GAVANA BOT Aruka viunzi, amtumpia mpira Msaidizi wake | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

GAVANA BOT Aruka viunzi, amtumpia mpira Msaidizi wake

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Bujibuji, Apr 15, 2010.

 1. Bujibuji

  Bujibuji JF-Expert Member

  #1
  Apr 15, 2010
  Joined: Feb 4, 2009
  Messages: 35,288
  Likes Received: 22,051
  Trophy Points: 280
  Wasalaam waheshimiwa,

  SAKATA la matumizi yenye kutia shaka ya fungu la fedha lililopitishwa na Bunge kwa ajili ya kuhami uchumi, maarufu kama stimulus package , sasa limemrudia Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Beno Ndulu, ambaye baada ya baadhi ya kampuni za ununuzi wa pamba kukosa mgawo huo katika mazingira yanayozua maswali zilimtaarifu naye akawajibu kuwa Serikali haina fedha.
  Hata hivyo, wakati Gavana akitoa majibu hayo kuwa “Serikali haina fedha” si fedha zote Sh. trilioni 1.7 zilizoidhinishwa na Bunge la Tanzania ndizo zilizotumika katika mpango huo wa kunusuru uchumi uliotikiswa baada ya uchumi wa dunia kuyumba.
  Wiki hii Gavana Ndulu amekwepa kuzungumzia suala hilo, akidai kwamba kwa sasa linashughulikiwa na mtu maalumu chini yake anayepaswa kutafutwa kuzungumzia suala hilo.
  Raia Mwema ilipozungumza na Profesa Ndulu, ambaye alieleza kuwa yuko mkoani Mwanza kwa ajili ya mkutano, alisema masuala ya ‘‘stimulus package’’ yamekabidhiwa mtu maalumu ndani ya benki hiyo, na kwamba si yeye anayeweza kuyazumngumzia.
  “Haya masuala ya stimulus package tumempa mtu maalumu ambaye ni mkuu wa kitengo cha sera na utafiti, mimi siwezi kuyazungumzia,” alijibu Ndulu hata alipotakiwa kujibu yale yanayomhusu moja kwa moja katika sakata hilo pia hakuwa tayari kuzungumzia.
  Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kuwa fedha zilizokwishakutumika ni sehemu tu ya Sh trilioni 1.7 zilizopitishwa na Bunge, ambazo ni takriban Sh bilioni 870.8. Fedha hizo Sh bilioni 870.8 kwa mujibu wa taarifa zilizopo ndizo zilizokwishakutolewa na Benki Kuu (BoT), chombo ambacho kimepewa mamlaka ya kutoa fedha hizo.
  Kwa mujibu wa utaratibu wa BoT, fedha hizo hutolewa kutoka benki hiyo kwenda katika benki ambazo zilikopesha kampuni zinazostahili kufidiwa, ambazo zimeathiriwa na mtikisiko wa uchumi duniani.
  Raia Mwema limepata kuripoti kuhusu utata uliopo katika benki hizo katika kufidia kampuni husika ikibainika kuwa baadhi ya michanganuo ya hesabu za kampuni husika inaonyesha hazikupata hasara lakini baadhi ya benki zilipendekeza kampuni hizo zilipwe fidia ya mabilioni.
  Mbali na baadhi ya kampuni kulipwa fidia pasipo kupata hasara kwa mujibu wa taarifa zao za kihasibu zilizowasilishwa katika benki husika, zipo kampuni nyingine ambazo zimebainika kupata hasara ndogo lakini ikipendekezwa zilipwe fedha nyingi zaidi kama fidia.
  Taarifa zaidi zinabainisha kuwa sehemu ya fedha hizo zimepelekwa kwa kampuni zinazohusika na mazao ya kahawa zao ambalo pia huuzwa katika soko la dunia kama ilivyo kwa pamba.
  Nyraka ambazo gazeti hili limepatiwa zinazoonyesha taarifa za benki na michanganuo ya kampuni husika, Benki ya CRDB ikipendekeza kampuni 26 zilipwe mabilioni kadhaa na mbili zikitupwa nje ya mgawo, wakati benki ya TIB ikiidhinisha malipo kwa kampuni moja ya Al-Adawi, kupewa fidia ya Sh milioni 405.6 ambazo mapendekezo ya awamu ya pili hayakuridhia malipo hayo.
  Benki nyingine zilizohusika ni Kenya Commercial iliyokagua mchanganuo wa kampuni ya Birchand Oil Mills Ltd, iliyopendekeza kampuni hiyo ifidiwe Sh bilioni 1.66, lakini mapendekezo mbadala ya watalaamu yalitaka kampuni hiyo ifidiwe Sh bilioni 4.642, Exim Bank Tanzania Ltd imependekeza kampuni ya Bio Sustain kufidiwa Sh milioni 597.7 lakini baada ya uhakiki mwingine kampuni hiyo ikapendekezwa kulipwa milioni 458.1 na Stanbic Bank ilipendekeza kampuni ya S & Ginning Co. Ltd kufidiwa Sh bilioni 5.69, lakini ikabainika inastahili kufidiwa Sh bilioni 2.86.
