Fulana zetu na ujumbe wa Mipasho

vukani

JF-Expert Member
Dec 30, 2009
245
165
Kama ningekuwa nimelisema hili humu katika kibaraza hiki, naamini wengi mungeniita mtabiri, lakini bahati mbaya nilikuwa bado sijajiunga na jamii forum.

Nakumbuka wakati fulani niliwahi kuwaambia wanafunzi wenzangu wakati huo nikiwa shule kuwa, tunapoelekea si ajabu kukaibuka fulana zenye ujumbe wa maneno ya Kiswahili kama vile yale yanayopatikana kwenye khanga. Hilo nililisema baada ya mwanafunzi mwenzetu mmoja kuvaa fulana ambayo aliiandika maneno ya Kiswahili kwa kutumia Marker Pen ambapo aliandika "MTACHONGA SANA" nadhani labda alikuwa akipeleka ujumbe kwa mahasimu wake ambao alitofautiana nao.

Hilo naona sasa limetimia. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao wamekuwa wakichapisha fulana kwa maneno yenye ujumbe tofauti tofauti kulingana na mahitaji ya jamii kwa kipindi hicho. Zamani tulizoea kuwa wanawake ndio wanaozodoana kwa kutumia maneno ya kwenye Khanga.

Kwa mfano maneno kama, "Utakufa nacho kijiba cha roho" Chuki nichukie roho yangu niachie" "kama unaweza panda juu ukazibe" Nakadhalika, nakadhalika, yalikuwa ni maneno yanayopatikana kwenye khanga peke yake na hiyo ndio iliyokuwa silaha pekee inayotumika na wanawake katika mapambano miongoni mwao hasa katika maeneo ya uswahilini.

Kwa kawaida kama wanawake wametofautiana katika mambo fulani fulani, badala ya kugombana kwa kupigizana kelele ilikuwa mtu ananunua khanga yake yenye ujumbe anaoutaka umfikie mbaya wake na kuvaa makusudi ili kufikisha ujumbe aliokusudia kwa mwenzake.
Niliwahi kusimuliwa wakati fulani kuwa hata wale wanawake wanaochukuliana mabwana, nao walikuwa wakipambana kwa kuvaliana khanga zenye ujumbe wa kuzodoana na wakati mwingine mtu anaweza kumchokonoa mwenzake kwa kuvaa khanga zenye ujumbe tofauti tofauti hata saba kwa siku na kujipitisha kwa mbaya wake ili kumpa ujumbe aliokusudia na mara nyingi ilikuwa ni kawaida kwa mahasimu hao kuanza kurushiana maneno na hata kupigana hadharani kutokana na mmoja kukerwa na maneno ya kwenye khanga alizovaa mwenzie.

Tofauti na zamani, siku hizi mambo yamebadilika, na sasa sio khanga pekee, bali hata fulana siku hizi zimekuwa zikibeba ujumbe tofauti tofauti ukiwemo wa maneno ya kuzodoana. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao huchapisha ujumbe wa maneno ambayo tulizoea kuyaona kwenye khanga na kuyaweka kwenye fulana na hata Blouse na watu wamekuwa wakizigombea.

Sio kwamba sifurahii ubunifu huo wa mavazi, bali ninachojaribu kutahadharisha hapa ni aina ya ujumbe unaowekwa kwenye hizo fulana, kuwa usije ukatufikisha mahali watu wakatumia nafasi hiyo kuweka ujumbe wa matusi au hata maneno ya uchochezi, kwani kuna uwezekano ukatufikisha mahali tusipopatarajia.

Naamini wengi mtakuwa ni mashahidi wa hizi fulana au blouse za mitumba zinazoingia kutoka katika nchi za Magharibi na Ulaya ambazo zina ujumbe wa maandishi au hata picha tofauti tofauti. Tumekuwa tukishuhudia ujumbe wa Matusi au hata uchochezi wa kiubaguzi kupitia fulana hizo, lakini kwa kuwa zimeandikwa kwa kiingereza au lugha zao inakuwa ni vigumu walio wengi kung'amua maana halisi ya ujumbe huo labda mpaka mtu aambiwe, wengi tunachojali ni uzuri wa fulana lakini sio ujumbe ulioko katika fulana hizo.
 
Back
Top Bottom