Saed Kubenea, Mwandishi, Mhariri, Mkurugenzi na Mmiliki wa kampuni ya Hali Halisi Publishers wanaomiliki MwanaHalisi,ametoa tamko na kuzungumzia kufungiwa kwa gazeti lake. Hata hivyo hajafichua siri ya mkakati wake namba mbili. Taarifa kamili ni kama ifuatavyo;
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
31 Julai 2012
NDUGU waandishi wa habari,
Natumaini mna taarifa kwamba tangu jana, serikali imefungia gazeti la MwanaHALISI kwa muda usiojulikana.
Kama inavyoelekezwa na sheria katili ya Magazeti ya Mwaka 1976, serikali hailazimiki kukwambia mapema wala kukueleza sababu.
Huo ndio ufedhuli wa sheria ambayo Tume ya Jaji Nyalali ilisema, zaidi ya miaka 20 iliyopita, kwamba ama ifutwe kabisa au ifanyiwe marekebisho makubwa.
Barua kutoka MAELEZO ilitoa maelekezo tu kwamba nimezuiwa kutoa gazeti na kwamba nisome kwenye Gazeti la Serikali Na. 258 la 27 Julai 2012.
Sheria hii katili ya magazeti ingali hai. Haijafutwa. Watawala wanaihitaji. Wanaitumia kutunyanganya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kuwasiliana. Wamefanya hivyo kwa MwanaHALISI. Wametishia kufanya hivyo kwa vyombo vingine vya habari. Hii ni hatari.
Lakini yote haya yanafanyika wakati serikali imekalia, kwa zaidi ya miaka miwili sasa, mapendekezo ya wadau wa habari yanayotafuta kuwepo sheria ya Uhuru wa Habari.
Serikali imetusikitisha. Imetuhuzunisha. Imetunyanganya uhuru na haki ya kuwasiliana. Imepora pia uhuru wa wananchi wa kupata taarifa na habari kutoka chombo madhubuti.
Aidha, tendo hili la serikali limedhamiria kuua wafanyakazi na watendaji wengine katika kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited inayochapisha gazeti hili. Dhamira hii imejikita katika kauli ya serikali kwamba gazeti limefungiwa kwa muda usiojulikana.
Si hao tu. Kuna wanaotegemea kuchapa gazeti hili na kupata ujira. Kuna wanaotegemea kuuza gazeti hili na kuendesha maisha yao. Wote hawa serikali imeweka maisha yao kiganjani mwake - kuwaamulia uhai au kifo. Hii ni hatari.
Hii si sahihi. Hii si haki. Tendo la serikali, licha ya kuwa la maangamizi kwa biashara yetu; linatishia uhai wa wafanyakazi na familia zao.
Tunaitaka serikali iondoe amri yake ya kufungia gazeti letu. Tunaitaka serikali iache kutishia maisha ya raia wake kwa njia ya kutuondoa katika biashara. Tunaomba wasomaji wetu na wadau wengine wa habari, wasimame nasi katika kudai uhuru na haki yetu ya kutafuta na kusambaza habari. Nchi hii ni yetu sote.