  Katika Benki ya CRDB utata unazidi miongoni mwa kampuni ambazo zimeomba fidia kupitia benki hiyo. Kampuni ya Badugu Ginning ya Musoma, ambayo hesabu zake zinaonyesha katika shughuli zake imetumia Sh bilioni 4.41, ikipata mapato ya Sh bilioni 2.94 kwa mauzo ya pamba na Sh milioni 727.6 kutokana na mauzo ya mbegu za pamba na pato lake la jumla ni Sh bilioni 3.7, ikiwa imetengeneza hasara ya milioni 742.2.
  Licha ya mchanganuo huo unaoonyesha kampuni hiyo kupata hasara ya Sh milioni 742.2 ilipendekezwa na Benki ifidiwe Sh bilioni 1.4, hata hivyo mapendekezo ya awamu ya pili yalipinga taarifa hizo na kutaka kampuni hiyo ifidiwe Sh milioni 742.2 tu.
  Kampuni ya Chesano Cotton Ginning Ltd ya Bariadi, Shinyanga imebainisha CRDB kuwa matumizi yake (ununuzi na uendeshaji) ni Sh bilioni 2.6, mapato yake kutokana na uuzaji nyuzi za pamba ni bilioni 1.99 (bilioni 2), mauzo yaliyotokana na uuzaji mbegu za pamba ni Sh milioni 586 na kwa hiyo mapato yake ya jumla ni sh bilioni 2.6.
  Utata unaojitokeza ni kwamba kwa mchanganuo huo wa Benki ya CRDB kampuni hiyo imepata faida ya Sh milioni 6.4, lakini benki hiyo hiyo ikapendekeza kampuni ifidiwe Sh milioni 580. Hata hivyo, ukaguzi zaidi wa hesabu ulipofanyika, kampuni hiyo haikupendekezwa kulipwa chochote. Kampuni nyingine ambayo fidia yake inaonyesha utata ni Gaki Investment Ltd ya Shinyanga.
  Gaki Investment Ltd imebainika kununua kilogramu takriban milioni 19.8 za pamba, ikitumia Sh bilioni 12.9, mapato yake baada ya biashara ya nyuzi za pamba ni Sh bilioni 12.15, mapato yaliyotokana na kuuza mbegu za pamba ni Sh bilioni 1.727 na kwa hiyo mapato yake ya jumla kwa msimu husika ni Sh bilioni 13.9, ikijizolea faida ya Sh bilioni 1, lakini ukaguzi wa kibenki (CRDB) ukionyesha imepata hasara milioni 146 na ifidiwe kiasi hicho, lakini ukaguzi wa pili huru ukapendekezwa kampuni hiyo kutolipwa chochote.
  Kampuni ya Igunga Cotton Ltd yenye makao yake makuu Dar es Salaam, hesabu zake zilizowasilishwa CRDB ambazo gazeti hili limepata mchanganuo wake zinabainisha ilinunua kilogramu milioni 2.8, ikitumia Sh bilioni 1.9, mapato kutokana na mazao ya pamba iliyonunua Sh bilioni 1.43, mapato kutokana na mauzo ya mbegu za pamba ni Sh 300.5, mapato yake ya jumla ni Sh bilioni 1.7, ikitajwa kupata hasara ya Sh milioni 205.
  Lakini licha ya kampuni hiyo kupata hasara ya Sh milioni 205, ilipendekezwa na watalaamu wa benki ya CRDB ifidiwe Sh milioni 839, hata hivyo uhakiki huru wa awamu ya pili ulipofanyika, kampuni hiyo ikatakiwa ifidiwe hasara yake halisi ya Sh milioni 205.
  Ipililo AMCOs Ltd ambayo katika msimu husika ilinunua pamba kilogramu milioni 101, ikitumia Sh milioni 82, na mauzo yake ya nyuzi za pamba yakiwa Sh 54.5 na mauzo ya mbegu za pamba yakiwa Sh milioni 10.8, mapato yake ya jumla yakiwa Sh milioni 65.35, ikitajwa kupata hasara ya Sh milioni 16.7 lakini ikapendekezwa na benki ifidiwe Sh bilioni 51, ukaguzi wa pili ulipofanyika ikapendekezwa ifidiwe hasara halisi tu, ambayo ni Sh milioni 16.7.
  Jambo Oil & Ginneries Ltd ya Shinyanga, katika msimu husika ilinunua kilogramu milioni 22.08, kwa gharama ya Sh bilioni 13.9. Mapato ya kampuni hiyo katika uuzaji wa nyuzi za pamba ni Sh bilioni 12.51, mauzo kutokana na mbegu za pamba yameiingizia kampuni hiyo Sh bilioni 2.4 na kwa hiyo mapato yake ya jumla ni Sh bilioni 14.9, ikijipatia faida ya Sh milioni 927.1, utata unaibuka pale benki baada ya kupitia mchanganuo huo wa hesabu kupendekeza ifidiwe Sh bilioni 1.06.
