Magazetini
JF-Expert Member
- Aug 16, 2014
- 593
- 1,713
WAKULIMA na wavuvi wa mjini Sumbawanga wameendelea kusota kutokana na kushuka kwa bei ya mahindi na samaki wabichi wanaovuliwa katika Ziwa Tanganyika wilayani Kalambo kwa kukosa soko la uhakika.
Uchunguzi wa mwandishi wa habari hizi aliofanyika hivi karibuni umebainisha kuwa bado bei ya rejareja ya mahindi inaendelea kuporomoka sokoni kutokana na bidhaa hiyo kuvunwa kwa wingi huku wakulima hao wakikosa soko la uhakika.
Katika baadhi ya masoko bei ya rejareja ya gunia la mahindi lenye uzito wa kilo 100 linauzwa kati ya Sh 12,000 na 15,000 ambapo msimu uliopita lilikuwa likiuzwa kati ya Sh 50,000 na 65,000 kwa uzito na ubora huohuo.
Kwa mujibu wa wachuuzi wa samaki wabichi maarufu hapa kama ‘migebuka' wanaovuliwa katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo, wanakiri kuwa bei ya rejareja ya kitoweo hicho sasa ni ‘bwerere' kwamba imeporomoka sana kutokana na samaki hao wabichi kuvuliwa kwa wingi na kufurika sokoni. Samaki watatu hadi wanne wenye uzito mkubwa katika soko la samaki la Nelson Mandela mjini hapa wanauzwa katik ya Sh 8,000 na Sh 10,000.
Hata hivyo, wakati wakulima na wavuvi wakilalamika kukosa soko na bei kuporomoka, neema inaonekana kuwaendea walaji ambapo baadhi ya wakazi wa mjini hapa na kwingineko wamekiri kuwa hii ni neema ya pekee kwani kila familia sasa ina uwezo wa kumudu bei ya mahindi na samaki kuliko ilivyokuwa awali.
"Mie nyumbani kwangu kila siku sasa tunakula samaki wabichi hadi wametukifu licha ya ufukara wetu, niseme kweli bei hii ya vyakula tunaimudu. Nilichokifanya nimenunua mahindi kwa wingi na kujiwekea akiba ya kutosha hata kama yatapanda bei tena," anasema John Simwanza, mkazi wa mjini Sumbawanga.
Baadhi ya wageni kutoka mikoa ya jirani na mbali waliozumgumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa wamekiri kuwa wanawaonea ‘wivu' wakazi wa mkoa wa Rukwa kwa neema ya vyakula vingi walivyobarikiwa kuwa navyo.
"Mie natokea Dar es Salaam, tatizo ni umbali, hakika ningeweza kununua magunia ya mahindi ya kutosha na kusafirisha hadi nyumbani kwangu. Bei hii mbona nzuri sana kwani gunia la mahindi hapa linauzwa kati ya Sh 12, 000 na Sh 15,0000 tu, hakika ni neema ya pekee kabisa, nawaonea wivu watu hawa," alibainisha Joseph Msemwa mkazi wa jiji la Dar es Salaam aliyepo mjini hapa.
Hata hivyo, wakulima nao wanaendelea kulia kuwa mahindi yamewadodea majumbani baada ya kukosa soko la uhakika wakidai kuwa kwa zao hili ni kila kitu kwao.
"Sijui tutakuwa wageni wa nani jamani mahindi tunayo tena kwa wingi yametudodea hatujui tuyapeleke wapi tulitegemea sana soko la Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) Kanda ya Sumbawanga lakini nao wamepangiwa kiasi ‘kiduchu' sana cha kununua msimu huu," alibainisha Emanuel Msemakweli, mkazi wa mkoani hapa.
CHANZO: Habari Leo