Fungate la Uwekezaji na Migogoro ya Maslahi Escrow

Companero

Platinum Member
Jul 12, 2008
5,562
2,000

Fungate la Uwekezaji na Migogoro ya Maslahi Escrow


Ufisadi wa Escrow ni ishara kuwa sasa tumemaliza rasmi fungate la uwekezaji Tanzania. Harusi tuliyofunga kwa chereko na nderemo nyingi na wawekezaji katika miaka ya 90 imegeuka shubiri. Kama wahenga wetu walivyonena, “kukopa harusi, kulipa matanga”.


Kwa hisani ya wafadhili wetu tulijiingiza kwenye sera za Serikali kukopa, kukodi, kununua, kuuza, kuwekeza na kuingia ubia kwa kutumia fedha za (mashirika ya) umma bila kuzingatia kwa kinadhana ya mgogoro wa maslahi katika mapana yake. Hivyo, kupitia Azimio la Zanzibar lililolizika rasmi Azimio la Arusha tumeishia kuwa na wanasiasa ambao wanavaa zaidi ya kofia moja. Japo sio vibaya kuwa na nyadhifa au shughuli zaidi ya moja ni hatari pale zilizo binafsi zinapogongana na za umma.


Mtu anaweza kuwa mwanasheria wa Serikali na wakati huo huo akapata ‘gawiwo’ litokanalo na hisa zilizopo kwenye kampuni inayochunguzwa na Serikali. Pia mtu anaweza kuwa mbunge, mmiliki wa kampuni binafsi na mwanasheria wa kampuni ya umma inayochunguzwa na Kamati ya Bunge. Kama hili haliwekwi wazi na kutatuliwa lazima mgongano wa maslahi unaoleta au unaoulinda ufisadi kama wa Escrow utokee.


Ni katika muktadha huu swali la kama fedha zilizochotwa katika akaunti ya Escrow ni za umma au za binafsi linapokuwa na uwili usio na tija. Ziwe za umma ama zisiwe za umma ukweli ni kuwa uchotaji wake ni zao la mgogoro mkubwa wa kimaslahi na kiuchumi. Hata kama Serikali itaweza kutumia uprofesa wa hali ya juu kututhibitishia pasipo shaka kuwa ni za binafsi, bado haiwezi kuepuka ukweli kuwa fedha hizo hawajapewa watu binafsi tu bali na wale ambao wana dhamana katika mihimili mikuu mitatu ya Serikali.


Hata hao watu binafsi wamegawiwa fedha hizo katika mazingira holela ya utoaji fedha na uhujumu uchumi. Inawezekana kabisa kuwa ‘utakatishaji wa fedha haramu’ na uingizaji huo wa fedha nyingi kiasi hicho kwa kasi hiyo katika mzunguko wa fedha wa nchi ndio umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka zaidi kwa mfumuko wa bei katika kipindi hiki. Kama alivyosema mchangiaji mmoja katika mtandao wa kijamii, hali hii inafanana na Mansa Musa wa Mali alivyopitisha dhahabu nyingi Misri na kudidimiza thamani yake nchini humo. Tofauti ni kuwa hakuwa Mmisri na wala hakuwa mtuhumiwa wa ufisadi.


Tatizo linalojitokeza katika mjadala wa Escrow ni wachangiaji wengi pia kugawanyika katika uwili huo – za binafsi au za umma. Na ni uwili huo huo unaopelekea kwa kiasi kikubwa ‘mashabiki’ wa kila upande kuvutia kwao na kupata tabu kukubali hata hoja yenye ‘mashiko’ kutoka upande mwingine. Pengine tutumie mfano wa Mbunge wa Jimbo la Mtera ambaye hoja na vioja vyake vimeacha gumzo kubwa mitaani na mitandaoni.


Pamoja na kuwa uwasilishaji wake uliomfanya ajulikane kwa jina la utani la ‘Kibajaji’ wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki unawakera watu wengi wenye staha, tunahitaji uvumilivu wa kutuwezesha kuchambua na kutenganisha mchele na chuya. Hapo chuya ni lugha yake isiyo ya ‘kistaarabu’. Mchele hapo ni hoja yake ya msingi kuwa kuna makundi kadhaa yenye maslahi katika mjadala wa Escrow.

Waziri mmoja anayetajwa kuwa miongoni mwa wenye nia ya kugombea Urais mwakani aliguswa na bainisho hilo na kujenga hoja kuwa mgombea Urais hapaswi kuwajengea zengwe wagombea wengine waondoke kwenye kinyang’anyiro bali anapaswa kuwa tayari kushindana na wenzake katika uchaguzi. Lakini hilo ni ‘tamanio’ tu la kisiasa, hali halisi inaonesha kuwa mbinu nyingi hufanyika ili kuhakikisha wagombea, hasa wale wenye nguvu ya umma au ya ufisadi, hawapati fursa ya kupitishwa kuwa wagombea na hivyo kutumia nguvu hizo kushinda uchaguzi wa kuteua mgombea katika vyama vyao.


Lakini kundi mmojawapo lililotajwa na Kibajaji ambalo pengine ndilo linaloelezea kwa ufasaha dhana ya fungate la uwekezaji na migogoro ya maslahi ni lile linalohusiana na ufanyabiashara. Hapa tunaona makampuni na hata nchi ambazo baadhi ya makampuni hayo yanatokea zikijaribu kujipenyeza kwenye michakato na mijadala inayohusiana na uwekezaji katika sekta ya umeme kulinda maslahi ya nchi zao na raia wao. Ndiyo maana mabenki kadhaa ya nje yamekuwa sehemu ya mjadala wetu wa sakata la Tegeta Escrow.


Ili kuelewa hii hoja iliyojifichajificha katika vioja vya Kibajaji nadhana ya CSC katika uwekezaji ni vyema turejee maneno ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mahesabu ya Serikali wakati anajumuisha hoja kuhusu Escrow. Ameitaja kwa jina benki mojawapo kubwa ya nje na kusema kuwa iliwahi kuja na balozi wa nchi yao [ambayo ni mfadhili mkubwa wa bajeti ya nchi yetu] ‘kulobi’, yaani kushawishi, ili “tuwaachie” tu “wachukue hela za Escrow”, ikabidi ampigie aliyekuwa Waziri wa Sheria kuhusu uvunjaji huo wa protokali/taratibu za kidiplomasia.


Sasa tujiulize kwa makini sana ni wanasiasa na viongozi wangapi wanaofuatwa na taasisi hizi za kifedha/kibiashara zinazohusika kwa namna moja au nyingine na uwekezaji katika sekta zetu za umma?Mara ngapi? Wangapi hukubali ushawishi wao badala ya kuhoji uvunjaji huo wa taratibu zetu na mgongano wa maslahi? Tutegemee tu ujasiri na kuamini(a) tu uadilifu wao wa moyoni utakaowapelekea kuvijulisha vyombo vyenye dhamana ya kulinda sheria au uzito na ‘ujeuri/ukali’ wetu wa kitaasisi na kidiplomasia wa kuzuia uingiliaji wa taasisi zetu za umma?Fungate la uwekezaji hakika limeisha. Harusi ya wanasiasa na wawekezaji imezalisha migogoro mingi ya maslahi. Wakati wa ku(wa)tenganisha (wana)siasa na (wafanya)biashara ni huu.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom