Upendeleo wa wawekezaji badala ya wananchi waanza kuleta yale tuliyokuwa tunayaogopa. Inasemekana wananchi waliokata tama baada ya Serikali kuwakumbatia wawekezaji badala ya wanachi, hatimaye maafa makubwa yametokea wilayani tarime kwenye mgodi wa Barrick.
Swali: Je, bila kuwa na sera makusudi zinazowanufaisha wanachi, je, Tanzania tutakuwa na amani kama haki haitendeki ? Soma habari ifuatayo- :
" WATU watano wameuawa na wengine kujeruhiwa katika mapambano kati ya polisi na raia wanaodaiwa kuvamia mgodi wa North Mara Barrick, wilayani Tarime jana alfajiri kwa lengo la kupora mawe ya dhahabu.
Watu wapatao 800 walivamia mgodi huo kwa lengo la kuchukua dhahabu kutoka kinu cha kusagisha mawe hali iliyowalazimu polisi kutumia risasi za moto.
Licha ya waliouawa, watu 10 wakiwamo polisi walijeruhiwa katika mapambano hayo ambayo wananchi walikuwa wakitumia silaha za jadi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tarime/Rorya, Constantine Massawe, alisema jana kuwa, kundi hilo la wavamizi lilikuwa na mapanga, marungu, makombeo na mawe.
Alisema, alituma kikosi cha Polisi waliokuwa na mabomu kuongeza nguvu katika mapambano na wavamizi hao waliojihami kwa mawe na marungu.
Alisema, polisi walilazimika kutumia risasi za moto baada ya kuzidiwa nguvu na kundi hilo.
Katika mtafaruku huo, magari ya Polisi na ya mgodi yaliharibiwa kwa kuvunjwa vioo kwa mawe. Hilo ni tukio la tatu mgodi huo kuvamiwa katika kipindi cha siku nne.
Alhamisi wiki iliyopita, Polisi ilisema watu zaidi ya 500 wa vijiji jirani na mgodi huo, walivamia kwa lengo la kupora mawe ya dhahabu.
Uvamizi mwingine ulifanyika Jumamosi. Miongoni mwa watu waliozungumzia hali hiyo ni pamoja na aliyekuwa Diwani wa eneo hilo lenye mgodi, Augustino Neto, aliyeishauri Serikali itafute utaratibu wa kuwapa wananchi maeneo ya kuchimba dhahabu ili kuepusha chuki iliyojengeka baina ya jamii dhidi ya mgodi huo. "
---------/
Chanzo cha Habari ni Gazeti la Habari leo
Imeandikwa na Samson Chacha, Tarime; Tarehe: 16th May 2011