GHARAMA ZA UONGOZI
Ni watu wachache sana wanaotambua adha, shida, manyanyaso, upweke, matusi, dharau, na mambo mengine magumu wanayopitia viongozi. Wengi wanapofikiri kuhusu majukumu na nafasi ya Uongozi wanavuta taswira ya heshima na utukufu dhana ambayo siyo sahihi hasa kama Uongozi huo unatoka kwa Mungu. Musa ni Kiongozi Mkuu aliyeheshimika sana na Mungu na wanadamu. Pia aliogopewa na maadui au nchi za jirani. Aliongoza taifa lililokuwa likiogopewa na kuheshimika na kutetemekewa sana. Uchumi wa nchi yake ulipoporomoka na baa la njaa lilipoingia, alitenda muujiza wa kuwalisha na pia kuwapa maji watu wake. Zaidi ya yote, alikuwa ndiye Baba wa Taifa la Israel aliyeongoza harakati za kulitoa taifa lake kutoka katika makucha au ukoloni wa Wamisri. Pamoja na hayo yote, wasaidizi wake wakuu tena ndugu zake (Haruni na Miriamu) waliongoza magenge ya kumpiga vita, kumtukana, kumchafua, na hata uasi uliozaa mapinduzi dhidi ya Kiongizi Mkuu Musa. Maasi na mapinduzi yale yalikuja kuzimwa na Mungu mwenyewe. Mungu alipotaka kuwaua wasaidizi wale ambao sasa waligeuka kuwa mwiba Musa aliwaombea msamaha kwa machozi hadi Mungu akawasamehe (Soma tukio zima katika Kutoka 12). Viongozi wengi wa Kanisa, jamii, siasa na hata serikali wanapitia katika changamoto za kutukanwa, kugeukwa, kuonewa wivu, kunyanyaswa, kuchafuliwa, na hata kusingiziwa! Kwamba hayo yanafanywa ma marafiki na sio maadui ndicho kinaongeza maumivu zaidi. Jaribu kubwa kwa kiongozi anayepitia changamoto hizo ni kutaka kujaribu kujibu mapigo jambo ambalo linapelekea uongozi wake uchuje mbele ya safari.
Ninao ujasiri kumtia moyo kila mtu anayetimiza majukumu na wajibu wa Uongozi ili atambue kuwa kashfa, matusi, wivu, na dharau dhidi ya wale walioitwa kutumikia wajibu wa Uongozi ni baadhi ya mitihani ambayo hatuna budi kuipitia. Kamwe tuepuke majaribu na misukumo inayotutaka tujibu mapigo. Zaidi ya yote tuepuke kutumia nafasi zetu ili kupambana nao au kuwanyamazisha. Kati yao wapo watakaotujia tena baadaye kwa kutaka kuomba ushauri na msaada. Tuwe tayari kuwasaidia na hatimaye Mungu atawatumia hao hao kutusafisha matope waliyoturushia. Furaha na kipimo cha Uongozi ni pamoja na kuwahudumia kwa furaha na upendo watu wote wakiwemo wale walioshiriki kutuchafua na kurarua mioyo yetu.