  Kahama Oil Mill Ltd ya Kahama yaShinyanga, ilinunua kilogramu milioni 24.9 na mchanganuo wa kampuni hiyo uliowasilishwa benki ukionyesha kuwa imetumia Sh bilioni 19.8, ikipata Sh bilioni 14.6 kutokana na mauzo ya nyuzi za pamba na Sh bilioni 2.7 za mauzo ya mbegu za pamba na kujipatia mapato ya jumla, Sh bilioni 17, ikipata hasara ya Sh bilioni 2.3, lakini benki ikipendekeza ifidiwe Sh bilioni 4.4.
  Kampuni ya Kisumwa Machinery Ltd, ambayo nyaraka zilizopo hazibainishi kama imewasilisha mchanganuo wake lakini wakati huo huo imependekezwa ilipwe fidia ya Sh milioni 377. Mbali na kampuni hiyo, kampuni nyingine ambayo ingawa mchanganuo wake haukubainishwa lakini ikipendekezwa kulipwa fidia ni Morogoro Canvas Mills (1998) Ltd, iliyopendekezwa na benki ilipwe fidia ya mtikisiko wa uchumi duniani, Sh bilioni 1.612.
  Sakata la fedha hizo lilianza mwaka jana wakati Serikali ilipowasilisha bungeni suala la ‘stimulus package’ ambapo Kiongozi wa Upinzani, Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, alisema fedha hizo hazina tofauti na fedha zilizoibwa BoT kutoka Mfuko wa Madeni ya Nje (EPA) kwa kuwa hazijawekewa utaratibu unaowezesha kuwapo uwazi na uadilifu.
  Akizungumza katika hotuba yake bungeni mwaka jana Hamad, kwa niaba ya wabunge wenzake kutoka vyama vya CUF, CHADEMA na UDP, alihoji masuala mbalimbali kuhusu matumizi ya fedha hizo za stimulus package, zipatazo Sh. trilioni 1.7, zilizokuwa zimetangazwa awali na Rais Jakaya Kikwete.
  “Tunataka sheria ya Appropriation Act iwe na Schedule maalumu ya Stimulus Package na iseme waziwazi nani atapata nini, kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge iwe inapata taarifa kila miezi mitatu ya utekelezaji wa hiyo stimulus package.
  “Ni ukweli uliowazi kuwa stimulus package inazinufaisha benki tu, kwa kuzipa mwanya wa kufanya biashara nzuri na Serikali kwa kutumia fedha za Serikali yenyewe, na ndiyo maana katika nchi nyingine Serikali imelazimika kuwa na hisa ili kuhakikisha kuwa fedha iliyotolewa ambayo inatokana na kodi za wananchi inadhibitiwa na kurudi kwa walipa kodi na wapiga kura,” alisema.
  Hamad alisema katika bajeti ya mwaka 2007/08 na ile ya 2008/09 Serikali ilijizuia kukopa kwenye mabenki, kwa kigezo kikubwa kuwa mabenki yaweze kufanya biashara ya kukopesha sekta binafsi na kuwa zuio hilo liliongeza ufanisi kwa mabenki kukopesha sekta binafsi kwani mikopo kwa sekta binafsi ilipanda hadi kufikia asilimia 40.
  Alisema Hamad: “Serikali imeamua kufidia vyama vya ushirika na kampuni zinazonunua mazao ya wakulima na kuyauza kwa hasara. Katika soko huria kuna kupata faida na kupata hasara. Wafanyabiashara makini wa mazao hupanga bei zao za kununulia mazao kwa kuzingatia bei walioipata katika soko la baadaye.
  “Hata hivyo wengine hawapendi kuchukua tahadhari kwa kutegemea kwamba bei itapanda na kwa hiyo watapata faida kubwa. Bei imeshuka kwa hiyo wamepata hasara. Je, hakuna wafanyabiashara wa mazao waliolipa mikopo waliokopa kwa kujibana. Serikali ina uhakika gani kuwa mikopo hii ilitumiwa vizuri?”
  Aliongeza: “Serikali imeamua kutoa udhamini wa madeni ambayo wakopaji kwa sababu ya msukosuko wa uchumi wa dunia wanapata matatizo kulipa kwa wakati. Serikali imeamua madeni haya yadhaminiwe kwa miaka miwili na si mwaka mmoja ili shughuli za Uchaguzi Mkuu wa 2010 ziwe zimemalizika. Hii itatoa mwanya kwa wanaodhaminiwa madeni wachangie kwenye kampeni na baada ya uchaguzi mzigo wa madeni ubebwe na Serikali.
  “Kuna hatari ya EPA nyingine kuzinduliwa. Ukaguzi wa kina wa mahesabu ya makampuni husika ufanywe na CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali) kwa gharama za mabenki yaliyokopesha kabla ya Serikali kuyadhamini makampuni haya,” alionya Hamad wakati huo.
  CHANZO: RAIA MWEMA.
   
Loading...