Filamu ya Mapanki, kwa maoni yangu, inaonekana kuwa na ukweli kidogo na chumvi nyingi. Sasa kwa filamu ambayo inatakiwa iwe si ya kubuni bali mambo halisi (non-fiction), nadhani hii si sawa hata kidogo. Nachelea kusema kuwa baadhi ya madai ya kuhusika kwa serikali yetu kuwasaidia "waasi" katika hizi nchi za Maziwa Makuu katika kuwafikishia silaha yanaweza kuwa ya kukisia (speculative). Kwa nini, kwa mfano, isichukuliwe kuwa hizo silaha zilikuwa kwa matumizi ya majeshi ya nchi husika?
Mfano mwingine wa "chumvi nyingi" ni madai kuwa Watanzania na hususan wakazi wa Mwanza hawanufaiki na biashara ya samaki. Ni wazi kuwa katika mfumo wa uchumi unaotawala dunia ya utandawazi baadhi ya watu watanufaika na wengine wataumia; huu ndiyo ukweli. Mwanza naifahamu vizuri, na siamini kama kuna watu wanakula samaki wenye kutoa funza eti kutokana na uhaba wa samaki! Huko ndiyo kuzidisha chumvi. Wazungu wanasema "fiction thrives on exaggeration" na ndiyo maana filamu hii, kwa kiasi kikubwa, inakosa sifa ya kuwa non-fiction!
Kwa mantiki hiyo, mtu unaweza kupata shaka kuhusu nia ya kuandaa filamu ya
documentary yenye mwelekeo au upendeleo fulani. Ikumbukwe pia japo filamu ilitengenezwa siku kadhaa zilizopita ni miezi michache tu iliyopita ambapo ilionyeshwa kwenye televisheni Uingereza. Tujiulize, kwa nini ionyeshwe wakati huo? Unaamini katika "coincidence"?
Hii filamu ya Mererani (sipendi hata kutumia jina lake!) nayo tunasikia itaonyeshwa hapo New York (UN) wakati huu. Ieleweke kuwa JK naye atakuwa hapo hivi karibuni. Na sentesi ya mwisho wa filamu hii ni swali kwa rais! Bila shaka waandishi wa habari watatumia swali hilo hilo pia kumuuliza JK.
Tanzania kuna ofisi za ILO-IPEC, lakini afisa wa ILO aliyeongea katika filamu hiyo yuko Kenya. Labda pia ni "coincidence" na si kitu sana! Kwani sote tuko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na tunapendana!!
Ili kuzidi kujifikirisha tujiulize baadhi ya maswali, kama vile:
Nani anafaidika na nani anaathirika na filamu hii?
Je, filamu hii inaweza kuathiri biashara ya tanzanite?
Watakaoathirika ni wachimbaji wadogo wazawa, au wachimbaji wakubwa (soma AFGEM/TanzaniteOne)?
Madhara ya filamu hii kwa taifa ni zaidi kwa uchumi (economic) au sifa/rekodi ya Tanzania kuhusu haki za watoto na binadamu kwa ujumla (human rights)?
Filamu inasaidia vipi kutatua umaskini wa Tanzania au inaishia tu kuonyesha athari za umaskini na utandawazi (soma utandawizi)?
Je filamu ina uhusiano wowote na yale yalijadiliwa humu ndani (barazani), mintarafu "Kampeni na ahadi za CCM/JK huko Mererani wakati wa Uchaguzi"?
Je, filamu hii ina uhusiano na njama za kuangusha biashara ya tanzanite, kama ilivyowahi kudaiwa na Marekani kuwa fedha za tanzanite kutoka Tanzania zilitumiwa na Osama bin Laden? (jamaa walitaka kuzuia biashara ya tanzanite)
Maswali na mifano ya namna hii ni mingi. Kuna wakati Marekani iliwahi kudai kuwa Tanzania si salama (kiugaidi) na hivyo kuonya raia wake kusafiri kwenda Tanzania! Baada ya kubanwa waliomba radhi.
Kuna wakati fulani baadhi ya Wanasayansi walidai kuwa Mlima Kilimanjaro ulikuwa umepoteza theluji yake na unateketea. Baada ya kubanwa pia walikula maneno yao.
Hebu tuangalie picha kubwa (big picture) ya nini kimekuwa kikiripotiwa katika vyombo vya habari nchini Tanzania katika siku za karibuni kuhusiana na rasilimali zetu. Nitatoa mifano miwili. Kumekuwa na habari za vifo vya sokwe mtu huko Kigoma (Mahale Game Reserve) na ugonjwa na vifo vya simba huko Serengeti. Hii ni "coincidence"?
Tanzania sasa inakabiliwa na matatizo ya umeme (usiulize jamaa wa NetGroup walikuwa wanafanya nini siku zote na hawakujua habari za Mtera na Kidatu). Nadhani hiyo mitambo ya gesi ya Ubungo toka ifungwe ishaharibika kama mara tatu hivi. Nafikiri wakati fulani JK alitembelea pale Ubungo kwenye mitambo, wakati imeharibika, akawauliza watu wa Wizara kuwa mitambo inapoharibika mkataba unasemaje? Hii, kwa maoni yangu, ni kutaka kuwabana hao jamaa wasije wakawa wanafanya njama mitambo "inaharibika" kumbe hiyo yote ikiwa ni kuhujumu uchumi.
Nihitimishe maoni yangu kwa kusema kuwa ni vema wakati mwingine tukawa tunayaangalia matukio kwa mapana na marefu, na pia kujiuliza kama kuna "coincidence" baadhi ya matukio yanapotokea. Nafikiri wenzetu Wazungu hawana mambo ya "coincidence" hasa inapokuwa wanasughulikia masuala yenye maslahi ya taifa. Wengine, na pengine, wamekwenda mbali zaidi kiasi cha kukana uwepo wa Mungu kwani hawaamini katika mambo kutokea kwa bahati tu.