa kumkamata kwani naye Dickson baada ya kuona hivyo, akaondoka zake.

Safari hiyo ilikuwa ni kwenda Msamvu, ilikuwa ni lazima aondoke mahali hapo, safari aliyoifikiria ni kwenda Dodoma kabla ya kuunganisha mpaka Singida, Tabora na kuanza mchakato wa kwenda jijini Mwanza.

Njiani, japokuwa watu walikuwa na hamu naye huku picha zake zikiwa zimebandikwa kila kona lakini hakukuwa na mtu aliyejua kwamba mwanaume waliyekuwa wakipishana naye alikuwa ni Dickson, waliendelea na mambo yao huku wakiwa hawana habari kabisa.
“Nataka kufika Dodoma…” alimwambia utingo mmoja, kofia na miwani vilikuwa kichwani na machoni mwake.
“Elfu saba…”
“Hakuna tatizo,” aliposema hivyo, akatoa hela, akalipia kisha kuingia ndani ya basi huku uso wake ukiwa chini. Akakifuata kiti alichoambiwa na kutulia hapo.

Wakati akiwa anafikiria maisha yake ya nyuma, ghafla macho yake yakatua kwa vijana wawili, walikuwa wakiongozana na polisi wawili waliokuwa na bunduki, walikuwa wakiwapa maelekezo yaliyompa wasiwasi.

Vijana wale wakalinyooshea vidole basi lile kisha kuanza kulifuata na polisi waliokuwa na bunduki mikononi mwao. Dickson alibaki akitetemeka, kitu kilichomjia kichwani kwa haraka zaidi ni kwamba vijana hao walimuona ndiyo maana waliwaita polisi hao kisha kuingia ndani ya basi hilo, abiria wote wakashtuka.
“Yupo wapi?” aliuliza polisi mmoja.

“Yupo kule, nimemuona kwa macho yangu,” alijibu kijana mmoja na kuanza kuelekea alipokuwa Dickson, polisi wale wakaandaa bunduki zao. Dickson akatamani kuruka kupitia dirishani, tatizo aliloliona madirisha ya basi hilo yalikuwa madogo hata kupenya kwa haraka, asingeweza.

* * * *
Japokuwa alikuwa mpelelezi lakini kwenye suala la mamba, alikuwa na hofu kupita kawaida, aliwaona mamba wale wakiingia mtoni pamoja naye na kuhisi kwamba wangeweza kumng’ata kama walivyofanya kwa wengine, alitamani kurudi lakini kila alipotaka kufanya hivyo, mzee yule akamwambia kwamba ni lazima asonge mbele.

Hakuwa na budi zaidi ya kuiamini dawa aliyopakwa na yule mzee, akaendelea kwenda mbele zaidi, alihisi kabisa akitembea pamoja na mamba hao waliokuwa chini lakini hakutakiwa kusimama, baada ya dakika tano kutembea mtoni, akafanikiwa kufika ng’ambo ya pili, alipoyapeleka macho kwa yule mzee, akamuonesha ishara ya dole gumba.

Hakutaka kubaki hapo, alikuwa na safari kubwa, alimtafuta Dickson ambaye aliambiwa kwamba alikuwa safarini kuelekea Mwanza hivyo ilikuwa ni lazima asonge mbele ili mwisho wa siku ampate mtu huyo ambapo moyo wake ulimfariji na kumwambia kuwa hakuwa mbali kutoka alipokuwa.

Safari ilikuwa ndefu, hakutaka kusimama, aliendelea mbele mpaka alipofika katika Mbuga ya Wanyama ya Mikumi, huko hakukuwa salama kwa maisha yake lakini hiyo haikumfanya kusimama.

Alikuwa na bastola mbili alizoziweka vizuri, moja kiunoni na nyingine mguuni mwake tena huku akiwa ameificha na suruali. Aliendelea mbele mpaka alipokutana na kundi kubwa la wanyama, walikuwa nyumbu na baadhi ya wanyama wengine kama pundamilia, tembo na wengine wanaokula majani.

Hakutaka kupita karibu nao, alikwenda kwa njia nyingine upande wa Magharibi, alitaka kutoka nje ya mbuga hiyo kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa, hakukuwa na amani hata kidogo.

Wakati akiendelea na safari yake hiyo, akaanza kusikia muungurumo wa helikopta ikipita angani. Kwanza akashtuka, hakujua upande ilikokuwa ikitokea helikopta hiyo, alichokifanya ni kuanza kukimbia.

Hakukuwa na mti mrefu, eneo kubwa lilikuwa na nyasi nyingi, alijua kwamba helikopta hiyo ilikuwa ikifanya doria kuzunguka mbuga hiyo kwa ajili ya majangili ambao walitishia uhai wa wanyama kipindi hicho.
Wakati akiwa kwenye kasi ya kukimbia kuelekea upande huo wa Magharibi, akaanza kusikia sauti kutoka kwa mtu aliyekuwa katika helikopta ambaye alishikilia kipaza sauti akimtaka kusimama.
“Simama hapohapo ulipo,” ilisikika sauti ya mwanaume.

Hakutaka kukaidi, akasimama na kuanza kuiangalia helikopta ile.
Hakuwa na hofu hata mara moja, helikopta hiyo ikaanza kuelekea chini.
Wakati akiisubiria ili atoe maelezo, mara kwa mbali mbele yake akawaona simba wakianza kukusanyika kuelekea kulipokuwa na helikopta hiyo.

Hiyo ilimuogopesha, hakutaka kusimama tena, tayari mbele yake kulionekana kuwa na hatari, alikuwa na bastola na kama angepiga risasi basi simba hao wangekimbia kama tu wangesikia mlio wa risasi, ila kwa sababu mlio wa helikopta ulionekana kuumeza mlio wa risasi hata kama angepiga, hakuona sababu ya kusimama akaanza kukimbia.
Watu waliokuwa wakifanya doria kwenye mbuga hiyo walipomuona akikimbia, nao wakaanza kumkimbiza kwa helikopta hiyo huku wakirusha risasi kwani waliamini mtu huyo alikuwa jangili na alikuwa akiwakimbia.

Hawakutaka kujiuliza zaidi juu ya sababu iliyomfanya Fredrick kukimbia, hawakujua kama mtu huyo aliwakimbia simba, wao walichojua ni kwamba aliwakimbia wao kwa kuwa walitaka kumkamata, hivyo wakaanza kumkimbiza huku wakijitahidi kumrushia risasi alizozikwepa kwa mtindo wa zig zag, yaani kwenda kulia na kushoto, kushoto na kulia, tena kwa kasi ya ajabu.

Je, Fredrick atakamatwa? Usikose kufuatilia hadithi hii ya kusisimua
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…